CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI
(TATAKI)

IDARA YA FASIHI, MAWASILIANO NA UCHAPISHAJI
KF: 204 FALSAFA YA KIAFRIKA NA NADHARIA YA FASIHI

SWALI:
Pamoja na mabezo mengi (hasa kutoka kwa G.W.Hegel) waliyorundikiwa Waafrika; bado Waafrika wenyewe wana tunu na lulu za kujivunia kifalsafa (Tumia jamii ya Wadogon kutoka Mali. Jadili dai hilo kwa mifano kuntu ya kitaaluma)

Falsafa ni neno la Kigiriki lenye ya maana upendo wa hekima. Ni jaribio la kuelewa na kueleza ulimwengu kwa kutumia akili inayofuata njia ya mantiki. Falsafa huchunguza mambo kama kuweko na kutokuweko, ukweli, ujuzi, uzuri, mema na mabaya, lugha, haki na mengine yoyote.[1]
Falsafa inazungumzia mfumo wa maisha tunayoishi kwa upana zaidi, pia ni kiongozi katika maisha kwa sababu masuala inayoyachambua ni ya msingi na yenye kuenea sehemu zote.[2]

Ni kweli kabisa kwamba mabezo mengi wamerundikiwa Waafrika kutoka kwa watu mbalimbali wenye mawazo ya kikoloni. G.W Hegel ni mojawapo wa watu ambao wametupa mabezo mengi sana. huyu alikuwa ni mwanafalsafa wa Kijerumani aliyeamini katika mtazamo wa kidhahania”[3]
Hata hivyo pamoja na mabezo hayo, wataalamu mbalimbali wenye mawazo ya mkondo wa  kama vile  Placide Frans Tempels (1906 - 1977) wamekanusha vikali hoja za Hegel kuhusu Waafrika. Mwenendo wa maisha ya waafrika kabla ya ukoloni yanaonyesha kupinga pia mawazo ya Hegel. Hivyo pamoja na mabezo hayo bado Waafrika wana falsafa ya kijivunia.  Mfano mzuri ni kabila la Wadogoni.
Wadogoni ni kabila moja la watu wanaoishi Mali. Mwanzoni walikuwa wakiishi katika milima ya Bandiagara na wakati huo walijulikana kama wakaaji wa milimani. Wao wana  utamaduni wao unaoonesha falsafa yao na mfumo maisha kwa ujumla.
Kwa kuangalia kabila la Wadogoni na maisha yao kwa ujumla, hoja za Hegel na wafuasi wake zinakuwa hazina nguvu hata kidogo. Sasa tutaangalia mabezo ya Hegel na moja kwa moja tutahusianisha na kabila la Wadogoni ambapo tunaona mifano ya tunu za kifalsafa za Kiafrika.
Hegel alibeza kuwa Afrika haina Mungu na hivyo hata watu wanaoishi hawana Mungu ndiyo maana ni makatili, hawana huruma na wako tayari kuuana wakati wowote.[4] Hoja hii imejaa uongo mwingi, kwani kabila la Wadogoni tangu zamani wamekuwa na Mungu wao Ama[5] nao huendelea kuwa waaminifu mno kwa ajili ya ibada ya mababu zao. Ama ni Mungu mkuu ambaye anafuatiwa na wengine wadogo zake.
Vile vile Wadogoni wana ibada za aina nyingi sana katika makazi yao, wanapokuwa katika kipindi cha kulima huwa wanaomba Mungu wao wa baraka ili awasaidie katika kilimo na kumuuliza kama mwaka utakaofuata utakuwa wa neema au la.[6]
Hegel anakaza kwamba Mungu wa wakristo ndiye Mungu wa kweli katika dunia hii, wengine wote sio Mungu. Mawazo haya yanadhilishwa na Fieser, J. (2009:42) wakati akinukuu mawazo ya Hegel kwamba “ ukiristo ndiyo dini bora zaidi” kwa kumwelezea Mungu, na Yesu ni mtu wa pekee. Hata hivyo ukiendelea kuchambua utagundua kwamba Hegel amekuwa na mkanganyiko mkubwa sana kuhusu fundisho la wakristo la utatu.
Wadogoni wamekuwa na dhana ya Mungu kwa muda mrefu sana. Ukiachilia mbali suala la Mungu Ama, pia walikuwa na miungu ambayo ilikuwa imegawana majukumu kuhakikisha kwamba Wadogoni wanakuwa salama.
