na mtaalamu wetu
       masshele blog tz
             ikisiri
teknolojia ya habari na mawasiliano imekuwa ikikua kila siku kutoka simu ya kukoroga hadi simu ya mkononi, matumizi ya wavuti na nyinginezo nyingi, kwa kweli ni hatua kubwa ya maendeleo katika teknolojia. hivi sasa watu wanawasiliana ndani ya sekunde chache kwa umbali wa kutoka bara hadi bara kupitia wavuti. katika hali kama hii lugha za ulimwengu nazo zimekuwa zikijitahidi kukabiliana na ukuaji huu wa teknolojia kwa kutafuta istilahi mpya ili kuelezea dhana mpya za kiteknolojia zinazoibuka. katika harakati hizi, kiswahili hakiko nyuma, istilahi mpya za kiswahili zimekuwa zikiundwa ili kukidhi haja ya kuwasiliana kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano. makala hii inalenga kuangalia hatua iliyofikiwa na kiswahili katika tasnia ya teknolojia ya habari na mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuchunguza istilahi za ki-tehama zinazotumika.

1. utangulizi
teknolojia ya habari na mawasiliano imekuwa kiungo muhimu sana katika maendeleo ya watu duniani. watu wamekuwa wakitumia teknolojia hii katika kufanya mawasiliano muhimu, kufanya bishara na mambo mengine mengi yanayowanufaisha watu. kompyuta/ talakirishi ni moja ya kifaa kilicholeta mapinduzi katika tehama kama asemavyo katambi (2011) “kompyuta ama tarakilishi katika lugha ya kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha kabisa mfumo wa maisha ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita. kutokana na kuwapo kifaa hiki dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi chochote kile katika historia ya kuwapo kwake. kifaa hiki kimeleta mabadiliko makubwa sana katika maisha ya kawaida ya binadamu. kifaa hiki kimesababisha mambo mengi kufanyika katika hali ambayo hakika isingewezekana au ambayo awali ingeonekana kama ya kufikirika!. kompyuta imeyafanya maisha kuwa rahisi zaidi. kompyuta imeifanya dunia kuwa kama kijiji kidogo ambacho unaweza kukizunguka katika muda mfupi sana wa sekunde chache”. maneno haya ya katambi yanaonesha ni jinsi gani kompyuta ilivyo muhimi katika tehama, mawasiliano yote ya teknolojia ya habari hufanywa kwa kutumia kompyuta, mfano; matangazo ya redio na televisheni, magazeti na n.k huandaliwa kwa kutumia kompyuta na kuwa tayari kwa ajili ya kupasha habari.
makala hii, kwa kuzingatia umuhimu wa tehama katika dunia ya sasa imejikita katika kuchunguza maendeleo ya kiswahili katika uga wa habari na mawasiliano kwa umahususi zaidi katika mawasiliano yanayohusisha matumizi ya kompyuta hususani wavuti na programu nyingine za kompyuta. tutaangalia umuhimu wa matumizi ya kiswahili katika tehama, maendeleo yaliyofikiwa, changamoto na mwisho ni hitimisho.
  
2. usuli
neno teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama) kwa ujumla wake hurejelea mifumo yote ya kiteknolojia inayotumika kutengeneza, kuhifahdi, kuchakata na kutumia habari katika mifumo yake tofautitofauti (data, picha, uwasilishaji wa medianuwai na mifumo mingine mingi) na mabayo huwezesha, kurahisha na kutegemeza mawasiliano. kwa umahususi zaidi, tehama inarejelea kukutana au kuingiliana kwamikroelektroniki, talakirishi na mawasiliano ya kutumia redio, simu au televisheni ambavyo hufanya kuwezekana kwa data, ikiwa ni pamoja na matini, video na ishara za video kuweza kusafirishwa mahali popote duniani ambapo ishara za kidijitali huweza kupokelewa… (howell na lundall, wakinukuliwa na akinyi 2010). kwa ujumla tehama inahusu mambo mengi sana, matumizi ya kompyuta, wavuti, matangazo ya redio na televisheni, satelaiti, picha na mambo mengine mengi yafananayo na hayo hujumuishwa katika teknolojia ya habari na mawasiliano.
