Uhakiki ,Ushairi karibu ndani ya kezilahabi

(a) Matumizi ya Lugha
Karibu Ndani imetumia lugha ya kishairi ambayo ndani mwake kuna misemo, nahau na tamathali za usemi - ambazo kwazo kutumika kwake vizuri kumefanya taswira mbalimbali zijengwe.
(i) Tamathali za Usemi
Ziko tamathali mbali mbali katika diwani hii. Tutataja na kuziainisha baadhi ya tamathali hizo.
Tashibiha
Tamathali ya kitashibiha ni ile inayolinganisha vitu viwili au zaidi vyenye sifa tofauti kwa kutumia maneno - mithili ya, mfano wa, kama na kadhalika. Katika Karibu Ndani tamathali hizi ni nyingi, na kila pale ambapo zimetumika husaidia kuibua hisi na kujenga taswira fulani. Mfano ni huu (kutoka “Mkesho” uk.4).
......Kama jua jekundu lichwavyo
Na mionzi hafifu ing’aavyo magharibi
Ndivyo mwendo wetu uchechemeavyo!
Picha inayojitokeza hapa ni kuwa mwendo u wa taratibu mno. Mwendo wa mashaka!
Mfano mwingine unaonekana katika shairi la “Matumaini” (uk. 6).
Akiyumbayumba
Na sarawili zee mawinguni
Kama mlevi mwenye mguu mmoja......
Tunaweza kumwona (huyu) anayeyumbayumba (kama) mlevi mwenye mguu mmoja. Huku si kuyumba kwa kawaida. Anayumba kihatari sana.
Sitiari
Kama tashibiha, sitiari ni tamathali inayolinganisha vitu viwili au zaidi vyenye sifa tofauti, lakini haitumii maneno ya viungo. Katika Karibu Ndani shairi la “Azimio” (uk. 27) lina mifano hii:
Azimio (sasa) ni mabaki ya chakula
(Kwenye sharubu za bepari)
Kalamu inayovuja
(Katika mfuko wa mwanafunzi)
Vumbi zito
(Baada ya ng’ombe kupita)
Ni punje za ulezi
......jangwani!
Kifungu hiki cha maneno kinaonyesha sitiari ilivyotumika. Maneno yaliyo kwenye vifungo hayahusiki, lakini yale yaliyoachwa ndiyo vifananishi halisi.
Sitiari nyingine zinajitokeza pia katika shairi la “Kujifunza Kuendesha” (uk. 29).
Nilijiona baharini,......
Wadogo samaki wakishangilia kichama
Bahari ikawa damu na damu ikawa bahari
Maneno yaliyoandikwa kwa italiki ndiyo yanaonyesha matumizi ya sitiari. Tunaweza kuiona “Bahari” ikiwa damu na “damu” ikiwa bahari. Picha inayopatikana hapa si nzuri ni ya kutisha!
Tashihisi
Tamathali hii huvipa uhai vitu ambavyo si binadamu na kuviweka vitende kama binadamu. Karibu Ndani imetumia pia tamathali za aina hii, Katika shairi la “Nondo” (uk. 13), tunaambiwa:
Nje kuna giza na upepo unaimba
Wimbo wa upweke na woga!
Nondo achew ngoma ya rnbawa zake.
Maneno “upepo unaimba” na “Nondo acheza ngoma” ni tashihisi. Mtu ndiye anayeimba na si upepo! Mtu hucheza ngoma, si nondo!
Kejeli/Dhihaka
Tamathali hizo zina uhusiano wa karibu na zinaonyesha pia zimetumika kwa kiasi chake. Katika shairi la “Matumaini” (uk. 6) tunaambiwa:
Akiyumbayumba
...
Kama mlevi mwenye mguu mmoja,...
Hali ya kuyumba kama mlevi ni kumkejeli (mtu) au kumdhihaki (mtu). Mara nyingi tamathali hizi zilipotumika zimeleta pia ucheshi, ambao nao umesaidia kuipa kazi hii nguvu kubwa za kisanaa.
Tasifida
Tamathali hii ni ile yenye kutumia maneno yenye kupunguza makali. Pengine huitwa semi zenye “adabu.” Katika Karibu Ndani, Shairi la “Karibu Ndani” (uk. 34 - 37) mshairi ametumia tasifida kubwa moja.
Kwa mfano, tunamsikia mshairi akinukuu kizee akisema:
