UCHAPISHAJI NA MAMBO YALIYOCHOCHEA KUTOKEA KWA UCHAPISHAJI


Wataalamu mbalimbali wamefasili dhana ya Uchapishaji na Uchapaji kama ifuatavyo.
Kwa mujibu wa Mulokozi (1993) Uchapishaji ni mbinu ya usambazaji wa habari, maarifa au fasihi kwa maandishi yaliyopigwa chapa au kunakiliwa katika nakala nyingi.
Tuki (1981) wanafasili Uchapishaji kuwa ni kazi ya kushughulika na utoaji wa vitabu na kuvitawanya kwa kuviuza kwa watu. Pia Wanafasili dhana ya Uchapaji kuwa ni kazi ya kutumia mashine au mitambo kutolea maandishi, mfano gazeti au vitabu.
Pia Ndalu na Babusa (2014) wanasema Uchapishaji ni hali ya kutoa maandishi kwa kutumia mtambo. Wanafasili dhana ya Uchapaji kuwa ni hali ya utoaji wa nakala za maandishi kwa kutumia mitambo maalumu.
Pia kwa mujibu wa kamusi teule ya Kiswahili wanafasili maana ya Unenaji kuwa ni jinsi ya kusema maneno.
Historia ya Uchapishaji na Uchapaji.
Itakumbukwa kuwa  Uandishi ulivumbuliwa Sumeria na Misri ambapo Wasumeria walitumia Cuneiform na Wamisri walitumia michoro ya picha ambayo baadae ilichanganywa na ishara za kifonetiki. Baadae taaluma hii ilienea mpaka china na kuanza kuandika kwa michoro na kuenea mashariki ya mbali kama Japani na Korea. Mnamo karne ya 11 Nchi za mashariki ya mbali China, Korea, na Japan ziligundua uchapaji wa maandishi yanayohamishika.
Mwaka 1440, Johannes Guternberg wa Ujerumani  aligundua namna ya kutengeneza herufi na michoro kwa kutumia taipu za metali zinazohamishika, ugunduzi ambao haukuwa tofauti sana na ule wa Wachina ila ulienea haraka zaidi na kutumika kwa mafanikio katika biashara. Ugunduzi wake ulisababisha utengenezaji wa herufi zinazohamishika na ambazo zingeweza kutumika kuchapa vitabu vingi.

Yafuatayo ni mambo yaliyochochea kuanzishwa kwa Uchapishaji na Uchapaji kutoka katika unenaji.
Dini.
Uwepo wa dini mbalimbali ulichochea kuibuka kwa uchapishaji na uchapaji. Mfano, Kitabu cha dini ya Buddha kiitwacho The Diamond Sutra ambacho kwa mujibu wa mtandao wa livescience kimehifadhiwa katika makumbusho ya mjini London, Uingereza kinaeleza namna mahubiri na maandishi ya dini ya Buddha ya zamani yalivyohifadhiwa. Kitabu hiki kiliandikwa mwaka 868 wakati wa enzi ya mtawala wa China aliyeitwa Tang na kilitengenezwa kwa mbao ngumu na mtindo huu ulitumika pia Korea na Japan tangu karne ya 8.          Kitabu hiki kiliandika mambo ya kidini na mikataba mbalimbali pamoja na historia.Hata wakati wa Gutenberg karne ya 14 na 15 masuala ya dini yalichochea kwani hata yeye mwenyewe aliweza kuchapisha mamia ya Biblia zilizoitwa Biblia za Gutenberg ambazo zilikuwa na mistari isiyozidi 40 kwa kila sura.
Shughuli za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Joseph Needhem (1945) anaeleza kuwa Mnamo karne ya 11 mkulima mdogo raia wa China aliyeitwa Pi Sheng alitumia mbao kutengeneza hati hamishiki ambazo alitumia kuwapasha wakulima wenzake habari mbalimbali zinazohusu kilimo. Kupitia ugunduzi huo alimtumia mwanasayansi aliyeitwa Shen Kuo kuzalisha mamia ya nakala ya hati hamishiki.Vilevile serikali ya China walitumia madini ya shaba kutengeneza na kuandika maandishi katika sarafu katika karne ya 14 na 15.
Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.
Kwa mujibu wa Mulokozi (1993) anafafanua kuwa Kadri siku zilivyozidi kwenda wanadamu walijighulisha kuboresha maisha yao ikiwemo kuboresha kazi za uchapaji. Ugunduzi wa maandishi ya shaba huko China na Korea karne ya 14 na mwanzoni mwa karne ya 15 ulirahisisha kazi ya Uchapaji hali iliyopelekea kuchapwa kwa nakala nyingi zaidi kazi na vitabu ambavyo vilisambazwa na hivyo kupelekea uchapaji kuendelea.



Kuendelea kwa Mifumo ya Kiutawala na Kisiasa.
