Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akizungumza na waandishi wa habari alipotangaza JKT na mgambo kufika ofisini kwake  kupatiwa ajira ya kusimamia usafi na kuwatoza faini wachafuzi wa mazingira jijini.  
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  amewataka vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo ambao hawana  kazi kufika ofisini kwake Ijumaa ya Julai 06 mwaka huu ili  kupatiwa ajira ya kusimamia usafi na kuwatoza faini wachafuzi wa mazingira katika jiji la Dar es Salaam.


Makonda amesema katika fedha itakayotozwa kwa wachafuzi wa mazingira asilimia 50% itakwenda kwenye halmashauri na asilimia 50% kwa vijana wa JKT na mgambo ambapo kabla vijana hao hawajakabidhiwa jukumu hilo watapewa mafunzo ya sheria ya usafi.


“Katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana sambamba na kuufanya mji kuwa katika hali ya usafi baada ya mbinu nyingi zilizokuwa zikitumiwa  kuhamasisha usafi kutokuwa na matokeo mazuri,  kwa hilo tunakwenda kuona Dar es Salaam ikiwa safi,” alisema Makonda.

Ameagiza pia makampuni yote yaliyopewa tenda ya usafi kwenye mkoa wake  kuanzia ngazi ya mitaa, kata na halmashauri kufika ofisini kwake Jumatano ya Julai 04  mwaka huu yakiwa na mikataba yao kwa ajili ya kujiridhisha uwezo wao wa kufanya kazi baada ya uchunguzi aliofanya kubaini uwepo wa kampuni zilizopewa tenda kubwa wakati hazina vifaa vya kutosha.


Hata hivyo Makonda ameziagiza Manispaa zote za jiji lake kuhakikisha kila mfanyabiashara na vituo vya daladala vinakuwa na sehemu ya kuweka taka.

Pia ametangaza fursa kwa wadau wenye vyoo vya kuhama (mobile toilet) kufika ofisini kwake ili wakutanishwe na halmashauri kwa ajili  ya kuweka makubaliano ya ushirikiano ili kuondoa tabia ya watu kujisaidia kwenye kuta na vichochoro.


Alisema, miongoni mwa majukumu ya vijana hao ni kuhakiki makampuni kwenye mitaa kama yapo na yanafanya kazi kweli, kujua wananchi wanapeleka wapi takataka, kukamata watupaji wa taka na kuwatoza faini ambapo kama mtu hana pesa atapewa adhabu ya kufanya usafi wiki nzima chini ya usimamizi mkali.