SINTAKSIA YA KISHAZI REJESHI KATIKA LUGHA YA KISWAHILI.

Utangulizi; Sintaksia ya kishazi rejeshi ni moja kati ya maeneo ya sarufi ambayo yanatoa fursa nzuri ya kueleza jinsi nadharia ya sarufi-geuzi-zalishi inavyoweza kutoa maelezo toshelevu juu ya mchakato wa urejeshi katika lugha ya Kiswahili.

Kwanza ni vema itambulike kwamba kishazi rejeshi ni kishazi tegemezi ambacho hukumusha kirainomino ambacho tayari ni kijenzi ndani ya kishazi kikuu. Kwa mujibu wa kanuni za sintaksia ya Kiswahili kirainomino kinaweza kujitokeza katika nafasi zifuatazo katika sentensi ya Kiswahili;

KIIMA; Watoto waliimba mashairi jana.

               Watoto walifundishwa vizuri jana.

YAMBWA;  Watoto wanachuma maua bustanini.

                        Maua yananukia vizuri.

YAMBIWA; Watoto walimwandikia mwalimu barua

                        Mwalimu anaumwa.

YAMBWA YA KIHUSISHI; Waashi wamejenga nyumba kwa tofali.

                                                    Tofali ni za kuchoma.

YAMBWA YA UMILIKI; Ukuta wa nyumba umebomoka.

                                                Nyumba ni ya mwalimu.

Kwa mujibu wa mifano hii ni dhahiri kuwa ili kuunda kishazi rejeshi sharti pawepo vishazi/sentensi mbili zenye nomino yenye kurejea kitu kilekile. Huku kurejea kitu kilekile ndiko kunakotoa mwanya wa kugeuza nomino mojawapo kuwa kiwakilishi rejeshi badala ya nomino kamili. Hii ndiyo hatua ya pili ya mchakato wa urejeshi.

Hatua ya tatu ni kuhakikisha kuwa kiwakilishi rejeshi kinafungashwa kwenye umbo linalokubali kukibeba. Kwa lugha ya Kiswahili, kiwakilishi rejeshi simofimuhuru bali ni kiambishi na pia umbo lake hubadilika kwa kufuatana na ngeli ya nomino husika. Maumbo ya viwakilishi rejeshi katika Kiswahili ni kama ifuatavyo;-

                Ngeli                        Umbo                                  Ngeli                            Umbo

      1                            – ye-                                         2                                -o-

      3                            – o-                                           4                               -yo-

      5                            – lo-                                          6                               -yo-

      7                            -cho-                                        8                               -vyo-

      9                            -yo-                                         10                              -zo-

      11                          -o-                                           12                              -zo-

      13                          –

Hatua ya nne ni kupachika kiwakilishi rejeshi kwenye kibebeo chake [shina la kukibeba] na mahali stahili; Katika Kiswahili vibebeo vya kiwakilishi rejeshi ni au umbo amba/au kitenzi, Yaani kiwakilishi rejeshi hutokea kama kiangami cha AMBA- kama kuna kiambishi kabla ya mzizi wa kitenzi au kiangami mwisho wa kitenzi kisicho na njeo maalumu. 

Hatua ya tano ni kuhakikishwa kuwa kiwakilishi rejeshi kinakaa mara baada ya kisabiti chake [yaani ile nomino yenye kurejea kitu kilekile]. Hapa ndipo penye changamoto kwa upande wa nomino zote ambazo katika mpangilio wakawaida hutokea baada ya kitenzi. Ili kukidhi madai ya kanuni hii ni lazima yafanyike mabadiliko makubwa ya kimfuatano baina ya vijenzi ndani ya kishazi rejeshi husika.  Rejea sentensi za namba 2 hapo juu;

  1. Watoto AMBA-O waliimba mashairi walifundishwa vizuri.
    1. Watoto walio-O- imba mashairi walifundishwa vizuri.
    1. Watoto waimba-O mashairi walifundishwa vizuri.
  1. Maua ambayo watoto walichuma bustanini yana harufu nzuri.
    1. Maua wali-yo-chuma watoto bustanini yana harufu nzuri.
    1. Maua wachuma-yo watoto bustanini yana harufu nzuri.
  • Barua ambayo watoto walimwandikia mama imepotea.
    • (?)Barua waliyomwandikia mama watoto imepotea.
    • *Barua wamwandikiayo mama watoto imepotea.

Katika urejeshi wenye kuhusu yambwa ya kihusishi na yambwa ya umiliki kuna marekebisho yanayolazimika kufanywa ili kupata sentensi yenye urari mzuri. Hii ni kwa sababu vijineno vyenye kuashiria uhusushi na umiliki haviwezi kuhamishwa pamoja na nomino husika bali hubaki nyuma na kuambatanishwa na kisiki cha kile kiwakilishi (trace) rejeshi kilichohamishiwa karibu na kisabiti chake;

Nyumba ambayo ukuta wake umebomoka ni ya mwalimu.

?? Nyumba iliyobomoka ukuta ni ya mwalimu.

?? Nyumba ibomokayo ukuta ni ya mwalimu.

Waashi walijenga nyumba kwa tofali Tofali zilikuwa za kuchoma.

Tofali ambazo waashi walijengea nyumba ni za kuchoma.

Tofali walizojengea nyumba waashi ni za kuchoma.

Tofali wajengeazo nyumba waashi ni za kuchoma.

  [Tanzania; jenga jengea]

Kishazi rejeshi bainifu na Kishazi rejeshi sibainifu (enye kutoa taarifa ya ziada).

Iko haja ya kutafiti kwa kina zaidi kama katika lugha ya Kiswahili wazungumzaji wanatambua kuwa kuna umuhimu wa kutofautisha kishazirejeshibainifu (=chenye kutambulisha/bainisha nomino ambayo kwa hulka yake ni ya jumla sana) na kishazirejeshi ambacho kinatoa taarifa zaidi juu ya kitu ambacho tayari ni bainifu.

Fikiria sentensi zifuatazo;

  1. Babangu mdogo ambaye alikuwa mgonjwa siku nyingi sasa amepatana fuu.
  2. Babangu mdogo, ambaye alikuwa mgonjwa siku nyingi, sasa amepata nafuu.

Je, unahisi tofauti yoyote baina ya sentensi hizi? [Una baba wadogo wangapi?]

D.J.Mkude