2.1 umuhimu wa tehama katika maendeleo kwa ujumla
teknolojia ya habari na mawasiliano kwa ujumla imechangia sehemu kubwa kuleta maendeleo hasa katika kipindi hiki cha karne ya 21 ambapo utandawazi umeenea ulimwengu mzima na kuifanya dunia kuwa kama kijiji ambapo watu huwasiliana na kufanya kazi na biashara kwa pamoja kama wapo katika kijiji kimoja, mambo haya yote yanafanikiwa kwa kuwezeshwa na tehama. kama asemavyo kamau (2009) kuwa ushirikiano wa kimataifa katika mambo kama vile siasa, biashara, uchumi , michezo n.k huwezeshwa na kurahisishwa na teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama) ambayo imeuunganisha ulimwengu mzima kimawasiliano. kwa maelezo haya tunaweza kuona ni jinsi gani tehama ilivyo kuwa muhimu katika ulimwengu wa sasa.
lugha ni muhimu sana katika suala zima la teknolojia ya habari na mawasiliano hatuwezi kuhamisha maarifa yaliyopo katika teknolojia hii bila kutumia lugha na kwa hiyo ili kuwapo na maendeleo endelevu kupitia tehama ni lazima pia lugha inayotumika kuhamisha maarifa ya teknolojia hii iwe inaleweka kwa watumiaji husika. hii itakuwa rahisi kwao kuilewa na kuitumia teknolojia hii vilivyo kwa sababu lugha inayotumika ni lugha wanayoifahamu na ni lugha yao.
kama tujuavyo bara la afrika halijaendelea sana kwa kiwango cha kuzalisha teknolojia zitakazo kubalika katika masoko ya kimataifa kama yafanyavyo mabara mengine hususani mabara ya ulaya na marekani, kwa hiyo kulingana na hali hii afrika imekuwa ikiingiza teknolojia za kigeni kutoka mabara mengine hasa marekani na ulaya, teknolojia hizi zimekuwa zikiingizwa kwa lugha za kigeni jambo ambalo hufanya watumiaji wengi wa waafrika kushindwa kumudu matumizi ya teknolojia hizi kwa sababu hawajui lugha iliyotumiwa. kwa mfano kompyuta zinazoingizwa afrika programu zake huwa zimeandikwa kwa lugha za kigeni hususani kiingereza, watu mabao wataweza kuzitumia kwa urahisi ni wale ambao wanazijua lugha hizi vilivyo na kuwaacha wale wasiojua wakiwa wameduwaa ambao kimsingi ni wengi kuliko wale wanaojua. kwa hiyo, ili kuondokana na tatizo hili, upo umuhimu mkubwa wa kuziendeleza lugha za kiafrika kiteknolojia. suala hili ni la msingi sana, kwani kwa kufanya hivi hatutakuwa tumeendeleza lugha tu bali pia tutakuwa tumeindeleza jamii yetu kiteknolojia.
2.2 kwa nini kiswahili katika tehama
wataalam wengi wanipigia upatu lugha ya kiswahili kuwa lugha ya utandawazi barani afrika, hii ni kwa sababu lugha ya kiswahili imeendelea sana kuliko lugha nyingine za kiafrika na ndiyo lugha pekee iliyoonekana kuwa tayari kupokea kwa haraka mabadiliko ya kiteknolojia yanayoibuka kila siku duniani. kwa maana kwamba lugha ya kiswahili ina utajiri mwingi wa msamiati kiasi cha kukabiliana na teknolojia za kigeni zinazoibuka bila matatizo yoyote. kama asemavyo kamau (2009) “kwa vile utandawazi huhusika na uunganishaji wa mataifa mbalimbali, basi afrika yahitaji lugha moja yenye asili ya kiafrika kama lugha ya kusambaza utandawazi. kwa sasa mfano mzuri wa lugha kama hii ni lugha ya kiswahili. lugha hii ndio lugha kutoka barani afrika ambayo ina matumizi mapana kuliko lugha nyingine hapa barani na kwingineko”. nukuu hii inatuonesha ni jinsi gani lugha ya kiswahili ilivyo muafaka katika suala zima la utandawazi wa afrika. kimsingi utandawazi husambazwa kupitia lugha na teknolojia, kwa hiyo tunaweza kuona jinsi lugha ilivyo chombo muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia na kwahiyo kiswahili kama lugha ya kiafrika ni muhimu iwe imejiendeleza na kujitosheleza kiteknolojia kwaajili ya mahitaji ya watu wake.
