Hakukuwa na haja ya mgogoro wa ushairi wa Kiswahili kwani washairi wa sasa wanaelekea kutunga tungo/ ushairi mchoro. Yapi maoni yako kuhusiana na hoja hii? Ipi dhima ya ushairi mchoro?



1.0 Utangulizi 

Kazi hii imegawanywa katika sehemu zifuatazo:- dhana ya ushairi na ushairi mchoro, dhana na historia ya mgogoro wa ushairi wa Kiswahili, sababu za mgogoro, hoja za wana ujadi na wanausasa, matokeo/suluhisho la mgogoro, maoni yetu kuhusiana na kuwepo na hoja ya mgogoro wa ushairi wa Kiswahili, dhima ya ushairi mchoro na mwisho ni hitimisho. 

Aidha, katika kulijibu swali hili tumeona kwamba kulikuwa na haja ya mgogoro wa ushairi wa Kiswahili ingawa washairi wa sasa wanaelekea kutunga tungo/ ushairi mchoro. Tutatoa sababu kueleza haja ya kuwapo kwa mgogoro (mjadala) wa ushairi wa Kiswahili tukihusianisha na washairi wa sasa kutunga tungo mchoro. Katika kujadili dhana ya ushairi wa mchoro, pamoja na kuwapo kwa maana yake ya msingi kwamba ni yale mashairi ambapo mtunzi huwasilisha ujumbe wake kwa kupanga beti na mishororo kufanana na umbo la jambo analowasilisha, tumebaini kwamba utungaji wa mashairi mchoro humaanisha utungaji wa mashairi huru yasiyokitwa katika kanuni maalumu. Hivyo, kauli ya “washairi wa sasa wanaelekea kutunga tungo/ ushairi mchoro” pamoja na kuwapo maana yake ya msingi kwamba ni yale mashairi ambapo mtunzi huwasilisha ujumbe wake kwa kupanga beti na mishororo kufanana na umbo la jambo analowasilisha, ina maana yake ya pili kwamba washairi wa sasa wanaelekea kutunga mashairi huru yasiyokitwa katika kanuni maalumu.

Hivyo, ingawa watunzi wengi wa sasa wanaelekea kutunga mashairi ya mchoro, hakuhalalishi kutokuwapo kwa haja ya mjadala kuhusiana na ushairi wa Kiswahili. Hii inatokana na sababu mbalimbali zitakazoelezwa hapo baadaye. Kabla ya kufikia sababu hizo, tutapitia sababu za jumla za kuibuka kwa mgogoro wa ushairi kisha tutaeleza haja au nia ya kuwapo kwa mgogoro huo. Katika kujadili haja za kuwapo mgogoro wa ushairi tutatumia istilahi ‘mjadala’ na si ‘mgogoro’ kwani ni muafaka zaidi kutokana na aina ya swali letu. Baada ya kujadili vipengele hivyo, tutamaliza sehemu ya mwisho wa swali letu kwa kueleza maana ya ushairi wa mchoro kisha kutoa umuhimu wake.



1.1 Dhana ya Ushairi wa Kiswahili

Wataalamu mbalimbali wanaelezea dhana ya ushairi wa Kiswahili. Abedi (1954:1) anaeleza kuwa shairi au utenzi ni wimbo. Hivyo, kama shairi haliimbiki, halina maana. Fasili hii ina dosari kwani imeegemea upande mmoja wa mashairi ya kimapokeo na kuacha mashairi wa kisasa. Pia, si kila kinachoimbika ni ushairi.

Mulokozi na Kahigi, (1982) wanasema, ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha, sitiari au ishara, katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kuelekeza tukio au hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.

Pia, dhana ya ushairi wa Kiswahili imeelezwa na wataalamu mbalimbali akiwemo Senkoro (1988) ambapo anaeleza kwamba, ushairi wa Kiswahili ni ule unaotungwa kwa Kiswahili, unaohusu watu watumiao Kiswahili katika maisha yao. Anaendelea kueleza kuwa, ushairi wa Kiswahili unahusu utamaduni wa waswahili wa Afrika mashariki na kati na si wale tu wa Pwani ya Afrika Mashariki. Pia, ushairi huu huweza kuwa na wahusika, mawazo, historia na mambo mengine yanayowasilisha maisha ya mswahili. Fasili hii, imeegemea zaidi katika kufafanua mawanda na sifa za ushairi wa Kiswahili kuliko kueleza muundo na mtindo wa ushairi wa Kiswahili.

Tofauti na Senkoro hapo juu, Samweli (2015) anaeleza kuwa, ushairi wa Kiswahili ni ule unaofuata urari wa vina na mizani na ule usiofuata. Unaweza kuwa katika fasihi simulizi au kuwa katika fasihi andishi. Fasili ya Samweli ina uelekeo wa kimtindo zaidi na ni bora zaidi kwani imehushisha aina zote za ushairi yaani; ushairi andishi na ule simulizi ama ukiwa unafuata kanuni ya urari wa vina na mizani au kutofuata kaida hiyo.


