Mabingwa watetezi wa taji la ligi kuu soka Tanzania Bara, Dar Young Africans watawakosa wachezaji wao muhimu katika mchezo wa ligi dhidi ya Mbao FC ‘Wabishi’, utakaofanyika Jumapili ya Disemba 31 kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza.
Wachezaji hao ni majeruhi Donald Ngoma, Thaban Kamusoko na Kelvin Patrick Yondani pamoja na Ibrahim Ajib Migomba ambaye yeye ataukosa mchezo huo kutokana na kuwa na kadi tatu za njano wakati Obrey Chirwa yeye akiwa bado hajarudi kutoka Zambia alipokwenda kwa ruhusa ya klabu.
Dismas Tena ambaye ni mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano cha klabu hiyo kongwe nchini, amesema kwa kuwa wanawachezaji wengi tayari mwalimu ameshatafuta wachezaji ambao wataziba pengo hilo.
-Tayari benchi la ufundi limeshaandaa kikosi kingine ambacho kitaziba mapengo hayo, timu yetu inawachezaji 29 ambao wamesajiliwa , kwa hiyo unaweza kuona kila mchezaji ana umuhimu ni benchi la ufundi tu kuamua nani na nani wa kuwatumia,” alisema Dismas.
Mbao ni timu ngumu.
Akiwazungumzia Mbao FC, Dismas amesema mbao ni timu ngumu na wao tayari wanalitambua hilo na ndio maana wamejipanga kuhakikisha wanafuta uteja kwa kuwafunga na kuendeleza juhudi zao za kutetea taji.
-Kucheza ugenini ni jambo gumu kidogo, lakini kucheza na Mbao FC kwenye uwanja wa CCM kirumba ni jambo gumu zaidi, kwa maana kwamba ni timu ambayo inakuwa inapata matokeo wakiwa nyumbani, sisi tumejiandaa vizuri tukijua mchezo huu utakuwepo, lengo letu ni kutetea taji hivyo tunaenda Mwanza tukiwa tunataka matokeo,” Dismas aliongeza.
Kuhusu maandalizi ya safari kwa ajili ya kuelekea Mwanza, Dismas amesema muda wowote kuanzia hivi sasa kikosi hicho kitaanza safari na kwamba maandalizi yote ya safari hiyo yamekamilika.
Hawajawahi kushinda.
Yanga wanaenda kucheza na Mbao FC wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza michezo miwili katika uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya timu hiyo yenye maskani yake katika soko la Mbao lililopo Ilemela Jijini Mwanza.
Mchezo wa kwanza Yanga walipoteza kwa bao 1-0 ukiwa ni mchezo wa nusu fainali ya kombe la Shirikisho Tanzania Bara, huku mchezo mwingine wa kukamilisha msimu wa 2016/17 wa ligi kuu Yanga pia wakapoteza kwa bao 1-0.