Kwa mujibu wa Shen kuo anaelezea kuwa ikumbukwe kuwa tangu enzi na enzi maisha ya binadamu yamekuwa yakipitia mifumo tofauti tofauti hasa katika masuala ya kiutawala. Masuala ya kiutawala yalikuwa yameendelea zaidi katika nchi za Ulaya na Asia.Watawala hawa walitumia Uchapishaji ili kupata nakala nyingi ambazo zingewasaidia katika kueneza itikadi zao au hata taarifa mbalimbali za kiutawala. Kwa mfano; katikati mwa karne ya 15 iligundulika michoro iliyochorwa juu ya mbao katika Bonde la Rhine mpakani mwa Ufaransa na Italia. Wataalamu wanadai kuwa michoro hii ilionyesha mipaka ya nchi hizo na maeneo mengine ya Iberia Peninsula na  ilitumiwa na serikali ya Ufaransa  kutatua migogoro ya ardhi. Vilevile wakati wa utawala wa Kijamaa wa Yuan nchini China karne ya 14, ugunduzi wa Pi Sheng uliisaidia sana serikali kwa kueneza sera zake na hata mipango yake ilienezwa kwa watu kupitia uchapishaji wa hati hamishiki ya mbao.
Maendeleo ya Elimu.
Kwa mujibu wa Parlemo (2014) anafafanua kuwa tangu kugunduliwa kwa maandishi yapata miaka zaidi ya 5000 iliyopita, wasomi mbalimbali walijishughulisha na namna ambavyo wangeweza kuyahifadhi maarifa yao na hata pengine kuyahamishia kwa watu wengine. Jambo hili lilipelekea kwa mbinu ya Uchapaji na Uchapishaji yapata miaka zaidi ya 500 huko Ulaya mashariki na Asia ya mashariki ya mbali. Kwa mfano; miaka zaidi ya 2000 katika nchi ya Ugiriki kuliibuka Wasomi na Wanafalsafa mbalimbalia kama Aristotle na Plato ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwafundisha watu katika jamii zao juu falsafa mbalimbali za Ulimwengu na jamii kwa ujumla kupitia maandishi na michoro katika mbao ngumu kwa kuandika na wino. Hata hivyo suala la elimu linatajwa kuendelea tangu karne ya 12 katika nchi za Ulaya ambapo vyuo mbalimbali ikiwemo kile cha Paris nchini Ufaransa walichapisha taarifa za kitaaluma katika vitambaa vigumu vilivyoandikwa kwa rangi.
Pamoja na kuwepo kwa sababu nyingi zilizopelekea kuanzishwa kwa Uchapaji na Uchapishaji, Uchapishaji na Uchapaji ulipitia nyakati tofauti tofauti na katika maendeleo ya ngazi tofauti tofauti. Mwanamama Elizabeth Palermo katika kitabu chake cha Who invented Printing Press anasema uchapashaji na uchapaji ulianza yapata miaka 600 kabla ya kuzaliwa kwa Johhanes Gutenberg. Elizabeth anaendelea kutueleza kuwa, watu mbalimbali hasa viongozi wa dini walitumia mbao ngumu kuchora michoro na maneno mbalimbali yahusuyo dini katika mbao hizo kama ilivyoelezwa katika hoja iliyotangulia ya namna dini ilivyochochea uchapishaji.
Kwa maana hiyo zipo  hatua na vipindi mbalimbali ambavyo vilipitiwa katika maendeleo ya Uchapishaji na Uchapaji. Zifuatazo ni baadhi ya hatua hizo:
Mwaka 50,000 Kabla ya Kristo.
Katika historia ya Uchapaji na Uchapishaji ni muhimu kukumbuka kuwa uchapishaji ulianza kwa binadamu kuchora michoro mbalimbali ambayo pengine iliwakilisha sauti au matendo fulani. Katika kipindi hiki jamii nyingi hasa za Kiafrika ziliishi maisha ya Kijima na jamii nyingi zilitegemea uwindaji. Hoja hii inathibika kwa uwepo wa michoro mbalimbali katika sehemu za Afrika kama Irangi Kondoa Afrika mashariki na Bonde la Rhine Ulaya ya kati. Katika michoro ya mapangoni huko Irangi, kunaonekana michoro inayoonyesha watu wakiwinda wanyama ambayo imechora katika mwamba mgumu na pia michoro iliyopo Rhine ilionyesha mipaka ya ardhi kwa wakati huo.
Mwaka 3400-3200 Kabla ya Kristo.
Katika mwaka wa 3400 Kabla ya Kristo nchi ya Misri ilkwishakuwa na hati ambayo waliweza kuiandika. Katika mwaka huu Wamisri walitumia michoro ya picha iliyoitwa Hierographics wakati maandishi hasa yalivumbuliwa huko Mesopotamia (Iraq) ambapo baadhi vyanzo vya habari vinadai kuwa maandishi haya yalikuwa ni kwa ajili ya kuonyesha mipaka yake na Syria, Iraq na nchi za jirani mpaka karne ya 4 baada ya Kristo. Pia inasadikika kuwa hata jina “Mesopotamia” lina maana ya “Ardhi” kwa Kigiriki. Baadhi ya Wataalamu wa historia kama Finkelstein 1962 anadai kuwa tangu mwaka wa 5300 Kabla ya Kristo tayari Mesopotamia walikuwa katika kipindi cha zama za chuma na walitumia zaidi shaba kuunda maandishi yao ukiachilia mbali suala la kuchonga sanamu mbalimbali.
