HIKI NI KIKOSI CHA KARNE SIMBA SC
GLORY MLAY NA SELEMANI MAJEMA (DSJ)
KIKOSI cha Simba cha msimu ujao kinaweza kuwa cha karne iwapo Wekundu wa Msimbazi hao watafanikiwa kumalizana na nyota kadhaa wanaodaiwa kusainishwa mikataba na timu hiyo.
Miongoni mwa nyota hao, yupo kipa mahiri aliyekuwa Azam, Aishi Manula, beki wa kulia, Shomari Kapombe (Azam), kiungo mshambuliaji, Haruna Niyonzima (Yanga), washambuliaji Emmanuel Okwi (SC Villa ya Uganda), John Bocco (Azam) na Donald Ngoma (Yanga).
Hakuna asiyefahamu ubora wa nyota hao kutokana na viwango walivyovionyesha misimu kadhaa iliyopita wakiwa na timu zao ambao wakiungana na wale waliopo kikosini Msimbazi, ni wazi timu hiyo itakuwa ni moto wa kuotea mbali.
Nyota wa Simba wanaoweza kuungana na wageni na kukifanya kikosi chao kuwa hatari msimu ujao, ni beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, mabeki wa kati, Abdi Banda na Jjuuko Murshid, viungo wakabaji, Jonas Mkude na James Kotei, winga Shiza Kichuya na mshambuliaji wa kati, Laudit Mavugo.
Wenyeji na wageni hao watakifanya kikosi cha kwanza kuundwa na; Manula, Kapombe, Tshabalala, Banda, Jjuuko, Mkude, Ngoma, Kotei, Bocco, Niyonzima na Okwi.
Kwa kikosi hicho, mfumo utakaokuwa mwafaka ni wa 4:3:3: ambapo Bocco, Ngoma na Okwi watasimama mbele, huku nyuma yao kukiwa na Niyonzima, Kotei na Mkude, wakati safu ya ulinzi itaundwa na Kapombe, Tshabalala, Banda na Jjuuko.
Upande wa benchi, kutakuwa na kipa Daniel Agyei, Javier Bokungu, Jamal Mwambeleko, Yusuph Mlipili, Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo, Said Ndemla, Shiza Kichuya, Mohammed Ibrahim ‘MO’ na Ally Shomari.
Wachezaji hao ni wa kiwango cha juu kiasi kwamba yeyote atakayeingia kuchukua nafasi ya wale wa kikosi cha kwanza, anaweza kufanya mambo makubwa na kuibeba mno timu.
Wapinzani wa Simba watake wasitake, kikosi cha Msimbazi msimu ujao kitakuwa ni balaa na huenda kikavifunika vyote vilivyopita kwa miaka ya hivi karibuni, lakini tu iwapo Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, atatuliza akili yake na kuwatumia ipasavyo wachezaji hao.
Pamoja na mambo mengine, kwa kuwa wachezaji hao wote ni masupastaa, watalazimika kujengwa kisaikolojia ili kila mmoja kuweka mbele masilahi ya timu badala ya jina lake au ukubwa wa dau alilosajiliwa Msimbazi.
Tayari Okwi ameweka wazi azma yake ya kucheza kwa uwezo wake wote ili kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao pamoja na kufanya vema kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, alikaririwa akisema: “Tunasajili wachezaji wa kiwango cha juu ambao tunaamini watatuwezesha kurejesha makali yetu ya miaka ya nyuma na kuifanya Simba kuwa tishio kuanzia kwenye mashindano ya ndani hadi ya kimataifa.”
Msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unatarajiwa kuanza Agosti mwaka huu ambapo mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa ligi hiyo, yaani Ngao ya Jamii, utaikutanisha Simba na watani wao wa jadi, Yanga mapema mwezi huo.
Share mtu wangu
Comments
Post a Comment