Istilahi za Ushairi Yafuatayo ni maneno ambayo mshairi au mwanafunzi wa fani ya ushairi atayapata mara kwa mara. Ni vema kuyaelewa na kuyajua kwa kina kwa sababu pasipo na hizi istilahi, hapana ushairi kamili. 1. Shairi Shairi ni tungo yenye muundo na lugha ya kisanii na unaofuata utaratibu wa vina na mizani, hisi au tukio juu ya maisha au jambo na hufuata utaratibu maalum wa urari na muwala unaozingatia kanuni za utunzi wa mashairi yanayohusika. 2. Vina Vina ni silabi za kati na mwisho wa mshororo au tenzi. Kwa mfano, katika ubeti ufuatao, vina vya kati ni ka ilhali vya mwisho ni ki. Jambo litatatulika, iwapo halibaniki, Halikosi bainika, faraja au la dhiki, Lazima litasomeka, iwapo halisemeki, Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki. 3. Mizani Mizani ni idadi ya silabi katika mshororo wa shairi. Kwa mfano, mshororo ufuatao una mizani kumi na sita: Mo-la ndi-ye hu-tu-li-nda, i-na-po-ku-wa tu-hu-ma 4. Mshororo Mshororo ni msta...