Sura ya 4: Mtindo wa magazetini na shughuli za kisiasa

Utangulizi
Magazeti ni chombo muhimu sana cha mawasiliano na umma. Na kusema kweli hiki ndicho chombo cha mawasiliano na umma kilicho kikongwe zaidi kuliko vyombo vingine kama vile redio, televisheni, sinema, video na kadhalika. Pia ni chombo kinachowashirikisha watu wengi sana kwa pamoja na kwa wakati mmoja katika kutoa mchango wao magazetini na kusoma yaliyoandikwa na wenzao. Tena hakina gharama kubwa katika kutumiwa na umma.
Kwa hali hii inaonekana kuwa magazeti ni chombo muhiinu cha kuelimishia umma. Dhima hii ni kubwa sana. Ili iweze kutckelezwa vema haitoshi tu kwa wale wanaowasiliana kwa kutumia chombo hiki kuwa na msamiati mkubwa wa Kiswahili na kuifahamu vema sarufi ya Kiswahili. Kilicho muhimu zaidi ni kujua jinsi ya kuzitumia zana bizi za kiisimu kwa namna inayofaa na inayokidhi mazingira haya maalmn ya mawasiliano.
Katika sura hii tutaonyesha na kufafanua sifa na taratibu zinazojitokeza katika mtindo wa magazetini ili kuwawezesha wale wanaokitumia chombo hiki kwa mawasiliano yao wazielewe kwa misingi ya kisayansi na waendelee kuzitumia kwa usahihi zaidi kwa nia ya kuongeza upeo wa ufasaha katika maandishi ya magazetini.
Sharti ifahamike kwamba mawasiliano ya magazetini hayafanywi kiholela. Na wengi wetu tunautambua ukweli huu. Jambo hili linawafanya baadhi ya wananchi hata wachelee kutoa mawazo yao kwenye magazeti kwa kuwa hawazielewi mbinu za kiisimu za kufanya hivyo. Ama wengine ni kweli wanajitoma magazetini kutoa mawazo yao, lakini wanashindwa kueleweka vizuri na umma kwa sababu ya kutoweza kuzitumia vema zana za kiisimu zilizopo kwa ajili ya mazingira hayo. Ni mategemeo yetu kuwa uchanganuzi wa sifa na taratibu hizi katika sura hii utatoa mchango mkubwa katika utatuzi wa matatizo haya.
Kwa upande mwingine shughuli za kisiasa kwenye karne yetu hii zimepamba moto mno hasa kutokana na mwamko wa kisiasa ambao umemfikia karibu kila mwananchi. Kama ilivyowahi kudokezwa na wanafalsafa wa siku za nyuma, siasa ni kipengee pekee ambacho mwananchi yeyote anaweza kujishughulisha nacho (na pengine kwa mafanikio makubwa kabisa) bila kulazimika sana kuwa na msingi wowote wa elimu ya darasani. Hivyo siasa ni kipengee kinachowajumuisha mamilioni ya wananchi - watoto kwa wakubwa, vijana kwa wazee, wake kwa waume, wasomi na wasio wasomi... na kadhalika.
Mawasiliano yanayojuiriuisha umma mkubwa namna hii hayawezi kufanywa kiholela bila kuleta mafarakano miongoni mwa watu hao. Sharti pawepo na taratibu maalumu za zana za kiisimu zinazotumika ili kuwepo na mwafaka katika mawasiliano hayo. Sura hii itazichambua vilevile sifa na taratibu zinazotumiwa kwenye mtindo wa sbughuli za kisiasa.
Magazeti na Shughuli za Kisiasa
Mtindo wa magazetini na shughuli za kisiasa ni ile namna ya mawasiliano yanayotumika:
(i) magazetini kwa mfano, UHURU, MZALENDO, MFANYAKAZI, KIONGOZI, LENGO, URUSI LEO na kadhalika,
(ii) katika majarida (yasiyo ya kitaaluma) kama vile NCHI YETU, MICHEZO, SAUTI YA URAFIKI... na kadhalika,
(iii) katika mikutano na majadiliano ya kisiasa kama vile kampeni za wagombea ubunge, majadiliano ya bungeni, vikao na mikutano ya chama... na kadhalika.
Sifa za Mtindo wa Magazetini na Shughuli za Kisiasa
Hapa, kama tulivyofanya kwa mitindo mingine iliyojadiliwa nyuma, tutatofautisha aina mbili za sifa: sifa zisizo za kiismu na zile za kiisimu.
Sifa Zisizo za Kiisimu:
Hizi ni zile sifa ambazo haziambatani moja kwa nioja na zana za kiisimu zinazotumika katika mawasiliano. Baadhi ya sifa hizi ni:
(i) Mwelekeo wa Kutoa Taarifa na Kushawishi
Sifa kuu isiyo ya kiisimu katika mtindo huu ni ule mwelekeo wa kutoa taarifa na kushawishi. Hii ioa maana kwamba mwandishi (au mzungumzuji) wakati wote hujitahidi sio tu kutoa habari au taarifa fulani, bali pia kuonyesha msimamo wake na uhusiano wake kwa hayo anayoyaandika (au anayoyazungumza) na kuibua uhusiano maaluma wa wasomaji (au wasikilizaji) kwa yale wanayoyasoma (au wanayoyasikiliza). Na ili mawasiliano ya namna hii yaweze kutekelezwa vizuri zaidi na kwa ufanisi wa juu ni lazima lugha mgusoitumike. Jambo hili limeuathiri sana mfumo wa zana za kiisimu katika mtindo wa mawasiliano ya magazetini na shughuli za kisiasa, kwani zana zote za kiisimu zinajitokeza katika hali hii ya kutaka kuleta mguso mkubwa katika lugha, na hivyo kuwasisimua na kuwapendeza wasomaji na wasikilizaji.
(ii) Upendeleo wa Wazi wa Mwandishi au Mzungumzaji
Katika utoaji hoja kwenye magazeti au kwenye mikutano ya kisiasa mtoa hoja sharti aonyeshe waziwazi upande anaoupendelea na kuunga mkono. Hata kama msunamo wa mtoa hoja huyo ni wa kutopendelea upande wowote basi sharti pia auonyeshe waziwazi.
