UHAKIKI WA RIWAYA 


Karibu tena katika mwendelezo wa makala haya yanayojikita katika kutoa maarifa ya Kiswahili kwa kidato cha tatu. Leo tutashughulika na uchambuzi wa riwaya ya Joka la Mdimu. Ambapo vipengele vya fani na maudhui vinajadiliwa kama ifuatavyo;

JINA LA KITABU: Joka la Mdimu

MWANDISHI: Abdallah J. Saffari

Utangulizi

Riwaya hii inaakisi matatizo ya kiuchumi yanayoikumba jamii. Msanii ameweza kuonesha namna wananchi wanavyopata shida katika kupata huduma za kijamii kama vile; usafiri, matibabu, mavazi, makazi n.k.

Pia, msanii amaeonesha matabaka. Katika jamii kuna tabaka tawala na tabaka tawaliwa. Tabaka tawala linaonekana kuwa na maisha bora zaidi wakati tabaka tawaliwa lina maisha ya taabu yaliyojaa dhiki.

Kutokana na hali ngumu ya maisha, wananchi wa tabaka la chini wanajiingiza katika matendo maovu kama vile; unyang’anyi, ukahaba na biashara za magendo. Kwa hiyo, dhamira kuu katika riwaya hii ni Hali ngumu ya maisha au Umasikini ambao msanii ameuonesha kuanzia mwanzo wa riwaya hadi mwisho.

MAUDHUI

Mwandishi ameonesha matatizo mbalimbali yanayowakabili wanajamii hasa wale wa tabaka la chini. Matatizo hayo ni kama vile mafuriko, ukosefu wa huduma za kijamii kama vile shule nzuri, barabara nzuri, masoko n.k. Kwa upande mwingine, msanii ameonesha ni kwa namna gani tabaka tawala linafaidi keki ya nchi. Wananchi waliopo katika tabaka tawala hujilimbikizia mali, ni mafisadi, wala rushwa na wanapenda starehe. Wanaishi maisha ya anasa bila kujali wananchi wengi wanaoteseka kwenye jamii.

Dhamira

Mwandishi ameonesha mambo mbalimbali yanayoikabili jamii. Mambo hayo ndiyo yanayojenga dhamira mbalimbali kama ifuatavyo;

Hali ngumu ya Maisha/Umasikini

Mwandishi ameonesha kuwa ugumu wa maisha hutokana na hali mbaya ya kiuchumi. Ugumu wa maisha unaonekana kwa namna mbalimbali kama vile; kukosekana kwa mafuta ya magari kunakofanya shughuli za usafiri kuwa za shida. Watu wanasafiri kwa kutumia maroli ya mizigo ambayo si salama sana na huchelewesha abiria kufika na kudumaza ufanisi wa kazi.

Pia, wananchi wa tabaka la chini wanakosa huduma za nishati ya umeme wa kuaminika. Mbaya zaidi hata mishumaa inakuwa adimu kupatikana.

Vivyo hivyo, wananchi wanakosa chakula bora na salama. Wananchi wanakula chakula kilinachouzwa kwenye mazingira machafu yanayohatarisha afya zao. Pia, kutokana na ukosefu wa mazao ya chakula wananchi wanakula ugali uliotokana na unga wa njano ambao hauna ladha nzuri.

Si hivyo tu, bali umasikini unadhihirika katika makazi ya wananch wa Sega. Makazi hayo ni duni ambayo si salama kwa afya na uhai wa wananchi. Yapo, kwenye mabonde ambapo mafuriko hutokea mara kwa mara lakini pia, yapo karibu na mto unaotiririsha maji machafu yanayotoka kiwandani.

Pamoja na hayo, msanii ameonesha ni mambo mbalimbali yanayosababisha umasikini katika jamii zetu. Mambo hayo ni kama yafuatayo;

Uhujumu uchumi ni sababu tosha inayodidimiza maendeleo ya kijamii. sanii ameonesha kuwa viongozi wengi ni wahujumu uchumi kwani hujilimbikizia mali, hukwepa kulipa kodi kwa kufanya biashara za magendo, kufanya ziara zisizo na tija, kujihisisha na ujangiri na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Ufisadi huu umesababisha nchi ikose barabara bora, huduma bora za afya, masoko, mafuta ya magari, chakula bora kwa wananchi, n.k

Kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, wananchi wa tabaka la chini wamejiingiza katika biashara za dawa za kulevya, uuzaji wa miili yao, ukuwadi, wizi, ubakaji, rushwa n.k.