1.2 Dhana ya Mgogoro wa Ushairi wa Kiswahili

Mgogoro wa ushairi ni mvutano au kutoelewana kati ya washairi wanajadi au wanamapokeo na wanamapinduzi mnamo miaka ya 1970 na 1980. Washairi wanajadi wanadai kuwa ili shairi liitwe shairi la Kiswahili ni lazima kuwe na ulinganifu wa idadi ya vina na mizani, kituo, idadi ya mishororo, muwala na lugha fasaha. Wanaotetea msimamo huu ni pamoja na Jumanne Mayoka, Muyaka bin Haji, Kaluta Amri Abedi. Andanenga, Abdilatif Abdalla na wengineo. Wanapinduzi nao wanadai kuwa shairi la Kiswahili ni lile lenye maudhui na wala halipaswi kufungwa na ulinganifu wa idadi ya vina na mizani. Wanaotetea msimamo huu ni E. Kezilahabi, M.M Mulokozi, T.Y.S Sengo K. Kahigi na wengineo. 


Aidha, Mulokozi (2017:179) anaeleza kwamba, mgogoro ulikuwa kati ya wanajadi ambao pia waliitwa wanamapokeo na wanamabadiliko au wanausasa. Wanajadi walidai kuwa ushairi wa Kiswahili sharti uwe na urari wa vina na mizani, wanamabadiliko walisema kuwa vitu hivyo si lazima japo vinaweza kuwepo. Mgogoro uliendeleshwa katika magazeti, vitabu, redio na makongamano.


1.3 Historia Fupi ya Mgogoro wa Ushairi wa Kiswahili

Kwa mujibu wa Mulokozi (keshatajwa:179) anaeleza kwamba, dalili za mgogoro zilianza kabla ya mwaka ya 1960 ambapo ushairi guni haukufuata urari wa vina na mizani. Mwaka 1960 hadi 1970 Nyerere aliandika mashairi ya masivina katika tafsiri zake za Shakespeare ambayo yalipingwa na Amri Abedi na Lyandon Harries. Ibrahim Hussein na Jaled Angira, Euphrase Kezilahabi walitunga mashairi yasiyo na urari wa vina na mizani. Mwaka 1974 ilichapishwa diwani ya Kichomi na Dibaji ya Farouk Topan. Mwaka 1973 Mulokozi alichapisha shairi katika gazeti la Uhuru akiuliza maana ya ushairi ni nini. Kati ya mwaka 1973 hadi mwaka 1985 makala, mashairi na tangulizi za diwani kadhaa vilichapishwa na washindani wa pande zote mbili. Mfano Mulokozi na Kahigi 1982 “Kunga za Ushairi na Diwani Yetu”. Mayoka (1984/1993) “Mgogoro wa ushairi na Diwani ya Mayoka.”

1.4 Sababu za Mgogoro wa Ushairi wa Kiswahili

1.4.1 Mabadiliko ya Kisiasa na Kiutamaduni Miaka ya 1960 

Mabadiliko hayo yaliambatana na madai ya uhuru katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kifikra. Hivyo, waandishi wa mashairi walikuja na uhuru wa kuandika mashairi yasiyofuata urari wa vina na mizani na ukaibua ushairi usiozoeleka ambao ukaitwa ushairi wa kisasa na ule uliozoeleka ukaitwa ushairi wa kimapokeo. Wanajadi walidai kuwa uandishi wa mashairi ya kisasa unavunja kanuni za uandishi wa mashairi ya kimapokeo. Hali hiyo ilisababisha malumbano kati ya wanajadi na wanausasa na hivyo, mgogoro wa ushairi wa Kiswahili kuibuka.

Mulokozi na Kahigi (1982) wanaeleza kuwa baada ya uhuru madai haya yalipenya katika utamaduni, katika fasihi na hasa katika ushairi. Mikatale ya kisiasa na kiuchumi ya ukabaila na ukoloni imekataliwa. Mikatale ya kisanaa (k.m katika ushairi) vilevile imekataliwa. Mipaka ya kisanaa iliyowekwa na jamii hizo kwa matumizi na manufaa ya mabwana wa jamii hizo imekiukwa.


1.4.2 Mazingira Mapya yenye Mahitaji Mapya yaliyodai Sanaa Mpya

Katika kipindi cha miaka ya 1960 dhoruba ya ubeberu katika umbo la ukoloni na baadaye ukoloni mamboleo ilizisukuma jamii zote hizi katika mfumo wa kibepari. Ukoloni ulikuwa umerutubisha mbegu za upinzani na utaifa na umejikuta ukikabiliwa na madai ya wananchi ya uhuru na demokrasia na usawa wa kiuchumi. Katika kipindi cha ukoloni waandishi wa mashairi waliandika kupinga ukoloni lakini baada ya uhuru iliwabidi waandike juu ya maudhui mapya kama vile uhuru na kazi, azimio la Arusha, ujamaa n.k.