(iii) Kawaida ya Kutekeleza Mawasiliano kwa Niaba ya Chama au Kundi Fulani la Watu
Kwa kuwa magazeti mengi humilikiwa na vyama vya kisiasa, serikali na taasisi mbalimbali; basi mara nyingi taarifa zinazotolewa humo huandikwa kwa niaba ya vyama na taasisi hizo. Kutokana na hali hii waandifhi pengine hujikuta hawana “uhuru” wa kutosha wa kujieleza kadiri watakavyo au wapendavyo. Uhuru kama ule wa waandishi wa kazi za sanaa - riwaya, tamthilia na kadhalika haupo hapa. Hata mhutubiaji kwenye mikutano ya kisiasa hujisikia naye amebanwabanwa kwa kiasi fulani kwanj hotuba yake sharti izingatie itikadi na maadili ya chama anachokiwakilisha.
(iv) Wingi wa Washiriki Katika Mawasiliano Haya
Kwa kawaida gazeti haliandikwi na cntu mrooja tu, bali linashirikisha watu wengi kwa wakati mmoja, kwa mfano, katika UHURU na MZALENDO hushiriki waandishi wa SHIHATA, waandishi wa MAELEZO, waandishi maalum na pia watu binafsi. Majadiliano ya kisiasa vilevile aghalabu hushirikisha watu wengi kwa pamoja na kwa wakati mmoja. Mkutano wa hadhara, kwa mfano, hauwezi kuwa wa mtu mmoja.
(v) Kuwepo kwa Mantiki Katika Jambo Linalojadiliwa
Kama ilivyo kwa mitindo iliyojadiliwa hapo nyuma suala la mantiki ni muhimu sana kwa mtindo huu. Maelezo katika magazeti na mtiririko wa majadiliano ya kisiasa lazima ufuate mantiki maalumu ili pawepo na maelewano baina ya wafuasi wa njia hiyo ya mawasiliano.
Sifa za Kiisimu:
Kama ilivyoelezwa katika sura za nyuma, hizi ni sifa abazo zinaambatananamfumo wenyewe wa zana za kiislmu na hujibainisha katika msamiati, sarufi maumbo fonetiki na miuno ya sentensi inayotumika.
Msamiati
Pamoja na matumizi mapana ya msamiati wa ujumla unaotumika karibu katika kila intindo, kuna aina fulani ya msamiati ainbao umejikita zaidi katika mtindo wa magazetini na shughuli za kisiasa. Msamiati huu una sifa zake za kipekee. Sifa hizi ni pamoja na:
(i) Matumizi Makubwa ya Msamiati na Istilahi Maalumu za Magazetini na Shughuli za Kisiasa
Kwa mfano mhariri, mwandishi, kuripoti, mhakiki, mpiga picha, SHIHATA, MAELEZO, habari, taarifa, kukariri; harakati, mapunbuo, uhasama, demokrasi, itikadi, ujamaa, sera, ukombozi, uchokozi, hujuma, njama, ukomonisti, unyonyaji, kibaraka, bepari, kampeni, opemhani na kadhalika.
Msamiati huu kusema kweli hutumika sana kadka mazingira ya magazetini na shughuli za kisiasa. Neno “taarifa” kwa mfano limetumika mm kadha karibu katika kila gazeti la UHURU na MZALENDO tulilolifanyia uchunguzi.
(ii) Matumizi Mapana ya Vifungu vya Maneno au “Nahau” za Magazetini Zilizokwisha Tayarishwa Tangu Awali
Uchunguzi uliofanywa umeonyesha kwamba waandishi wa habari wa magazetini mara nyingi hutumia vifungu vya maneno au nahau maalumu ambazo tayari zimeshabuniwa tangu zamani. Wanachokifanya ni kuzitumia tu na pengine kuzifanyia mabadiliko madogo madogo tu ili kuleta upatanisho mzuri zaidi wa kisarufi.
Baadhi ya vifungu hivyo vya maneno ni hivi vifuatavyo:
kuhujumu uchumi,
msaada wa hali na mali,
ujamaa na kujitegemea,
kampeni ya nguvu-kazi/kampeni ya mtu ni afya,
tabaka la wafanyakazi/tabaka la wakulima,
maoni y mhariri
kutia saini (mkataba),
kuzindua rasmi (k.m. barabara),
utawale dhalimu (wa Makaburu),
(kuwa katika) mstari wa mbele,
ukoloni mamboleo,
Serikali ya Chama, Serikali ya Mapinduzi...
na kadhalika.
Hebu tuangalie kwa mfano jinsi kifungu cha maneno “kutia saini mkataba” kilivyotumiwa na waandishi wa UHURU na MFANYAKAZI.
(i) UMOJA wa Vijana Tanzania (VUANA)umetiliana saini mikataba ya udurikiano wa kirafiki na Umoja wa Vijana wa nchi sita za Kijamaa za Ulaya ya Mashariki ili kukuza umoja na kuleta maendeleo ya vijana wa nchi hizo (UHURU. Desemba 23, 1983:5).
(ii) SHIRIKA la Akiba ya Wafanyakazi limetoa mkopo wa sh.10 milioni kuendeleza ujenzi wa Hosteli Wilayani Temeke... Ofisa mmoja wa NPF alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kwambaMkataba wa mkopo huo ulitiwa sainiJumamosi iliyopita na Mkurugenzi Mkuu wa NPF... (MFANYAKAZI. Desemba. 10/1983:1).
Katika majadiliano ya kisiasa vilevile kumejitokeza vifungu fulani vya maneno ambavyo hutumika mara kwa mara bila kufanyiwa mabadiliko makubwa. Kwa mfano:
kutoa shukurani/pongezi za dhati,
kwa heshima na taadhima,
kwa unyenyekevu mkubwa
Mheshimiwa Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa...
Mbunge wa... kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa
Waziri, nina swali la nyongeza.
(iii) Matumizi ya Msamiati Unaoonyesha Wazi Upendeleo wa Mwandishi (au Mzungumzaji)
Uandishi wa magazeti na shughuli za kisiasa unahitaji kuonyesha, waziwazi msimamo wa mwandishi au mzungumzaji na upande anaouunga mkono. Hakuna nafasi ya unafiki hapa. Kwa hiyo maneno (msamiati) yanayotumiwa katika mtindo huu huonyesha mara moja msimamo na upendeleo huo. Neno “ndugu” kwa mfano katika magazeti ya Tanzania hutumiwa kuwataja wale tu ambao msimamo wao wa kiitikadi unakubaliana na maongozi na maadili ya Chama kinachoongoza pamoja na serikali yake. Hata viongozi wa serikali wa ngazi za juu wanapokiuka maadili hayo hupoteza mara moja hadhi hiyo ya “ndugu”.
