Sura ya 3: Mtindo wa kirasimu

Utangulizi
Taaluma ya lugha tayari imeshatudhihirishia kwamba ili mtu aweze kushiriki kwa ufasaha zaidi katika mawasiliano kwa kutumia lugha fulani, haitoshi tu kwa mtu huyo kuwa na msamiati mkubwa na kuifahamu sarufi ya lugha hiyo, bali muhimu zaidi ni kujua jinsi ya kuzitumia zana hizi za kiisimu, jinsi ya kuyaambatisha maneno na semi kadha wa kadha na mazingira maalum ya matumizi.
Kiswahili, ikiwa ni lugha ya taifa, kinatumika sana kama njia ya mawasiliano katika nyanja nyingi za shughuli za kiserikali. Mojawapo ya nyanja iliyofaulu sana kukipenyeza Kiswahili karibu katika mawasiliano yake yote ni ile ya urasimu. Mawasiliano mengi katika ofisi za serikali, za Chama, za jumuiya, mahakama (za mwanzo) na mahali pengine pa kazi yanatekelezwa kwa kutumia Kiswahili.
Mawasiliano haya hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na kanuni maalum zilizojitokeza na kujishamirisha katika mazingira haya kutokana na kutumiwa kwake kwa muda mrefu kwenye mazingira yaleyale. Kwa maneno mengine zana za kiisimu zilizopo hapa hutumiwa kwa mpango maalum.
Na kwa kuwa taratibu na kanuni hizi huenda hazitambuliwi kwa uwazi zaidi na baadhi ya hao wanaozitumia, ni nia ya sura hii kuzichambua kwa undani zaidi taratibu na kanuni hizi kwa lengo la kuongeza upeo wa ufasaha katika mtindo wa kirasimu.
Mawasiliano ya Kirasimu
Mtindo wa urasimu ni ile namna ya mawasiliano yanayotumika:
1. katika mazungumzo na maandishi yaliyo rasmi maofisini au mahali popote pa kazi;
2. katika mahakama na mawasiliano mengineyo ya kisheria;
3. katika mawasiliano ya kidiplomasia;
4. katika mikataba, katiba, matini za sheria, maazimio, miongozo, maagizo na amri (za kiserikali) na hati mbalimbali zinazoandikwa baina ya ofisi na ofisi k.v. barua, matangazo (ya semina, mikutano, tanzia n.k.), nyaraka (au sekula) n.k.;
5. katika kumbukumbu na ripoti za mikutano, vikao n.k.
Kwa ujumla mtindo wa kirasimu ni mtindo wa mawasiliano katika nyanja za utawala, uendeshaji wa uongozi pamoja na masuala ya kisheria. Mawasiliano haya yanaweza kutekelezwa kwa njia ya maandishi na/au mazungumzo.
Sifa za mtindo wa kirasimu:
Hapa tutatofautisha sifa za aina mbili: zisizo za kiisimu na zile za kiisimu.
Sifa zisizo za kiisimu:
Hizi ni sifa ambazo haziambatani moja kwa moja na zana za kiisimu zinazotumika katika kutekeleza mawasiliano. Baadhi ya sifa hizi ni:
(i) Usahihi wa Mambo Yanayojadiliwa
Katika mawasiliano ya kirasimu suala la usahihi na ukweli wa mambo yanayojadiliwa ni muhimu sana. Mfumo wa lugha ihayotumika katika matini za sheria, kwa mfano, ni ule unaosisitiza kabisa usahihi ili kujaribu kuzuia ufafannzi unaogongana na sheria hizo. Haraka ya kulieleza au kulielewa jambo katika mfumo huu haitiliwi maanani sana. Na hii ni kweli; kwani ni mara ngapi tumeona wanasheria wakiisoma sheria moja kwa kurudiarudia mara mbili au tatu au hata zaidi bila kujali muda mrefu wautumiao katika kufanya hivyo? Tuangalie, kwa mfano, mahojiano yafuatayo:
Wakili wa Utetezi:
Nakuuliza jaribio la kutaka kupindua serikali litakuwa kosa la namna gani katika sheria za Kenya?