1.4.3 Mwamko wa Kitamaduni (Kurejea katika Uafrika)

Baada ya uhuru Waafrika wengi walitaka kujua wapi walikotoka katika kutafuta matumaini mapya kwa umma uliwachochea watu waanze kutafuta asili, mapokeo yake mazuri na mabaya yakafanya waanze kutafuta miundo mipya ya kijamii, kisiasa yenye kusadifu vizuri zaidi hali iliyokuwepo. Miundo mipya ya kisanaa ikaibuka hususani kwenye ushairi wa Kiswahili na miundo hii ikawa tofauti na ile ya zamani kikawa chanzo cha mgogoro wa ushairi wa Kiswahili.


1.4.4 Athari za Elimu ya Kimagharibi

Baada ya uhuru kulikuwa na mabadiliko ya kiutamaduni, kukua na kupanuka kwa elimu kuanzia elimu ya msingi, sekondari, vyuo na chuo kikuu. Kupanuka kwa elimu hiyo kulisababisha nafasi kubwa ya kukuza udadisi wa kitaaluma. Masuala mengi ya kifasihi ukiwemo ushairi yakaibua swali la nini maana ya ushairi ambapo udadisi huo ukatofautiana na ule wa wanamapokeo, hivyo mgogoro wa ushairi ukaibuka.


1.4.5 Upotofu wa Fikra kuwa Vina na Mizani ni Roho na Uti wa Mgongo wa Ushairi wa Kiswahili

Wanamapokeo walidai kuwa urari wa vina na mizani ni roho na uti wa mgongo wa ushairi wa Kiswahili, kanuni hiyo haiwezi kubadilika milele ambapo wanausasa wanapinga kwa kusema kuwa urari wa vina na mizani si roho na uti wa mgongo wa ushairi wa Kiswahili. Wao wanaamini kuwa vina na mizani ni sehemu ya sanaa ya ushairi wa Kiswahili.


Kutokana na maelezo hapo juu, maoni yetu ni kwamba kulikuwa na haja ya mjadala wa ushairi wa Kiswahili kwa sababu ulikuwa ni uwanja mzuri wa pande zote mbili kujibu madai ambayo yalitolewa na pande zote kuhusiana na ushairi wa Kiswahili. Katika aya ifuatayo, tutaeleza hoja za pande mbili na kuonesha namna mjadala ulivyokuwa na umuhimu katika pande hizo mbili kufikia hitimisho ingawa watunzi wa sasa wanaelekea kutunga mashairi mchoro. 

Mosi, Wanajadi walitoa hoja kwamba ushairi ni wimbo, wenye maneno ya hekima, wenye lugha ya makato na kueleza kwa muhtasari, wenye lugha nzito, wenye urari wa vina na mizani na wenye hisia (unaovuta moyo) ambapo wanausasa walitofautiana kimtazamo na wanajadi kwa kueleza kuwa ushairi ni sanaa inayotawaliwa na mpangilio maalumu wa maneno teule, matumizi ya picha, matumizi ya tamathali za semi, matumizi ya takriri, ridhimu, usambamba na mbinu nyingine za kimtindo, hisia za kishairi, ufungamano wa fani, maudhui, muktadha na makusudio ya mtunzi. Kuwapo kwa mitazamo hii miwili kulisababisha kutoelewana kati ya washairi wanajadi na wanausasa na hivyo kusababisha mjadala ambao ungeweza kuwafikisha katika hitimisho la upi ni ushairi wa Kiswahili ingawa mjadala umekuwapo mpaka leo na watunzi wa sasa wanatunga mashairi ya mchoro, mathalani Kithaka wa Mberia.


Pili, Wanamapokeo walidai kuwa tungo zisizokuwa na urari wa vina na mizani ni insha na si mashairi kwa sababu hazina urari wa vina na mizani. Pia, wanadai kuwa tungo hizo zimeigwa kutoka tungo za kigeni. Kwa mfano, shairi la “Kuusemea ushairi” ubeti wa 2 katika Diwani ya Ustadhi.

Kuuhami ushairi, washairi yatubidi

Weshaingia mathori, wajinadio weledi

Kwa kupotowa nadhari, sanaa yetu ya jadi

Washairi yatubidi, kuuhami ushairi.


