Watu wawili wakazi wa wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wamefariki dunia baada ya kula nyama ya ng'ombe anayesadikiwa kuwa na ugonjwa wa kimeta huku wengine zaidi ya watu 30, wakilazwa hospitalini.


Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mtu mmoja anayedaiwa kujifanya mtaalamu wa mifugo na kuthibitisha nyama hiyo ni salama, mtu huyo yupo mahututi katika Hospitali ya Ngoyoni Rombo.

Taarifa iliyotolewa jana Alhamisi Oktoba 21, 2021 na Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai, amesema watu hao walikula nyama hiyo Oktoba 6, 2021 baada ya mtu aliyejifanya mtaalamu wa mifugo kuthibitisha nyama hiyo ni salama na kuipiga mihuri feki.

Kagaigai amesema zaidi ya watu 30 waliokula nyama hiyo waliathirika ambapo wawili wamefariki dunia, huku wengine wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Ngoyoni iliyopo Wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

"Oktoba 6, 2021, eneo la Mamsera, nyumbani kwa mwananchi mmoja, kulikuwa na Ng'ombe watatu na mmoja alikufa, mtu moja alijitokeza kuwa ni mtaalamu wa mifugo akathibitisha ng'ombe yule alikuwa mzima hana matatizo akagonga na mihuri ambayo nafikiri ilikuwa feki,"amesema RC Kagaigai.

"Baada ya kuchinja, mtu yule alianza kuugua, na waliokula nyama ile wote wakaanza kuugua, ikawekwa mashaka na walipofuatilia ikaonekana kuna dalili za kimeta,"amesema na kuongeza kuwa tayari Serikali imechukua hatua mbalimbali.

Chanzo :Jamii