Kamishina Msaidizi:
(Baada ya kupewa kitabu cha sheria za Kenya na kukisoma) Ni kosa la uhaini.
Wakili wa Utetezi:
Ulichukua muda mrefu kufikia jibu hili. Washitakiwa wawili hawahusiani na makosa haya?
Kamishina Msaidizi:
Sijui.
(UHURU, 26 Agosti 1982:4, mikazo ni yangu).
Hali kadhalika wakili anaweza kutumia muda mrefu sana kujieleza na wala asijali kabisa afanyavyo hivyo. Katika kesi tuliyodondoa hapojuu kwa mfano, wakili wa utetezi alitumia saa nne (!) kutoa maelezo yake ya kuiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam kutupilia mbali ombi la Kenya kutaka irudishiwe askari hao wawili waliowateka wenzao. (UHURU, 17 Septemba 1982:1).
Na hali hii ya kutumia muda mrefu saha kujieleza mahakamani haitokei kwa wanasheria tu, bali kwa mtu yeyote yule. Mathalani kwenye kitabu cha Rwezaura (1981:52) tunasoma hivi:
Katika shauri la Mussa V. Chausiku bint Omari, Daawa la Mahakama Kuu ya Tabora Na. 248/73, Chausiku bint Omari alidai talaka katika Mahakama ya Mwanzo ya Usoke, Tabora, kwa sababu ya ukatili wa mume wake. Mdai alitoa ushahidi wake kwa muda wa siku mbili mfululizo... (msisitizo wangu).
Chausiku si mwanasheria, ni msichana wa kawaida kabisa wa kijijini. Lakini mazingira ya mahakamani na mfumo wa lugha inayotakiwa kutumika hapo vilimlazimisha achukue muda mrefu kiasi hicho ili ajieleze na kueleweka vizuri.
Hali kama hii ni ya kawaida kabisa katika mahojiano ya mahakamani. Hapo kwa kawaida hakuna haraka. Muhimu ni kila mtu (hakimu, mwendesha mashitaka, wakili, mdaawa, shahidi n.k.) kujieleza kinaganaga bila kujali sana urefu wa muda anaotumia, almradi tu kile anachokieleza kieleweke barabara.
(ii) Kuwepo kwa Mantiki Katika Jambo Linalojadiliwa
Kama ilivyo katika mtindo wa kitaaluma mawasiliano katika shughuli za kirasimu hayafanywi ovyoovyo tu bila kufuata mpangilio maalum wa matukio, bali hufuata mtiririko maalum unaoleta maana kamilifu. Mahojiano ya mawakili katika mahakama kwa mfano, hutiririka kwa kufuata mantiki fulani. Vivyohivyo tuandikapo barua za kiofisi mtiririko wa mawazo yetu hufuata mpangilio wa namna fulani ambao ni lazima ufuatwe na kila mwandishi ili kusadifu taratibu na kanuni za uandishi wa barua za aina hii.
(iii) Kawaida ya Kueleza Mambo kwa Kutumia Mbinufanani
Kwa kawaida katika mtindo wa kirasimu kuna matumizi makubwa ya namna fulani ya “klishe” (mihuri ya zana za kiisimu) zilizotayari na zinazorudiwarudiwa sana bila kubadilishwa. Mathalani, tuandikapo barua za kiofisi aghalabu hujikuta sote tunatumia klishe zilezile zilizokwisha shamiri katika mawasiliano ya namna hii. K.m. Ndugu; Kuhusu: “.....” husika na somo la hapo juu; husika na kichwa cha habari hapo juu; rejea barua yako (yahgu) kumbukumbu Na. ............; Asante; Wako mtiifu; Wako katika ujenzi wa taifa; ... n.k.
Aidha matumizi ya fomu maalum zenye nafasi za kujazwa na wahusika ni mfano mzuri wa kutumia zana za kiisimu zinazofanana za kueleza mambo.
Sifa za Kiisimu
Hizi ni zile sifa zinazoambatana na zana za kiisimu na kujitokeza katika msamiati, sarufi maumbo fonetiki na miundo ya sentensi inayotumika.
