SOMO LA PILI

 ISBN NA MSIMBOMILIA/BAKODI (BARCODE)

Wapendwa, karibuni katika somo letu la pili. Mara nyingi tumekuwa tukiona vitabu mbalimbali vikiwa na vinambanamba na vimistari vilivyosimama (hasa nyuma ya jalada). Kwa kuwa tumedhamiria kuandika kitaalamu ni vizuri tukafahamu mambo haya ili hata tukiulizwa na wasomaji walau tuwe na majibu.

*ISBN ni kitu gani?*
ISBN ni kifupi cha maneno ya Kiingereza *International Standard Book Number.* Maneno hayo yanamaanisha nini? *Kwa ufupi kabisa ISBN ni namba za kipekee (unique) za kimataifa ambazo huwekwa kwenye kitabu ili kukipa utambulisho binafsi.* Hii ni sawa na kusema kwamba ISBN inayowekwa kwenye kitabu chako ina namba ambazo hazifanani na namba za kitabu kingine chochote duniani. Namba hizo, kimantiki, zinalenga kusajili kitabu chako kimataifa.

*ISBN zilitoka wapi?*
Vyanzo mbalimbali vya taarifa, vinadai kwamba muundo wa ISBN ulibuniwa mwaka 1967 huko Uingereza na mtu anayeitwa *David Whitaker.* Huyo ndiye anayeheshimiwa kama baba wa ISBN. Mwaka 1968, mfumo wa ISBN uliingizwa huko Marekani na mtu anayeitwa R.R. Bowker. Huyo akawa wakala/ajenti wa ISBN huko Marekani. *Kwa hiyo, kwa sasa, kila nchi duniani ina mawakala wa ISBN. Kwa Tanzania, ajenti wa ISBN yuko Maktaba Kuu ya Taifa.* Ukienda pale utakutana na BODI inayoitwa *Tanzania Library Services Board (TLSB).* Bodi hiyo ndiyo Wakala wa ISBN. Ndiyo maana sasa, ukitaka kupata namba hiyo lazima uende huko ukasajiliwe kama mwandishi au unaweza kuipata kupitia Mchapishaji wako.

Aidha, kuna simulizi nyingine nyingi kuhusiana na asili ya ISBN. Vyanzo vingine vinaeleza kwamba ISBN ilitokana na SBN (Standard Book Numbering system), ambao ulikuwa ni mfumo wa kusajili vitabu huko Uingereza ulioanzishwa na Chama cha Wachapishaji na Wasambazaji. Kwamba, baadaye kuna michakato ilifuata ikisukumwa na UNESCO na wadau wengine wa elimu, na hatimaye kuja na mfumo huo wa ISBN ambao ni wa kimataifa zaidi ya ule wa mwanzo. Kwa minajili ya somo letu, vyanzo mbalimbali vya simulizi tofauti kuhusiana na asili ya ISBN visitupatie shida. *Hoja yetu kubwa tu iwe ni kufahamu maana ya ISNB na inasaidia nini kwenye tasnia yetu ya uandishi.*

Ukienda kusajiliwa kama mwandishi kule Maktaba Kuu, unaambiwa kwamba kila utakapotaka kuchapisha kitabu njoo uchukue ISBN. *Naomba nieleweke kwamba kila kitabu kina ISBN yake. Hivyo, kuchukua ISBN ya kitabu kimoja na kuipachika kwenye vitabu vyako vingine ni kosa ambalo halitarajiwi kabisa.* Ukifanya hivyo, maana yake unauambia mfumo wa utambuzi duniani kwamba vile vitabu vyote ulivyopachika ile ISBN ni kitabu kimoja hichohicho. *Kwenye maktaba yetu ya EWCP, tuna waandishi ambao wamefanya kosa hili (sitaji hata mmoja kwa sababu ya maadili). Kwa kuwa sasa tumefahamu, tusifanye kosa hilo na pia tuwaelekeze wengine.*

Usajili wa mwandishi kule Maktaba Kuu hufanyika mara moja tu. Ukishajisajili na kulipia *sh. 30,000/=* (kama haijabadilika), utakapokuwa unakwenda kuomba namba za ISBN kwa ajili ya vitabu vyako, utakuwa unapewa bure kabisa. Hakuna malipo kwa sababu ISBN zinatolewa bure. Kwa mchapishaji binafsi, unaweza kupewa kifurushi cha ISBN za vitabu 10 kwa wakati mmoja. Unashauriwa kuzitumia na siyo ukahifadhi nyumbani. Kama ni Kampuni ya uchapishaji, yenyewe inaweza kupewa mpaka ISBN za vitabu 100 kwa wakati mmoja.

