Makala

Na: Jumaa H Heshima

Sitoanza kwa salamu kama ilivyo kawaida ya kile kiitwacho ustaarabu wa
Waswahili. Kimsingi hakuna ustaarabu wa Waswahili. Ustaarabu ni wa Waarabu ila tunazo amali tulizozisaliti kwa kuzinasibisha na Uarabu.

Basi ya nini kuzibebesha amali zetu adhimu majina yanayozinyima Uafrika
wake? Tutafute jina sahihi kuzirejelea amali hizi.

Hasira za makala haya ni juu ya athari za "ukoloni lugha'' unavyonyonya na
kufifisha ubunifu wa vijana wasomi wa taifa hili pendwa, Tanzania.

Sote tunafahamu kuwa Kiswahili ni lugha ya taifa hili, Tanzania. Mwanazuoni
mmoja katika kongamano la Kiswahili pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
aliuliza  swali; ``je, Kiswahili ni lugha ya taifa kikatiba au kimazoea?''

Ukumbi mzima ulitumbua macho pasi na kujibu.

Sababu hakuna andiko lolote lile kwenye katiba wala sheria yoyote ile nchini
humu inayoeleza na kuelekeza kuwa lugha yetu ya taifa  ni Kiswahili. Hii
ni lugha ya taifa kimazoea ni si kimaandiko.

Na sote tunatambua nguvu ya maandiko dhidi ya maneno matupu ya kupiga domo,
hasa ukihitajika  msaada wa kisheria.

Ila kwa majirani zetu Kenya katiba yao inatanabaisha wazi katika Sura ya
pili ibara ya saba kuwa lugha ya taifa nchini humo ni Kiswahili ( 7.1 The
national language of the Republic is Kiswahili ).

Wacha nisiwapoteze; narudi kwenye mada kuu.

Ni zaidi ya miaka thelathini sasa Tanzania inatafuta jibu la kitendawili
cha Sera ya lugha katika swala zima la elimu.

Jambo lenye utata zaidi likiwa Je, Kiswahili kitumike kama lugha ya
kufundishia katika elimu ya sekondadi na vyuo au kibaki kufundishwa kama
somo mojawapo?

Mjadala huu umekua mzito na kupelekea ukinzano mkubwa, wengine wakitetea
Kingereza wengine Kiswahili.

Wanaotetea Kingereza kimantiki hakuna hoja yenye mashiko kwa mtazamo wangu.

Hoja zao maarufu ni kuwa Kingereza ni lugha ya Kimataifa, ni lugha ya
kibiashara na kiuchumi Ulimwenguni n.k

Lakini kichekesho ni kwa wale walimu na wanazuoni wa masomo ya Sayansi. Wao
wanadai kuwa kuna maneno katika Sayansi hayana Kiswahili chake pia kuna dhana ambazo ni ngumu kufasiriwa kwa Kisawahili ili zieleweke.

Lakini wanasahau kuwa maneno kama Bacilus, data, chytridiomicota na
ascomycota ambayo wanayatumia kwenye Sayansi sio ya Kingereza, yamekopwa tu.

Maneno mengi ya kitaaluma yana asili ya lugha za Kilatini, Kiarabu na
Kigiriki au Kiyunani.

Tukiachana na walimu wapo wanaodai kuwa Kiswahili bado ni kichanga
kimsamiati. Sasa sidhani kama kukitelekeza kabisa kwenye maswala muhimu
kutatatua tatizo hilo.

Lugha ya Kingereza asili yake si Wingereza ni Ujerumani. Ila Waingereza
walipoipata tu wakaithamini na kuiweka kwenye mifumo yao yote na leo
imekua kama tuionavyo.

Sisi bado tuna ngojangoja. Jambo la kustaajabisha ni kumuona mtu
anaishi nyumba ya kupanga hata baada ya kujenga nyumba yake nzuri.

Wakati huohuo ukamkuta mwenziwe amehamia kwenye nyumba yake ambayo bado
haijaisha akiimalizia kuijenga huku anaishi. Wasambaa wanaita ``cha mumo''
yaani cha humohumo (kujenga hali ya kuwa unaishi kwenye nyumba unayoijenga).

Cha mumo ikifanyika kwenye Kiswahili itasaidia sana kwani tutakijenga kwa
kasi tukihofia wingu la mvua kutusaliti.

Jambo la kufundisha masomo kama Fizikia, Kemia, Bayolojia, Jografia na
Hisabati kwa kutumia Kingereza halijatuacha salama.

Wanafunzi hawaelewi wanachofundishwa na walimu. Wakati mwingine walimu nao hawaelewi
wanachokifundisha kwa namna itoshayo kumuelewesha mwanafunzi.

Kikwazo kikubwa kikiwa ni jinamizi Kingereza. Hivyo walimu huona Kiswa-nglish (kuchanganya Kiswahili na Kingereza) ndio njia mbadala.