Msamiati
Pamoja na matumizi ya ule msamiati wa jumla ambao hutumika karibu katika mitindo yote, upo baadhi ya msamiati unaotumika katika mawasiliano ya kirasimu wenye sifa kadha za kipekee. Sifa hizi ni pamoja na:
(i) Matumizi Makubwa ya Istilahi (Maalum) za Kirasimu
Istilahi hizi hasa zinahusu mambo ya ofisini, ya kisheria na diplomasia k.m. uteuzi, waraka, mkataba, posho ya maili, taarifa, azimio, agizo, amri, mirathi, wahazili, mhuri, kumbukumbu, faili, unyumba, shauri, daawa, batili, mfaruku, mtalikiwa, maharimu, madaraka n.k.
(ii) Matumizi Mapana ya Msamiati Unaoonyesha Vyeo au Nyadhifa za Watu
K.m. Rais, Waziri Mkuu, Mwenyekiti, Katibu, Mkurugenzi, Jaji, Mwanasheria Mkuu, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mkuu wa Chuo, Jaji Kiongozi, Afisa Mkuu Taaluma, Mchunguzi Mwandamizi, Daktari, Karani, Mratibu, Mhasibu, Mhazili, Balozi, Mwambata n.k.
(iii) Kutotumika (Kabisa) kwa Misimu, Nahau, Mafumbo, Lahaja na Maneno Mguso
Hii ni mojawapo ya sifa hasi za msamiati unaotumika katika maandiko na mazungumzo ya kirasimu. Shughuli za kirasimu kwa kawaida zinahitaji matumizi ya msamiati ulio wazi kabisa na wa kudumu na usioleta mguso sana. Kwa mfano katika ibara ya 19, kifungu na. (2) ya Katiba ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tunasoma yafuatayo:
Ni mwiko kwa kiongozi kupokeamapato ya kificho au rushwa au kushiriki katika mambo yoyote ya magendo. (Katiba ya CCM 1982:18).
Katika matini hii haingefaa kabisa kutumia misimu “chauchau” au “chai” badala ya mapato ya kificho au rushwa, kwani hii ni matini rasmi ya kisheria na ya kudumu. Misimu, ambayo ni maneno ya kupita tu, haiwezi kutumika katika uandishi wa Katiba. Hali kadhalika nahau, mafumbo na lahaja haziwezi kutumiwa kwenye matini rasmi (mfano mikataba, katiba, sheria n.k.) kwa sababu zina utata katika fasiri zake na katika kuzielewa maana zake.
(iv) Kawaida ya Vifungu Vingi vya Maneno Kuwa na Visawe Katika Lugha ya Kawaida ya Kila Siku
Imeonekana kuwa maneno mengi au vifungu vingi vya maneno yanayotumika yakiwa na “kivuli” cha urasimu huwa na visawe (synonyms)vyake katika lugha ya kawaida ya matumizi ya kila simu. K.m.
Matumizi Rasm iya Kirasimu
Matumizi ya Kawaida
kabiliwa na mashitaka
shitakiwa.
patikana na hatia
kosa, wa na hatia.
mwingilia mke wako
lala naye, yaani fanya mapenzi naye.
kutwanakosa
wanakosa.
kwendajela
fungwa (gerezani)
kwamujibuwa
kufuatana na
dhifa (ya taifa)
tafrija, karamu
shambulio la kawaida
kipigo (k.m. mtu kumpiga mwenzie).
tembea (na mke wa mtu)
fanya mapenzi (na mke wa mtu).
toa shukrani (pongezi) za dhati
shukuru (pongeza) sana.
kuwa ndani
kuwarumande.
Kuyatumia maneno haya yenye kivuli cha urasimu katika mazingira ya kawaida (yasiyo rasmi) kutakuwa ni kosa kimtindo na matokeo yake ni kuleta kichekesho. Mathalani, itakuwa kichekesho kumkaribisha rafiki yako nyumbani kwa tafrija ndogo na ukasema eti umeandaa dhifa. Hali kadhalika kumweleza mkeo nyumbani: “kwa taadhima kubwa nakutolea shukurani zangu za dhati kwa...” kunachekesha. Kwa kawaida katika mazingira haya tunasema: “nakushukuru sana mke wangu kwa...”
