mashele Swahili
info.masshele@gmail.com
www.masshele.blogspot.com


Dhana ya vikoa vya maana
Vikoa vya maana ninini?
Umuhimu wa vikoa vya maana
Sifa za vikoa vya maana
Marejeleo kuhusu vikoa vya maana
Vikoa vya maana PDF.



Utangulizi
Swali hili limegawanyika katika sehemu tatu, utangulizi, kiini na hitimisho. Utangulizi unajumuisha ufafanuzi wa nadharia ya vikoa vya maana, fasili mbalimbali ya vikoa vya maana pamoja na maelezo mafupi kuhusu vikoa vya maana pamoja na sifa za vikoa vya maana, katika kiini maelezo kuhusu umuhimu wa vikoa vya maana na mwisho ni hitimisho la swali.
Nadharia ya vikoa vya maana imeasisiwa na Mjerumani Jost Strier (1930) akiegemea katika msingi wa kusema kuwa kuna maneno yanayofanana yanaweza kuwekwa pamoja. Mawazo haya ya Strier, Lyons (1970) anadai kuwa hayakuwa mawazo ya Strier bali yalikuwa ni ya Mjerumani mwenzake Von Hambolt. Wataalamu wengine waliokubaliana na mawazo ya Strier ni pamoja na Idsen, Jolls pamoja na Gao na Xu (2013). Hivyo basi, fasili ya vikoa vya maana imetolewa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo:
1.1 Fasili ya Vikoa vya Maana
Resani (2014) anasema vikoa vya maana ni seti au kifungu cha maneno kilicho katika mpangilio fulani, au ni seti ya maneno yanayowekwa pamoja kwa njia fulani hususani kwa kuzingatia uhusiano wa kimaana. Kwa mfano, neno mnyama ni kikoa cha binadamu, simba, chui, mbwa, nyati, nyani, sungura na wengine wengi. Kutokana na fasili hii inaonesha udhaifu kwani haioneshi dhahiri mpangilio wa vikoa kwamba ni kikoa kipi kinaanza na kipi kinafuatia.
Hambwe na Karanja (2004) wanasema kikoa cha maana ni mahusiano ya kimuundo ambapo kuna ufinyu na upana wa maana, ambapo neno moja tu hutumika katika lugha fulani na kutaja kitu ambacho hutajwa kwa maneno mawili au zaidi katika lugha nyingine. Kwa mfano neno Uncle katika lugha ya Kiingereza ni neno lenye maana pana ambapo ndani yake hujumuisha maneno mengine kama vile mjomba, baba mdogo na baba mkubwa lakini katika Kiswahili neno hili lina maana finyu ambalo ni mjomba. Kutokana na fasili hiyo dhana ya ufinyu na upana wa maana ni katika idadi ya maana zinazopatikana katika vikoa vinavyoambatana na kikoa hicho.
Kwa ujumla, vikoa vya maana ni seti za maneno zenye maana zinazohusiana ambazo maana zake zinategemeana, na kwa pamoja zinatoa dhana ya kimuundo yenye uhalisia ndani yake. Kwa mfano miti ni kikoa cha maneno mengine kama mchongoma, mkaratusi, mparachichi, mchungwa, mwembe, na mingine mingi.
1.2 Uhusiano wa Kiwima na Kimlalo katika Vikoa vya Maana
Kwa mujibu wa Resani (k.h.j), vikoa vya maana huweza kuwa na mahusiano ya namna mbili. Mahusiano ya kiulalo na mahusiano ya kiwima. Mahusiano ya kiwima ni mahusiano yanayoruhusu maneno kubadilishana nafasi na neno jingine hasa yale yanayokubali kupokea nafasi hiyo huwa ndiyo yenye maana.
                        Kwa mfano:  Chakula - ugali, kande, ndizi, wali, tambi
                                              Udongo - mfinyanzi, kichanga, tifutifu.
                                              Vitafunwa - maandazi, chapati, vitumbua, sambusa, kachori.
Vilevile uhusiano wa kiwima yanayotokea katika vipashio vya tungo. Mahusiano haya uhusu neno kubadilishana nafasi ileile na neno jingine katika tungo. Mathalani, katika tungo nomino inaweza kubadilishana nafasi na nomino ama kiwakilishi kulingana na sentensi.