kutokana na umuhimu wa tehama kama ilivyofafanuliwa hapo juu na kutokana na umuhimu wa lugha katika maendeleo ya kiteknolojia, tunaweza kuona jukumu la lugha ya kiswahili katika teknolojia ya habari na mawasiliano. lugha ya kiswahili imebeba jukumu kubwa la kuhakikisha wakazi wa afrika mashariki wanaipata na kuitumia teknolojia mpya kwa lugha wanayoifahamu ambayo ni kiswahili. kwa kufanya hivi matumizi ya teknolojia yataimarika katika ukanda huu wa afrika mashariki. kwa misingi hii naweza kusema ndio sababu pekee iliyonisukuma kuichunguza lugha ya kiswahili katika uwanja wa teknolojia ya habari na mawasiliano.

3. hatua iliyofikiwa na lugha ya kiswahili katika tehama
kwa kweli lugha ya kiswahili imepiga hatuta kubwa sana katika teknolojia ya habari na mawasiliano. kama tulivyo kwisha kusema huko awali kwamba tehama ina uwanja mpana sana, tunapozungumzia tehama tunazungumzia vitu vingi sana kama vile matangazo ya redio na televisheni kwa namna yanavyofanywa, matumizi ya kopmyuta kwa namna yake n.k. katika makala hii tutajikita zaidi katika matumizi ya kompyuta kwa namna yake, tutajikita hapa kwani hii ndio inaonekana kuwa teknolojia mpya kabisa katika mazingira ya lugha ya kiswahili na dhana mpya zinazidi kuibuliwa kila siku katika matumizi ya kompyuta.
kompyuta kimekuwa kifaa muhimu sana katika shughuli nyingi za kimaendeleo, kwa kutumia kompyuta watu wamekuwa wakifanya mambo chungu nzima na kwa urahisi sana. bila shaka umekwisha sikia kuwa unaweza kununua bidhaa kwa kutumia kompyuta ukiwa nyumbani kwako bila ya hata kwenda huko sokoni au dukani. bila shaka umekwisha sikia kuwa mabenki, hospitali, taa za kuongozea magari barabarani, kamera za usalama, ndege za abiria na kivita na hata lift unazopanda kila siku unapoingia na kutoka ofisini katika jengo refu huendeshwa kwa msaada wa kompyuta. bila shaka umekwisha jionea mwenyewe au kusikia habari kama hizi. umekwisha sikia kuwa mtu anaweza kumchagua mgombea wa urais au ubunge kwa kutumia kompyuta! haya na mambo chungu nzima hufanyika kwa msaada wa kompyuta. katika nchi zilizoendelea matumizi ya kifaa hiki yanaendelea kushika hatamu kiasi kwamba kila kitu sasa kinafanywa kwa kutumia mashine zinazoongozwa kwa kompyuta.
kwa hiyo unaweza kuona ni jinsi gani matumizi ya kompyuta yalivyokuwa muhimu sana katika maisha ya kila siku. serikali za jumuia ya afika mashariki zimekuwa zikisisitiza matumizi ya kompyuta kuanzia shule za awali, kwa kuzingatia kwamba matumizi ya kompyuta yameongezeka sana katika ulimwengu wa sasa lakini changamoto zinazoikabili progaramu hii imekuwa ni lugha ya kufundishia. kwa mfano tanzania somo la tehama linafundishwa kuanzia shule za msingi; shule za msingi kwa tanzania hutumia lugha ya kiswahili kama lugha ya kufundishia na kwa kuwa programu za kompyuta zimeandikwa kwa kiingereza, italazimika programu hizo zitafsriwe katika kiswahili ili ufundishaji uweze kuwa rahisi. na hapa ndipo tunapata istilahi mpya za kiswahili katika teknolojia ya habari na mawasiliano.
licha ya uhitaji wa kufundishwa somo la kiswahili katika shule za awali lakini pia makampuni makubwa yanayohusika na mawasiliano ya kompyuta yamekuwa yakitafuta nija ya kujiimarisha kibishara katika maeneo mbalilimbali duniani. mbinu moja wapo amabyo wemekuwa wakiitumia ni kuhakikisha wateja wao wanapata huduma kwa lugha yao. kwa mfano kampuni ya microsoft kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ilianzisha mradi wa kutafsiri program zake kwa kiswahili. kama asemavyo king’ei (2010) “kampuni ya talakirishi iitwayo microsoftilitekeleza hatua ya kihistoria mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi maalumu inayowawezesha watumiaji wa talakirishi kutumia lugha ya kiswahili katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta. programu hii mpya inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote”.