Kwa ujumla hali ngumu ya maisha inapaswa ipigwe vita kwani wanaoathirika ni tabaka tawaliwa ambao ndiyo wengi zaidi. Hali hii inapoteza utu wao na kuwafanya waishi maisha yasiyo ya kibinadamu.

Rushwa

Msanii ameonesha kuwa watu wengi wanakosa hai zao kwa sababu ya rushwa kwani viongozi hawawezi kuwahudumia wananchi mpaka watoe rushwa. Mwananachi hawezi kupata fedha za kigeni bila kuhonga.

Pia, rushwa imefika hadi kwa wananchi wa tabaka la chini kiasi kwamba hawawezi kununua baadhi ya huduma mpaka watoe rushwa. Kwa mfano hawawezi kupata tiketi za safari na mafuta ya magari pasipo kutoa rushwa.

Uhujumu Uchumi

Mwandishi ameonesha kuwa katika jamii zetu uhujumu uchumu umekithiri. Amemtumia Brown Kwacha kuonesha namna anavyowatumia wafanya biashara kuuza pembe za ndovu na wa humtumia ili kukwepa kodi. 

Pia, Brown Kwacha anatumia ofisi yake kama sehemu ya kujipatia kipato kisicho halali kwa kupokea rushwa na kupitisha pasi za fedha za kigeni kwa matakwa yake binafsi. Pale aliposhindwa kutoa hesabu ya matumizi ya fedha za kigeni aliamua kuchoma ofisi ambayo ni mali ya serikali ili kuficha ufisadi wake.

Kwa upande mwingine msanii ameonesha namna mafuta ya magari na bidhaa zingine zinavyouzwa kimagendo. Wale tu waliojua namna ya kuzipata ndiyo waliofaidika.

Matabaka

Msanii ameonesha kuwa katika jamii zetu kuna tabaka tawala na tabaka tawaliwa. Tabaka tawala ndilo hufaidi matunda ya nchi wakati tabaka tawaliwa limekumbwa na hali duni ya kimaisha. Haya tunaweza kuyathibitisha kwa kurejelea maisha ya Brown Kwacha kama muwakilishi wa tabaka tawala na maisha ya akina Tino, Amani, Jinja Maloni na wengine wawakilishao tabaka tawaliwa.

Umalaya na Uuzaji wa Dawa za Kulevya

Mwandishi anaonesha namna wanajamii wanavyojiuza ili kujikimu na maisha. Tunaona pale ambapo Amani alipompeleka baharia kwenye moja ya kasino akiwa pamoja na msichana anayejiuza.

Vivyo hivyo, madereva wanaowatafutia wasichana mabaharia huwa wanalipwa vizuri na mabaharia hao. Pia, hata mabaharia wa kike nao hufanya umalaya kama starehe.

Pia, Brown Kwacha anatembea na wanawake wengi ili kujistarehesha. Kwacha alitembea na Leila, Josephine na wengine wengi na bado alikuwa akimtamani Pamela.

Pamoja na umalaya, msanii ameonesha kuwa vijana wengine hujipatia kipato kutokana kuuza dawa za kulevya kama vile bhang n.k.

Mapenzi na Ndoa

Katika riwaya hii msanii ameonesha kuwa katika jamii kuna mapenzi ya kweli na mapenzi yasiyo ya kweli.

  • Mapenzi ya Kweli

Kwa upande wa mapenzi ya kweli msanii amemtumia Tino ambaye anaonekana kuwa na mapenzi ya kweli kwa familia yake kwani anahakikisha inapata mahitaji yote muhimu.

Vivyo hivyo, Amani ana mapenzi ya kweli kwa Tino kwani anamsaidia katika kutatua matatizo mbalimbali yanayomkabili kama vile kufanikisha safari yake na kumsaidia kupata pesa kwa ajili ya matibabu ya Cheche (mtoto wa Tino).

Mke wa Brown Kwacha anaonekana ana mapenzi ya kweli kwa familia yake kwani anaihudumia na kukaa karibu nayo kila wakati.

Pia, Wema (mke wa Tino) ana mapenzi ya kweli kwa familia yake kwani anavumilia hali ngumu waliyonayo na anaitunza vyema familia yake.

