HII NDIO SIMBA MPYA
NA ZAITUNI KIBWANA,
SIKU chache baada ya Simba kubeba Kombe la FA na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, timu hiyo imepanga kuboresha kikosi chao kwenye maeneo kadhaa.
Tayari Wekundu wa Msimbazi hao wana uhakika wa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku tiketi ya Ligi ya Mabingwa ikienda kwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga.
Kutokana na hilo, Simba wamepanga kuingia sokoni kununua wachezaji ambao wataweza kuwa na timu imara itakayoweza kuhimili mikikimikiki ya michuano ya kimataifa.
Tayari nafasi kadhaa zimeanza kutajwa kufanyiwa marekebisho, ikiwamo eneo la ulinzi, kiungo mwenye nguvu na safu ya ushambuliaji.
Nyota wanaotajwa kuingia kwenye kikosi hicho msimu ujao ni kipa Aishi Manula aliyemaliza mkataba wake Azam ambaye atachukua nafasi ya Mghana Daniel Agyei anayetajwa kuwa mbioni kuondoka Msimbazi.
Wachezaji wengine ambao wapo kwenye hesabu za Simba, ni kiungo mkabaji wa Mbao FC, Yusuph Ndikumana, mshambuliaji wa Azam, John Bocco anayetajwa kumalizana na Wekundu wa Msimbazi hao, lakini pia mshambuliaji wao za zamani, Mganda Emmanuel Okwi na beki wa Tanzania Prisons, Salum Kimenya.
Iwapo usajili huo mpya utafanikiwa, ina maana kuwa kikosi cha kwanza cha Simba kitapanguliwa kwa watano hao kuchukua nafasi za wengine na kuwa kama ifuatavyo:-
Kipa atakuwa ni Manula, beki wa kulia Javier Bokungu wa kushoto ni Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, mabeki wa kati James Kotei na Jjuuko Murushid, wakati kiungo mkabaji ni Ndikumana, huku kiungo mshambuliaji akiwa ni Mzamiru Yassin.
Winga wa kulia atakuwa ni Shiza Kichuya, winga wa kushoto Okwi, huku washambuliaji wa kati wakiwa ni Bocco na Laudit Mavugo ambapo mfumo utakaowafaa ni wa 4-4-2.
Kwa upande wa benchi, kutakuwa na Agyei au Manyika Peter Jr, Kimenya, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto, Abdi Banda, Jonas Mkude, Ibrahim Ajib na Mohammed Ibrahim ‘MO’.
Kwa upande wa Bokungu, mchezaji huyo amejikuta akibaki kikosini kutokana na kiwango cha juu alichokionyesha kama ilivyokuwa kwa Tshabalala aliyeibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara na Murushid, Kotei, Mzamiru, Kichuya na Mavugo, huku Mkude akionekana kuwa njiapanda kutokana na hofu ya Simba kumpoteza kama ilivyo kwa Ajib wanaotajwa kukaribia kumaliza mikataba yao.
Juu ya ingizo jipya hasa katika safu ya ushambuliaji, MASSHELE BLOG ilizungumza na Mavugo ambaye alisema: “Mimi nipo tayari kucheza na yeyote, hivyo atakayekuja nitafanya naye kazi, siwezi kubagua kwa kuwa najua soka ni kipaji cha wengi hivyo huwezi kuwa na kinyongo.”
Comments
Post a Comment