majina ya waliopata mikopo elimu ya juu
Hiyo ni sawa na asilimia 30.1 ya waombaji wote.
Serikali yatenga mikopo ya Sh570 bilioni kwa wanafunzi 162,000.
Majina ya waliopata mikopo kuwa wazi kabla ya Oktoba 25.

Dar es Salaam. Wakati Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ikijiandaa kuwapangia wanafunzi wa elimu ya juu mikopo yao mwezi huu, wanafunzi wa 26,688 walioomba mikopo hiyo kwa mwaka 2021/22 hawataweza kupata mikopo hiyo.
Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo HESLB, Dk Veronica Nyahende amesema majina ya wanafunzi waliopata mikopo wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu mwaka 2021/22 yatatangazwa mapema kabla ya vyuo kufunguliwa kuanzia Oktoba 25 mwaka huu.
Hadi kufikia Septemba 30, HESLB ilikuwa imepokea maombi 88,688 na kati ya maombi hayo; 85,706 yalikuwa kamilifu na kutoa siku nne kuanzia Oktoba 4 hadi 7 kwa maombi yenye kasoro kufanyiwa marekebisho. 
“Katika uhakiki wa maombi tumebaini waombaji 2,982  fomu zao zina kasoro. Tumetoa muda wa siku nne, na baada ya hatua hiyo kukamilika tutaanza mchakato wa kupanga mikopo kwa wanafunzi wenye sifa na uhitaji”, amesema Dk Nyahende wakati akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) leo Oktoba 5.
Hata hivyo, bodi hiyo haitaweza kutoa mikopo kwa wanafunzi wote walioomba kwa sababu ya kutokuwa na bajeti ya kukidhi mahitaji ya waombaji wote.
Katika mwaka wa masomo 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha Sh570 bilioni kwa ajili ya bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu 162,000 wakiwemo wanafunzi 62,000 wa mwaka wa kwanza.
Wanafunzi 26,688 wa mwaka wa kwanza sawa na asilimia 30.1 ya waombaji wote hawatapata mikopo hiyo au sawa na kusema wanafunzi watatu kati ya saba hawatapa mikopo hiyo.
Kwa mujibu wa Dkt. Nyahende waombaji ambao maombi yao yamekamilika wanapaswa kutembelea akaunti zao za SIPA (Student’s Individual Permanent Account) ili kupata taarifa za mikopo watakayopangiwa baadaye mwezi huu.
Mikopo hiyo husaidia wanafunzi kuweza kumudu gharama za masomo na maisha wakati akisaka elimu hiyo ya juu.