Golikipa wa vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba SC Aishi Manula amefanikiwa kujiwekea rekodi ya pekee tangu ajiunge na klabu hiyo mwezi Juni 2017 akitokea Azam FC.

Manula ameichezea Simba mechi 20 ambapo kati ya hizo mechi 14 hajaruhusu lango lake kufungwa hata bao moja hivyo kuwa msaada mkubwa kwa kikosi hicho kinachoongoza ligi kwa alama 35.

Katika rekodi hiyo ya Manula  mechi za kukumbukwa zaidi ni mechi yake ya kwanza ndani ya Simba ambayo ilikuwa siku ya Simba Day dhidi ya Rayol Sports ya Rwanda. Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mechi nyingine ni ile dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Hisani ambayo ilikuwa ni mechi yake pili kwake na timu hizo zilitoka sare ya 0-0 katika dakika 90. Mechi ya kwanza ya ligi kwa Manula akiwa na Simba ilikuwa ni ushindi wa 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting.

Mechi nyingine ambazo zimebaki kama alama ya uwezo wa Manula ndani ya Simba ni mechi tatu za mwisho kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi, Simba ikishinda 4-0 dhidi ya Singida United, 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na ushindi wa jana 4-0 dhidi ya Majimaji FC.