Na HUGHOLIN KIMARO

Masshele blog

Kwa Mukhtasari

Mhariri wa Kiswahili wa matbaa ya Longhorn Kenya, Bw James Mwilaria, amesema uchapishaji wa vitabu katika awamu hii ya utandawazi umekumbwa na changamoto tele ingawa upo uzuri wake pia.




MHARIRI wa Kiswahili wa matbaa ya Longhorn Kenya, Bw James Mwilaria, Alhamisi aliwaelezea wataalamu, wasomi na wapenzi wa Kiswahili kwamba uchapishaji wa vitabu katika awamu hii ya utandawazi umekumbwa na changamoto tele ingawa upo uzuri wake pia.

Kulingana na Bw Mwilaria, ingawa uchapishaji wakati huu wa utandawazi ni rahisi, unakabiliwa na changamoto si haba. “Waandishi na wachapishaji wamekuwa wakichangamkia sana uchapishaji wa kidijitaji bila kujua kuwa unazo changamoto zake.  Wenyewe ni rahisi kwani hata baadhi ya waandishi wamekuwa wakijiandikia na kujichapishia miswada.

Lakini mambo si shwari kama inavyofikiriwa. Kuna tatizo la kudhibiti hakimiliki za wachapishaji. Unapochapisha  vitabu katika enzi hizi inakuwa vigumu kuidhibiti hati ya umiliki wa kazi zako. Ni kazi ambayo inaweza kufikiwa na kila mtu; inaweza kusomwa ama hata kuchapishwa na watu wengine wanaoweza kuifikia mtandaoni.



Mrabaha

Aidha, kunakuwa na ugumu katika ulipaji wa mrabaha. Aghalabu, waandishi hupunjwa katika ulipaji huo kwani inakuwa vigumu kujua idadi kamili ya nakala zilizochapishwa mtandaoni.

Licha ya hayo, kunao baadhi ya wale ambao wangetaka kuifikia kazi iliyo katika mtandao ambao kutokana na kutoijua teknolojia ya kisasa wanakuwa wamekwazwa.

Changamoto nyingine ni kwamba viwango vya lugha vyaweza kuvurugwa pia. Watu wanapoamua kuandika, kujitathminia kazi zao na kisha kuzichapisha wanakabiliwa na hatari ya kuchapisha kazi duni kutokana na kuamini kuwa kila kitu walichoandika ni sahihi. Wanahitaji kuwa na mtaalamu wa kuwarekebisha hapa na pale ili kazi zao zinyooke.”

Hata hivyo, kwa mujibu wa Bw Mwilaria, utandawazi umekuza lugha kwa kiwango kikubwa. Mitandao ya Masshele blog, Swahili hub na Chomboz kwa mfano ina Makala tele ya lugha ya kuvutia ambayo hurejelewa kila mara na watu watakao kujikuza katika lugha.