              Kwa mfano:  Mwalimu anafundisha Kiswahili
                                  Mwanafunzi anafundishwa Kiswahili
                                 Yule anajifunza Kiswahili
                                 Maji anajifunza Kiswahili
                                yote anajifunza Kiswahili
Katika mifano hiyo hapo juu, maneno kama mwalimu, mwanafunzi na yule yanaweza kuchukuliana nafasi, hivyo yana uhusiano wima, lakini maneno maji na yote hayawezi kuchukua nafasi ya maneno ya juu, hii ni kwasababu hayawezi kubadilishana nafasi.
Vilevile, mahusiano ya kimlalo ni yale ambayo vipashio huwa nayo kwa kutokea pamoja na vipashio vingine. Mahusiano haya ni ya kimfuatano au namna yanavyopangana katika tungo.
        Mfano1: Mwanafunzi mrefu amechelewa shuleni.
Katika mfano huo kuna uhusiano kati ya ‘mwanafunzi na mrefu’, ‘chelewa na shule’, ‘mwanafunzi na kuchelewa’.
        Mfano 2: Msichana mzuri ameolewa na mwanaume tajiri.
Katika mfano huo, mahusiano yaliyojitokeza ni kati ya ‘msichana na mzuri’, ‘msichana na olewa’, ‘olewa na tajiri’.
1.3 Sifa za Vikoa vya Maana
Vikoa vya maana vina sifa zifuatazo. Kila kikoa kinaweza kuzaa vikoa vingine vidogo vidogo ndani yake kwa mfano, majira - vuli, kipupwe, masika, kiangazi. Pia hakuna kanuni wala mpangilio maalumu wa kupanga vikoa vya maana, yaani kubainisha ni kikoa kipi kinaanza na kipi kinafuata, kwa mfano; rangi - nyekundu, kijani, blu, njano, nyeusi. Japokuwa kuna vikoa vighahiri ambavyo huenda katika mpangilio maalumu wa kimfuatano kwa mfano namba, siku miezi na vipimo.
 Aidha vikoa vya maana huwa na sifa ya kuhusiana kwa msingi wa usiganifu yaani maneno huwa na ufanano lakini pia huweza kuwa na tofauti kwa mfano katika kikoa cha ndege – kuku, kunguru, njiwa, mwewe, ndege hawa wanasifa zinazofanana [+ndege] lakini wanatofautiana katika sifa ya [+kufugwa] na [-kufugwa].
Kiini
Katika kiini ufafanuzi juu ya umuhimu wa vikoa vya maana umetolewa kama ifuatavyo:
2.1 Umuhimu wa Vikoa vya Maana katika Taaluma ya Maana
Mosi, Mdee (2010) anaeleza kuwa vikoa vya maana husaidia katika utunzi wa kamusi, Massamba (2004) kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno katika lugha yaliyopangwa kwa utaratibu maalumu pamoja na maana au fasili zake. Hivyo, kikoa cha maana kinapoingizwa katika kamusi hutolewa maana kama kidahizo na kuonesha uhusiano na vikoa vingine vya maana kwa mfano, ndege ni kikoa cha maana kilichoingizwa kama kidahizo katika kamusi kisha kutolewa maana na mifano inayohusiana na kikoa hicho, na mifano hiyo huwa ni sehemu ya vikoa vya  ndege na vikoa hivyo huweza kusimama kama vidahizo. Mathalani, katika TUKI (2004).
         Kuku nm ndege anayefugwa na anayefanana sana na kware mkubwa.
         Kurumbiza nm ndege mdogo mwenye kichwa cheusi, mgogo na mbawa za.
           kahawia, rangi iliyoiva kifuani na tumboni.
Pili, husaidia kuonesha uhusiano wa maneno wenye sifa sawa au zinazoelekeana kimaana. Resani (k.h.j), katika kuweka vikoa vya maana ndani ya kikoa kikuu kimoja kunahitaji kubainisha kama sifa za kikoa hicho kinaendana na vikoa vinavyoambatana navyo pamoja na maana. Hivyo basi, vikoa vidogovidogo vya maana vinavyotokana na kikoa kimoja kikuu huwa na sifa zinazofanana au zinazoelekeana.  Kwa mfano, lazima ujue sifa za kikoa kikuu ni zipi, ambacho ni mti ndipo uweze kutaja au kuorodhesha miti inayojenga kikoa hicho kama vile mchongoma, mkaratusi, mchungwa mzambarau. Kwa ujumla vikoa hivi huchangia sifa zinazofanana au kuelekeana ambazo ni:
                                    Mti
                                  +matawi
                                  +mizizi
                                  +shina
                                  +maua
Tatu, husaidia kurahisisha mawasiliano, katika mawasiliano matumizi ya neno moja pana linalorejelea maana nyingine ndogondogo, husaidia kuokoa muda baina ya wazungumzaji.