(v) Matumizi ya Istilahi (Maneno) Zikiwa Katika Jozi za Mhalafa (Vinyume)
Baadhi ya maneno yanayotumika katika mtindo huu hujitokeza katika jozi za mhalafa. Kwa mfano:
wakili wa upande wa utetezi
- wakili wa upande wa mashitaka
mlalamikaji
- anayelalamikiwa (yaani mshitakiwa)
mshitaki
- mshitakiwa
mdai
- mdaiwa
haki
- wajibu
demokrasia
- udikiteta
mwendesha mashitaka
- wakili
mpangishaji
- mpangaji
mume
- mke
(tukizichukulia kama istialhi za sheria).
(vi) Matumizi ya Maneno ya Zamani/Kale na Yale Yanayoambatana na Historia
Ni hali ya kawaida katika shughuli za kirasimu hasa katika nyanja za sheria na diplomasia kutumia maneno ambayo kwa sasa, kulingana, kwa mfano, na hali ya Tanzania, tungesema yameshapitwa na wakati au yanatukumbusha enzi fulani za kihistoria zilizokwishapita. Mifano ya maneno ya aina hii ni: Mtukufu (Rais); Mheshimiwa (Mbunge), Chifu, Bwana, Mtemi, Moses S/o Kauzibe, Chausikud/o Omari. Baadhi ya maneno haya hutumika sana kwenye mazungumzo au dhifa za kiserikali katika kuwataja wageni mashuhuri wanaoitembelea nchi yetu.
Hata uandikaji wa baadhi ya maneno katika mtindo huu huwa na hali ya ukale. Kwa mfano, uandishi wa maneno aina ya: yeyote, wowote, vilevile, popote n.k. katika matini nyingi za kiofisi (mfano Katiba) bado unafanywa kwa njia ya kizamani inayoyatenga maneno haya katika makundi mawili: ye yote, wo wote, vile vile, po pote, ko kote, (Taz. Katiba za TANU na CCM).
Sarufi Maumbo
Baadhi ya sifa za kisarufi maumbo zinazoupambanua waziwazi mtindo wa kirasimu ni hizi zifuatazo:
(i) Matumizi mapana ya nomino zinazotaja watu kufuatana na uhusiano wao wa muda katika shughuli fulanifulani, kwa mfano: mshitakiwa, shahidi, mpangaji, mdai/mlalamikaji, mlezi, mkopaji n.k.
(ii) Matumizi Makubwa ya Nomino Kuliko Viwakilishi
Katika mtindo wa mawasiliano ya kirasimu aghalabu hutumika zaidi nomino kuliko viwakilishi vyake. Ili kuzuia uwezekano wa mambo kutoeleweka vizuri kwa kawaida nomino hazibadilishwi na kuwa viwakilishi hata kama nomino hizo zimo katika sentensi zinazokaribiana (zinazofuatana). Badala yake nomino hizi hurudiwarudiwa ili kuifanya taarifa iwe wazi kabisa na kueleweka na kila mmoja kwa urahisi.
Mfano: 11. Maombi ya uwanachama yatafikiriwa kwanza na Halmashauri Kuu ya Tawi. Halmashauri hiyo itapeleka mapendekezo yake katika Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya ambayo tawihilo limo. Uamuzi wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya ndio utakuwa wa mwisho kuhusu kukubaliwa au kukataliwa kwa ombi Jolote la kuwa mwanachama, lakini mwombaji aliyekataliwa anaweza kuomba tena. (Katiba ya CCM, 1982:13).