Hali kadhalika wale “wahaini” waliotaka kuiangusha/kuipindua serikali ya muungano ya Tanzania mwanzoni mwa mwaka 1983 walipoteza “undugu” mara tu baada ya njama zao kufichuliwa. Hebu tuangalie jinsi UHURU ilivyoripoti tukio hili.
Tume yaundwa kuchunguza “wahaini” walivyotoroka
SERIKALI imeunda Tume ya Wabunge wanne kuchunguza kitendo cha kutoroka kwa washitakiwa wawili kati ya 30 waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhaini kutoka katika gereza la Keko mjini Dar es Salaam, usiku wa Juni 11 mwaka huu. Wajumbe wa Tume hiyo ni Mbunge wa Mtwara Mjini,Ndugu Austin Shaba, Profesa A. Meena (Moshi Vijijini), Ndugu H.N. Mfaume (Shinyanga Mjini) naNdugu G.A.L. Senyengwa (Mpwapwa). Katibu wa Tumc atatoka Ofisi y.i Kais. Akitangaza hatua hiyo katika Bungc jana asuhuhi, Waziri Mkuu, NduguEdward Sokoine, pia aliscma walinzi wote waliokuwa zamu Keko usiku huo walitiwa ndani siku iliyufualii baada ya kugunduliwa kuwa washitakiwa hao walitoroka.Ndugu Sokoine alikuwa akitoa tamko kuhusu kutomka kwa Pius Mtakubwa Lugangira (40), mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, na Hatty Macghee (37) mshitakiwa wa pili.... (UHURU, Juni 22, 1983:1)
Kama inavyoonekana hapo juu Lugangira na Macghee hawana hadhi ya “ndugu” tena, ambapo maofisa wengine wote waliotajwa wameendelca kuwa “ndugu” kwani bado hawajakiuka maadili ya Chama na Serikali yao.
Aidha matumizi ya maneno kama vile:
Haini lan Smith,
Kaburu Pik Botha,
Nduli Idi Amini,
Mtukufu Rais,
Vita vya Ukombozi,
Kiongozi/Rais wa Urusi, Ndugu
Wazalendo wa Namibia,
Wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini,
Magaidi wa UNITA.... n.k.;
katika magazeti mbalimbali ya Kiswahili yanaakisi kwa kiasi kikubwa sana msunamo na itikadi ya vyama, serikali na taasisi nyinginezo zinazoyamiliki.
Kusema kweli hakuna taarifa au habari yoyote katika gazeti ambayo haina insunamo wa kiitikadi. Habari yoyote lazima ionyeshe kama inawapendelea wajamaa, wakulima na wafanyakazi au inasimamia na kutetea maslahi ya mabepari wanyonyaji. Kimsingi habari nzuri magazetini ni zile zinazozingatia maadili na itikadi ya vyombo vinavyoyamiliki magazeti hayo.
(iv) Matumizi Mapana ya Visawe
Kama inavyojulikana gazeti ni chombo cha mawasiliano ambacho husomwa na maniilioni ya watu kila uku. Baadhi ya habari zinazochapishwa magazetini ni za mambo ambayo hurudiwarudiwa mara kwa mara katika maisha ya wanadamu. Matukio kama ya michezo, shughuli za kikazi za viongozi wa vyama na serikali hufanyika kila siku na lazima yaripotiwe katika magazeti, kwani gazeti ni chombo kimojawapo muhimu cha kutoa habari kwa haraka. Ili kuwafanya wasomaji wasichoshwe na msamiati wa nina moja kila wasomapomagazeti, basi waandishi wa habari hulazimika kutumia visawe vya aina mbalimbali kwa tukio moja hilohilo kwa lengo la kuwavutia zaidi wasomaji wao. Kwa mfano, kitendo cha kufungwa/kushindwa katika mashindano ya mpira wa miguu, mchezo ambao huchezwa na kuripotiwa karibu kila siku, kinaweza kuelezwa kwa kutumia visawe chungu nzima, kama vile:
timu ilishindwa kutamba,
timu ililambwa mabao 2 - 1,
timu ilikung'utwa 5 - 0,
timu ilibandikwa 3 - 1,
timu ililaruriwa niabao 2 - 0,
timu ililazwa 1 - 0,
timu ilitandikwa 3 kavu (yaani 0),
timu ililowa 1 - bila (yaani 0),
timu ilinywea 2 - 1,
timu ilinyukwa bao 1 - 0,
timu ilikubali 3 - 2,
timu ilimezwa 4 - 2,
timu ilichapwa 3 - 0,
timu ilichakazwa 4 - 2,
timu ilichabangwa 4 - 0,
timu ifibwagwa 4 - 1,
timu ililambishwa 1 - 0,
timu haikuliona lango kabisa (haikufunga)... n.k.
Visawe vya namna hii vinapotumika kwenye taarifa za michezo vinawafanya wasomaji wasichoshwe na ukurasa huu wa michezo, kwani huwa wanajihisi kana kwamba wanasoma matukio mapya kila siku na yaliyoandikwa kwa kutumia zana tofauti kabisa za kiisimu.
Tena visawe vinavyopendelewa kutumiwa kwenye magazeti ni vile vinavyoleta mvuto na msisimko zaidi. Kwa mfano, kati ya maneno “ngumi”, “masumbwi”, “ndondi”, na “makonde” maneno matatu ya mwisho yatapendelewa zaidi na mtindo huu wa magazetini.
(v) Matumia Mapana ya Maneno Mapya
Gazeti ni chombo cha kutolea taarifa hasa zilizo mpya. Baadhi ya taarifa hizi pengine huhusiana na uvumbnzi mpya wa kisayansi na kiteknolojia na yamkini hulazimika kuelezwa kwa kutumia msanuati na istilahi mpya za nyanja hizo za sayansi au teknolojia. Hali hii inaweza kuwafanya wasomaji wakumbane na maneno mengi mapya kadka magazeti. Hivi karibuni maneno mapya kama: “skania” (kwa maaoa ya dumuzi, mdudu anayetoboa nafaka), Sungusungu (au Wasalama) (kwa maana ya walinzi wa kijadi), nguvu-kazi, Sekretarieti, Oganaizesheni... n.k. yamekuwa yakitumika sana katika magazeti ya Kiswahili ya Tanzania.
