Lakini, wapenzi, ijapokuwa twanena hayo, katika habari zenu tumesadiki mambo yaliyo mazuri zaidi, na yaliyo na wokovu.  Maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia.  Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho;  ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu. Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapia, aliapa kwa nafsi yake,  akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza.  Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi.

Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha.  Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati;  ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu;  tuliyo nayo kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia,  alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki #WAEBRANIA 6:9-20

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo mpendwa wangu.
Namshukuru Mungu kwa upendo na neema zake ambazo anaendelea kutukirimia. Napenda kuwakumbusha Watu wa Nachingwea kwamba wiki hii tarehe 13-15 (Ijumaa hadi Jumapili) tutakuwa na Semina ya Neno la Mungu kwenye ukumbi wa kwa Kanindo, kuanzia saa 9 alasiri katika siku hizo 3. Napenda kuwakaribisha wote tule na kunywa mbele za Mungu. Maombi na maombezi yatafanyika kwa watu wote.

Usiache sasa kutuombea ukipata nafasi ya kutuombea kwamba Bwana atupake mafuta yake matakatifu kwa ajili ya huduma hii. Nakusihi tuombee.

Mpendwa mwana wa Mungu, maandiko yanasema na Bwana mwenyewe amethibitisha mara nyingi kwamba hakika Mungu tunayemuamini na kumtumikia sio Mungu dhalimu hata aisahau kazi yako mpendwa na upendo ambao umekuwa ukimwonyesha kwa kujitolea kwa ajili ya Injili.

Nyakati fulani wanafunzi walimuuliza Bwana Yesu tutapata nini sisi tulioacha kila kitu tukakufuata wewe? BWANA aliwajibu “Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” #Marko 10:29-30

Ndugu yangu, kazi yako ya kuwatia moyo wale waliokata tamaa na kuwasaidia kupata nguvu mpya ya kusonga mbele katika wokovu, kazi ambayo umekuwa ukiifanya kwa nguvu zote Mungu hataisahau kamwe. Wewe ndugu yangu ambaye umejibidiisha kuwashuhudia watu habari njema Bwana hatasaisahau kazi yako mwana wa Mungu.

Wewe ambaye umetoa muda wako kuwaombea watu, kwamba waokoke, kwamba waponywe, kwamba wajazwe na nguvu upya ya Mungu, kwamba wahuishwe ndani yao, kwamba Bwana awatembelee katika ndoa zao, kwamba Mungu akutane na matatizo kwenye maisha yao, kwamba Bwana afanye mabadiliko ndani ya maisha yao Mungu hataisahau kamwe kazi yako katika jina la Yesu.

Mwana wa Mungu wewe ambaye umekuwa ukijitoa fedha na mali zako kwa ajili ya watumishi wa Mungu hakika Bwana hataisahau kazi yako. Wewe ambaye umejitoa kuwalisha wajoli wa Bwana, wewe ambaye umejitoa kwa ajili ya yatima na wajane walioko mtaani kwako, wewe ambaye umejitoa kwa ajili ya maskini walioko mtaani kwako, hakika Bwana hataisahau kazi yako katika jina la Yesu Kristo aliye hai. Maana Mungu tunayemuabudu ameahidi mwenye kwamba hakika yake kukubariki atakubariki. Hiyo ndo ahadi yake.

Mungu akubariki sana wewe ambaye umekuwa ukijitoa hata kuwapa mavazi watu walio na uhitaji huo. Mungu akubariki wewe ambaye umekuwa ukijitoa muda wako kwenda kuomba na watu magerezani, mahospitalini, na maeneo mbalimbali, Bwana hataisahau kazi yako mwana wa Mungu.

Wewe ambaye umekuwa ukijitoa kufunga na kuomba kwa ajili ya kumlilia Mungu kwa ajili ya watumishi mbalimbali, kuomba kwa ajili ya huduma mbalimbali, Mungu hataisahau kazi yako. Usidhani unapoteza muda wako bure. Usione wale unaowaombea kwamba hawaokoki basi unakata tamaa, yako majira ya Mungu kwa mwanadamu kubadilishwa. Haupotezi muda ndugu yangu. Haupotezi muda nakwambia katika jina la Yesu. Usiache kuwaombea watu. Kazi yako si bure mwana wa Mungu na Bwana hataisahau kamwe ndivyo alivyoahidi.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nawe mwana wa Mungu na ikiwa umebarikiwa basi share ujumbe huu kwa mwingine naye abarikiwe

“YASIYOWEZEKANA KWA WANADAMU, YAWEZEKANA KWA MUNGU” #LUKA 18:27

Kwa maombezi, unataka kupokea uponyaji au kufunguliwa kwenye kifungo chochote kile, ushauri au unatamani ujitoe kikamilifu kumtumikia MUNGU na UNATAKA KUMPOKEA BWANA YESU AWE BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YAKO NA AKUSAMEHE DHAMBI ABADILISHE MAISHA YAKO NA TABIA MBAYA ZILIZOKUSHINDA basi wasiliana nasi kwa msaada wa Roho Mtakatifu tukusaidie +255 758 443 873. Ukipiga simu isipopokelewa tafadhali acha sms.