msanjila na wenzake (2011) pia wanasema hadi wakati huu lugha ya kiswahili imekwisha ingizwa katika mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi na mikrosofti. wanaendelea kusema, kuingizwa kwa kiswahili katika mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa kiswahili akiamua kufanya hivyo.
kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu hawa ni wazi kwamba mpaka sasa hivi kiswahili kinatumika katika baadhi ya mifumo ya kompyuta. katika kufanikisha hili ujanibishaji wa programu kadhaa za kompyuta ulifanyika. kahigi (2007) anasema “mradi wa ujanibishaji wa office 2003 na windows xp kwa kiswahili sanifu ulitekelezwa katika kipindi 2004-2005. malengo ya maradi yalikuwa: (1) kuandaa istilahi za kompyuta kwa kiingereza-kiswahili, na (2) kutafsiri programu nne za kawaida za office (outlook, excel, word na powerpoint) na windows xp”. hii inamaanisha kwamba programu hizi zinapatikana katika lugha ya kiswahili. hebu tuangalie mifano ya istilahi kutoka katika programu hizi za office 2003 na windows xp kama zilivyoorodheshwa na kahigi, ni istilahi zaidi ya 600 lakini hapa tutaangalia chache tu:
  fikia access 
  kibonye fikishi access key 
viziada accessories 
 amilisha activate 
kirekebu adapter 
kihadharishi alert box 
program matumizi application 
 makaaba archive 
vitome mchoro bit map 
kiashiri mada book mark 
sakura browse 
kisakuzi browser 
 kwa kaida by default 
  msabidi configuration 
sabidi configure 
puna crop 
kielekezi cursor 
tanafsi custom 
pakua download 
kijachini footer 
nakala bayana hard copy 
kidakuzi cookie 
sanidi install 
kicharazio keyboard 
kiolezo template 
tafutatua trouble-shoot 
sanidua uninstall 
sasaisha update 
 kidhulishi highlighter 
kichapishi printer 
kingavirusi antivirus     
hizi ni baadhi tu ya istilahi kati ya nyingine nyingi zilizoundwa katika mradi wa kujanibisha programu za office 2003 na windows xp. jitihada za kampuni yamicrosoft hazikuishia hapo tu, mnao mwezi mei mwaka 2011 kampuni hii ilizindua programu ya windows 7 kwa kiswahili, hatua hii imezidi kukiimarisha kiswahili katika teknolojia ya habari na mawasiliano. haya ni maendeleo makubwa katika lugha ya kiswahili. kwa hiyo sasa mtumiaji wa kiswahili anachaguo la kufanya, ama kuendelea kutumia programu hizi kwa lugha ya kiingereza au kwa lugha ya kiswahili.
4. changamoto zinazoikabili lugha ya kiswahili katika teknolojia ya habari na mawasiliano
kila jitihada zinazofanywa katika kufikia malengo fulani huwa hakukosi changamoto. katika jitihada za kufanya kiswahili kuwa lugha ya kiteknolojia kumetokea changamoto nyingi, moja wapo iliyo kuu kabisa ni kwamba lugha ya kiswahili haimilikiwi na taifa lolote tajiri kwa hiyo katika harakatika za kuendeleza inakumbana na changamoto nyingi kama vile ukosefu wa fedha na hata utayari wa viongozi wa kisiasa kukiendeleza kiswahili ni mdogo sana, hata hivyo harakati hizi zinapingwa na mataifa ambayo lugha zao zimeendelea sana kiteknolojia kwa kuhofia kwamba zitafunikwa na matumizi ya kiswahili. wapo tayari kutoa misaada ili kuendeleza lugha zao kukididimiza kiswahili kitu ambacho kinafanya harakati za kukiendeleza kiswahili kuwa ngumu kwani nchi kinamozungumzwa kiswahili hazina pesa za kupambana na mataifa makubwa yanayopigia upatu lugha zao.
