Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Mwigulu Nchemba amewataka wananchi wa Tanzania kujiandikisha kupata kitambulisho cha Taifa kwani si zoezi la hiari na kwamba ni lazima kwa mtanzania aliyeko ndani ya mipaka ya nchi ili kutambuliwa.

Amesema hayo akizindua zoezi la kujiandikisha kupata kitambulisho  cha Taifa na kugawa vitambulisho katika Mkoa wa Ruvuma na kukagua zoezi hilo linaendaje kwa mikoa ya Nyanda za Kusini hasa iliyoko mipakani mwa nchi.

Waziri Nchemba amewataka wananchi waache mazoea ya kutafuta kutambuliwa mpaka wanapokuwa na shida hasa za kutaka hati ya kusafiria au migogoro ya ardhi pale anapoambiwa yeye si raia wa Tanzania.

Mh. Nchemba amewagiza viongozi wa wilaya na vijiji kutokuunganisha zoezi la kuandikisha wananchi kupata vitambulisho vya uraia na zoezi lingine lolote akitolea mfano baadhi ya viongozi kuchangisha fedha za kijiji kwa kuwaambia kuwa hutopata kitambulisho mpaka utakapo lipa fedha unazo daiwa na kijiji.

"Hili zoezi la vitambulisho vya utaifa ni lalazima kwa kila mtanzania aliye nchini, ni kosa kubwa kama wewe ni raia ukaamua kukaidi ikiwa Rais wetu Magufuli ameamua kutoa vitambulisho hivyo bure bila malipo yoyote.

“Hili ni jambo la Nchi na ni kubwa hivyo tusililinganishe na jambo lingine lolote, baada ya mchakato huu kuisha tukamkuta mtu hana kitambulisho maelezo yake yatakuwa ni magumu kueleweka kama kweli yeye ni mtanzania halali”
 –Dr Nchemba