Bezo lingine ni kuwa hakuna ulimwengu wa Kiafrika bali  kuna Afrika katika vitabu ambayo si katika uhalisia wake. Pia anaendelea kusema kuwa Afrika si sehemu ya historia ya kiulimwengu maana hakuna lolote lilifanyika Afrika, hivyo Afrika sio bara la kihistoria[7].
Hoja hii nayo inadhilisha uongo wa akina Hegel, hii inatokana na kwamba Wadogoni wamekuwa na historia kubwa na maendeleo. Wadogoni wamekuwa na historia ndefu kabla ya kuvamiwa na waislam. Kihisoria, walifika katika eneo la Bandiagara walikimbilia katika eneo hili kutokana na kuepuka uisilamu kwani  wengi wao hawakutaka kusilimishwa kwa sababu walikuwa na dini zao za kijadi.[8] Hivyo kusema kwamba Waafrika hawana historia au eti kwamba historia yao ni ya kwenye kitabu tu ni jambo ambalo sio sahihi kwani “ni mojawapo ya bara kati ya mabara saba yaliyopo duniani, jina la Afrika lilitoka na lugha ya kilatini ya Waroma…na asili yake ni kabila la Afriglililoishi sehemu za Tunisia.”[9]
Duquette, (2003) akifafanua mafundisho ya Hegel  anasema kuwa Hegel amewahi kudokeza kuwa inawezekana kabisa India kuiweka katika historia lakini kamwe Afrika haiwezi kuingia katika historia. Hoja hii ni butu kwa sababu Waafrika wamekuwa na historia ndefu sasa kusema kwamba leo hawana historia ilikuwa ni aina fulani ya kuhalalisha ukoloni katika bara la Afrika kwa madai kwamba wanataka kuleta historia kwani tumeona hapo juu namna Wadogoni wamekuwa na historia ndefu.
Hoja ya Hegel na wafuasi wake kwamba waafrika hawafikirii mambo za kiroho inapingwa vikali . Wadogoni katika dini yao wanaamini kwamba vitu vyote vya asili na nguvu vina roho iliyo hai. Katika ulimwengu wa wadogoni kila kitu kinachowazungumka kina maana yake. Mfano mti wa mbuyu huwa haukatwi wala kuuzwa kwani ni mti unaotumika kutambikia, wanyama kama vile mbweha, nyoka, na mamba [10]
Kabila la wadogoni limejulikana sana kwa elimu ya nyota. Inasemekana kwamba Wadogoni kwa miaka mingi wamekuwa wakiitaja nyota aina ya Sirius katika simulizi zao, hata hivyo kinachowashangaza wanasayansi ni kwamba nyota hii haionekani kwa macho ya kawaida. Wadogoni waliijua nyota hii hata kabla ya wataalam kutoka Magharibi hawajavumbua vifaa vya kuona nyota kwa mbali. Jambo ambalo wakoloni walipokuja waliwaambia Wadogoni kwamba utaalamu wao wa kuangalia nyota ni wa kishirikina na kichawi[11]. Mambo haya yako wazi kabisa kwamba ni tofauti na mawazo ya akina Hegel.
Wadogoni wana desturi ya kutahiri watoto wao wa kiume wenye umri kuanzia miaka tisa hadi kumi na mbili, na tohara kwa watoto wa kike wenye umri kuanzia miaka saba hadi nane.[12]Hii inaonyesha kwamba watu hawa walikuwa makini na familia zao, walifikiri juu ya familia na kupanga utaratibu wa namna ya kuishi katika familia. Kinachotofautisha hapa ni kwamba kila utamaduni unafaa kwa watu wake. Si lazima utamaduni wa watu fulani umfae kila mtu.
 Hivyo basi ni wazi kuwa kutokana na jamii ya wadogoni, jamii za kiafrika zilikuwa na falsafa yao tofauti na mawazo ya Hegel. Hegel hatambui Ujumi mweusi ambao huchunguza kanuni au mtazamo wa binadamu kuhusu uzuri, mila na desturi[13], yeye alitaka mila na desturza kizungu zifuatwe. Hivyo waafrika wana tuna ya kujivunia kifalsafa. Hata hivyo tunapaswa kukumbuka kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaonekana kuzidi kuondoa utamaduni wa waafrika na falsafa yao na kuendelea kukumbatia falsafa za watu wa magharibi na kusahau kabisa falsafa ya kiafrika. Hii ni changamoto kwetu sote.