(vi) Matumizi Makubwa ya Tamathali za Usemi, Misimu, Maneno ya Lugha za Kienyeji na za Kigeni
Lugha inayotumiwa magazetini na kwenye shughuli za kisiasa kwa ujumli ni ile yenye kuvutia sana, iliyopambwa vizuri ili kufanya msomaji au msikilizaji awe na ari na mvuto na ajisikie kuibuliwa na hisia fulani. Hisia hizo zinaweza kuwa za furaha, huzuni, masikitiko, chuki na kadhalika. Hivyo zana za kiisimu zinazotumika bapa, hasa msamiati sharti ziweze kukidhi vizuri haja hii. Uchunguzi umeonyesha kwamba tamathali za luenii kama vile sitiari, tasfida, ufananishiAilinganishi, tashibihi/mishabaha... na kadhalika husaidia sana kuleta msisimko katika mawasiliano ya mtindo huu.
Mifano ya matumizi ya tamathali za usemi katika magazeti ni mingi sana. Tutadondoa vichwa vya habari viwili tu kuthibitisha kauli hii:
(i) Moi awapiga darubini viongozi
(UHURU, Oktoba 17,1983:1).
(ii) Jaribio la kumwangusha Rene lafichuliwa
(MZALENDO, Desemba 4,1983:1).
Hapa ziinetumiwa sitiari.
Aidha uchuoguzi umeonyesha kuwa kuna maongczeko makubwa wna ya matumizi ya simo na maneno ya lugha za kienyeji na za kigcni katika magazeti ya Kiswahili. Tunafikiri sababu kubwa ya roatumizi ya robinu hizi ni kuyawezesha mawasiliano yawe mafupi na yanayoeleweka kwa baraka, Kwa mfano:
(i) MABASI madogo “Dala dala”yameamriwa kusiinamisha safari zake za kuchukua abiria mara moja nje ya Jiji ropaka kwanza yakaguliwe lu kupewa masharti kuhusu matumizi ya leseni zake...
(UHURU, Julai 11, 1981:5).
Katika matini hii simo “dala dala” imetumiwa ili nisomaji (hasa wa Dar es Salaam) aweze kuelewa kwa haraka na kwa usahibi zaidi Jarobo linalozungumziwa. Kotumia ufafanuzi mrefu, mathalani, 'mabasi madogo yanayochnkua abiria chioi ya 50 kutoka jijini hadi nje ya jiji kwa nauli ya shilingi 5' kungechelewesha maelewano na kuchukua nafasi kubwa gazetini.
Angalia vilevile kichwa cha habari “Hupati behewa bila 'Mchicha' (UHURU, Januari 16, 1984:1).
(ii) CHUMVI imeadimika Mbeya mjini na inauzwa kwa bei ya shs.5.00 kwa “ndonya” isiyozidi robo kilo badala ya bei ya serikali ya shs.3.00 kwa kilo moja, ilifahamika jana.
“Ndonya” ni jina linalotumiwa na wakazi wa Mbeya kuelezea vibakuli vidogo vinavyopimiwa chumvi, unga na mchele sokoni (UHURU, Desemba, 23. 1983:5).
Neno “ndonya” ni la kienyeji (la Kinyakyusa) na limewezesha mawasiliano yawe mafupi, yachukue nafasr ndogo tu gazetini na yaeleweke kwa haraka na wanaohusika.
Sarufi Maumbo
Sifa kuu za kisarufi maumbo zinazoubainisha mtindo wa magazetini na shughuli za kisiasa ni hizi zifuatazo:
(i) Kawaida ya Kutoonyesha Viakati Magazetini
Viakati ni vijisehemu vidogo-vidogo vya neno vinavyoonyesha wakati katika tendo - kwa mfano - na-, -li- na -ta-. Uchunguzi umeonyesha kuwa waandishi wa habari kwa kawaida huwa hawatumii viakati hasa wanapoandika vichwa vya habari. Kwa mfano:
(i) Mwakyusa achaguliwa kuwa Askofu

(LENGO, Oktoba 6 - 19, 1983:1).
(ii) Tanzania yapata vifaa vya ujenzi

(UHURU, Februari 25, 1983:1).
Akifafanua sababu zinazowafanya waandishi wa habari wasitumie viakati kwenye vichwa vya habari mwanaismu mmoja aliwahi kusema:
Waandishi wa habari wanapoandika taarifa za habari bila kuonyesha viakati huwa na maana maalumu, pia huweza kuipa habari mwonjo na mguso mzito zaidi kuliko kama wangetumia viakati. Mojawapo ya malengo ya waandishi wa habari ni kuuathiri umma, upate msisimko kutokana na vichw vya habari, hatimaye uweze kupata shauku na hamasa y kusoma habari zilizopo. Mwandishi wa habari anapoacha kuandika viakati katika vichwa vya habari, huwa ham lemo la KUVURUGA SARUFI YA KISWAHILI bali huwa na nia ya kuleta taharuki ili wasomaji wafikiri kuwa yuuhwayo ai ya “wakati wa sasa” Kwa kawaida, wasomaji wa magazeti, na hasa wasomaji wa UHURU hupenda kusomajuu ya matukio ya “sasa” au “yafanyikayo sasa”. Kwa hiyo, ni muhimu waandishi wa habari wajaribu kukwepa niatunuzi ya viakati vya wakati uliopita, kwani, matumizi ya viakati vya namna hiyo humfanya msomaji afikiri kuwa habari hizo ni za zamani. Mtindo mzuri ni huo wa kudondosha viakati na kuifanya kauli isionekane kufungamana na wakati wowote. Kwa mfano, kichwa cha habari, cha “Wajadili hali ya uchumi” kinaweza kumvuta msomaji hata akafikiri kuwa, hali ya uchumi inajadiliwa sasa, kwa hiyo inafaa kuisoma habari hiyo kwani haijapitwa na wakati.
Pamoja na hayo, mwanaisimu huyo alitahadharisha na kuonya kwamba “magazeti si vyombo vya ghiliba na udanganyikfu, kwa hiyo, baada ya kuandika kichwa cha habari kisicho na kiakati, ni muhimu habari ifuatayo izingatie matumizi ya viakati kwa usahihi”. Na ukweli ni kwamba waandishi wa magazeti wamefaulu vizuri sana katika kutekeleza suala hili. Mifano hii miwili ifuatayo inatosha kudhihirisha kauli hii:
(i) Mawaziri wengi washinda uchaguzi
Mawaziri wengi wameshinda ambapo wabunge wengi wa zamani wakiwemo mawaziri wawili wawepoteza viti vyao kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi tuliyoyapokea kutoka wilaya mbalimbali...