(iii) Matumizi Mapana Sana ya Vitenzi-jina (infinitives)
Uchunguzi umeonyesha kuwa katika mtindo wa kirasimu kuna matumizi makubwa sana ya vitenzi-jina ikilinganishwa na hali ilivyo katika mitindo mingine yote. Na jambo hili halikutokea bila sababu maalum. Vitenzi-jina vinajitokeza sana katika mtindo huu kwa sababu mawasiliano katika mazingira haya yana mwelekeo zaidi wa “kinguvunguvu” - yaani kueleza matakwa ya serikali, vyama, sheria n.k. kwa wananchi. Mawasiliano ya namna hii yanatekelezeka vizuri zaidi kwa kutumia vitenzi-jina. Kwa mfano:
(1) II Madhumuni ya CHAWATA yatakuwa:
1. Kukuza na kuratibu utafiti wa taaluma ya sanaa ya kutafsiri kwa njia ya:
Kuandaa mikutano ya mara kwa mara na semina ili kutoa fursa ya kubadilishana mawazo na kuchochea hamasa kwa wachunguzi katika uwanja wa tafsiri.
ii Uchapishaji wa jarida na makala nyingine zifaazo.
2. Kusaidia watu binafsi, vyama, mashirika ya kimataifa na Idara mbalimbali za serikali katika kuwapata wafasiri na wakalimani wenye sifa zifaazo.
(Katiba ya Chama cha Wafasiri wa Tanzania (CHAWATA), 1982:1).
Kimsingi sio “CHAWATA yenyewe” itakayotekeleza madhumuni haya, bali wana-CHAWATA. Hivyo CHAWATA hapa inawataka tu na kuwahimiza wana-CHAWATA wayatekeleze madhumuni hayo.
Angalia pia:
5. Kwa hiyo lengo na madhumuni ya Chama yatakuwa kama ifuatavyo:
(1) Kulinda na kudumishaUhuru wa nchi yetu na raia wake.
(2) Kujenga Ujamaa kwa msingi wa kujitegemea.
(3) Kuhakikisha kwamba shughuli zote za umma zinaendeshwa chini ya uongozi na usimamizi wa Chama.

(Katiba ya CCM, 1982:6 - 7).
(iv) Matumizi Maalum ya Wakati Ujao
Katika maandishi ya katiba wakati mwingine wakati ujao kimsingi huwa na maana ya wakati uliopo. Kwa mfano:
JINA:
Jina la Chama litakuwa Chama cha Wafasiri wa Tanzania, kwa kifupi/CHAWATA/. Jina la Chama kwa Kiingereza litakuwa The Tanzania Association of Translators, kwa kifupi/T.A.T/.
II MALENGO:
Madhumuni ya CHAWATAyatakuwa: ......

(Katiba ya CHAWATA, 1982:1)
Kusema kweli kimsingi taarifa hii inatueleza kuwa jina la Chama ni CHAWATA na kwamba madhumuni yake ni hayo yafuatayo. Yaani taarifa imezingatiwa katika wakati uliopo, sio ujao.
Fonetiki na Ortografia
(i) Tahijia na Matamshi Kufuata Taratibu za Sarufi
Kama ilivyo katika mtindo wa kitaaluma maneno mengi katika mtindo wa kirasimu kwa kawaida huandikwa na kutamkwa kikamilifu kwa kufuata taratibu na kanuni za kisarufi. Endapo kuna haja ya kutumia vifupisho, hasa vile vya vyama, mashirika, kampuni, viwanda n.k. basi ni vile tu vilivyokubaliwa rasmi ndivyo vinaweza kutumiwa, tena baada ya kuandika au kutaja kwanza majina yao kamili, k.m.
Chama cha Mapinduzi (CCM),
Umoja wa Vijana (VIJANA),
Umoja wa Wanawake wa Tanzania (U.W.T.),
Umoja wa Wazazi (WAZAZI),
Jumuiya ya Wafanyakazi wa Tanzania (JUWATA),
Muungano wa Vyama vya Ushirika (WASHIRIKA),
Kiwanda cha Zana za Kilimo cha Ubungo (KIZAKU),
Shirika la Habari la Tanzania (SHIHATA).
Kuandika au kutaja jina kamilifu la Chama au Shirika kwa Kiswahili na halafu kuweka kifupi chake kwa kukitumia kifupi cha Kiingereza cha Chama au Shirika hilo ni kukiuka taratibu za kisarufi, na hivyo ni kosa. Kwa mfano, ni makosa kuandika: Mamlaka ya Kahawa Tanzania (C.A.T.) kwa sababu C.A.T. sio kifupi cha Mamlaka ya Kahawa Tanzania, bali ni kifupisho cha “The Coffee Authority ofTanzania”. Na kwa bahati mbaya makosa ya namna hii yameenea sana katika mawasiliano ya kirasimu na hata katika vyombo vyetu vingi vya habari.
