Wanafunzi wakionyesha vitabu wanavyosoma.Picha 
Wanafunzi wakionyesha vitabu wanavyosoma.Picha  kwa hisani ya blogui ya maendeleo vijijini
By Abdullah Saiwaad at MASSHELE BLOG
Muulize mzee yeyote aliyepitia shule, lazima kuna kitabu kilichomvutia enzi zake.
Aghalabu vitabu hivyo atakuwa amevisoma zaidi ya mara moja. Wengine hata hukariri ukurasa mzima.
Kwa mfano, wazee wengi walisoma vitabu kama Machimbo ya Mfalme Suleiman, kitabu kinachohusu Makhumazan, Umsolopagas, Gagula na Twala.
Ni ndugu yangu mmoja, Kitwana Mohamed, alifikia hatua ya kuandika neno Foulata katika pikipiki yake. Foulata ni mwanamama anayesimuliwa katika kitabu hicho.
Wapo pia wanaokikumbuka kitabu cha Robinson Krusoe kiitwacho ‘Kisiwa chenye hazina’ Binafsi nakikumbuka; The Ancient Briton.
Nilikipenda kitabu hiki kwa sababu ya visa vingi vya William. Siku moja alirudishwa shule mapema. Alipoulizwa akamwambia mama yake kuwa aliitwa kwa mwalimu mkuu akaambiwa; “William wewe mwerevu kuliko sisi. Kwa hiyo leo tunakupa ruhusa kwenda kupumzika nyumbani.”
Kwa nini tulipenda kusoma vitabu zamani?
Vitabu hivi vilikuwa chachu ya kupenda kujisomea kwa burudani. Vilitusaidia katika uelewa wa lugha na hivyo kuturahisishia masomo mengine. Vitabu hivi havikuwa sehemu ya masomo, lakini vilikuwa muhimu. Tulikuwa tukivipata maktaba.
Katika mazungumzo na wazee waliosoma vitabu hivi, huniulizia vinapopatikana. Pia, husikitika wanapobaini kuwa havipatikani.
Hata hivyo, vitabu vingi enzi hizo vilijaa dhana ya kutukuza wazungu dhidi ya wasiokuwa wazungu. Baadhi vilikuwa vya kibaguzi dhahiri.
Kubadilika kwa maudhui ya vitabu
Baada ya uhuru kulikuwapo juhudi za kubadilisha vitabu vya kujisomea vya burudani na vya fasihi vinavyoendana na mahitaji ya Waafrika.
Kwa mfano, ilianzishwa East African Cultural Association, iliyokuwa na wadhamini ambao ni marais wa tatu wa Afrika Mashariki.
Chama hiki ndicho kilichoanzisha kampuni ya uchapishaji ya East African Publishing House mwaka 1965, kwa lengo la kuchapisha vitabu vya burudani vinavyoakisi utamaduni wa Mwafrika.
Matunda ya chombo hiki yalikuwa kuchapishwa kwa vitabu kama vile Nyungu ya Mawe na The Majimaji War in Ungoni.
Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuna watu Tanzania walitaka kuhodhi mali za kampuni hususan jengo lililokuwa mtaa wa Samora.
Lakini Mwalimu Julius Nyerere aliagiza liachwe, kwani itakuja siku watu watazinduka na kuhitaji kuendeleza utamaduni wa Afrika Mashariki.
Juhudi nyingine ya kuandika vitabu vya kujisomea kwa ajili ya Afrika mpya ilifanywa na kampuni ya Heinemann, kwa kuanzisha mfululizo wa vitabu vilivyoandikwa na Waafrika.
Hapa ndipo walipoibuka kina Wole Soyinka, Ngugi wa Thiong’o, Chinua Achebe na wengineo. Kwa Tanzania kuliwakuwapo kina Martha Mvungi aliyeandika; Three Solid Stones, na Profesa Pallangyo aliyeandika Dying in the Sun.
Vitabu hivi vilitoa msisimko kwa vijana wapya wa Afrika kwa kuwa viliakisi maisha yao. Vijana wa miaka hiyo walijifananisha na Boneless Wonder, Zambo, kutokana na uhusika wao katika kitabu cha Mission to Kala.
Maana ya vitabu vya kujisomea
Asilimia kubwa ya waandishi hawakuwa walimu. Uandishi ni kipaji wanachopata watu wachache. Vitabu hivi kwa sasa huitwa vitabu vya ziada.
Huku ni kupotosha maana na umuhimu wa vitabu hivi. Vitabu vya kujisomea vinahitajika kuwa vitabu vya lazima na siyo vya ziada.
