Watu wanne wamefariki dunia Wilayani Kiteto mkoani Manyara baada ya kusombwa na maji yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali hapa nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magessa leo Ijumaa amesema vifo hivyo vimetokea kwenye matukio tofauti katika kata za Matui, Engusero na kijiji cha Ndaleta kata ya Njoro.

Magessa amesema tukio la kwanza lilitokea jana Alhamisi jioni kwenye kijiji cha Matui, ambapo watu wawili walisombwa na mafuriko wakati wakielekea nyumbani kwao.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Alhaman Gola (37) mkulima wa Matui na Abuu Juma (27) mkulima wa Kijiji cha Chapakazi.

Amesema mtu mwingine Hamis Chilogola (22) alikuwa na wenzake wawili wakielekea Kituo cha Afya Matui kwa ajili ya kutembelea mgonjwa lakini wakiwa njiani walisombwa na maji kwenye korongo wenzake walifanikiwa kuvuka yeye akafa kwa kusombwa na maji.

Amesema mtu wa nne kufariki dunia ametambulika kwa jina la Ally Hamis (25) mkazi wa kijiji cha Chilongola ambaye alikuwa anapita na pikipiki kwenye korongo akavutwa na maji na kufariki dunia.

Amesema mvua zilizonyesha kwa sasa ni kubwa hivyo tahadhari zinapaswa kuchukuliwa ili kuepukana na madhara ikiwemo watu kufa kwa kusombwa na mafuriko wakati wakipita barabarani.

Amesema miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye hospitali ya wilaya hiyo kwa uchunguzi zaidi kabla ya kufanyika maziko.