Aidha majina ya watu katika mawasiliano ya kirasimu lazima yawe makamilifu na aghalabu hutanguliwa na majina ya vyeo au nyadhifa zao (ambazo pia huandikwa na kutamkwa kikamilifu), pamoja na neno “Ndugu” au “Mheshimiwa” (kama anayetajwa ni Mbunge).
Kwa mfano Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Ndugu XYZ.
Kulingana na hoja hii itakuwa kichekesho kuwasikia mathalani, watoto wa Ndugu XYZ (au hata mkewe) wakimwita baba yao katika mazingira ya kinyumbani “Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Ndugu XYZ”... Mazingira ya namna hii yanahitaji Ndugu XYZ aitwe “baba” tu, au “baba fulani” - kwani haya si mazingira rasmi ya kirasimu.
Kwa hiyo basi kuandika au kuita majina ya watu, nchi, miji n.k. kwa kukatiza kama vile:
Tz
-
badala ya Tanzania,
Moro
-
badala ya Morogoro,
Z'bar
-
badala ya Zanzibar n.k.
katika taarifa za kirasimu hakuwezi kuchukuliwa kuwa ni sahihi.
Hata hivyo hii haina maana kuwa vifupisho (au maneno ya mkato) havitumiki kabisa katika mtindo wa mawasiliano ya kirasimu. Kuna baadhi ya vifupisho, hasa vya mashirika ya kimataifa ambavyo kwa tabia yake vimezoeleka kutumika kama vilivyo katika lugha mbalimbali duniani, k.m. UNESCO, UNICEF, n.k. Aidha ili kuharakisha mawasiliano, kwa mfano, baina ya viongozi katika Idara, Kurugenzi, Taasisi moja n.k. viongozi hao wanaweza kubuni vifupisho fulani vya kutumia katika mafaili na hati zao na wakaokoa muda mwingi na kupunguza matumizi ya wino na karatasi. Kwenye Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, kwa mfano, vifupisho vifuatavyo hutumiwa:
TUKI
-
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili,
M
-
Mkurugenzi,
MT
-
Mkuu wa Sehemu ya Utawala/Afisa Tawala,
MK
-
Mkuu wa Sehemu ya Kamusi,
MF
-
Mkuu wa Sehemu ya Fasihi,
MS
-
Mkuu wa Sehemu ya Isimu,
MIT
-
Mkuu wa Sehemu ya Istilahi na Tafsiri,
MU
-
Mratibu wa Uchapishaji.
Lakini vifupisho hivi hutumiwa katika maandishi tu, tena kwenye mazingira maalum tu (yaani hasa kwenye mafaili na juu ya sekula zinazotakiwa kupitiwa na viongozi hawa). Mchunguzi kwa mfano, hawezi kusema: “Ninahitaji kumwona M. ili kuomba ushauri wake juu ya mswada wangu”. Hali kadhalika Mchunguzi hawezi kumwandikia barua rasmi Mkurugenzi na akamwita M.. Mathalani: “Ndugu M.”. Tafadhali rejea barua yako kumbukumbu na....”. Katika mazingira haya ni lazima tuandike na kutamka kikamilifu, yaani tutumie neno “Mkurugenzi”.
Hali kadhalika matumizi ya vifupisho vya majina ya magonjwa na madawa vinavyoandikwa na madaktari huko katika zahanati na hospitalini, vifupisho vya kihandisi na nyanja nyinginezo hufanywa kwa misingi kama iliyojadiliwa hapo juu.
Kuhusu matamshi katika mtindo wa mawasiliano ya kirasimu, ni kwamba haitoshi tu kuyatamka maneno kwa ukamilifu, bali muhimu zaidi ni kuyatamka kwa kutumia lafudhi sanifu, lafudhi kuntu - kama inawezekana, na sio kujitamkia kiholela tu kama mtu apendavyo. Mathalani, lafudhi ya akina “Pwagu na Pwaguzi” haiwezi kukubaliwa itumiwe katika mazingira haya.