(UHURU, Oktoba 29, 1980:1).
(ii) Tanzania Yapata Vifaa vya Ujenzi
Tanzania itapata vifaa vya ujenzi wa barabara vyenye thamani ya shilingi 39,564,385.00 chini ya mpango wa Benki ya Dunia.... Mwenyeketi wa Kampuni ya UAC, Tawi la Tanzania, Bwana P.A.J. Cole, alisema mjini Dar es Salaam jana.
(ii) Matumizi ya Vitenzi-jina Kuonyesha Wakati Ujao
Uandishi wa vichwa vya habari magazetini kwa kutumia vitenzi-jina ili kuonyesha wakati ujao vilevile hutumika sana. Mifano:
(i) Rais kwenda Nairobi leo (yaani ataondoka leo mchana)
(UHURU, Februari 17, 1983:1).
(ii) Uhuru wa Namibia kujadiliwaDelhi (yaani utajadiliwa hivi karibuni - mwezi Machi)
(UHURU, Februari 22, 1983:1).
Katika mazingira ya kawaida (yasiyo ya gazetini) kwa kawaida hatutumii vitenzi-jina kuonyesha tendo la wakati ujao, bali tunatumia kiakati balisi kinachohusiana na kazi hiyo - yaani kiakati “-ta-”.
(iii) Matumizi Makubwa ya Nafsi ya Kwanza
Hii hujitokeza zaidi kwenye barua za wuomaji wanazompelekea mhariri na kwenye hotuba za wanasiuea kwa sababu hapa kuna mwelekeo mkubwa wa mtu kuandika au kuzungumza kwa “niaba yake” mwenyewe. Mathalani:
(i) Ndugu Mhariri,
Hakika nasikitika kuhusu utumiaji wa njia ya rejista katika kutuma fedha mahali mbalimbali. Miminilituma fedha katika posta ya Kibao, wilaya ya Mufindi, kwenda....
(UHURU, Februari 24, 1983:7).
(ii) Katika makala hayahaya siku za nyuma tumepata kutoa tahadhari kuhusu matamshi ya kiserikali kuhusu sera au maelekezo kuhusiana pa masuala fulani ambayo hutolvwa mara kwa mara na viongozi mbalimbali kupitia kwenye vyorobo vya habari.
(MFANYAKAZI, Februari 9, 1983:2).
(iii) Nafurahi kuwa nanyi leo katika sherehe ya ufunguzi wa semina yenu ya Waandishi wa Kiswahili,Nimefurahi kuwa semina yenu....
(Siwale, 1980:1).
(iv) Matumizi Mapana ya Nafsi ya Tatu
Kama tunavyofahamu Jukurou la waandishi wa habari ni kutoa taarifa au ripoti za matukio mbalimbali yanayotokea nchini na nje ya nchi. Kwa kuwa matukio haya hufanywa na watu wengine, kama vile, viongozi wa Chama na Serikali wa ngazi mbalimbali, basi matumizi ya nafsi ya tatu katika kuyaripou matukio hayo hayawcsci kukwcpeka. Kwa mfano:
Rais wa Zanzibar na Mwenyekitl wa Baraza la Mapinduzi alisema jana kuwa serikali za mikoa inabidi zipewe madaraka kamili ili aweze kuteketeza wajibu wake ipasavyo kulingana na Katiba.
Ndugu Jumbe alikuwaakizungumza baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa mitano ya Tanzania Visiwani....
(MZALENDO, Februari 27, 1983:1).
(v) Matumizi ya Umoja (wa Mtendaji) kwa Maana ya Wingi (wa Watendaji) na Wingi kwa Maana ya Umoja
Huko nyuma tumewahi kudokeza kwamba katika mawasiliano kwa kutumia gazeti dhana ya uwakilishi inajitokeza sana. Yaani mwandishi anaweza kuandika jambo ai kwa niaba yake tu, bali kwa niaba ya kundi zima la watu. Katika hali hii yeye atakuwa anawawakilisha tu wenzake. Najambo hili la uwakilishi lazima lifanyike kwa sababu gazeti ni chombo “finyu” na hivyo hakina nafasi ya kutosha kwa kila mtu kutoa mawazo yake. Ili kuonyesha dhana hii ya kuwakilishana waandishi wa habari hulazimika kutumia wingi kwa maana ya umoja au kinyume chake. Kwa mfano:
(i) Chuna cha mptra nehini (PAT), juzi kilitangaza kwamba viingilio katika mchezo wa ligi ya kandanda kwenye Uwanja wa Taifa leo baina ya timu za Simba na Yanga, vitakuwa Shs.121.00, 71.00, 41.00 na 21.00 kwa watoto. Viwango hivi vipya ni vikubwa kulinganisha na viwango vya juu kabtea ambavyo viinewahi kutozwa huko nyuma. Lakini ftmakumbuka kwamba viwango vingine vya juu vya shs.101.00, 31.00 na 21.00 vilivyowahi kutozwa vilipigiwa kelete na wananchi kwamba vilikuwa juu mno.
(UHURU, Februari 12, 1983:6).
Kimsingi haya ni mawazo ya mtu mmoja, mwaodishi wa makala ya “Maoni Yetu”, lakioi anatumia wingi wa watendaji ili kumyesha kuwa yeye anayawakilteha maoni ya wapenzi wenzake wa kandanda.
(ii) Ni jambo la kutia moyo sana kuona budhi ya vyombo vya serikali vinavyohusika na suala zima la kilimo nchini, navyo mwaka huu, vimechukua hatua ya haraka ili kuhakikisha kwamba zana zote za kilimo zinamfikiamkulima katika wakati unaofaa.
(MFANYAKAZI, Januari 29, 1983:2).
Hapa “mkulima” huyu anawawakilisha wakulima wote wa Tanzania.
