ENDOMETRIOSIS NI UGONJWA GANI?| FAHAMU ZAIDI KUHUSU UGONJWA WA ENDOMETRIOSIS




Ukuta wa ndani wa kifuko cha uzazi unaitwa endometrium. Ukuta huu hujengeka na kubomoka kila mwezi na kusababisha hedhi kwa wanawake. Kujengeka na kubomoka kwa ukuta huu wa ndani wa kifuko cha uzazi kunasababishwa na mabadiliko ya kiasi cha hormoni za uzazi mwilini.
Endometriosis ni ugonjwa unaosababishwa na uwepo wa tishu zinayofanana na ukuta wa ndani wa kifuko cha uzazi (endometrium) sehemu nyingine kwenye mwili. Mara nyingi tishu hizi huota kwenye sehemu ya chini ya tumbo (pelvis) karibu na ovari, kifuko cha uzazi, kibofu cha mkojo na njia ya haja kubwa. Kama ilivyo kwa ukuta wa ndani wa kifuko cha uzazi (endometrium), tishu hizi zinazopatikana nje ya kifuko cha uzazi pia hujengeka na kubomoka kutokana na mzunguko wa hedhi. Kwa sababu hii, hata dalili za uwepo wa ugonjwa wa endometriosis hufuatana na mzunguko wa hedhi.

Kitu kinachosababisha ugonjwa huu hakifahamiki kwa uhakika lakini inaaminika kuwa kiasi kidogo cha damu kinachoingia tumboni wakati wa hedhi kupitia mirija ya uzazi hubeba seli za endometrium ambazo huota ndani ya tumbo.
Kutokana na uwepo wa endometriosis ndani ya tumbo, damu inayotokana na kujengeka na kubomoka kwake kila mwezi hukosa njia ya kutokea. Kwa sababu hii, damu hii huganda na kusababisha makovu kwenye sehemu ya ndani ya tumbo (abdominal cavity). Ugonjwa ukiendelea muda mrefu makovu haya huweza kushambulia kiungo kilichokuwa na endometriosis na kukiharibu. Kwa mfano, endometriosis ikishambulia ovari inaweza kuziharibu na kusababisha mwanamke kushindwa kutoa mayai na kupata mtoto, ikishambulia njia ya mkojo inaweza kuiziba njia hiyo na kusababisha mafigo kuharibika , ikishambulia njia ya haja kubwa inaweza kusababisha maumivu wakati wa haja kubwa. Vilevile endometriosis inayoshambulia ovari inaweza kusababisha uvimbe wa ovari hiyo (ovarian cysty).

Aina mojawapo ya endometriosis ni endometriosis inayopatikana ndani ya msuli wa kifuko cha uzazi. Aina hii ya endometriosis inaitwa adenomyosis. Vilevile endometriosis huweza kutokea kwenye kovu la operation ya kujifungua mtoto ( caesarean section scar). Kovu lenye endometriosis hutoa majimaji wakati wa hedhi na kwa kipindi hicho huwa na maumivu. Mara chache hutokea endometriosis kuwa sehemu zilozo mbali na viungo vya uzazi kama vile kwenye mapafu, jambo ambalo husababisha kukohoa damu wakati wa hedhi (catamenial hemoptysis).
Dalili za uwepo wa endometriosis ni maumivu wakati wa hedhi (dysmenorrhoea), kutokwa na damu nyingi za hedhi au siku za hedhi kuwa nyingi zaidi ya siku 5, kushindwa kupata ujauzito (sterility), maumivu wakati wa kufanya tendo la ndoa (dyspareunia) na maumivu wakati wa haja kubwa au ndogo.

Mwanamke mwenye dalili za endometriosis anatakiwa kupimwa na daktari ili aweze kupewa ushauri wa matibabu. Zipo aina kuu tatu za vipimo – kupimwa kwa mikono ya daktari, kupimwa kwa njia ya ultrasound na kupimwa kwa njia ya upasuaji wa matundu madogo (laparoscopy). Njia ya upasuaji wa matundu madogo ndio inayotumika zaidi kwenye kugundua uwepo wa endometrisis na hapohapo ugonjwa huweza kuondolewa. Daktrari hupeleka sehemu ya ugonjwa aliyoitoa kwenye vipimo vya maabara (pathology) ambayo huthibitisha uwepo wa tishu aina ya endometriosis. Kutokana na kutokuwepo kwa njia hii katika vituo vingi vya huduma nchini Tanzania, ugonjwa wa endometrisis hausikiki sana nchini, lakini upo na wanawake wengi wenye maumivu yasiyotibika kwa dawa wakipimwa wanauwezekano mkubwa wa kukutwa na ugonjwa huu.

Ugonjwa huu unatibika.
Njia ya uhakika ya kutibia endometriosis ni upasuaji. Katika upasuaji huo eneo liliothirika huondolewa. Baada ya matibabu haya wanawake wengi hupona kabisa na kuendelea na maisha ya kawaida bila maumivu na huweza kupata ujauzito na kujifungua bila matatizo iwapo ugonjwa haukuathiri ovari zote. Upasuaji huu mara nyingi hufanyika kwa njia ya upasuaji wa vitundu vidogo bila kufungua tumbo ( laparoscopy). Hata hivyo iwapo vifaa vya upasuaji huu havipo, unaweza kufanyika upasuaji wa kawaida wa tumbo (laparotomy).

Dawa zinazotumika kwenye matibabu ya endometriosis ni dawa ambazo zinapunguza kiwango cha hormoni zinazosababisha kukua kwa ukuta wa ndani wa kifuko cha uzazi. Dawa hizi ni pamoja na dawa za uzazi wa mpango . Hata hivyo dawa hizi haziondoi endometriosis ila huzuia ukuaji wake. Mgonjwa anapoacha kunywa dawa endometriosis huendelea kukua tena.
Kwa kutuliza maumivu dawa za maumivu kama ibuprofen, mefenamic acid, naproxen na nyinginezo husaidia hasahasa kipindi cha hedhi.
Picha inaonyesha sehemu mbalimbali za mfumo wa uzazi zinazoshambuliwa na ugonjwa wa endometriosis.

Image may contain: text

Comments

Popular posts from this blog

HIZI HAPA SMS TAMU ZA KUMTAKIA USIKU MWEMA MPENZI WAKO

SMS na MESEJI 900+ za mapenzi

MIAKA 22 SASA TANGU KUZAMA KWA MELI KUBWA YA MV BUKOBA, TANZANI TUMEJIFUNZA NINI?