Nchi kama Kenya kwa mfano, asilimia 10 ya ruzuku ya kununua vitabu vya shule, lazima itumike katika kununua vitabu vya kujisomea vya burudani.
Uhaba wa vitabu vya watoto
Utafiti wa hali ya vitabu vya watoto mwaka 1988, ulionyesha uhaba mkubwa wa vitabu vya watoto vya kujisomea vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili.
Chama cha Wachapishaji Vitabu (PATA) kilionyesha uwezo wa wachapishaji wazalendo katika kutimiza kikamilifu mahitaji yote ya vitabu nchini.
Mwaka 1989, PATA iliamua kuwa vitabu vya watoto wa Tanzania, kiwe kipaumbele cha Watanzania. PATA ilifanikiwa kuibua miswada minne bora ya watoto. Chama kilitafuta ufadhili kwa wachapishaji vitabu ili vitabu viwepo sokoni.
Hivyo, vitabu kama Karamu ya Mfalme Nyani, Ndege Mzuri, Vita vya Mianzi na Paka, vilikuwa vitabu vya kwanza vya watoto kuchapishwa Tanzania na waandishi wa Kitanzania.
Utafiti pia, ukatoa pendekezo la kuanzishwa Mradi wa Vitabu vya Watoto (CBP)Tanzania mwaka 1991.
Kimsingi, mradi ulikaribisha miswada ya vitabu vya watoto kutoka kwa wachapishaji nchini. Miswada ilitathminiwa ubora na kupendekeza vitabu kuchapishwa. Mchapishaji alichapisha vitabu 5,000 lakini mradi ulinunua 3,000. Vilivyobaki mchapishaji alitakiwa kuuza katika soko huria.
Kujisomea na athari katika ufaulu
Vitabu vilivyonunuliwa husambazwa katika shule za mradi. Shule huviweka vitabu katika maktaba na kupanga muda wa wanafunzi kuvisoma.
Tafiti mbalimbali zilizofanywa na wadau, zimedhihirisha kuwa wastani wa ufaulu wa masomo yote katika shule hizi, ni angalau alama 20 zaidi ya wastani wa Taifa.
Kutokana na ushiriki wa wachapishaji, vitabu hivyo hupatikana maduka ya vitabu. Hivyo mwanafunzi akipoteza kitabu, mwalimu anaweza kuagiza mtoto aliyepoteza kitabu kwenda kununua na kurejesha nakala nyingine.
Mradi wa vitabu vya watoto umeibua na umekomaza waandishi. Umeimarisha idadi ya vitabu vya watoto nchini. Mwaka 1990, vilichapishwa vitabu vine pekee, lakini sasa CBP imefanikisha kusaidia kuchapisha vitabu zaidi ya 300. CBP.
Vitabu vya CBP pia vinatumika katika kuongeza usomaji katika mpango wa KKK katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Njombe. Pia vilitumika katika mradi wa EQUIP(T) katika mikoa saba. Aidha, vitabu hivyo hutumika Kenya, Uganda, Sudan ya Kusini na Rwanda. Pia vitabu hupatikana katika mfumo wa e-books duniani.
Miradi ya usomaji isiyo endelevu na athari zake
Miradi mingine ya kuhimiza usomaji yanakosa uendelevu kwa kutowashirikisha wachapishaji. Hii ina maana mradi ukiisha muda na vitabu vyake havitopatikana tena.
Hali kadhalika mtoto akipoteza kitabu wakati mradi unaendelea, hakuna atakapoweza kukipata.
Cha kustaajabisha ni kwamba katika nchi yetu, kila fedha za ununuzi wa vitabu zinapopatikana, unaanzishwa mradi wa kuandika, kusanifu na kuchapisha.
Serikali pia haitengi fedha za ununuzi wa vitabu vya kujisomea. Katika nchi zote jirani, miradi ya kuboresha usomaji hununua vitabu vilivyopo madukani.
Tujifunze
Iwapo hatutakuwa makini na kutegemea miradi ya vitabu inayoweka pembeni tasnia ya uchapishaji, tuwe tayari kuona vitabu lukuki vya ovyo itokanayo na miradi ya ajabu.
Watakaoathirika ni watoto wa walahoi na baadaye Taifa. Vitabu vya kujisomea vya watoto ni muhimu kupita kifani. Viandaliwe mkakati na wasiachiwe wenye fedha kutuamulia au kutuchezea.
Abdullah Saiwaad ni mdau wa sekta ya uchapishaji vitabu nchini: abdullahsaiwaad@gmail.com