UHAKIKI WA ROSA MISTIKA
UHAKIKI WA RIWAYA YA ROSA MISTIKA

 UHAKIKI WA RIWAYA YA ROSA MISTIKA


Riwaya ya Rosa Mistika iliyoandikwa na E. Kezilahabi mwaka 1971, ni moja kati ya riwaya zinazotumika katika utafiti huu kama data ya msingi. Kwa kiasi kikubwa, masimulizi ya riwaya hii yamejikita katika kueleza maisha ya mhusika, Rosa, tangu akiwa mtoto mpaka kifo chake na maisha baada ya kifo. Masimulizi yamehusisha maisha ya wahusika wengine ambao kimsingi ndio ambao wamemjenga mhusika mkuu Rosa. Hivyo, katika utafiti huu, wahusika, Regina ambaye ni mama yake Rosa, Zakaria baba yake Rosa, Flora mdogo wake Rosa, Charles mpenzi wa Rosa na Padre anayetaka kuokoa nafsi ya Rosa, wamechambuliwa.

Kwanza tunaona wasifu wa Rosa akiwa mtoto mdogo. Mwandishi anamchora Rosa kama kifungua mimba cha familia ya Zakaria na Regina kati ya wasichana watano na mvulana mmoja. Rosa akiwa mtoto mdogo anaonekana ni msichana mrembo na mwenye aibu, mrefu kiasi, mnyenyekevu na mkakamavu.  
Rosa anakua chini ya malezi ya baba yake aliye na mtazamo hasi juu ya wanawake. Zakaria akiwa kama mwalimu aliyeachishwa kazi kwa sababu ya ulevi, anamtesa mke wake kwa kumpiga na kutomjali pamoja na familia yake kwa sababu ya kuzaa watoto wa kike wengi. Kama riwaya isemavyo (uk.3):
…..Regina tangu aolewe hakuwa na raha: alikuwa akisumbuliwa na kuteswa na mumewe kwa kosa lisilo lake. Katika kijiji chote cha Namagondo hapakuwa na mwanamke aliyekua akipigwa karibia kila juma kama Regina.