      Mfano 1: mtu anapoandikiwa dawa na daktari hawezi kuambiwa “nenda ukachukue, paracetamol, albendazol, mucolin, flagil” lakini husema kwa ujumla “nenda ukachukue dawa dirishani”. Hivyo, dawa imetumika kama kikoa kikuu chenya vikoa vingine ndani yake vinavyoweza kurahisisha mawasiliano.  
              Mfano 2: “mama alienda sokoni kununua: vikombe, sahani, bakuli, ndoo, jagi na sufuria”, lakini likitumika neno vyombo ambavyo ndiyo kikoa kikuu, linarahisisha mawasiliano kwa kujumuisha vitu vyote vilivyotajwa.
Nne, huwasaidia wanaisimu kujua sifa mbalimbali za maneno yanayosigana kimaana. Katika lugha kuna maneno yanayoandikwa sawa na kutamkwa sawa lakini yana maana tofauti. Hivyo vikoa vya maana vinaweza kumsaidia mwanaisimu kubaini sifa za maneno hayo na uhusiano wake na vikoa vingine vinavyo husiana navyo.
               Kwa mfano maneno yenye utata kama vile: pamba
                                                                                          kata
                                                                                          kaa
                                                                                        mbuzi
Maneno hayo huwezwa kuwekwa katika kikoa fulani kwa kuzingatia sifa za kikoa hicho. Mathalani, ili kujua mbuzi  yupo katika kikoa cha wanyama ni lazima kujua sifa bainifu za mbuzi anayezungumziwa.
Tano, husaidia kupata kamusi zenye  makundi maalumu. Kikoa cha maana kimoja chenye maana pana kinaweza kusaidia kupata kamusi mbalimbali kama vile, kamusi ya wanyama, kamusi ya mavazi, kamusi za vyakula, kamusi tiba ya magonjwa, kamusi ya misuko ya nywele. Kwani kikoa kimoja cha maana huwa na vikoa vidogovodogo ndani yake na vikoa hivyo huwa na vikoa vingine.
 Sita, hurahisisha michakato ya ujifunzaji lugha, vikoa vya maana husaidia kumuelekeza mjifunzaji lugha, ili kujua vitu mbalimbali vilivyowekwa katika kundi fulani. Kwa mfano mjifunzaji lugha huweza kujifunza kuwa dhana ya neno nafaka  hurejelea, mahindi, uwele, mtama, maharage na ngano. Hivyo mjifunzaji lugha anapotajiwa miongoni mwa vitu vilivyo orodheshwa hapo juu atajua kuwa ni nafaka.


Hitimisho
Kwa ujumla, dhana ya vikoa vya maana vina changamoto mbalimbali. Kama vile, kuna baadhi ya vikoa vya maana vina maana zaidi ya moja mfano ndege, kuna ndege kiumbe hai na ndege chombo cha usafiri. Hivyo kumfanya mtumiaji wa lugha kupata utata wakati wa uainishaji wake hasa muktadha wa utumizi usipowekwa wazi. Kwa hiyo, ili kuondoa changamoto ya upangaji wa vikoa vya maana ni vyema kujua sifa na uhusiano wa maneno katika lugha.  
 
















MAREJELEO
Habwe J na Karanje P, (2004), Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Phoenix Publishers Ltd.
                                                   Nairobi kenya
Massamba, D.P.B (2004) Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha, Taasisi ya Uchunguzi
                                               wa Kiswahili (TUKI): Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mdee J. S (2010) Nadharia na Historia ya Leksikografia TUKI: Dar es Salaam
Resani M (2014) Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili. Karljamer Print Technology:
                                                     Dar es Salaam, Tanzania  
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu: New York: Oxford University Press; East Africa.