Kabla ya mwaka 2005, namba za ISBN zilikuwa chache. Baada ya mwaka 2005, utabaini kwamba namba ziliongezeka na kuwa 13. Katika namba hizo nyingi, kuna namba zinazotambulisha nchi na pia kuna namba zinazomtambulisha mchapishaji/mwandishi.

*BARCODE (tuiite BAKODI) ni kitu gani?*
Kwanza, kwa uchapishaji wa siku hizi bakodi katika vitabu huunganishwa na ISBN. Hivyo, ni vizuri kama tutakuwa tunaiita Bakodi ya ISBN. Kimaana, *Bakodi, ni mfumo wa kikompyuta ambao unawezesha data za namba kuwakilishwa katika umbo la kuonekana kwa macho (kama michoro ya mistari iliyosimama) na namna inayoweza kutambuliwa na kusomwa na mashine maalumu za kielekroniki.* Mashine hizi zinazosoma Bakodi huitwa *Barcode readers.*

Bakodi ni mfumo wa kibiashara unaotumiwa hivi sasa katika kuhifadhi taarifa za bidhaa kikompyuta na kuziuza kwa mfumo wa kisasa zaidi. Kwa hiyo basi, *Bakodi ya kitabu inalenga kuhifadhi taarifa za kitabu chako kibiashara.* Maana yake sasa, Bakodi zinawasaidia zaidi wauzaji wa vitabu wanaouza katika maduka ya kisasa ambapo kumbukumbu za bidhaa huhifadhiwa kielekroniki. Kitabu chako kikiwa kinauzwa kimataifa, *maana yake mtu akimulika mashine kwenye Bakodi ya kitabu chako atapata bei na taarifa nyinginezo.* Kwa hiyo, Bakodi inalenga kusajili kitabu chako na kukipa namba za utambuzi.

Kwa taarifa yako Bakodi nyingi za kitabu hutengenezwa kutokana na namba za ISBN za kitabu chako. *Wataalamu wanachukua namba za ISBN yako na kuziingiza kwenye Kompyuta yenye programu maalumu. Kisha namba hizo hujitokeza kama picha za mistari ili mashine iweze kusoma na kupata taarifa.*

Tena, kwa taarifa yako, Bakodi zinatolewa bure kule Maktaba Kuu ya Taifa. *Ukienda kuomba ISBN ya kitabu chako, mwambie mhudumu kwamba naomba ISBN zisomeke kwenye Bakodi.* Hapo watakuambia uwaachie baruapepe (email) ili mhusika akutengenezee na kukutumia mara moja. Hautalipia chochote kama ulishasajiliwa kama mwandishi au mchapishaji.

Aidha, kuna watu mitaani wana programu za kupakua mitandaoni, ambazo zinaweza kutengeneza Bakodi. Ukiwaona hao watakutengenezea na kukutoza pesa kama 100,000/= za Kitanzania. *Sasa kuanzia leo usiibiwe tena. Bakodi inatolewa bure kule Maktaba kuu ya Taifa, kule posta.*

*ISBN na BAKODI PAMOJA*
Nikiwa na kipicha cha Bakodi naweza kuelewa namba za ISBN na Bakodi yenyewe? Kama nilivyobainisha hapo awali, mchoro wa Bakodi na ISBN vinapaswa kuwa pamoja kwa sababu Bakodi imetokana na ISBN.

Ikiwa ISBN na Bakodi viko pamoja, basi tutakuwa na sehemu kuu tatu.

1. Utaona namba za ISBN juu. Hizo zimewekwa kwa namna ya kusomeka kwa macho ya anayetazama.

2. Utaona vimichoro kama mistari chini yake. Hiyo ndiyo misimbo (code) au alama ambazo sasa husomwa na mashine. Wewe kwa macho unaona ni vimisitari vilivyosimama. Lakini mashine ikisoma yenyewe itapata taarifa za bidhaa husika. Taarifa zinaweza kuwa *mahali bidhaa ilipotengenezwa, mwaka wa kutengenezwa, bei ya bidhaa husika, n.k.*

Namba zitakazoonekana juu ya Bakodi na chini ya Bakodi zitakuwa katika mafungu tofauti. *Zile za ISBN zitakuwa juu katika mafungu matano.* Namba zikishawekwa kwenye Bakodi, utaona zikiwa *chini katika mafungu matatu.*

Yako mengi sana ya kusema kuhusiana na ISBN na Bakodi. *Lakini haya ni machache tu ambayo nimekuandalieni ili walau mpate maarifa muhimu kuhusiana na uandishi na uchapishaji wetu.*

MWISHO WA SOMO LA PILI
================

*© L.H. Bakize (11/03/2020)*
*(EWCP na Ushirikishanaji Maarifa)*