MAREJELEO
Changamotoyetu.blogspot.com/…/jungu imepakuliwa tarehe 29/12/2013 saa 2:00 usiku
Bakize, L. (2013).Ujumi Mweusi.(notisi za mihadhala ya darasani)
Dogon People, Wikipediaen.wikipedia.org/wiki/Dogon_people 29/12/2013 saa 2:14usiku
Dogon TraditionsCustoms.com, traditionscustoms.com/people/dogon 29/12/2013 saa 4:30 usiku
Dogon Tribe History, Culture and African art - For Africa imepatikana katika .www.forafricanart.com/dogon_tribe.html 30/12/2013 saa 2:00asubuhi
Duquette, D.A.(2003). Hegel’s History of philosophy. New interpretation. USA: University of New York Press, Albany
Fieser, J. (2009).Art, Myth and Society in Hegel’s Aesthetics. London: Continuum International Publishing Group
Georg Wilhelm Friedrich Hegel - Wikipedia, the free encyclopedia en.wikipedia.org/wiki/ tarehe 2/1/2014
Hegel, G.W.F. (n.d)The Philosophy of History. inapatikana katika www.scribd.com/.../G-W-F-Hegel-The-Philosophy-of-History-imepakuliwa 1/1/2014
John, I.(2005).Hegel’s Idea of The Absolute and African Philosophy. Iliyopatikana Katika htt://www.frauzu.com/.imepakuliwa tarehe 30/12/2013 2:00
Olufemi, T. (n.d ) Exorcising Hegel's Ghost: Africa's Challenge to Philosophy. inapatikana katika www.africa.ufl.edu/asq/v1/4/2.htm tarehe 1/1/2014
Pays Dogon, Dogon Country » People and Culture. Iliyopatikana katika www.dogoncountry.com/about-pays-dogon/people-and-culture 4/1/2014
Philosophy. Meaning. Imepatikana katika www.atlassociety.org/ what_ is_ philosophy
Siyantemi, R.( n.d) Bara la Afrika. Julias Nyerere, Nelson Mandela na Kwame Nkrumah. DVD .African creative
Unique Dogon Culture Survives in West Africa iliyopatikana katika http/.www.news.nationalgeographic.com/news/2003/05/0529_030529_dogon.html. imepakuliwa tarehe 3/1/2014
Wikipedia kamusi elezo huru en.wikipedia.org/wiki/Philosophy. Imepakuliwa  2/1/2014: 2:00am





[1] Wikipedia kamusi elezo huru en.wikipedia.org/wiki/Philosophy
[2] www.atlassociety.org/ what_ is_ philosophy
[3] Georg Wilhelm Friedrich Hegel - Wikipedia, the free encyclopedia en.wikipedia.org/wiki/
[4] Dogon Culture Survives in West Africa..John Inyanga.htt://www.frauzu.com/
[6]news.nationalgeographic.com/news/2003/05/0529_030529_​dogon.htm
[7] Ibid (kile kile kilichotajwa)
[8] Dogon Tribe History, Culture and African art - For Africa .www.forafricanart.com/dogon_tribe.html
[9] Siyantemi Renatus( n.d) Bara la Afrika. Julias Nyerere, Nelson Mandela na Kwame Nkrumah. DVD .African creative
[10] Dogon TraditionsCustoms.com, traditionscustoms.com/people/dogon
[11]  changamotoyetu.blogspot.com/…/jungu
[12] Dogon People, Wikipediaen.wikipedia.org/wiki/Dogon_people
[13] Bakize, L. (2013).Ujumi Mweusi.(notisi za mihadhala ya darasani) 
Asante kwa kusoma Masshele blog karibu tena