  • Mapenzi yasiyo ya Kweli

Mwandishi amaeonesha kuwa serikali haina mapenzi ya kweli kwa wananchi wake kwani hawawajibiki katika kutatua matatizo yanayowakabili.

Pia, Brown Kwacha hana mapenzi ya kweli kwa nchi yake na kwa jamii kwani anajihusisha na rushwa na ufisadi ambao ni chanzo cha kudidimiza uchumi wa nchi.

Wafanya biashara wengi hawana mapenzi ya kweli kwa nchi yao na kwa jamii kwani wanakwepa kodi na kujihusisha na magendo mambo yanayodidimiza uchumi wa nchi.

Vivyo hivyo, Leila na Josephine hawana mapenzi ya kweli kwani wanajihusisha na mapenzi na Brown Kwacha kwa ajili ya kunufaika kifedha tu na si kingine. Leila ametembea na wanaume ambao hawahesabiki.

Kutowajibika

Msanii ameonesha kuwa viongozi wengi siyo wawajibikaji. Kwani hukwepa majukumu yao mpaka wahongwe. Suala hili linafanya wananchi wa kawaida kukosa huduma za haraka na kufanya mdororo wa kiuchumi.

Uongozi Mbaya

Viongozi wa jamii zetu hawataki kutekeleza majukumu yao badala yao wamekuwa chanzo cha kudunisha maisha ya wananchi wengi. Haya hutokea pale ambapo viongozi hubadilika na kuwa wala rushwa, wasiowajibika, wanafiki na wanaojihusisha na ujangiri na biashara za magendo.

Nafasi ya Mwanamke katika Jamii.

Mwandishi ameweza kumchora mwanamke katika nafasi mbalimbali kama ifuatavyo;

  • Mwanamke ni mlezi wa familia. Hapa tunamuona mke wa Brown Kwacha na Wema ambao hutunza watoto na wame zao.
  • Mwanamke ni kiumbe dhaifu. Kwa kumtumia mke wa Brown Kwacha mwanadishi anaonesha kuwa mwanamke hawezi kufanya maamuzi yoyote ya kifamilia bila kuwepo kwa mume wake. Pia, hawezi kushirikishwa kwenye suala lolote la kimaendeleo.
  • Mwanamke ana mapenzi ya kweli. Wema na Mke wa Brown Kwacha wana mapenzi ya kweli kwa familia zao. Kwani hutoa muda wao ili kuzilea na kuhakikisha watoto wana furaha.
  • Mwanamke ni jasiri. Ujasiri wa mwanamke tunauona kwa Leila ambaye bila kujali jinsia yake hufanya kazi kwenye shirika la ndege.
  • Mwanamke si mtegemezi. Suala hili linathibitika kwa Leila ambaye hategemei mwanaume yeyote katika maisha yake. Anafanya kazi na kujikimu kimaisha.
  • Mwanamke anapenda starehe. Msanii amamtumia Josephine na Leila ambao wanapenda starehe. Josephine anapenda kwenda nchi za Ulaya ili kufanya manunuzi na pesa hizo anazitoa kwa Brown Kwacha. Pia, Leila anapenda kutembelea sehemu za starehe kama vile mbuga za wanyama n.k.
  • Mwanamke ni shupavu na ana msimamo. Ushupavu wa mwanamke unaonekana kwa Pamela ambaye bila kujali fedha za Brown Kwacha alisimamia msimamo wake wa kutokuwa nae kimapenzi.
  • Mwanamke ni chombo cha starehe. Wanaume wengi huwatumia wanawake kwa ajili ya kujistarehesha tu. Jambo hili linaonekana kwa Brown Kwacha na kwa Mabaharia wanaonunua wanawake ili wajistareheshe tu.
  • Mwanamke ni msaliti. Usaliti wa mwanamke unaonekana kwa Esther na Leila. Esther anamsaliti mchumba wake na kujihusisha kimapenzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mila na Utamaduni. Pia Leila alijihusisha kimapenzi na wanaume wengi wasiohesabika. Josephine anajihusisha kimapenzi na Brown Kwacha ilhali akijua kuwa ni mume wa mtu.

