Kocha wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania Dokta Mshindo Msolwa, ameitabiria Timu ya Azam kuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu huu.
Akizungumza na kipindi cha michezo cha EFM, Msola amesema hayo ni kutokana na klabu hiyo kuwaandalia mazingira mazuri wachezaji wake ndani na nje ya uwanja.
-Azam wana huduma zote facilities, mishahara, mazingira kila kitu kizuri", amesema Msolwa.
Kuhusu uwezo wa Azam kutwaa ubingwa wa ligi ya Vodacom, Msolwa amesema amebaini kuwa Timu hiyo ina msingi thabiti baada ya kuamua kuwekeza kwenye soka la vijana pamoja na kuwapa nafasi.
Msingi dhabiti
-Nilijua Azam watafanya vizuri walipofanya mabadiliko ya kutumia vijana na kuacha mazoea ya kusajili majina makubwa tena vijana wasiokuwa na majina", amesema Msolwa.
Kadhalika Msolwa amesema kuwa hatua hiyo imeiwezesha timu hiyo kufanya vizuri kwa kuwa vijana hao wana umoja wanapocheza tofauti na wachezaji walio na majina makubwa ambao hucheza kwa maslahi yao na si ya Timu.
Pamoja na hayo ameisifia safu ya ulinzi na ushambulizi ya timu hiyo na kusema umoja wa safu hizo husaidia timu kupata matokeo mazuri.
-Timu yoyote inahitaji defence nzuri, kwani husaidia safu ya mashambulizi", ameongeza Msolwa  ambaye amekuwa mdau mkubwa wa soka la vijana nchini.
Azam Fc wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo wakiwa na alama 26 sawa na vinara wa ligi Simba SC wanaoongoza kwa wingi wa mabao.