Na: Jumaa H heshima

Kifungo kwa maana ya kawaida kabisa ni hali ya kuzuia mtu au kiumbe katika mazingira fulani na kukiwekea mipaka kufika baadhi ya maeneo au kufanya baadhi ya mambo.

Neno huru linaashiria hali ya kuamua kufanya jambo mtu alitakalo bila vizuizi. Dhana ya uhuru ni tata kidogo, katika jamii yoyote ile uhuru huwa na mipaka. Mfano kila mtu anao uhuru wa kuvaa nguo aitakayo kwa namna apendavyo ila tu nguo hiyo isioneshe tupu zake. Pia kuna uhuru wa kuongea unalolitaka ila sio kumtukana mtu au kumdhalilisha na kumvua utu wake. Utata uko hapa kwenye kuamua unalolitaka na kisha kuwepo kwa mipaka.

Ajira kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21 ni kazi ya kulipwa mshara. Maana hii inatuacha na swali juu ya ajira binafsi (self emloyment). Je, muajiriwa analipwa mshahara na nani? Tunaweza kujiridhisha kuwa katika hali hiyo mfanyakazi huyo analipwa mshahara na kazi hiyo anayoifanya na isipomlipa anavyotaka basi ataiacha kama ilivyo kawaida kwa waajiriwa wengine.

Je, kifungo huru cha ajira ni nini? Na kwanini kiwe kifungo  na uhuru uhusike wakati huohuo? Na kifungo hicho kinazuia mambo gani? Kutokana na maana hizo za awali tunaweza kuelezea kifungo huru cha ajira kama hali ya kuwepo vizuizi kwa muajiriwa kufanya ama kufanikisha baadhi ya mambo mathalani ya muhimu kwake na wanaomzunguka.

Kwa hakika mada hii inahitaji kitabu cha kurasa 100 kuichambua kwa kina, hapa tutaifupisha kadri iwezekanavyo.

Jambo la kwanza la kuzingatia hapa ni kuzitambua aina za ajira na ajira zipi tunazozisema zina kile tunachokiita kifungo huru.

Zipo aina nyingi za ajira kama ajira za muda mfupi, ajira za muda mrefu, ajira binafsi n.k Hapa tutaangalia sana aina ya ajira ambayo mwajiriwa hupewa "uhakika wa maisha'' ndani ya kipindi fulani cha uhai wake.

"Uhakika wa maisha" unaolengwa hapa ni ile hali ya kujihakikishia kupata mahitaji muhimu ya kila siku kama vile kula, kuvaa na kulala. Bila kusahau uhakika wa kupata tiba katika maradhi, kupata mkopo, kupata posho, gawio la kuchukua likizo pia pensheni baada ya kustaafu kazi husika.

Aina hii ya ajira huwa na kiwango fulani cha masaa ambacho mfanya kazi atatakiwa kufanya kazi hiyo kila siku katika kipindi chote atakachopaswa kuwa kazini hadi kustaafu kwake.

Bila kutumia mfululizo wa maneno yatakayochanganya sana na si kuelewesha, aina hii ya ajira ndiyo hasa yenye "kifungo huru cha ajira" labda mtu anaweza kushangaa kwanini niseme hivi? Hali ya kuwa kuna muda ambao muajiriwa huwa nao kufanya mambo mengine.

Trump D. na Kiyosaki R. katika kitabu chao walichokiita kwa Kingereza "Why We Need You to Be Rich" kwa tasiri rahisi "Kwanini Tunataka uwe Tajiri" wanafananisha kuajiriwa kwa aina hii na "ufungwa wa gerezani".

Mfungwa akiwa gerezani huwa na "uhakika wa maisha" atakula, atalala, ataenda haja halikadhalika akiumwa atauguzwa.
Mfungwa huyu kama alihukumiwa kukaa jela miaka 30, baada ya kumaliza kifungo chake atatoka jela kama alivyoingia atatoka na suruali yake na shati lake tu. Alipewa "uhakika wa maisha" kwa kipindi fulani na kuupata kweli ila umefikia kikomo, anauacha na kurudi mtaani ambako hana `be' tuache `a'.

Muajiriwa nae baada ya kuishi katika uhakika huu kwa kipindi chote cha ajira (kifungo huru) unafikia wakati anastaafu. Anatoka jela. Tofauti iliyopo kwake na mfungwa aliyetoka gerezani ni kuwa yeye atapata pensheni na labda pesa ndogondogo za kutumia kila baada ya mwezi au miezi.

Jambo baya zaidi nikuwa,  kazi hizi huwabana waajiriwa wake kimaslahi na ki wakati (muda) nakuwapa kitu kidogo wakati mwingine hakitoshi hata kuendesha maisha yao ya kila siku.

Mara nyingi mwajiriwa wa aina hii hawezi mathalani kujenga hata nyumba ya kumsitiri yeye na familia yake. Baadae anapomaliza muda wake wa ajira na kupata mafao yake ya kustaafu ndipo hujenga nyumba ya kuishi.