Mwaka wa 3200 K.K - 1088 B.K
Katika kipindi hiki sehemu nyingi ulimwenguni hasa nchi za Ulaya na Asia zilikuwa zimepiga hatua kubwa katika Uchapishaji. Katika nchi kama China tayari kulivumbuliwa hati hamishiki ambazo ziliweza kupangwa katika kuandika maandishi mbalimbali ingawa maandishi haya yaliandikwa katika vipande vya mbao lakini tayari hawakuwa wakitumia michoro bali herufi. Shen Kuo akinukuliwa na Joseph Needham 1954 katika kitabu chake kilichoitwa The Dream Pool Essays anadai kuwa kupitia hati hizi hamishiki kulichapwa mamia ya nakala ambazo zilihusu kilimo na watu wakazisoma. Vilevile nchi mbalimbali kama vile Ethiopia, Mexico, India, Misri, Syria na kwingineko katika kipindi hiki tayari kulivumbuliwa hati ambazo ziliwekwa katika maandishi ya kisasa yaani abjadi na picha.
Mwaka 1088 B.K -  Karne ya 15 (Wakati wa Gutenberg ).
Kama watangulizi wake waliotangulia ambao tumewatazama hapo awali Bi Sheng, Wang Chen, Baegun na wengine , Johannes Gutenberg alitamani kuiboresha kazi ya Uchapishaji na Uchapaji huku akitaka kujikita zaidi katika namna ambao kazi hii inaweza kufanyika kwa umaridadi na wakati mfupi zaidi ingawa alijua kuwa kunahitaji umuhimu mkubwa. Wanahistoria wanamwelezea Gutenberg kuwa ni kijana aliyetokea katika familia ya wahunzi wa vifaa vya dhahabu na chuma katika mji mdogo wa Strasbourg nchini Ujerumani. Yeye aliandelea na mfumo wa watangulizi wake wa kutumia mbao ingawa alizikata katika vipande vidogo vidogo kulingana na herufi na alama mbalimbali za uandishi.
Baadaye Gutenberg alikata vipande vya chuma na kuzichonga herufi moja moja na kutengeneza hati hamishiki. Baada ya kufanikiwa katika hili, aliweza kugundua kuwa kumbe angeweza kutengeneza wino kwa kutumia rangi na mafuta tofauti na watangulizi wake wakina Bi Sheng, Shen Kuo na wengine ambao walitumia maji pamoja na rangi.
Kadri siku zilivyokwenda Gutenberg alifikiri kuboresha kazi yake ya uchapishaji, safari hii alikuja na wazo la kuziunganisha zile herufi za chuma katika mstari mmoja kwa kupitia skuruu na kuwa kama sentensi kabla kugundua kuwa angeweza kupaka wino juu ya zile herufi katika mstari kisha akachuku karatasi na kuibandika kwa juu na kuitoa ikiwa ina maandishi yanayosomeka.
Kwa ujumla kutokana na hatua hizi zote mpaka wakati wa Gutenberg, jamii zilipata uzoefu na namna ya kutengeneza maandishi na kufanya kazi ya Uchapaji na Uchapishaji kwa ufanisi. Ingawa ugunduzi wa Gutenberg ulionekena kama ni hatua kubwa zaidi kuwahi kufikiwa, Uchapaji huu wa Gutenberg haukupendwa kutumiwa na mataifa mengi ya Ulaya na Asia. Hii ilitokona na sababu kuu tatu.
Kwanza, kwa wakati huo jamii za Ulaya na Asia zilikuwa na hati nyingi hivyo kutumia mbinu ya Gutenberg kungetumia muda mrefu kuandaa vitabu na machapisho.
Pili, kwa kuwa aina hii ya Uchapishaji ilitumia chuma, jamii na watu wa nchi hizi waliogopa kutumia gharama. Tatu, kwa kuwa Uchapishaji huu ulitumia nguvu za mikono, nguvu nyingi ilitumika pia vitabu viliuzwa ghali sana. Hali hii ilipelekea jamii nyingi kupendelea zaidi mfumo ule wa awali wa kuandika juu ya mbao na vitambaa.














MAREJELEO
Finkelstein, D. (1962). Social Justice in the Ancient World. Amazon: Greenwood Publishing           
                                     Group.
Mulokozi, M. M. (1993). Fasihi, Uandishi na Uchapishaji. Dar es salaam: Dar es salaam
                                         University Press.
Ndalu E. A. & Babusa H. (2014). Kamusi teule ya Kiswahili. Kilele cha Lugha. Kenya:
                                                       East African Educational Publishers Ltd.
Palermo, E. (2014). Who Inveted Printing Press. Washington: Washington University Press.
Shen Kuo. (1088). The Dream Pool Essays. China: Sichuan People’s Publishing House 2008.
TUKI. ( 1981). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: Oxford University Press.