Fonetiki na Ortografia
(i) Matumizi Mapana ya Vifupisho na Maneno ya Mkato
Kuna tunavyofohunu mwandishi wa habari ana habari nyingi za kuandika, laldni pia ana nafasi kidogo sana gazetini. Kwa hiyo jitihada za kufupisha maandishi sharti zitiliwe mkaco. Na njia hii ni ya kawaida sana katika magazeti. Kwa mfano:
(i) Umeme kurejea sehemu kadhaDar leo

(UHURU, Januari 24, 1984:1),
(ii) Michuano ya Ligi Z'bar kuanza kesho

(UHURU, Januari 24, 1984:1),
(iii) Mabalozi kupanda mlimaK'njaro
(iv) Vifaa vya michezo virudishweBMT

(UHURU, Januari 20, 1985:12),
(v) Wakuu wa Idara za CCMwatajwa Oodoma, Kondoa

(UHURU, Januari 2, 1984:3)
Hivi ni vidiwa vya habari magazetini. Lakini, kwa kawaida vifupisho vilivyotumiwa hapa hufafanuliwa kwa kirefu/kikamilifu katika maelezo yanayofuatia vichwa hivyo vya habari. Kwa mfano, chini ya kichwa cha habari“Vifaa vya michezo virudishwe BMT”tunasoma maelezo yafuatayo:
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mjini Arusha juzi iliamuru vifaa vya midiezo vyenye thamani ya Shs.40,000.00 vilivyokuwa vimeibiwa virudishwe kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) baada ya watu wote sita wanaoshukiwa kuhusiana na wizi huo kukana kuwa vifaa hivyo si mali yao.
Hata hivyo kuna baadhi ya matumizi ya vifupisbo ambayo yanakiuka nusingi ya samfi ya Kiswahili. Mathalani, kutumia vifupisho vya Kiingereza (pengine badala ya vile vya Kiswahili) katika magazeti ya Kiswahili kuna hali fulani ya kukera na kukwaruza machoni na masikioni mwa msomaji. Kwa bahati mbaya mtindo huu mpotofu ndio ulioenea sana kwenye magazeti yote ya Kiswahili. Kwa mfano:
(i) TRC yataja nauli mpya
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limetangaza nauh mpya za abiria wa treni na meli katika maziwa pamoja na gharama za kusafirisha mizigo kuanzia keshokutwa.

(UHURU, Januari 14, 1984:1).
Swali la kuwauliza waandishi wa habari hapa ni je, ni kweli kuwa kifupisho cha Shirika la Reli Tanzania ni TRC? Tunadhani hivyo si sahihi kabisa, kwani TRC ni kifupisho cha “Tanzariia Railways Corporation”. Tunashindwa kabisa kuona sababu zozote za kimsingi zinazofanya shirika hili lisiitwe SHIRETA au SRT katika Kiswahili. Mbona Shirika la habari Tanzania limetumia kifupisho sahihi cha “SHIHATA” na watumiaji Kiswahili wote tumeridhika nacho.
(ii) Kipo kitambaa cha kutosha - TEXCO

(UHURU, Januari 10, 1984:1).
Hapa tumeelezwa kuwa TEXCO ni kifupisho cha Shirika la Nguo la Taifa!
(iii) A.T.C. kununua 'Boeng' ya 3

(UHURU, Januari 6, 1984:1).
Hapa inadaiwa kuwa A.T.C. ndicho kifupisbo cha Shirika la Ndege la Tanzania.
Pamoja na mtazamo huo kuna baadhi ya vifupisho, hasa vya mashirika makubwa ya kimataifa, ambavyo vinaonekana kama kwamba “vimekubaliwa” vitumike kama vilivyo katika lugha ya Kiingereza bila kubadilishwa, kwa mfano UNESCO, UNICEF na kadhalika. Lakini hata hapa sahihi zaidi ingekuwa kuviandika vifupisho hivi kwa tahijia ya Kiswahili, kama vile “YUNESKO”. Kifupisho cha namna hii ni rahisi kusomeka na kutamkika katika Kiswahili badala ya kile cha UNESCO ambacho ni cha Kungereza. Magazeti y Kirusi, kwa mfano, yanaandika vifupisho vya namna hii kwa kutumia tahijia ya lugha ya Kirusi (kwa Kirusi UNESCO huandikwa I-OHECKO).
(ii) Kuandika Neno la Kwanza la Aya ya Kwanza Katika Herufi Kubwa
Imedhihirika kwamba karibu katika magazeti yote ya Kiswahili neoo la kwanza la kila aya ya kwanza huaadikwa kwa herufi kubwa. Ni tearifa chache sana ambazo hazifuati utaratibu huu. Tunafikiri sababu kubwa ya kufanya hivi ni kunadhifisha maandishi ya gazetim. Kwa mfano:
(i) Madaftari yakosa wanunuzi
SHIRKA la Vifaa vya Elimu Tanzania (T.E.S.) tawi la Mkoa wa Rukwa, limelalamika kalundikana kwa madaftari 483,400 yenye thamani ya Shs. 1,079,960.00 kwenye ghala lake lilitopo mjini Sumbawanga.

(MFANYAKAZI, Januari 28, 1964:1).
(ii) Ojok afa kwa ajali
MKUU wa Utawaia katika Jeshi la Uganda, Meja Jenerali David Oyite Ojok amekufa katika ajali ya helikopta, Makamu wa Rais wa Uganda, Ndugu Paulo Muwanga alitangaza kwa njia ya Redio Uganda jana.

(MZALENDO, Desemba 4, 1983:1).
(iii) Halmashauri Kuu yaendelea
KIKAO cha dharura cha Halmashauri Kuu ya Taifa chiiu ya Mwenyekiti wa Chama, MwaHmu Nyerere leo kinaingia siku yake ya tano mjini hapa (Dodoma) kujadili hali ya hewa ya kisiasa iliyochafuka ya Muungano wa Tanzania Bara na Visiwani.

(UHURU, Januari 28, 1984:1).
Katika maandishi ya mitindo mingine hatuliandiki neno la kwanza kadka aya ya mwanzoni kwa herufi kubwa. Hii ni “fasheni” ya gazetini tu.
(iii) Kawaida ya Kuonyesha idadi ya Vitu kwa Namba Iliyokamili
Kwa kawaida ripoti za magazetini zinapohusu idadi fulani ya vitu, basi idadi hiyo kwenye kichwa cha habari hutajwa kwa tarakimu zilizo kamili (kwa Kiingereza tungesema: in round figures). Idadi inayotajwa kwenye hicho kichwa cha habari aghalabu huwa pungufu kidogo ikilinganishwa na idadi halisi inayotolewa katika maelezo yanayofuatia kichwa cha habari. Mtindo huu vilevile unaepusha ubadhirifu wa muda na nafasi katika gazeti. Mifano:
(i) Tumbaku yaingiza sh. milioni 35
WAKUUMA wa tumbaku mkoani Iringa wamepata jumla yashs.35,367,886.00 kutokana na mauzo ya karibu tani miliom 1.8 za tumbaku katika msimu wa 1982/83.
