Utakubaliana na mimi kwamba, kitendo cha mtu kubanwa na haja ndogo siyo kitu cha hiyari kwamba sasa mtu anaamua ngoja nibanwe na mkojo, hili ni jambo la asili na ni matokeo ya vyakula, matunda au vinywaji tunavyotumia. Kwa lugha nyingine tumekuwa tukiita kuwa ni wito wa asili au nature’s call. Yawezekana mtu akawa katika mkutano, safarini, akawa katika mitandao ya kijamii anachati au popote pale akiwa anafanya jambo fulani na kutokana na jambo hilo, mtu akaendelea kujibana na kutokwenda kuyapunguza maji haya kutoka katika kibofu cha mkojo kwa kutoa kipaumbele kwa shughuli anayoifanya kuliko kusikiliza kwanza wito huu wa asili. Mambo haya tunayafanya sana, utasikia, mkojo umenibana kweli, ila ngoja nimalizie hii kazi halafu niende kujisaidia, hivi ndivyo watu wengi wanafanya. Kutokana na vyakula na vinywaji tunavyotumia, kibofu cha mkojo huanza kujaa mkojo, mkojo unapofikia karibu mililita 50 mpaka 500 mtu huanza kuhisi hitaji la kwenda kukojoa. Kibofu cha mkojo kimezunguk...