Mlinzi wa pembeni wa klabu ya Simba Sports Club Shomari Kapombe amesafiri na timu kuelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Mapinduzi Cup.
Kapombe ambaye alisajiliwa na timu hiyo akitokea Azam ameshindwa kucheza mchezo wowote hadi hivi sasa kutokana na kuwa na majeraha aliyoyapata wakati akiitumikia timu ya Taifa dhidi ya Rwanda Julai mwaka uliopita.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha klabu ya Simba Haji Sunday Manara amesema Kapombe ataanza kuonekana kwenye michuano hiyo pamoja na wachezaji Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi ambao nao walikuwa na majeraha.
-Wachezaji Salim Mbonde na Said Mohammed 'Nduda' wao tumewaacha Dar, Ila Kapombe tutajiunga naye Zanzibar ameshaanza mazoezi mepesi mepesi kwa hiyo tutakuwa naye, na Okwi yeye ameshatua nchini na tutakuwa naye," Manara amesema.
Simba wamesafiri asubuhi hii kuelekea visiwani Zanzibar ambapo katika michuano hiyo wataanza kwa mchezo dhidi ya timu ya Mwenge FC Jumanne ya Januari 2, 2018.
Pole kwa Yanga. 
Aidha katika hatua nyingine Manara ametuma salamu za pole kwa watani zao Dar Young Africans kwa kuchezea kichapo cha mabao 2-0 katika mchezo wa ligi dhidi ya Mbao mchezo uliofanyika Jumapili Ya Disemba 31, 2017 kwenye uwanja wa CCM Kirumba.