(UHURU, Novemba 7, 1983:1).
(ii) Tanesco yapata milioni 509.6/-
SHIRIKA la Umeme (TANESCO) lilipata shs.509,628,362.00 kutokana na mauzo ya umeme mwaka 1981 kulingamsha na sh.479,966,410.00 mwaka 1980, ripoti ya Shirika hilo kwa 1981 inaeleza.
(UHURU, Desemba 19, 1983:5).
Miundo ya Sentensi
Miundo ya sentensi zinazotumiwa katika mtindo wa magazetini (hasa zile za vidiwa vya habari) inatofautiana sana na sentensi zinazotumiwa katika mazingira ya kawaida. Baadhi ya sifa bainifu za sentensi hizi ni hizi zifuatazo:
(i) Matumizi Mapana ya Sentensi za Vitenzi-jina
Sentensi za vitenzi-jina hutumiwa sana katika vichwa vya habari. Mifano:
(i) Sare ya marudufu kutumiwa kwa muda (UHURU, 25 Januari, 1984:1).
(ii) Kamati Kuu kukutana Dodoma (MZALENDO, 4 Desemba, 1983:1).
Sababu kubwa ya matumizi ya vitenzi jina ni kuwezesha kukwepa utumiaji wa viakati ambao umuhimu wake tayari tumeshaueleza.
(ii) Muundo Maalum wa Sentensi Zinazoashiria Mwito
Mifano:
(i) Zingatieni bajeti - Sokoine (UHURU, 24 Januari, 1984:1).
(ii) Mabald ya walanguzi yafagiliwe - Nyang'anyi (MZALENDO, 4 Desemba, 1984:1).
(iii) Mwito kuepuka mgongano (UHURU, 28 Januari, 1984:5).
Miundo ya sentensi ya namna hii kusema kweli tunaipata katika magazeti tu. Katika mazingira ya kawaida tungesema mathalani, “Sokoine ametoa mwito wa kuzingatia bajeti”. Miundo tuliyoitoa inafanya taarifa iwe fupi na isichukue nafasi kubwa gazetini.
(iii) Matumizi Mapana ya Sentensi Zinazotegemeana na Kujalizana
Mifano:
(i) Mwalimu asisitiza: Umoja ndio njia ya ukombozi (UHURU, 20 Januari, 1983:1).
(ii) Ligi ya Taifa: Coastal yajiimarisha zaidi (MZALENDO, 27 Februari, 1983:8).
(iii) Kesi ya uhaini: Washitakiwa watajwa (UHURU, 26 Februari, 1983:1).
Katika miundo hii maalum ya sentensi sehemu ya kwanza ya sentensi peke yake haiwezi kutoa dhana ya taarifa inayokusudiwa kutolewa. Taarifa inayotakiwa kuelezwa itakamilika iwapo tu tungo hizi mbili zitatokea pamoja na kuunganishwa. Kimsingi lengo la sentensi za namna hii ni kutoa “muhtasari” wa taarifa inayofuatia kichwa cha habari. Kwa mtu atiye na haraka inatosha tu kusoma muhtasari huo wa habari na akajua kuna matukio gani muhimu katika jumuiya anamoishi.
(iv) Matumizi Makubwa ya Sentensi za Ripoti Zenye Mpangilio Maalum
Kwa kawaida sentensi za namna hii aghalabu huonyesha tukio lililofanywa, mahali tukio hilo lilipotokea, na aliyelifanya tukio hilo.
Kwa mfano:
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imefanikiwa kueneza huduma za benki kwa wananchi, Mwenyekiti na Mkunigenzi Mtendaji wa NBC, Ndugu Amon Nsekela, alisema mjini Dar es Salaam jana.
Akizungumza kwenye kuamu ya chakula cha mchana katika hotdi y Kilimanjaro kwa ajili ya kutoa ripoti ya mwaka ya NBC, Ndugu Amon Niekela, aluema mwaka 1981/82 ulikuwa wa mafanikio kwa Benki hiyo, lakini akaongeza kuwa Benki bado haijaridhishwa na mafanikio hayo. (UHURU, 26 Februari, 1983:1)
Mpangilio wa namna hii hatuutumii katika mazungumzo na maandishi ya kawaida yasiyo ya gazetini.
(v) Matumizi ya Sentensi za Mkato
Ili kupunguza ubadhirifu wa nafasi katika magazeti waandishi wa habari wakati mwingine hutumia sentensi za mkato katika kuandika vichwa vya habari.
Kwa mfano:
(i) Hatimae... (MFANYAKAZI, 19 Februari, 1983:1).
Matatizo Katika Mtindo wa Magazetini
Pamoja na huduma nzuri inayotolewa na magazeti ya Kiswahili kwa wananchi, uchunguzi umeonyesha kuwa kuna matatizo kadha ambayo yanapunguza ubora wa huduma hii. Baadhi yao ni:
(i) Uingizaji wa Maneno ya Kiingereza Magazetini
Baadhi ya waandishi wa habari bado wanaenddea na mazoea ya kutumia maneno ya Kiingereza katika taarifa zao za Kiswahili. Hali hii sio tu inakiuka misingi ya kisarufi, bali inaonyesha vilevile udohoudoho wa lugha ya Kiswahili, jambo ambalo si dhahiri kabisa.
Angalia, kwa mfano, taarifa ifuatayo iliyotolewa na gazeti la MFANYAKAZI la tarehe 29 Januari, 1983 ukurasa wa 8 inavyotumia maneno ya Kiingereza bila kuonyesha wasiwasi wowote wa mwandishi:
Spea Zadokolewa Ujenzi Dar es Salaam
SPEA za magari ya Idara ya Comworks (Ujenzi) Mkoani Pwani yasemekana zimekuwa zikipotea mara kwa mara kutoka kwenye Yadi ya Idara hiyo bila kumbukumbu nzuri.
Afisa mmoja wa Comworks amesema kwamba 'Alternators,Vioo vya Landrover, Air compressors, Injector Pumps naMotor Starters' ni miongoni mwa spea ambazo yasemekana zimekuwa zikipotea kutoka kwenye Yadi hiyo ya Barabara ya Pugu katika siku za hivi karibuni.
Bila shaka watumiaji wa Kiswahili wengi tutakerwa sana na hali ya namna hii katika maeazeti va Kiswahili.