Ujumbe

Kutokana na dhamira tulizoziona, mwandishi amekusudia kutoa jumbe mbalimbali kama zifuatazo:

  1. Rushwa ni adui wa maendeleo. Kutokana na rushwa wananchi wengi wanakosa huduma muhimu na kuathiri uchumi wao.
  2. Mapenzi ya dhati ni muhimu katika familia na katika ujenzi wa jamii mpya.
  3. Uongozi mbaya ni chanzo cha matatizo katika jamii. Uongozi mbaya huweza kusababisha maovu kuibuka katika jamii.
  4. Uovu siyo suluhisho la matatizo. Kwa mfano, wizi siyo suluhisho la umasikini.
  5. Tabaka la chini ni lazima lithaminiwe ili nchi iweze kupiga hatua za kimaendeleo.
  6. Uwajibikaji ni muhimu katika kujenga jamii mpya.

Migogoro

Msanii ameonesha mikinzano iliyojitokeza baina ya wahusika kama ifuatavyo;

  • Mgogoro kati ya Wavuta Makwama.

Mgogoro huu unatokea baada ya mizigo kufika kisha wakaanza kugombea mizigo hiyo na kusababisha wapigane. Mwisho wanachoka na kuacha wenyewe na mizigo mingine mingi zaidi inafika na kila mmoja kufanya kazi.

  • Mgogoro kati ya Jinja na Vibaka

Mgogoro huu unatokea baada ya Jinja Maloni kuwazuia vibaka wasitimize haja zao. Vibaka wanaamua kupigana lakini Jinja anawashinda na wanakimbia.

  • Mgogoro kati ya Mke wa Brown Kwacha, Brown Kwacha na Josephine.

Mgogoro huu unatokea baada ya mke wa Brown Kwacha kuwafumania Brown Kwacha na Josephine. Vurugu inatokea hata hivyo Brown Kwacha haachani na Josephine.

  • Mgogoro kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mila na Utamaduni na kijana.

Mgogoro huu unatokea baada ya katibu kumuona Esther akiwa na kijana mwingine kwenye sherehe. Vurugu inazuka kijana na katibu wanapigana na mwisho kutumbukia kwenye bwawa la kuogelea.

  • Mgogoro wa nafsi

Mgogoro huu unatokea baada ya Tino kuwa njia panda alipotajiwa gharama za kumtibu Cheche. Hakujua atatumia mbinu gani kumudu gharama hizo.

Pia mgogoro huu unatokea kwa katibu ambaye alihisi kumkosa Esther waliyeomba udhuru lakini hakuwepo nyumbani kwake.

Kwa ujumla migogoro hii imeonesha ni kwa namna gani wanajamii hukutana na vikwazo katika maisha yao ya kila siku.

Mtazamo wa Mwandishi

Mwandishi ana mtazamo wa kiyakinifu. Ameweza kuonesha matatizo yanayoikabili jamii na namna ya kukabiliana nayo. Matatizo hayo yanatokana na uhujumu uchumi, rushwa, kutokuwajibika kwa viongozi n.k. Ili kupingana na matatizo yanayoikumba jamii ni lazima tupige vita uovu wote unaodidimiza uchumi.

Falsafa ya Mwandishi

Mwandishi anaelekea kuamini kuwa chanzo cha matatizo yanayoikumba jamii husababishwa na tabaka tawala.

FANI

Msanii ametumia ufundi kwa namna mbalimbali ili kufanya kazi yake iwe na mvuto kwa hadhira. Ufundi huo umejikita katika vipengele vya fani. Vipengele hivyo vinadadavuliwa kimoja baada ya kingine hapo chini.

Muundo

Riwaya ya Joka la Mdimu ina jumla ya sura kumi ambazo zimepewa majina kutokana na majina ya wahusika, mahali na matukio yanayobeba kisa kizima. Kila kisa kimeelezwa kwa masimulizi ya msago ambapo tunaona chanzo cha kisa hadi mwisho wake. Kwa hiyo riwaya hii ina muundo wa moja kwa moja.

Mtindo

Riwaya hii imetumia mitindo tofauti tofauti kama ifuatavyo:

  • Kuna matumizi ya nafsi ambapo nafsi ya tatu imetumika zaidi wakati nafsi ya pili na ya kwanza imetumika palipo na majibizano baina ya wahusika.
  • Kuna matumizi ya nyimbo kama vile wimbo wa Chaupele unaoonekana hapo chini,

“ Chaupele mpenzi haya usemayo

Kama ni maradhi yapeleke kwa daktari

Sitaweza kuliacha rumba kwa sababu yako…”

Pamoja na wimbo huo, msanii ametumia nyimbo nyingine nyingi za mitindo tofauti ambazo zilitajwa tu kama vile; Mama Ide, on the line n.k.

