Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema wizara yake imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila mwanafunzi anayenufaika na mkopo wa elimu ya juu, anarejesha mkopo wake.

Dk Ndalichako alitoa kauli hiyo juzi wakati akifanya mahojiano katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na TBC 1. Alisema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB) ilianza kutoa mikopo kwa wanafunzi mwaka wa fedha 1994/1995. Wakati Rais John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015, fedha zilizokuwa zimerejeshwa ni Sh bilioni 75.9, lakini baada ya mwaka mmoja tangu awepo madarakani wamekusanyaSh bilioni 211.

Ndalichako aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017, bodi ilikusanya Sh bilioni 116, hivyo ukilinganisha na fedha zilizokusanywa katika mwaka mmoja wa fedha ni zaidi ya fedha zilizokuwa zimekusanywa katika miaka 10 tangu kuanzishwa kwa bodi ya mikopo. Aidha, alisema kabla ya serikali ya Rais Magufuli kuingia madarakani, HESLB walikuwa wanakusanya kiasi cha Sh bilioni mbili kwa mwezi, lakini kwa sasa wanakusanya kiasi cha Sh bilioni 13 kwa mwezi.

“Mwito wangu kwa wanufaika wa mikopo hii waendelee kujitokeza kulipa ili fedha ziweze kuwasaidia na wengine, kwa mwezi Novemba tu bodi imevunja rekodi, imekusanya bilioni 16, haya ni mafanikio makubwa, katika mwaka huu wa fedha tuliweka lengo la kukusanya bilioni 140 mpaka mwisho wa mwaka, na kwa miezi mitano tu tumeshakusanya Sh bilioni 72,”alisema Ndalichako.

Alisema siri ya mafanikio makubwa ya ukusanyaji huo ni pamoja na kufanya mabadiliko makubwa katika bodi ya mikopo kuanzia watendaji, mifumo ya watendaji na kuboresha kanzidata ya ufuatiliaji.

Alisema kwa mfumo wa zamani, bodi ilikuwa imejisahau na walikuwa haioni kama ina jukumu la kufuatilia mikopo. Akizungumzia sera ya elimu bure, Ndalichako alisema kwa sasa baada ya Rais kutangaza kuwa elimu ni bure, mzazi anapaswa kutoa nauli na madaftari na endapo ana mtoto katika shule za bweni, atapaswa kutoa fedha ya chakula.

“Sera ya elimu bure haijakataza uchangiaji wa maendeleo, sera imeondoa ada na michango isiyo ya lazima kwa wanafunzi, zamani shule ilikuwa kama uwanja wa mpira, bila kiingilio hukanyagi pale; na kama Januari walikuwa wanazikusanya kweli kweli, unaambiwa uje na mchango wa dawati, mara mchango wa karatasi za mitihani, michango ilikuwa mingi, ambayo serikali imeitoa mwanafunzi anaenda shule bila kikwazo,” alisema.