Jambo la kukipa kipaumbele Kimombo humnyima mwanafunzi uhuru wa kuwasilisha fikra na
mawazo yake. Profesa mmoja alitoa ushuhuda kuwa katika darasa lake la shada
ya uzamili (Masters), mwanafunzi mmoja aliomba kuchangia mada kwa lugha ya
Kiswahili.

Profesa akamkatalia na kumwambia atumie Kingereza mwanafunzi huyo akakaa
kimya na kutowasilisha kile alicho nacho.

Sasa huyu ni mwanafunzi wa uzamili anatafuta digrii ya pili lakini anakosa
uhuru wa kuwasilisha alicho nacho kwa Kingereza. Je, hali ikoje kidato cha 1, 2, 3 mpaka cha 6? Usinipe jibu baki nalo tu.

Wengi tunajiuliza kwa nini tuna wahandisi na wanasayansi wengi na bado wengine wanaendelea
kuzalishwa vyuoni lakini matokeo yao tarajiwa hayaonekani katika swala zima la Teknolojia na ubunifu kwa ujumla?

Hebu tupitie nukuu za wataalamu hawa wachache.

Bwana mmoja aitwae Marshal (mwaka sijaupata) alipata kuandika maneno haya ``Maendeleo ya watu yanategemea uwezo wao wa kutumia lugha katika maswala mbalimbali''

Jambo hili halina ubishi, ili kiwanda kifanye kazi kwa ufanisi huhitaji wafanyakazi kuelewana katika lugha waitumiayo au kuelewa lugha itumikayo kuendeshea mitambo hali kadhalika maofisini, masokoni n.k

Go uun (1990) anaeleza kuwa ``Tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa japokuwa mtu anaweza kufahamu lugha mbalimbali, ni lugha moja tu kati ya hizo ndiyo ataielewa vizuri sana ambapo ataweza kutengeneza/kubuni kazi za kisayansi na kisanaa kwa lugha hiyo. Ni wazi kuwa lugha hiyo ni lugha yake ya kwanza''

Katika nukuu hii naweza pinga swala la kuifahamu vizuri zaidi lugha moja tu ambayo ni ile ya kwanza ila nashawishika kuunga mkono hoja baada ya bwana Go uun kusema kuwa lugha hiyo ndiyo itamuwezesha kubuni kazi za kisayansi na kisanaa.

Hapa ndipo tunaweza jijibu lile swali la letu la mwanzo.

Wanasayansi wapo wengi nchini tena wa ngazi za juu kabisa kielimu mathalani maprofesa ila ubunifu na ustadi wao kisayansi na kiteknolojia uko wapi?

Uwezo wa kubuni na kutengeneza kazi mbalimbali kwa matokeo makubwa zaidi upo katika matumizi ya lugha ifahamikayo vizuri.

Unaweza zalisha watumishi wazuri (kama walimu, mafundi, madaktari n.k) kwa kutumia lugha ya kigeni lakini kamwe huwezi zalisha wanasayansi mahiri na wabunifu kiteknolojia kwa lugha hiyo bali lugha ifahamikayo zaidi, ambayo ni lugha ya kwanza.

Ozturk (2002) anatunong'oneza kuwa ``Mtu ambaye anaweza kuhoji, kutafiti, kutengeneza tatizo na kulitatua anafikiri huru na kwa mapana ikiwa Elimu anayoipata inatolewa kwa Lugha yake''

Hili naliunga mkono 100% hebu kumbuka mfano ule wa profesa na mwanafunzi wake wa shahada ya uzamili.

Nchi za wenzetu wanagundua mambo mengi kwa jambo hili. Tuache maswala ya Teknolojia, Wao hugundua matatizo mfano magonjwa kama vile Ebola na labda kuyajaribu kwetu kisha Elimu yao inawawezesha kutatua matatizo hayo kwa kuleta chanjo.

Kwetu sisi mambo haya kwa mwenendo huu tutasubiri sana.

Elimu ni swala nyeti na tete sana katika maendeleo ya taifa lolote lile
na kutoweka misingi mizuri ya elimu yenye matokeo chanya, Kimaendeleo ni kulisokomeza taifa hili katika bahari ya sahau.

Kabla ya kumaliza andiko langu hili msikilize mwanazuoni huyu.

Kavcar (1999) anasema ``katika swala hili, Elimu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya watu na jamii, lazima itolewe kwa lugha inayotafahamika, ambayo ni lugha yao ya kwanza''

Maoni yangu:

1.Viongozi wa taifa hili la Tanzania wenye dhamana katika swala hili wafanye haraka katika kuimarisha sera ya lugha katika mfumo wetu wa elimu.

2.Na uimarishaji huo ukipe Kiswahili  kibali cha kuwa lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya awali mpaka vyuo vikuu.

Kiswahili kwa matokeo makubwa.

                *MWISHO*

Mwandishi: Jumaa Hassan Heshima
                     Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
                     20/12/2017
                     0714 638277