Wakorea Kusini: Hatutaki Marekani iweke ngao yake ya makombora nchini kwetu
Wakorea Kusini: Hatutaki Marekani iweke ngao yake ya makombora nchini kwetu
Raia wa Korea Kusini wamefanya maandamano kulalamikia uamuzi wa serikali wa kukubali kuweka ngao ya makombora ya THAAD katika ardhi ya nchi hiyo.
Maandamano hayo yameshuhudiwa katika kaunti ya Seongju, kusini mashariki mwa Korea Kusini ambapo waandamanaji hao wameunda mnyororo wa mshikano wa watu wenye urefu wa kilometa mbili na mita 600, kuonyesha upinzani wao juu ya uamuzi wa Marekani wa kuweka ngao hiyo ya makombora katika mji huo. Washiriki wa mnyororo huo wa mshikano wa watu, sambamba na kutoa nara za kupinga hatua hiyo ya Washington, wamelalamikia uamuzi wa serikali ya Seoul ya kuridhia kuwekwa ngao hiyo karibu na makazi ya raia.
Maandamano hayo ya sasa ya kupinga uwekaji ngao ya makombora ya THAAD kwa kimombo "Terminal High Altitude Area Defense" ambayo imetajwa kuwa na madhara mbalimbali ya kimwili na kwa kilimo, yameifanya serikali ya Korea Kusini kuanzisha uchunguzi mpya wa suala hilo, hususan mahala pengine tofauti na hapo. Mbali na mji wa Seongju, kadhalika wakazi wa mji wa Gim Chan, ulioko karibu na mji wa Seongju, nao wameandamana kupinga mpango huo wa uwekaji ngao tajwa ya Marekani katika maeneo hayo. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, malalamiko hayo ya raia wa Korea Kusini, ni pigo kwa siasa za Marekani na muitifake wake yaani serikali ya Seoul katika eneo. Hayo yanajiri katika hali ambayo uchunguzi wa maoni unaonyesha kwamba asilimia 53 pekee ya raia wote wa Korea Kusini, ndio wanaounga mkono uwekaji ngao hiyo ya makombora ya Marekani nchini humo.
Kwa kuzingatia kuwa hadi sasa wakazi wa mji wa Seongju bado hawajaweza kuwashawishi raia wote wa nchi hiyo kuungana nao katika kupinga suala hilo, ndio maana wakaanzisha maandamano ya mnyororo wa mshikano wa watu ambayo wamesema yatakuwa endelevu. Hii ni katika hali ambayo Jumatano ya jana rais Donald Trump wa Marekani aliitisha kikao cha baraza la seneti kujadili kadhia ya Korea Kaskazini. Kikao hicho kilifanyika katika hali ya faragha.
Comments
Post a Comment