Wakati huu kikosi cha Simba kikianza mazoezi jana katika Uwanja wa Boko Veterani, wachezaji Juuko Murushidi na Emmanuel Okwi wataendelea kukosekana.

Wachezaji hao wawili wapo kambini na timu yao ya taifa ya Uganda kwa ajili ya michezo ya kirafiki ya kalenda ya FIFA.

Jana Okwi na Murushid waliichezea Uganda mchezo wa kwanza wa kirafiki kwa mwaka dhidi ya Sao Tome na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Baada ya mechi hiyo, Uganda itakuwa ina mchezo mwingine Jumanne ya wiki ijayo dhidi ya Malawi itakayofanyika Uwanja wa Namboole nchini humo.

Uganda inacheza michezo hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019) nchini Cameroon dhidi ya Taifa Stars, Septemba 7 mwaka huu katika Uwanja wa Namboole nchini humo.

Uganda imepangwa Kundi L ikiwa na timu za Tanzania, Lesotho na Cape Verde.