Editors Choice

3/recent/post-list

Wizara ya elimu kutumia maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru kukitangaza Kiswahili Kimataifa


 


Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru ambayo huadhimishwa Desemba 9 kila mwaka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema itatumia maadhimisho hayo kwa ajili ya kuitangaza lugha ya Kiswahili kimataifa kwa kupandisha bango maalumu Mlima Kilimanjaro bango lenye  ujumbe wa  kukitangaza Kiswahili kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo Prof. James Mdoe amesema watatumia maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili Duniani ambapo kwa sasa mataifa mengi yanahamasika kutumia lugha ya Kiswahili.

“Sisi Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ndio wenye dhamana ya kusimamia elimu hapa nchini kwahiyo tumeona ni wajibu kusimamia katika kukitangaza Kiswahili zaidi Duniani” amesema.

Aidha amebainisha kuwa kwa sasa takribani watu milioni 250 ulimwenguni wanazungumza lugha ya Kiswahili na ukizingatia Shirika la umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO tayari imeitambua lugha ya Kiswahili na kuitengea siku maalumu ambayo ni July 7 kila mwaka.

“Ukizingatia Kiswahili ni Lugha ya kwanza kutambuliwa na UNESCO na kukitengea siku maalumu na sisi kama Wizara ya Elimu tunawajibu kwa kuendelea kukitangaza Kiswahili zaidi kimataifa” amesema.

Ameongeza kuwa  “Mwaka huu tutafanya maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru kwa namna tofauti, tutapandisha bango la Kiswahili Mlima Kilimanjaro, lengo ni kueneza Kiswahili kwa mataifa mengi zaidi kuliko ilivyo sasa,”amesema.

Hata hivyo, amesema lugha ya Kiswahili kwa sasa inapendwa na watu wengi na kuzungumzwa ikiwamo nchini Misri ikiwa moja katika ya nchi inayofundisha lugha ya Kiswahili tangu mwaka 1964.


“Kuna vyuo 150 vinafundisha Kiswahili, pia  redio na runinga 300 ulimwenguni ambazo zinarusha vipindi kwa lugha hiyo hapo ni nje ya Vyuo vya hapa nchini pia  vyuo vya Tanzania vina makubaliano na vyuo vya nje kwa ajili ya kuendelea kufundisha lugha hii na tayari mikataba minne imeingiwa na Wizara.”

“Tunaendelea na mazungumzo na wizara hizo za nje ya nchi yakikamilika mikataba mingine mitano itasainiwa ili kuwezesha uanzishwaji wa madarasa ya kufundishia lugha hiyo nchini,” amesema.

Aidha amebainisha kuwa kwa sasa nchi jirani na Tanzania zinazungumza lugha ya Kiswahili  nchi hizo ni kama Uganda, Kenya, Sudani Kusini, Malawi na Mashariki ya Kongo.

“Na hivi juzi tu kwa kushirikiana na ubalazi wa Tanzania nchini Malawi  tumefungua darasa la kufundisha lugha ya Kiswahili  Malawi na tumekuwa tukisisitiza Mabalozi wetu wote kuzungumza na nchi husika” amesema.

Kwa upande wake Mwalimu wa Lugha ya Kiswahili na mwandishi wa vitabu kwa lugha ya Kiswahili Menna Yasser raia wa Misri amesema Kiswahili kinanafasi kubwa kwa mataifa mbalimbali ni muhimu kuendelea kukitangaza zaidi.

“Hii ni lugha ambayo mataifa mengi yanatumia, kuna umuhimu wa kukuza lugha ya Kiswahili, hii lugha imenipa fursa nyingi na nimeisomea,” amesema.

Naye, mtunzi  wa mashairi kwa lugha ya Kiswahili Meja Mwinyikombo Ally amepongeza Wizara ya Elimu kwa kubuni njia hiyo kukitangaza Kiswahili na kuamini kuwa Kiswahili ni kama bidhaa inayouzika nchini na nje ya nchi.

Post a Comment

0 Comments