  • Pia kuna matumizi ya simu ya maandishi (uk. 79).
  • Matumizi ya maneno ya kanga kwa mfano;

Maji marefu”, “Kama Mvuvi Vua. Usichezee Mashua”, na “Cheupe Dawa”

(uk 70).

Mandhari

Msanii ametumia mandhari mbalimbali ili kuonesha uhalisia wa kimazingira.

Mandhari yaliyotumika kwa kiasi kikubwa ni ya kubuni ingawa msanii amaetumia baadhi ya majina ya sehemu ambazo zinafahamika kama vile London, Brussels na Glosgrow.

Pamoja na hayo, msanii ametumia mandhari mbalimbali kama kielelezo cha hadhi ya wahusika. Kutokana na mandhari tunaweza kun’gamua utabaka uliopo katika jamii. Kwa mfano wakazi wa Boko na Sega ni wa hadhi ya chini (masikini) lakini wale wanaoishi Mindule ni wa kipato cha juu (matajiri).

Pia maeneo kama London, Brussels na Glosgow ni maeneo ambayo wananchi wa tabaka la juu huenda kwa ajili ya matibabu na kufanya manunuzi.

Wahusika

Tino

Mvuta Kwama

Ni mchapakazi

Ana huruma

Ana mapenzi ya kweli kwa familia yake.

Ni mcheza mpira wa miguu.

Ni baba wa Cheche, Subira na Tabu.

Mume wa Mwema.

Anapora pesa benki kwa ajili ya kumtibu Cheche.

Amani

Ni dereva tax.

Ni mchapa kazi na anahuruma.

Ana hekina na busara.

Ana mapenzi ya kweli kwa Tino na jamii kwa ujumla.

Anamsaidia Tino kupata kibali cha pesa za kigeni.

Anashirikiana na Tino kuiba pesa benki.

Brown Kwacha

Ni mkurugenzi wa Idara ya Fedha za Kigeni katika Wizara ya Fedha.

Ni mhujumu uchumi kwani hupokea na kutoa rushwa.

Anajihusisha na ujangiri.

Hana mapenzi ya kweli kwa familia yake na kwa nchi.

Anapenda starehe.

Ni mhuni anajihusisha kimapenzi na wanawake wengi.

Alifanya mpango wa kuchoma jengo la Wizara ya Fedha.

Ni tajiri.

Jinja Maloni

Ana mapenzi ya dhati kwa jamii yake.

Anafanya kazi za nguvu kama vile; kuzibua vyoo na kuchimba makaburi.

Anamuokoa mwanamke aliyekabwa na vibaka.

Ni rafiki na mwenyenyumba wa Tino.

Ni mcheshi na anapenda starehe.

Cheche

Ni mtoto wa Tino na Mwema.

Mwanafunzi

Ni mtoto mwenye tabia njema na heshima.

Ni mwanamichezo anapenda kucheza mpira na riadha.

Anavunjika kiuno wakati wa kusherehekea sikukuu ya uhuru.

Anasababisha baba yake (Tino) kujihisisha na uporaji wa fedha benki.

Anapata tiba nje ya nchi (Glasgow) na kupona kabisa.

Josephine

Ni mwanamke mrembo.

Kimada wa Brown Kwacha.

Anapenda starehe.

Hana mapenzi ya kweli.

Anafumaniwa na mke wa Brown Kwacha lakini haachani na Kwacha kimapenzi.

Ni rafiki wa Pamela.

Leila

Ni msichana mrembo.

Mfanyakazi wa shirika la ndege la Ethiopia.

Ni kimada wa Brown Kwacha.

Anapenda starehe.

Ni mchapa kazi.

Ana msimomo kwa kazi yake.

Hana mapenzi ya kweli anajihusisha kimapenzi na wanaume wengi.

Anapenda wanyama.

Shiraz Banji

Mhindi anayeishi Afrika.

Ni mfanya biashara mwenye maduka ya urembo na tax.

