ABI-2_1522240763-1600x705
Ahmed anatoka katika kabila kubwa zaidi nchini Ethiopia la Oromo ambalo limekuwa likifanya maandamano ya kuipinga serikali tangu mwaka 2015.

Daktari Abiy Ahmed Ali, anayetoka jamii ya Oromo yenye watu wengi Ethiopia, amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa muungano unaotawala EPRDF, hatua itakayomfanya kuwa Waziri Mkuu mteule wa nchi hiyo.

 Ahmed alichaguliwa kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali na atachukua wadhifa huo kutoka kwa Hailemariam Desalegn aliyetangaza ghafla kujiuzulu mwezi uliopita.

Taifa hilo kwa sasa liko katika hali ya dharura iliyotangazwa kwa ajili ya kumaliza maandamano ya takriban miaka mitatu dhidi ya serikali.

Dkt Ahmed, 42, anatazamwa na wengi kama mwenye kuzungumza kwa uwazi, mwenye ujuzi na uzoefu, na mwenye kukumbatia uongozi wa kuwashirikisha wote.

Anaaminika kuwa na ufuasi mkubwa miongoni mwa vijana wa Kioromo na pia katika jamii nyingine.

Wakosoaji wake hata hivyo wanasema ni mtu wa ndani katika chama na hivyo basi, hakuna matumaini ya kutekelezwa kwa matakwa ambayo yamekuwa yakiitishwa na waandamanaji.

Ahmed anatoka katika kabila kubwa zaidi nchini Ethiopia la Oromo ambalo limekuwa likifanya maandamano ya kuipinga serikali tangu mwaka 2015.

Majuzi, alichaguliwa mwenyekiti wa chama cha Oromo People's Democratic Organisation (OPDO).

Miaka ya nyuma aliwahi kuhudumu kama waziri na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha shirika la ujasusi la taifa hilo.

Wakosoaji wake hata hivyo wameelezea hofu zao juu ya ikiwa atapewa nafasi na mamlaka ya kutekeleza mageuzi yaliyodaiwa na waandamanaji.


(Chanzo:BBC)