Ligi Kuu soka Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea Ijumaa, Disemba 29 baada ya mapumziko ya takribani wiki tatu kupisha michuano inayosimamiwa na baraza la vyama vya soka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati 'CECAFA Challenge' iliyomalizika nchini Kenya wiki iliyopita kwa wenyeji, Harambee Stars kuwa mabingwa wakiwafunga Zanzibar katika fainali.
Ratiba inaonesha kuwa siku hiyo ya Ijumaa, kutakuwa na mchezo mmoja kwa mabingwa mara moja wa taji hilo Azam FC ‘Wanarambaramba’ kuwa wenyeji wa Stand United ‘Chama la Wana’ mchezo ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku.
Jumamosi kutakuwa na michezo mitatu, Lipuli FC ‘Wanapaluhengo watacheza na na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Samora, Iringa kuanzia Saa 8:00 mchana, huku Mtibwa Sugar na Maji Maji wakicheza kwenye uwanja Uwanja wa Manungu complex, Turiani, Morogoro.
Mchezo wa Tatu siku hiyo  Ndanda FC ‘Wanakuchele’ watakuwa na kibarua kizito pale watakapomkaribisha Mnyama Simba SC katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mechi za Jumapili.
Jumapili, mabingwa watetezi, Dar Young Africans watakuwa wageni wa Mbao FC ‘Wabishi’ katika uwanja mgumu wa  CCM Kirumba, uliopo Jijini Mwanza wakati Njombe Mji FC wataikaribisha Singida United kuanzia saa 8:00 mchana katika Uwanja wa Saba Saba, uliopo Njombe.
Mechi za kukamilisha mzunguko wa 12 zitachezwa mwaka mpya, Januari 1 ambapo Mbeya City ‘Wanakomakumwanya’ watacheza na Kagera Sugar ‘Wanankurukumbi’ katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya  na Mwadui wakiikaribisha Ruvu Shooting katika uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga.
Itasimama tena.
Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi ambapo mechi zake zitachezwa kati ya 13 na 17, mwakani.
Ratiba ya VPL Kwa Ufupi.

Disemba 29, 2017.
Azam FC Vs Stand United.
Disemba 30, 2017.
Lipuli FC Vs Tanzania Prisons.
Mtibwa Sugar Vs Maji Maji FC.
Ndanda FC Vs Simba SC.
Disemba 31, 2017
Njombe Mji Vs Singida United.
Mbao FC Vs Young Africans.
Januari 1, 2018.
Mbeya City Vs Kagera Sugar.

Mwadui FC Vs Ruvu Shooting.
Asante kwakusoma masheleblog