Zakaria alizoea kumlaumu Regina kwa kuzaa watoto wa kike na kudai amemletea matatizo katika nyumba yake. Ingawa Regina alipigwa na mumewe kwa lakini hakutaka kuachana na mumewe sababu ya mategemeo yake juu ya maisha ya baadae ya watoto wake. Ndiyo maana katika ukurasa wa 3 twaambiwa kuwa mawazo yake yalikua juu ya furaha ya watoto wake katika maisha yao ya baadae.
Kutokana na kuwa na watoto wa kike wengi katika nyumba yake, Zakaria anatumia ukali kama silaha ya kuwalinda dhidi ya wanaume. Ingawa Zakaria anawapenda watoto wake lakini mfumo wa kijamii unamkandamiza. Hajui lipi ni jema kwake kutenda kama mwanaume katika familia iliyojaa wanawake. Mawazo na imani ya wanajamii ni kwamba ili familia iheshimike ni lazima kuwepo na mtoto wa kiume. Kukiwa na mtoto wa kiume hata ndege na wanyama wanaiheshimu na kuiogopa. Lakini nyumba iliyojaa wanawake haiheshimiki. Hili tunaliona katika (uk 15-16):
…….Vilikuwa kumi, sasa vimebaki vitatu!” Flora alishangaa. Rosa alikaa chini tena kunyolewa. Muda si mrefu mwewe alirudi. Safari hii Honorata alikuwa wa kwanza kumwona.
“Swa! Swa! Swa!” alitupa mikono juu, “swa!”Mwewe alikuwa amekwisha chukua kifaranga kingine. Zamu hii hakwenda mbali. Alitua juu ya mti karibu na mji. Wasichana walianza kumtupia mawe lakini hayakumfikia. Mwewe alikula kifaranga bila ya kujali.Alipomaliza aliruka kwa raha ya shibe. Vifaranga vilibaki viwili. Ilionekana kana kwamba hata mwewe alifahamu kwamba huu ulikua mji wa wanawake.
Mtazamo kama huu ndio unaomkandamiza Zakaria, anashindwa kutafuta njia iliyo sahihi katika kuwalea binti zake. Hajui jinsi ya kukabiliana na Rosa aliye katika hatua muhimu katika makuzi yake. Tunaona Zakaria hana muda wa kuzungumza na binti zake juu ya hisia zao. Pia hawaelezi ni nini wanakabiliana nacho katika hatua hiyo ya makuzi. Wala hawajulishi nini wafanye ili kuyazima matamanio yao.Tunaona jinsi anavyompiga Rosa akiwa nusu-uchi sababu ametumiwa barua na pesa toka kwa mwanaume. Mwanaume mwenyewe aliyetuma barua hiyo ni Charles, kijana aliyekuwa rafiki yake Rosa kwa muda mrefu na wazazi wote walijua juu ya urafiki huo. Urafiki wao ulikuwa umeunganishwa zaidi na masomo. Rosa na Charles wanakatazwa kuwasiliana tena baada ya Zakaria kujua juu ya barua aliyopokea Rosa. Tunaona baada ya kitendo hicho Zakaria anajisifia na kujitakia amani, “amani Duniani kwa watu wenye malezi mema”.
Tunaona mtazamo wa mwandishi kuhusu malezi ya namna hii, malezi ya baba kwa binti yake, hususani katika kipindi cha makuzi ya hatua ya kingono (uk.9):
Hivyo ndivyo Rosa alivyolelewa, hivi ndivyo alivyotunzwa, hivi ndivyo alivyochungwa na baba yake. Tangu siku hiyo alikoma kutembea na mvulana yeyote. ….. hakufahamu kwamba Rosa alikuwa katika rika baya, na kwamba ukali ulikuwa haufai; hakufahamu kwamba mabinti wanahitaji uhuru fulani kutoka kwa baba zao; hakufahamu kwamba kumpiga binti yake alikuwa anaingilia utawala usio wake, na kwamba katika masuala ya ndoa yeye alifaa kidogo sana, na hakufahamu kwamba Rosa alihitaji kuwafahamu wanaume. Kwa hiyo kutokana na malezi ya namna hii, Rosa alianza kuwatazama wanaume kama watu asiopaswa kuandamana nao na hata kuzungumza nao. Alianza kufikiri kwamba alitakiwa kujitosheleza. 
Kwa upande wa mama yake Rosa, yeye alitumia muda wake mwingi wa kuwafundisha binti zake namna ya kuenenda vizuri kama wanawake. Alitumia muda wa usiku wakiwa wanakula chakula cha usiku kuwaonya na kuwafundisha jinsi ya kuishi na mambo gani ya kuepukana nayo na mambo ya kuyaacha. Alifanya hivyo kwa kila mtoto kulingana na umri wake.
Rosa alikuwa amevunja ungo na amefaulu kwenda kusoma mbali na nyumbani. Jambo kubwa alilousiwa na mama yake ni kutowasahau wazazi wake na kukaa mbali na wanaume.
Mwanangu, wewe sasa umeshakua mtu mzima. Karibu utakwenda huko ng’ambo Usukumani. Usitusahau sisi wazee wako - tuandikie barua mara kwa mara. Jambo moja ningependa hasa kukuhadharisha: wavulana wakorofi. Huenda wakakutaka kimapenzi, nia yao ikiwa tu kukupa mimba itakayokukatisha masomo yako. Daima wakwepe hao. Na ikiwa utakuwa mpumbavu ukapata mimba usiitoe. Tunasikia kwamba siku hizi wasichana wengi wanaosoma wanafanya hivyo ili wapate kuendelea na masomo yao. Wanapenda masomo zaidi kuliko watoto.
Mawazo ya Regina sio mabaya. Jambo kubwa analopigania ni kutafuta maisha bora kwa ajili ya binti zake wakiwa watu wazima, na kujaribu kuwapatia ukombozi ambao yeye hakuupata. Lakini Regina anashindwa katika kumalizia maonyo, anamuonyesha Rosa ubaya wa wanaume tu hamuambii inakuaje mpaka ndoa inatokea. Hatujui kwa nini haongelei juu ya furaha inayoweza kupatikana kati ya mwanamke na mwanaume isiyoleta maumivu kwa upande wowote na bila kuwaumiza watu wengine. Inawezekana Regina haoni kama kuna umuhimu wa uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke kwa sababu ya mateso anayoyapata toka kwa mume wake Zakaria. Kutokuwa wazi kwa Regina juu ya maisha ya mapenzi kwa binti zake kunasababisha wabaki katika kitendawili, hawajui uhakika wa mambo hayo ni upi, wakizingatia jinsi wanavyojisikia na jinsi ambavyo watu wanaowazunguka wanafanya.
Regina na mumewe Zakaria, kama wazazi wengine, wana wasiwasi na maisha ya baadae ya watoto wao hususani baada ya kufikia kipindi cha kubalehe. Hawajui jinsi ya kukabiliana na hali inayowakumba binti zao. Tofauti na jamii zingine za Watanzania wanaopeleka watoto katika umri huu jandoni au unyagoni, Kama Senkoro (1997:100) anavyosema:
Mpito toka utotoni mpaka utu uzima ni kikwazo au wakati mwingine tatizo kwa wazazi walio wengi katika jamii yetu. Muunganiko sawia wa kibaiolojia au mabadiliko ya kihomoni za kisaikolojia na majukumu ya kijamii katika balehe inatengeneza tabia tofauti tofauti ambazo sio lazima zilingane na nini wazazi au watu wazima katika jamii kwa ujumla wangetaka. Aina hii ya tatizo linashughulikiwa na jamii nyingi za Kiafrika kwa njia ya kufundwa katika jando na unyago.
Kulingana na jinsi mwandishi alivyoichora jamii ya Wakerewe, watoto wanapokua hawapewi mafunzo yoyote yanayohusu mambo watakayokabiliana nayo watakapokuwa watu wazima. Inawezekana kutokuwepo kwa mafunzo haya ndiko kunakoleta matatizo, kwani Regina anashindwa kuwafundisha binti zake kwa mapana zaidi hususani kuhusu mambo yanayohusu mahusiano; mafunzo ambayo wangeyapata kama kungekuwapo na jando na unyago. Kwa kawaida katika jamii nyingi za Kiafrika, mambo haya hayafundishwi na wazazi; badala yake mashangazi, makungwi au somo ndio wanaohusika kuwafundisha mabinti kuhusu masuala ya mahusiano wanapovunja ungo.