Miundo ya Sentensi
Miundo ya sentensi za mtindo wa kirasimu inafanana na ile inayotumika kwenye mtindo wa kitaaluma. Lakini hata hivyo kuna tofauti kidogo zinazojidhihirisha wazi.
(i) Matumizi ya Sentensi Changamano, Ndefu na Zinazotegemeana
Sentensi za aina hii aghalabu hutumiwa sana katika uandishi wa maazimio, imani na madhumuni ya vyama, katika mikataba na matini za kisheria. Kwa mfano:
AZIMIO LA MKUTANO MKUU WA TAIFA WA PAMOJA WA TANU NA ASP.
Kwa kuwa Mkutano Mkuu wa pamoja, kwa niaba ya Wana-TANU na wana-ASP, kwa pamoja unaelewa na kukubali kwamba jukumu letu katika historia ya Taifa ni kuimarisha umoja, kuleta mapinduzi ya kijamaa Tanzania na kuendeleza mapambano ya ukombozi katika Afrika na kote duniani;
Kwa kuwa tunatambua...
Kwa kuwa tunazingatia...
Kwa kuwa tunatambua...
Kwa kuwa tunatambua...
Kwa kuwa kihistoria tumeongozwa na kumbukumbu ya kitendo kama hiki cha kimapinduzi na busara ambacho waanzilishi wa TANU, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius K. Nyerere, walikifanya hapo awali cha kuvunja Chama cha African Association na kuunda TANU; na waanzilishi wa ASP, chini ya uongozi wa marehemu Abeid Amani Karume, walikifanya hapo awali cha kuvunja vyama vya African Association na Shirazi'Association na kuunda ASP, shabaha yao wote ikiwa ni kuunda Chama kipya madhubuti na cha kimapinduzi chenye uwezo mkubwa zaidi wa kuongoza mapambano ya wananchi wetu katika mazingira mapya ya wakati huo; Kwa hiyo basi:
(1) Sisi, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa pamoja wa TANU na ASP, tuliokutana leo tarehe 21 Januari, 1977 mjini Dar es Salaam, chini ya uongozi wa pamoja wa Ndugu Julius K. Nyerere, Rais wa TANU, na Ndugu Aboud Jumbe, Rais wa ASP, kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP), ifikapo tarehe 5 Februari, 1977, na wakati huohuo kuundwa kwa Chama kipya cha pekee kwa Tanzania nzima, na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba.

(Katiba ya CCM, 1982:1 - 3)
Sentensi ndefu namna hii na zenye hali hii ya utegemeano kwa kawaida hazitumiki katika mitindo mingine ya mawasiliano. Licha ya hivyo mara nyingi sentensi hizi hujitokeza katika maandishi tu, na sio katika mazungumzo (kwa sababu ala za matamshi haziwezi kutamka sentensi ndefu namna hii bila kuwepo matatizo).
(ii) Matumizi ya Nafsi ya Mtendaji Isiyosisitizwa
Katika baadhi ya mawasiliano ya kirasimu, hasa ripoti na kumbukumbu za mikutano kuna matumizi mapana sana ya sentensi ambazo zinatilia msisitizo zaidi tendo lenyewe lililofanyika, na sio nafsi ya mtendaji aliyetekeleza tendo hilo. Kwa mfano:
1) 89.1.2
Kuh. 85.1.5 Iliarifiwa kuwa Prof. Ohly alipata maswali toka kwa mchunguzi mmoja tu, kwa hiyo anangojea maswali mengine. Ilikubaliwa kuwa afanye semina kujibu maswali hayo kwa sababu inaonekana kuwa yanatosha.

(Kumbukumbu za Mkutano wa Sehemu ya Kamusi, 17.4.1982:1).
2) Kumb.
Na. 2.1 Ilielezwa kuwa vitomeo lazima viwe ni msamiati hai ambao unatumiwa katika lugha.

(Kumbukumbu za Mkutano wa maandalizi ya jopo la kamusi ya Kiingereza - Kiswahili, 6/8/1982:1).