(ii) Kutokuwepo kwa Sera Thabiti ya Kuandika Majina ya Kijiografia
Hadi sasa hakuna sera rasmi iliyotolewa kuhusu uandikaji wa majina ya kijiografia. Majina hayo ni pamoja na majina ya nchi, miji, mito n.k. Inavyoonekana majina haya ama huandikwa kwa kutumia alfabeti za Kiingereza (yaani kama yanavyosomeka kwa Kiingereza) ama jina la Kiingereza na lile la Kiswahili huchukuliwa kama visawe vinavyoweza kubadilishana nafasi wakati wowote. Kwa mfano, katika magazeti ya Kiswahili tumewahi kusoma: Seychelles na Shelisheli.
Kwa kweli hakuna sababu zozote za kimsingi zinazowafanya waandishi wa habari wa magazeti ya Kiswahili waandike:
Nigeria
-
badala ya Naijeria
Morocco
-
badala ya Moroko
Canada
-
badala ya Kanada
Ouagadougou
-
badala ya Wagadugu
Culcutta
-
badala ya Kalkata
London
-
badala ya Landani
Nile
-
badala ya Naili
Iwapo taarifa tunazoziandika ni kwa ajili ya magazeti ya Kiswahili, basi ni busara zaidi kuziandika taarifa hizo katika Kiswahili safi - fkiwa ni pamoja na majina ya kijiografia.
Tena yaelekea waandishi wa habari wenyewe hawana msimamo thabiti kuhusiana na suala hili la kutumia majina ya Kiswahili au ya Kiingcreza. Kwa mfano, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani hufiipishwa kama JKU, lakini Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani sikn zote hufupishwa kama FRG. Sababu za kufanya hivi hazieleweki.
(iii) Kutumia Kiswahili cha Tafsiri za Dhana za Kiingereza
Kutokana na kuathiriwa na lugha ya Kiingereza wakati mwingine waandishi wa habari hupotosha kabisa dhana ya taarifa zao za Kiswahiti kwa sababu ya kutafsiri dhana hiyo kutoka lugha ya Kiingereza. Kwa mfano, kwenye gazeti la UHURU la tarehe 30 Januah, 1984 ukurasa wa 1 chini ya kichwa cha habari kisemacho “Afariki katika ajali” tunasoma taarifa ifuatayo:
MTU mmoja alikufa papo hapo na wengine 73 kujeruhiwa wakati lori walilokuwa wakisafiria lilipopinduka katika makutano ya njia ya reli na barabara itokayo Mwanza kwenda Shinyanga mjini juzi jioni.
SHIHATA imeripoti kuwa majeruhi hao pamoja na mtu aliyekufa aliyetambuliwa kwa jina la Mathias Kasula (27) wa kijiji cha Uzogolewalikimbizwa hospitali ya mkoa wa Shinyanga ambako wote walilazwa kutokana na majeraha makubwa.
Katika muktadha huu “kukimbizwa hospitali” maana yake ni kufukuzwa (tena kwa mbio) kutoka hospitali - jambo ambalo haikuwa nia ya taarifa hii. Lengo la taarifa hii ilikuwa kutujulisha kwamba majeruhi hao walipelekwa kwa haraka hospitalini. Hapa bila shaka mwandishi alipotoshwa na dhana ya Kiingereza ya“to be rushed to the hospital”.
Mfano mwingine tunaweza kuusoma kwenye gazeti la UHURU la tarehe 25 Januari, 1983 uk. 7 ambamo chini ya kichwa cha habari “Usalama wa abiria uangaliwe sana”, polisi wa idara ya reli(railway police) walifasiriwa kuwa “polisi-reli”.
Kuwepo kwa Mchanganyiko wa Sifa za Mtindo wa Kitaaluma na Mtindo wa Kirasimu Katika Mtindo wa Magazetini
Baadhi ya wanaelimumitindo wametoa hoja kuwa katika mtindo wa magazetini kuna mpenyezo wa kutosha wa sifa za mtindo wa kitaaluma na zile za mtindo wa shughuii za kirasimu. Kauli hii ni kweli kabisa na mchanganyiko wa namna hii unajitokeza kwa sababu gazeti ni chombo cha umina na hivyo hata wataalarnu na viongozi wa serikali wa ngazi mbalimbali wakati mwingine hutoa taarifa zao kupiiia chombo hiki. Maoni kama vile ya wahariri, utabiri wa hali ya hewa, taarifa za maendeleo ya viwanda na kadhalika lazima yatumie mtindo wa kitaaluma ambapo taarifa kama vile za mahakama, matangazo ya mikutano, matangazo ya minada, ya nafasi za kazi, ya upoteaji wa pasipoti na kadhalika yanabidi yaandikwe kwa mtindo wa kirasimu.
Kwa hali hii ni kweli kwamba katika magazeti kuna maingiliano ya mitindo hii tofauti, lakirii maingiliano haya sio ya kiholela. Yana misingj na taratibu zake maalum.
Hitimisho
Katika sura hii tumejaribu kuonyesha dhana ya mtindo wa magazetini na shughuli za kisiasa kulingana na mtazamo wa kielimu-mitindo. Tumeonyesha kwamba kihistoria jukumu kuu la kwanza la gazeti Ulikuwa kutoa habari kwa haraka iwezekanavyo kabla hazijazeeka. Lakini baadaye gazeti lilijiongezea majukumu Ukawa jukwaa la kupigia propaganda, la kuelezea itikadi za vyama na serikali. Ni kutokana ha hali hiyo ndio maana gazeti lazima liwe chombo ama cha chama, aiha cha serikali, ama cha jumuiya fulani, mathalani Jurnuiya ya Wafanyakazi. Gazeti pia rii chombo cha kuelimisha umma na kusambaza habari mpya za uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia.
Kutokana na dhima hii kubwa ni dhahiri kwamba mawasiliano yanayotumia chombo hiki hayawezi kufanywa kiholela, bali kwa kufuata kanuni na taratibu maalum. Kanuni na taratibu hizi, pamoja na sifa za mtindo huu wa magazetini zimejadiliwa kwa kirefu katika sura hii.
Ni matumaini yetu kuwa hoja zilizojengwa hapa zitasaidia kuongeza ubora wa mawasiliano ya magazetini na ya shughuli za kisiasa.
Sasa hebu tuuangalie mtindo wa mawasiliano yasiyo rasmi, ambayo ni mada ya sura ifuatayo.
Mashele blog