Degedege

WEDNESDAY, JULY 29, 2015 Degedege Degedege  ni maradhi yanayoambatana na mwili wa mtu kutikisika kwa haraka  huku mwili ukikosa uwezo wa kudhibiti hali hiyo. Wakati wa degedege, misuli ya mwili hukakamaa na kulegea mara kwa mara. Katika jamii yetu maradhi haya yamekuwa yakihusishwa na imani za kishirikina na uchawi.  Hata hivyo maradhi haya husababishwa na magonjwa mbalimbali.Mara nyingi degedege hujitokeza katika watu ambao wana familia yenye  historia ya degedege au ugonjwa wa kifafa.  Pia imekuwa ikidhaniwa kuwa watoto ndio huathirika  na maradhi haya. Dhana hii haina ukweli wowote. Watu wa rika zote wanaweza kuathiriwa na degedege. Hata hivyo watoto na vijana ndio huathirika zaidi na degedege.  Degedege inapojirudia huitwa Kifafa.  Imani  hizo zimechangia kuongezeka kwa vifo au mtindio wa ubongo  ambavyo hutokea iwapo  maradhi haya hayakutibiwa kwa haraka na kwa ufasaha.   Dalili za degedege  Wakati mwingine sio rahisi kubaini iwapo mtu amepatwa na degedege. Baadhi ya watu wengine hushikwa na bumbuwazi  (huduwaa ) kwa muda mfupi hivyo sio rahisi kugundua kama amepata degedege.  Dalili hutegemea sehemu ya ubongo ambayo imeathirika na hujitokeza kwa haraka. Baadhi ya dalili hizo ni  •Kupoteza fahamu au kuzimia ikifuatiwa  na kuchanganyikiwa (mgonjwa anapoteza kumbukumbu)  •Kushindwa Kuzuia mkojo au haja kubwa  •Kutikisika au kukakamaa kwa mwili mzima  •Kuanguka chini kwa ghafla  •Kung'ata meno  •Kushindwa kupumua  •Kutokwa udenda au mapovu mdomoni  •Kuzungusha macho  •Kuunguruma  •Mabadiliko katika tabia mfano mtu kuvuta vuta nguo au nywele zake  Mgonjwa anaweza kuwa na dalili hizo katika kipindi kifupi sana  na wakati mwingine kufikia hata dakika 15. Mara chache sana dalili hizo huendelea kwa muda mrefu zaidi.  Degedege husababishwa na nini?  Degedege sio ugonjwa bali ni maradhi yanayosababishwa na magonjwa mbalimbali. Degedege hutokana na kuvurugika kwa mfumo wa umeme katika ubongo. Yafuatayo ni magonjwa ambayo ambayo yanaweza kusababisha  degedege  •Maambukizi kwenye ubongo na uti wa mgongo mfano  •Homa ya Uti wa mgongo   •Kupungua kwa kiwango cha sukari au madini ya chumvi katika damu  •Kuumia ubongo kunakoweza kujitokeza wakati wa  kujifungua  •Uvimbe kwenye ubongo  •Ugonjwa wa  malaria  •Utumiaji wa madawa ya kulevya  •Kifafa  •Homa kali hasa kwa watoto wadogo  •Kuumia kichwani  •Kuongeza kwa joto  •Sumu  •Sumu ya nyoka au wadudu  •Kifafa cha mimba  •Magonjwa ya figo na ini  •Shinikizo la damu  •Magonjwa ya moyo  •Kuacha kutumia pombe au madawa ya kulevya baada ya kutumia kwa muda mrefu. Matibabu ya Degedege  Matibabu ya Degedege hutegemea nini kilichosababisha. Mfano iwapo degedege imesababishwa na malaria au homa ya uti wa mgongo mgonjwa atatumia dawa za kutibu malaria na antibiotiki. Pia mgonjwa huweza kutumia dawa zinazosaidia kudhibiti degedege.  Ufanye nini unapokuwa nyumbani na mgonjwa mwenye degedege?  Mara nyingi degedege hukoma yenyewe. Hata hivyo wakati mtu anapokuwa na degedege anaweza kujiumiza au kudhurika.  Lengo kuu ni kuhakikisha unamsaidia mgonjwa asiumie anapopata degedege. Hivyo unashauriwa kufanya mambo yafuatayo :  •Mzuie mgonjwa asianguke. Msaidie mgonjwa kumlaza katika eneo ambalo ni salama. Ondoa vyombo au vitu vyenye ncha kali vinavyoweza kumdhuru mgonjwa  •Zuia kichwa cha mgonjwa kwa kutumia mto  •Legeza nguo zilizobana hasa maeneo ya shingo.  •Usimuache mgonjwa pekee yake. Hakikisha unabaki na mgonjwa mpaka anaporudia hali ya kawaida au anapopata matibabu.  •Mgeuze mgonjwa upande. Hii itasidia  kuzuia matapishi kuingia kwenye njia ya hewa iwapo mgonjwa atatapika.  Usifanye haya kwa mgonjwa mwenye degedege   •Usijaribu kuzuia degedege kwa kumshikilia au kumdhibiti mgonjwa. Unaweza kusababisha mgonjwa kuumia zaidi  •Usiingize kitu chochote mfano kidole,kijiko, kipande cha nguo kwenye kinywa cha mgonjwa.  •Usimbebe mgonjwa kama eneo hilo  salama na haliwezi kuhatarisha maisha yake  •Usimpatie kitu chochote cha kula au kunywa wakati wa degedege isopokuwa baada ya Degedege na mgonjwa anamerudiwa na fahamu  Iwapo mtoto ana homa unaweza kumkanda na maji ya baridi. Usitumie maji yaliyo ganda.  Unaweza kumpatia panadol ili kushusha homa baada ya Degedege.  Hitimisho Maradhi haya yamekuwa tangu mwanzo wa historia ya binadamu.  Hivyo ni vyema kutafuta ushauri wa kitaalamu unapokuwa na mgonjwa mwenye degedege. Kuchelewa kupata matibabu huweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo Kupoteza maisha. 

Comments

Popular posts from this blog

HIZI HAPA SMS TAMU ZA KUMTAKIA USIKU MWEMA MPENZI WAKO

SMS na MESEJI 900+ za mapenzi

MIAKA 22 SASA TANGU KUZAMA KWA MELI KUBWA YA MV BUKOBA, TANZANI TUMEJIFUNZA NINI?