kutokana na sababu hizo, kasi ya uundaji wa istilahi za kiteknolojia imekuwa ndogo sana, kwani kufanya hivyo pia kunahitaji pesa, na mara nyingi pesa zimekuwa zikitolewa na wahisani au makampuni yanayohusika kitu kinachotokea mara moja baada ya muda mrefu sana.
pia, viongozi wa serikali hawajatilia mkazo suala hili, hawajaona umuhimu wa kukiendeleza kiswahili kitenolojia. nguvu zao nyingi wameziweka katika miradi mingine ya kimaendeleo huku wakisahau kabisa kuwa kiswahili pia kinahitaji kwenda sambamba na maendeleo hayo. kwa hiyo hii imekuwa ni changamoto katika maendeleo ya lugha ya kiswahili.
kwa kuwa istilahi hizi zimekuwa zikifanywa na watu tofautitofauti, ni muhimu kuwapo na jopo maalumu la kusanifisha istilahi hizi kabla hazijasamabazwa. kwa kufanya hivi hakutakuwa na matumizi tofauti ya istilahi katika dhana moja. hali hii inajitokeza sana endapo uundaji wa istilahi utakuwa umefanywa katika makundi tofauti.
utayari wa watumiaji; watumiaji wengi wa lugha ya kiswahili wamekuwa wakilalamika kuhusu kutumia programu za komyuta kwa lugha za kiswahili. madai yao ni kwamba istilahi za kiswahili ni ngumu sana na hivyo si rahisi kuzitumia, kwa mfano, wengi wamezoea kusemapassword na kwa hiyo ukiwaambi kwamba password kwa kiswahili huitwanywila au mouse inaitwa puku watabaki wakikushangaa na watona kama unawapa kazi kubwa sana. kwa hiyo hii nayo inasabaisha matumizi ya kiswahili katika vifaa vya kiteknolojia hususani kompyuta kuwa hafifu.
5. hitimisho
katika makala hii tumeona tehama ni kitu gani na umuhimu wake katika maisha ya kila siku ya binadamu, tumeona umuhimu wa lugha za kiafrika kuendelezwa katika teknolojia ya habari na mawasiliano kwa umahususi zaidi tumeona jinsi kiswahili kilivyo muhimu zaidi katika uwanja wa maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano. tumengalia pia maendeleo yaliyofikiwa na lugha ya kiswahili katika tehama huku tukionesha baadhi ya istilahi za kiswahili zinazotumika katika matumizi ya kompyuta, pia tumeangalia changamotozinazo ikabili lugha ya kiswahili katika jitihada za kuiendeleza kiteknolojia. sasa tuangalie mapendekezo juu ya nini kifanyike ili kuhakikisha lugha ya kiswahili inashika hatamu katika teknolojia ya habari na mawasiliano:
viongozi wa ukanda wa afrika mashariki waungane kuhakikisha wanaunda sera nzuri kuhusiana na maendeleo ya lugha ya kiswahili ikiwa ni pamoja na kuandaa mradi maalumu wa kuunda istilahi mbalimbali za kiteknolojia, hii itasaidia lugha ya kiswahili kuimarika katika matumizi ya teknolojia. pamoja na hilo pia itenge bajeti maalumu kwa ajili ya kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuunda istilahi za kiswahili katika teknolojia zinazoibuka ili kuahakikisha wazungumzaji wa lugha ya kiswahili hawaachwi nyuma katika matumizi ya teknolojia mpya ziibukazo.
pia kutokana na changamoto ya kutokuwapo na jopo maalumu la kuunda istilahi za kiteknolojia pindi mradi kama huu unapotokea, hali hii imesababisha kuwapo kwa istilahi ambazo hazijasanifishwa na pengine kuwapo na istilahi zaidi ya moja inayorejelea dhana moja, hii ni kwa sababu miradi kama hii hufanywa na watu tofautitofauti na pengine wataalamu hawa wana ujuzi katika lugha tu lakini katika teknolojia hususani kompyuta hawana maarifa ya kutosha au hawana kabisa. katika hali kama hii ni vigumu kuunda istilahi zinazofanana au zinazobeba dhana kamili kama ilivyokuwa ikikusudiwa katika lugha chanzi. kwa hiyo katika uundaji wa istilahi za kiteknolojia ni vema kuwepo na jopo maalumu amablo lina ujuzi wa kutosha katika lugha na masuala ya kiteknolojia, hii itasaidia kutoa istilahi nzuri na zinazoeleweka kwa urahisi kwa watumiaji.
