DHANA YA URADILI YA KIMOFOLOJIA


KISWAHILI
DHANA YA URADIDI KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI
LEARN SWAHILI 10:43:00

UTANGULIZI
Dhana ya uradidi,
Kwa mujibu wa Rubanza (1996), anafasili uradidi kuwa ni njia ya kuunda maneno mapya katika Kiswahili, kama ilivyo katika lugha zingine ni kurudufu au kwa maneno mengine ni kurudia maneno. Neno lote zima linarudiwa au sehemu ya neno linarudiwa. Linaporudiwa neno zima kitendo hicho huitwa urudufu kamili na linaporudiwa sehemu ya neno ni urudufu nusu.
Kwa mujibu wa Matinde (2012), uradidi ni utaratibu unaotumika katika kuunda maneno ambayo sehemu ya neno lote hurudiwa na kuunda neno au msisitizo fulani.
Fasili ya Matinde ina upungufu katika kufasili hasa nini maana ya uradidi kwani si lazima neno lote lirudiwe, huweza kuwa sehemu tu ya neno.
Hivyo tunaweza kusema kuwa uradidi ni kanuni au utaratibu katika lugha wa kuunda neno/maneno mapya kwa namna ya kurudia sehemu ya neno au neno zima. Ili hali sehemu ya neno ikirudiwa huitwa urudufu nusu na ikiwa ni sehemu nzima ya neno hujulikana kama urudufu kamili.
Mfano,
Nungu + nungu = Nungunungu
Pilika + pilika = Pilikapilika
Kizungu + zungu = Kizunguzungu
Kimbele + mbele = Kimbelembele
Aina za uradidi.
Kuna aina mbili za uradidi kutokana na namna ambavyo neno hurudiwa. Aina hizo ni:
(i) Uradidi kamili
(ii) Uradidi nusu
Uradidi kamili,
Rubanza (1996), anafasili kuwa uradidi kamili ni aina ya uradidi ambayo kwayo ni neno zima hurudiwa ili kuunda neno moja. Na hicho kitendo huitwa uradidi kamili.
Massamba (2009), anafasili kuwa uradidi kamili (complete reduplication) ni uradidi ambapo neno lote hurudiwa.
Kwa mfano,
Kanuni: Neno + neno = Neno jipya.
Peta + peta = petapeta
Pole + pole = polepole
Haraka + haraka = harakaharaka
Cheka + cheka = chekacheka
Pilika + pilika = pilikapilika
Pika + pika = pikapika
Shamra + shamra = shamrashamra
Cheza + cheza = chezacheza
Kimbia + kimbia = kimbiakimbia
Uradidi nusu,
Kwa mujibu wa Rubanza (1996), anaeleza kuwa uradidi nusu ni aina ya uradidi katika uundaji wa maneno ambayo kwayo sehemu ya neno hurudiwa ili kuunda neno jipya/ maneno mapya katika lugha. Hali hii hujulikana kama urudufu nusu.
Massamba (2009), anafafanua kuwa uradidi nusu (partial reduplication) ni uradidi ambao kwao sehemu tu ya neno hurudiwa, kwa mfano: pepeta.
Hivyo maneno hayo hurudiwa kwa madhumuni ya kutilia msistizo au hali fulani.
Kwa mfano:
Ki + zungu + zungu = kizunguzungu
Ki + wili + wili = kiwiliwili
Ki + nyume + nyume = kinyumenyume
Ki + nyevu + nyevu = kinyevunyevu
Ki + mbele + mbele = kimbelembele
Katika mifano hiyo tumeona uambatanishaji wa mofimu tatu, yaani mofimu {ki-} na mofimu huru mbili. Kiambishi awali {ki-} kinadondoshwa katika neno la pili.
Kanuni: {ki} +{m-huru} + {m-huru} = Neno.
Dhana ya uambatanishaji.
Matinde (2012), anadai kuwa uambatanishaji ni mbinu ambayo huhusisha kuunganishwa kwa maneno mawili kuunda neno moja jipya ambalo maana yake huwa tofauti na maneno ambayo yametumika kuunda neno hilo.
Rubanza (1996), anaeleza kuwa uambatanishaji ni dhana ihusuyo uwekaji pamoja wa maneno mawili au zaidi ili kuunda neno moja. Uambatanishaji, badala ya kunyumbua mofimu katika mzizi sasa tunaweka maneno mawili au zaidi pamoja. Maneno hayo yanaweza kuwa huru au kuambatanishwa na kunyambulishwa na mofimu.
Hivyo tunaweza kusema kuwa, uambatanishaji ni kanuni au taratibu ihusuyo uundaji wa maneno mapya katika lugha kwa namna ya kuunganisha maneno mawili tofauti na kuunda neno moja. Uunganishaji huo wa maneno huweza kuwa ya kategoria moja au kategoria tofauti.
Mfano:
Nomino + nomino
Mwana + siasa = mwanasiasa
Bata + mzinga = batamzinga
Mwana + jeshi = mwanajeshi
Njugu + mawe = njugumawe
Askari + kanzu = askari kanzu
Nomino + kivumishi
Pembe + kali = pembekali
Mwana + haramu = mwanaharamu
Mwana + mkaidi = mwanamkaidi
Mja + mzito = mjamzito
Mbuzi + jike = mbuzi jike
Kitenzi + nomino
Piga + mbizi = pigambizi
Pima + maji = pimamaji
Chemsha + bongo = chemshabongo
Zima + moto = zimamoto
Nomino + kitenzi
Bongo + lala = bongolala
Nyama + choma = nyama choma
Kitenzi + kielezi
Ona + mbali = onambali
HITIMISHO
Njia hizi mbili za uundaji wa maneno hazina tofauti kubwa,tofauti iliyopo ni kuwa katika uambatanishaji maneno mawili tofauti yanaunganishwa pamoja. Matendo haya mawili ya uambatanishaji na uradidi yana msingi mmoja ulio sawa. Maana ya neno mojamoja hailingani na maana ya maneno mawili yanapoungwa pamoja.
MAREJELEO.
Massamba, D. P.B (2009). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar-Es Salaam: Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.
Rubanza, Y. I. (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar-Es Salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.
SWALI: Ushairi andishi umetokana na ushairi simulizi. Jadili kwa kutumia mifano hai
TAMTHILIA YA KISWAHILI
Historia ya tamthilia ya Kiswahili



CONTACT US
   
YOUTUBE INSTAGRAM RSS FACEBOOK TWITTER
Created By and Paul Msabaha | and Paul Msabaha +255765194400

Comments
Post a Comment