PENGO LA NIYONZIMA YANGA LAZIBWA
NA EZEKIEL TENDWA
KIUNGO Zimiseleni Moyo anayefukuziwa na Yanga, amemchana Haruna Niyonzima akisema Mnyarwanda huyo asidhani kama ameacha pengo Jangwani kwani anao uwezo wa kufanya mambo makubwa na mashabiki wa timu hiyo kumsahau kabisa fundi wao huyo anayeelezwa kutua Msimbazi.
Mido huyo wa Zanaco ya Zambia, yupo mbioni kutua kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwamba mambo yakienda vizuri akamalizana na uongozi, msimu ujao atakuwa katika uzi wa rangi ya kijani na njano.
Yanga wapo kwenye mawindo makubwa kwa kiungo huyo ili kuziba pengo la Niyonzima, ambaye amesaini Simba baada ya kushindwana na Wanajangwani hao baada ya kudaiwa kutaka fungu kubwa.
Masshele blog ilizungumza na kiungo huyo ambapo alisema mpaka timu hiyo inaamua kumfukuzia, inamaanisha kwamba wameona anao uwezo mkubwa, hivyo kama watafanikiwa kumalizana, wenyewe watafurahi namna atakavyowaburuza wapinzani wake.
“Mimi ni mchezaji na popote naweza kucheza, sasa kama ikitokea Yanga wakanisajili nadhani watafurahi wenyewe na nikuhakikishie tu kwamba ninao uwezo ndiyo maana unasikia baadhi ya timu zikinihitaji, mimi kazi yangu ni mpira, wasisikitike kuondokewa na Niyonzima.
“Yanga ni timu kubwa na kongwe barani Afrika, hakuna asiyeijua, wachezaji wengi wamekuwa wakiiongelea na mimi ni mmoja wa watu ninaotamani siku moja kuvaa jezi zao na kufanya nao kazi kama wakinihitaji,” alisema.
Kigogo mmoja wa Yanga amesema kwamba, kwa sasa wanafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha wanamsainisha kiungo huyo mwenye uwezo wa kucheza namba zaidi ya moja, ili kuimarisha kikosi chao msimu ujao.
“Hiki ni kipindi cha usajili na sisi kama mabingwa wa ligi kuu lazima tuangalie kwa jicho la tatu kuona nani na nani watatufaa, ni kweli huyo kiungo ametuvutia sana tangu siku ambayo tulicheza na Zanaco, ndiyo maana tunaangalia uwezekano wa kumchukua,” alisema.
Kuonyesha kwamba wamedhamiria kuimarisha safu yao hiyo ya kiungo, Wanajangwani hao wanatajwa pia kuingia kwa miguu miwili wakiitaka saini ya kiungo mwingine kutoka Zesco, Cletus Chama, ambapo mmoja kati yao lazima aingie kwenye mtego.
Comments
Post a Comment