Ni mwajiri wa Amani.

Anashiriki biashara za magendo.

Ni mtoa rushwa.

Hana mapenzi ya kwenli kwa nchi na jamii.

Zitto

Rafiki wa Amani na Tino.

Mcheza mpira.

Anafanya kazi bandarini.

Wahusika wengine ni; Wema, mke wa Brown Kwacha, Subira, Kashogi, Fundi, John, Mzungu (baharia), Dakta Mikwala, mlinzi n.k.

Matumizi ya Lugha

Msanii ametumia lugha rahisi inayoelewa na ametumia vionjo mbalimbali vinavyoipa radha kazi yake. Vionjo hivyo ni kama vifuatavyo;

Matumizi ya Semi

Msanii amaetumia semi mbalimbali kama ifuatavyo:

  • Kapuku kama mimi (uk 121)
  • Mmetupa jongoo na mti wake (uk 64)
  • Kama mvuvi vua, usichezee mashua (uk 65)
  • Chambilecho asali haichonvywi umoja (uk 98)
  • Mtaka waridi sharti avumilie miiba (uk 98)
  • Ukiona mwenzako anyolewa, tia maji (uk. 83)
  • Asilolijua mtu ni usiku wa kiza (uk 77)
  • Bubu kasema kwa uchungu wa mwanae (uk 160)

Tamathali za Semi

Msanii ametumia tamathali mbalimbali za semi kama ifuatavyo;

Tashibiha

  • Zilper 6 ile iliunguruma kama simba dume aliyeghadhibishwa (uk. 9).
  • Maduka makubwa yalichipua mithili ya uyoga (uk. 26).
  • Miguu yake ilikaza mithili ya upinde uliotaka kufyatuliwa (uk. 33).
  • Wote walikimbilia kule wakiminyana….kama kaa wanaogombea mavi

(uk. 33).

  • Uso wa Tino uliangaza kwa muda kama radi ya kiangazi…(uk. 144)
  • Moyo wake uliimarika mithili ya tofali lililotiwa ndani ya tanuri (uk. 145).

Sitiari

  • Sote ni kobe (uk. 12).
  • Sarahange wetu mboga kweli siku hizi (uk. 15).
  • Ule si moto, jahanam (uk. 144).
  • Alikuwa tomvyara mwenye umbo la simba…. (uk. 106).
  • Brown Kwacha alikuwa kinyonga…(uk. 91).

Mbinu Nyingine za Kisanaa

Onomatopeia/Tanakali Sauti

  • Saa mezani iliendelea kugonga taratibu, ta, ta, ta… (uk. 4).
  • Akazungusha ufunguo wa gari…lakini sauti kali ikatokea ta nyenye… (uk. 10).
  • Ule upepo wa stova ulilia shshsh…. (uk. 67).

Takriri

  • Funga, shinda! funga shinda… (uk. 56).
  • Shetani! oyee! shetani oyeee!…(uk. 58).
  • Nani! Nani! Nani!…(uk. 131).
  • “Mwizi!” “mwizi!”… (uk. 151).
  • “Jambazi! “jambazi” (uk. 151).

Tashititi

  • Uhuru upi? uhuru gani? uhuru wa nini na nani? (uk. 72).
  • “Nilitaka tupate wasaa”…. “wasaa? alijifanya kushangaa (uk. 93).
  • Josephine alimuona Brown Kwacha anatoka na bado alimuuliza “….unatoka? (uk. 97).

Tashihisi

  • Utumbo ulimlaumu…(uk. 12).
  • Mvua ilirindima kwa kiburi na kuviadhibu vibati vibovu…(uk. 27).
  • …Fikra zao zilikuwa kama zimempiga change (uk. 4).
  • Mahandaki yaliyomeza matairi na kuyacheua (uk. 84).
  • Moto ule uliendelea kwa kiburi… (uk. 143).

Mubaalagha

  • Njiani kulikuwa na mahandaki yaliyomeza matairi na kuyacheua (uk 84)
  • Mtupie bata ugali wa njano ataukimbia (uk. 16).
  • Vilima vya bidhaa zile vilipungua kadri jua lilivyokweza (uk. 33).
  • Jicho alilionitupia, lingekuwa mshale saa hizi marehemu. (uk. 98).