Ai! Mimi mmeza nyoka,
Kisha nyuma akatokea!
Mwandishi anamjenga huyu kizee anayemeza nyoka, kisha nyuma akatokea! Badala ya kusema: kisha (matakoni) akatokea.
(ii) Mbinu Nyingine za Kisanaa
Ziko mbinu nyingine ambazo mshairi amezitumia. Mbinu hizo tutazi-chambua moja baada ya nyingine.
Takriri
Takriri ni mbinu ambayo kwayo msanii huamua kurudia maneno au miundo fulani katika kazi ya kifasihi ili kuiimarisha na kuipamba kazi ya sanaa. Karibu Ndani imetumia takriri mbalimbali na kwa uwingi.
Takriri zinazojitokeza ni pamoja na takriri-miundo (taz. Kifo cha Mende Wekundu, uk. 33), takriri-neno (taz. Sisi kwa Sisi, uk. 19), takriri-mistari (taz. mashairi mbali mbali) na kadhalika.
Tashtiti
Hii ni mbinu ya kuuliza swali ambalo jibu lake linafahamika. Mbinu hii huambatana na mbinu za kushangaa mambo mbalimbali katika baadhi ya misemo. Kuna mifano mingi katika Karibu Ndani. Shairi la “Sisi kwa Sisi” (uk. 19 - 21) lina mifano ya tashtiti, Angalia.
Ooo! leo tunamla Mwanasheria! O! na Askofu
O! Keshokutwa tutawala wadhaifu! Na walio mbele!
Kote barani! O! O! O! Marais!
Hii ni baadhi tu ya mifano mingi.
Onomatopeia/Tanakali Sauti
Hii ni mbinu inayoiga sauti ya mtu, kitu na/au mnyama katika kazi ya sanaa. Lengo ni kuipamba kazi hiyo ya kisanaa. Mashairi ya “Karibu Ndani” na “Sisi kwa Sisi” ina mifano hiyo ya Onomatopeia.
(iii) Ujenzi wa Taswira
Hiki ni kiegezo muhimu cha sanaa katika kazi za fasihi. Taswira na ishara katika ushairi ni ufundi wa mshairi wa kuweza kusawiri hali au dhana anayoiongelea kwa njia inayogusa vionjo mbalimbali vya watu. Vivyo hivyo aghalabu hupewa umbo kamili akilini mwa msomaji au msikilizaji.
Katika diwani hii, yako mashairi mbalimbali ambayo yanajenga taswira mbalimbali. Labda - tujue kwanza taswira maana yake nini? Kifupi, taswira ni picha ambayo hutokana na kupangwa vyema kwa maneno yanayotumika. Picha hiyo yaweza kuwa ya kitu, hali, wazo, dhana au uzoefu fulani wajamii au sehemu yajamii katika mawazo ya wanaopokea shairi linalohusika.
Kwa upande wa ishara, hii ni dhana au wazo (ma) mbalimbali anayotumia msanii katika kazi yake ya fasihi kuwakllisha vitu, dhana au mawazo mengine. Katika shairi la “Hatumwoni” (uk. 31) tunajengewa taswira ya watu wengi waliosimama ambao wanafanya (mtu) wanayemtaka umma asionekane. Tena tunajengewa taswira ya kelele - “...acheni kelele!.” Tunaweza kuona pia taswira ya wasaliti wanaotarajiwa kubanikwa - taswiraya kubanikwa imejitokeza wazi.
Shairi/Mashairi mengine ambayo taswira mbalimbali zinajitokeza ni pamoja na “Kifo cha Mcnde Wekundu” (uk. 33), “Kisima” (uk. 25), “Sisi kwa Sisi” (uk. 19), “Safari” (uk. 6) na kadhalika.
Mchangamano wa taswira mbalimbali ndio unaoelezea na kuonyesha ufundi wa kisanaa wa E. Kezilahabi. Kila msomaji anayo nafasi ya kuichambua mbinu hii na kuiona jinsi ilivyoimarisha kazi ya Karlbu Ndani



Comments

Popular posts from this blog

HIZI HAPA SMS TAMU ZA KUMTAKIA USIKU MWEMA MPENZI WAKO

SMS na MESEJI 900+ za mapenzi

MIAKA 22 SASA TANGU KUZAMA KWA MELI KUBWA YA MV BUKOBA, TANZANI TUMEJIFUNZA NINI?