baada ya kuundwa istilahi hizi inatakiwa zisambazwe kwa watumiaji kwa kiwango kinachoridhisha ili waweze kujifunza na kuzifahamu na hatimaye kuzizoea katika matumizi yao ya kila siku katika teknolojia ya habari na mawasiliano. nasema hivi kwa saba usambazaji wa istilahi hizi umekuwa haufanywi kwa kiwango kinachohitajika, na katika usambazaji, vyombo vya habari vipewe kipaumbele, kwani istilahi hizi zikitumiwa na vyombo vya habari itakuwa rahisi sana kwa watumiaji wengine kuzitumia.
wazungumzaji wa kiswahili pia wawe tayari kutumia istilahi hizi au programu za kiswahili katika matumizi yao ya kopmyuta. programu kadhaa za kompyuta zimejanibishwa kwa kiswahili lakini wazungumzaji wengi wa kiswahili bado wanatumia programu zilizoandikwa kwa lugha ya kiingereza, program ya windows 7 inapatikana kwa kiswahili lakini nina wasiwasi kama miongoni mwetu kuna mtu hata mmoja anayetumia windows 7 ya kiswahili. kwa hiyo napendekeza kwenu suala hili, kwa kuwa sisi tumejitoa kueneza na kuienzi lugha ya kiswahili pia ni jukumu letu kuchangamkia fursa kama hizi, tuwe wa kwanza kutumia programu kama hizi kwa kiswahili pindi zinapotokea, kwa kufanya hivi tutakuwa tunakienzi kiswahili na kukikuza kwani watu wanaotuzunguka watakapotuona tunatumia windows ya kiswahili watashawishika na wao kuitumia, hivyo kwa njia hii tutakuwa tumefanikiwa kukuza na kuienzi lugha ya kiswahili.
ninaamini kila mmoja wetu ana ndoto za kuona lugha ya kiswahili siku moja inakuwa lugha ya bara zima la afrika, kwa maana kwamba kiswahili kinazumgumzwa kila kona ya bara hili, basi kama ndio ndoto zetu sote hatuna budi kupigania maendeleo ya lugha ya kiswahili kwa nguvu zetu zote, tukifanya hivi kwa pamoja kwa kijishughulisha na masuala yanayohusika na kiswahili, kwa kuandika, kufanya utafiti katika nyanja mbalimbali za lugha ya kiswahili ndoto zetu zitatimia na kumbukumbu zetu zitakumbukwa katika vizazi vinavyokuja kama anavyokumbukwa leo hii shaaban robert. ninaamini kuwa tunaweza!!
kiswahili, hazina ya afika kwa maendeleo endelevu!

marejeo
akinyi, j.j. (2010). kiswahili usage in ict in nepad secondary schools in kenya. katika thejournal of language, technology & entrepreneurship in africa, vol. 2. no.1. www.ajol.info/index.php/kcl/article/viefile
kahigi, k.k (2007). ujanibishaji wa office na windows xp kwa kiswahili sanifu. katika kioo cha lugha juzuu la 5. dar es salaam. tuki.
kamau, s.n. (2009). kiswahili, utandawazi na umoja wa afrika. katika journal of language, technology& entrepreneurship in africa vol.1. www.ajol.info/index.php/kcl/article/viefile
katambi, s (2011). teknolojia ya habari na mawasilianao (tehama). dar es salaam: modecs solutions
king’ei, k (2010). misingi ya isimujamii. dar es salaam. taasisi ya uchunguzi wa kiswahili.
msanjila,y.p, kihore,y.m na d.p.b massamba (2011). isimujamii sekondari na vyuo.
                    dar es salaam. taasisi ya uchunguzi wa kiswahili.
osborn, d. z. (2006). african languages and information and communication technologies: literacy, access, and the future. katika selected proceedings of the 35th annual conference on african linguistics, ed. john mugane et al., 86-93. somerville, ma: cascadilla proceedings project. www.lingref.com, document #1299.
osborn, d. z. (2010). african languages in a digital age. cape town: hsrc press.
http://www.africanlocalisation.net/projects
http://www.kamusiproject.org/