Katika tungo hizi jambo muhimu niiliarifiwa, ilikubaliwa na ilielezwa.Suala la nani aliyearifu, aliyekubali na aliyeeleza hatulitilii maanani sana. Kusema kweli katika tungo za namna hii nafsi ya mtendaji haionyeshwi waziwazi isipokuwa tunabunia tu kuwa lazima alikuwepo mtendaji. Na kimsingi katika mazingira haya mtendaji ni uongozi au utawala wenye madaraka kisheria.
(iii) Matumizi ya Tungo za Kauli ya Kutendwa
Kama ilivyo kwa mtindo wa kitaaluma tungo za kauli ya kutendwa hutumika sana katika mtindo wa kirasimu hasa kwenye matini za sheria. Kwa mfano:
Ndoa ambayo imefungwa bila kuwa kinyume cha sheria hii, itakuwa ndoa thabiti bila kujali kukosa kutoa taarifa ya nia ya kufunga ndoa au taarifa ya kupinga ndoa inayokusudiwa kuwa imetolewa nahaikutekelezwa au kupotoka kokote kwa utaratibu wa kufunga ndoa.
(Rwezaura, 1981:29).
(iv) Matumizi Mapana ya Viunganishi vya Sentensi
Mtiririko mzuri wa mawazo katika mawasiliano ya kirasimu husisitizwa na kushamirishwa zaidi kwa kutumia viunganishi maalum vya sentensi. Kusema kweli viunganishi hivi ni vijenzi muhimu sana vya mantiki katika mtindo huu. Baadhi ya hivi viunganishi ni:
kwanza, ...... pili, ....
(hali) kadhalika,
kwahiyo (basi),
kwa ajili hiyo (basi),
ndiyo kusema,
hii ina maana kwamba,
hii maana yake ni ..., n.k.
Viunganishi hivi vya sentensi tuliviona vikitumiwa sana vilevile katika mtindo wa kitaaluma kwa lengo hilihili la kuwezesha kuwepo kwa mtiririko mzuri wa mawazo.
(v) Matumizi Makubwa ya Fomu Maalum za Kujaza
Kwa kuwa baadhi ya shughuli za kirasimu zinawahusu watu wengi mno na hufanyika mara kwa mara, kumekuwepo na ulazima wa kutumia fomu maalum (zilizoandaliwa kwa wingi) zenye nafasi zilizoachwa wazi ili zijazwe na wahusika kama ipasavyo. Na tungo zinazotumiwa kwenye fomu hizi ni za aina ya kipekee. Aghalabu huwa zimekatizwakatizwa. Matumizi ya fomu za aina hii yanarahisisha kazi ambayo ingebidi irudiwe kila mara. Kwa mfano:
Serial No........................
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
JESHI LA POLISI TANZANIA
KIBALI CHA KUENDESHA GARI SIKU YA JUMAPILI
Kibali kimetolewa kwa .............................................................................
Kuendesha gari Reg. No .........................................................................
Siku za Jumapili baada ya saa nane katika barabara kati ya ...................
................................................................................................................
Kupitia barabara ya .................................................................................
Kati ya saa...............................................................................................
Kibali kinakwisha tarehe ..........................................................................
Tarehe ............................................................. Sahihi ............................
KAMANDA WA POLISI
[Kibali hiki kilitolewa na Ofisi ya Mkuu wa Polisi (M), Tanga, Machi 1982 wakati mwandishi alipokuwa anafanya uchunguzi wa lahaja mkoani Tanga.]
Hitimisho
Sura hii imefafanua kwa undani zaidi dhana ya urasimu kama inavyoeleweka katika taaluma ya elimumitindo, njia za kutekeleza mawasiliano katika mtindo wa kirasimu na sifa zinazoutofautisha mtindo huu ulinganishwapo na mitindo mingine. Ni matumaini yetu kuwa kwa kurejea nyingi ya hoja zilizotolewa katika sura hii watumiaji wa Kiswahili wataongeza upeo wa ufasaha wao katika mawasiliano rasmi ya maofisini na mahali pengine pa kazi.
Katika sura inayofuata tutaujadili mtindo wa magazetini na shughuli za kisiasa.
Massheleblog