Yaani pesa ambayo anatakiwa aitumie kuweka miradi itakayomfaa yeye na familia yake ndio inambidi aitumie kujenga nyumba, hili ni tatizo. Ila tuseme basi yafaa kujenga, lakini mtu anastaafu ndio anajenga nyumba? Kweli jamani...! Miaka 50 au 60? Amefanya kazi kwa miaka 30 wengine 40...! Sasa hapo hiyo raha ya nyumba yake ataionea wapi? Miaka 60 kwa dini ya Kiislam ndio miaka ambayo Izraili anakuwa karibu sana na wewe. Basi sawa wataishi watoto na wajukuu.

Hali huwa mbaya zaidi kwani wakati mwingine watu hawa huwa choka mbaya kiasi cha kushindwa kumudu hata maisha yao na ya familia zao miaka michache tu baada ya kustaafu.

Tofauti ya huyu na yule mfungwa aliyekaa jela miaka thelathini na kutoka hana kitu ni ndogo sana labda tuseme huyu mstaafu ndio ana balaa zaidi maana ana mizigo tele ya familia.

Hakika ni kifungo huru. Kwa kiasi kikubwa aina hii ya ajira humpa uhuru mdogo muajiriwa kufanya mambo mengine huku ikimlipa mshahara usiotosha kufanya mengi ambayo angepaswa kuyafanya kwa manufaa makubwa ya watu walio nyuma yake.

Ili kuelewa zaidi hapa unaweza kurejea muajiriwa, ndugu yako ama jamaa yako wa karibu ambaye unahisi kwa ajira yake moja kwa moja ataingia katika kundi hili. Tazama alianza kufanya kazi kipindi gani? Anatumia muda gani kazini? Je, "hali yake ilivyo" ni sawa na nguvu azitoazo kuitumikia ajira yake? Sisemi muwaangalie wastaafu maana ndio wanaumiza zaidi.

Kigugumizi juu ya lile kundi la wachache wanaolipwa fedha nzuri kwa namna hii au ile mguu wao mmoja umo ndani ya gereza hili. Wanapata mshahara mzuri unaowaruhusu kujitosheleza haswa lakini wanavyotumika kazini wenyewe ndio wanajua. Wanakosa uhuru wa muda wa kuzitilia mbolea pesa zao kwenye mambo mengine. Hivyo kuzichezea kamari kwa kuwadhamini watu wasimamie mambo yao. Hapa uwezekano wa kufusa na kufuswa ni "fifty fifty". Wenyewe hawana muda.

Wapo ambao wananufaika kwa mshahara mzuri na uhuru mkubwa lakini kundi hili ni dogo sana, sana, sana.

Moja ya swali nilitarajialo hapa ni Je, kila mmoja akiacha kazi hizo nani atafanya na huduma zitatolewa na nani?

Mwanaharakati mmoja maarufu kwa jina la Marx aliajiriwa na kampuni fulani nchini kwao baada ya muda mfupi tu akaacha kazi. Akapata kazi sehemu nyingine akaacha tena na mara nyingine vivyohivyo. Alipoulizwa ni kwanini anaacha kazi alijibu kuwa, Kazi alizokuwa akizifanya katika kampuni hizo hazikulingana na kile alichokuwa analipwa hivyo aliona kuwa ananyonywa. Kwake ni bora kukaa bila ajira kama ajira zilizopo ni za kinyonyaji.

Ni vema kwa watu kufanya kazi lakini malipo yalingane na kile wanachokitoa. Mfanyakazi unayembana wakati wote na kumuachia muda mchache wakurudi kwake acheze na wanae sebuleni kisha alale mapema kesho adamkie kazini kwako, yakupasa kumlipa malipo yatakayomuwezesha kujimudu kweli na sio tu kula na kulipa kodi ya nyumba.

Uhalisia wa maisha ya sasa haimtoshi mtu kumudu maisha yake na familia yake kwa kutegemea mshahara kichele toka kwa muajiri wake. Watu wanavumilia tu kama mshumaa.

Moja kati ya mambo haya mawili likifanyika litakua mkombozi kwa watu hawa.

Kwanza waongezewe mishahara ili kulimudu lundo la majukumu waliyo nayo na kujiandalia mapumziko ya kweli wakitoka kwenye kifungo hiki cha ajira, wasidhalilike.

Au wawekewe mazingira rafiki yatakayowaruhusu na kuwapa uhuru na nafasi ya kufanya miradi mingine wakiwa kazini ili wajazie kile kinachopelea kazini.

Buffett W. anatwambia kuwa "kama huwezi kuingiza pesa ukiwa umelala basi utafanya kazi kwa maisha yako yote"

Rafiki yangu mmoja wakati tunajadili maswala ya ajira binafsi alinambia kuwa "ni heri utumie miaka mi 5 au 10 kusimamisha biashara yako kuliko kuajiriwa kwa miaka 30"

Nilimuona ananipigia kelele tu kwa kuwa mtaji ni taji la ufalme ambalo halikufundishwa kutamka neno Masikini.

                       *MWISHO*

Mwandishi:   Jumaa H Heshima
                       Chuo Kikuu cha Dar es          Salaam
                       0714-638277.
                        07-01-2017
Gmail Jumaahassan.jh@gmail.com