Matumizi ya maneno ya mkopo

  • I know his case (uk. 135).
  • Appointment (uk. 90).
  • Foreign exchange (uk. 90).
  • Hey man, you will pay extra dollahs (uk. 24).
  • Inn Lillah wa Inna Ilayhi raajiuna (uk. 42).
  • Salaam aleikum mayitun (uk. 45).

Matumizi ya Kiswahili chenye Lafudhi ya Kihindi

  • Jambo bibi? (uk. 91).
  • Bana kuba ipo? (uk. 92).
  • Diyo, hata veve tafurahi (uk. 95).

Matumizi ya Taswira na ishara

Msanii ametumia taswira na ishara mbalimbali ili kufikisha ujumbe kwa hadhira yake.

Taswira

Taswira zilizotumika ni kama ifuatavyo;

  • Hospitali kuu ya Mindule ilikuwa na mchanganyika wa majengo ya zamani na machache mno ya sasa… Huku na huko kulikuwa na nyumba za kuishi watu (uk. 125).
  • Dakta Mikwala alikuwa na umri wa miaka arobaini na tano. Mwembamba kuliko kawaida… uso wake ulikuwa mwembamba kama ilivyokuwa pua yake (uk. 131).
  • Brown Kwacha hakuwa wa kuvutia kwa umbo, macho makali, pua fupi, pana, midomo yenye mbalanga… (uk 91).
  • …. Nyumba hizo zimesongamana bila ya mpangilio zimejengwa vilimani, maondeni na hata maporomoni kwenye mabonde ya mpunga (uk 27).
  • Joka la Mdimu inatupa picha ya nyoka anayeishi katika mti wa ndimu.

Ishara

  • Joka la mdimu limetumika kuashiria viongozi wanafiki.
  • Mandhari ya hospitali ya Mindule inaashiria huduma mbovu za afya.
  • Mazingira ya Sega yanaashiria umasikini.
  • Mandhari ya ofisi ya Kwacha yanaashiria maisha ya hali ya juu.
  • Ugali wa njano unaashiria ukosefu wa chakula bora.

JINA LA KITABU

Joka la Mdimu ni jina la kitabu ambalo limejengwa kwa lugha ya picha. Joka la mdimu ni nyoka aishiye kwenye mti wa ndimu na huwa na rangi ya kijani. Kutokana na rangi yake, majani ya mti hufanya asionekane kirahisi. Kwa hiyo, jina hili huashiria unafiki.

Msanii anaona kuwa unafiki upo katika jamii zetu. Watu ambao ni wanafiki ni kama vile; wafanyabiashara za magendo, viongozi, watoa rushwa na wote wanaojihusisha na mambo kama hayo.

Kwa ujumla jina la kitabu linasadifu mambo yaliyomo katika kitabu hiki. Mambo hayo yanasababishwa na viongozi na watu wanafiki ambao hawapendi maendeleo ya nchi yao hivyo kusababisha; umasikini, ukosefu wa huduma za afya, rushwa, miundo mbinu mibovu, ukosefu wa mafuta ya magari na mengine mengi kama hayo yanayofanya wananchi wajiingize katika wizi, uuzaji wa dawa za kulevya, umalaya n.k.

KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI

Kufaulu

Mwandishi amefaulu kifani na kimaudhui kama ifuatavyo;

  • Kifani

Mwandishi amefaulu kwani ametumia lugha iliyosheheni tamathali za semi na mbinu mbalimbali za kisanaa.

Pia, amefaulu kutumia mandhari yanayoonesha uhalisia wa maisha hasa ya mwananchi wa kipato cha chini pia kwa kiasi ya wa tabaka tawala.

Vivyo hivyo amejenga wahusika wanaowakilisha tabia za wanajamii wa kweli ambao hutoa ujumbe halisi.

Pamoja na hayo, ametumia mitindo na miundo mbalimbali ili kuipa uzuri kazi yake.

  • Kimaudhui

Mwandishi amefanikiwa kuonesha matatizo mbalimbali yanoaikumba jamii, sababu za matatizo hayo na ni kwa namna gani wanajamii wanaweza kuyatatua.

Kutofaulu

Mwandishi ameshindwa kuonesha utatuzi dhahiri wa matatizo yanayoikumba jamii. Pia, ametumia masuluhisho mabaya ambayo yanashadidia uovu. Kwa mfano, wizi na uchomaji