Hoja hii inapingwa na wanausasa kwa kudai kuwa tungo zisizokuwa na urari wa vina na mizani si insha bali ni ushairi kwa kuwa umefuata sifa zote na kukubalika kuwa ni ushairi kwa sababu kanuni za urari na mizani zimepitwa na wakati na zinazuia ubunifu katika ushairi. Mfano shairi la Kezilahabi la “Moshi ukizidi Pangoni” katika Karibu Ndani, ubeti wa 2 (ukurasa 11)

Wenzetu wali pangoni, giza likiwagubika

Kweli wali hawaioni, kasumba iliyowasuka

Ndipo likapigwa kundini, la machozi likapasuka

Wakaidi wakabana kutani, wapate salimika

Na vina wakaweka nyusoni, aibu yao kuficha

Walipoona uzito, wa fani ilovunja

Urari wa mizani, vina vilochujuka.


Msigano wa kimtizamo baina ya wanazuoni hawa ulihitaji mjadala wa kina ili kuweza kufikia hitimisho. Hivyo, mjadala ulikuwa haukwepeki ili kufanikisha wanazuoni kueleza hoja zao kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na magazeti, vitabu na mijadala ya ana kwa ana pamoja na kwamba watunzi wengi sasa wanaogelea katika uhuru wa kiutunzi wa mashairi ya mchoro.

Tatu, Wanaujadi walidai kuwa vina na mizani ndio uti wa mgongo wa ushairi wa Kiswahili, bila vitu hivyo utungo hauwezi kuitwa ushairi na upekee wa ushairi wa Kiswahili umo katika urari wa vina na mizani. Wanausasa wanadai kuwa fikra ya kuwa na vina na urari wa mizani ni roho na uti wa mgongo wa ushairi imepotoka kimsingi ni nadharia ya ushairi ambayo haiwezi kuthibitika katika uchambuzi thabiti wa kitaaluma. mathalani, Kezilahabi katika diwani yake ya “Kichomi” dibaji iliyoandikwa na Topan inaeleza kuwa muundo wa mashairi haya haukufungika upande wa mistari: si lazima kila ubeti wa shairi kuwa na idadi maalumu ya mistari: haukufungika upande wa vina: si lazima mistari yenyewe iwe na vina; haukufungika upande wa mizani: si lazima kila mstari uwe na idadi sawa ya mizani. Mashairi yale yaimbwa haya hayaimbwi. Hivyo, kwa namna yoyote ile mjadala ulikuwa haukwepeki ili kuweka mambo sawa ambapo hatimaye pande mbili zilikubaliana kuvumiliana. 


Nne, wanaujadi walidai kuwa ushairi wa Kiswahili ni tofauti na ushairi wa Kiarabu na wa mataifa mengine lakini Mulokozi na Kahigi (wameshatajwa), wanasema wanajadi mathalani Amri Abedi alidai kuwa wasemao kuwa mashairi ya Kiswahili asili yake ni Kiarabu wanazua. La wangekuwa wanajua Kiarabu wasingesema hivyo. Taratibu za mashairi ya Kiarabu na ya Kiswahili ni tofauti kabisa. Ukweli ni kwamba waislamu waliandika habari na masimulizi ya dini na nyimbo au ushairi wa Kiarabu kwa herufi za Kiarabu. Lakini kanuni za mashairi ya Kiarabu ni tofauti kabisa na za mashairi ya Kiswahili. Wanausasa walidai kuwa kauli ya Amri Abedi ni potofu kabisa. Ushairi wa Kiswahili na ushairi wa Kiarabu si tofauti kabisa kwani kanuni ya kujitosheleza pia imo katika ushairi wa Kiarabu. Vilevile, urari wa mizani katika beti zote za shairi ni kanuni katika ushairi wa kiarabu na Kiswahili. Hivyo, kutokana na mikanzano ya kimtizamo baina ya pande hizi mbili kulikuwa na haja ya mjadala zaidi ili kuweza kutafuta upande upi ulipotoka zaidi na upi ulikuwa sahihi pamoja na kwamba tungo nyingi sasa kutungwa katika mchoro.


Tano, wanaujadi walidai kuwa wanausasa wameshindwa kutunga mashairi ya Kiswahili kutokana na ugumu wake, hivyo wanakimbilia kutunga tungo zisizo na urari wa vina na mizani kwa kuwa ni rahisi. Wanausasa nao walidai kuwa mashairi ya kimapokeo si magumu kutunga kama wasemavyo wanajadi kwani hata wao wamediriki kuyatunga bila tatizo. Mulokozi na Kahigi (1973) katika “Mashairi ya Kisasa” wameweza kutunga mshairi ya kimapokeo ambayo yana vina na mizani. Kwa mfano ubeti wa shairi la “Nikifa” (ukurasa 31)

Nikifa, usiudhike, kunitlea machozi,

Bali keti uridhike, na kusahau majonzi,

Cheka ukafurahike, kaimbe nyimbo na tenzi,

Ya nini usumbuke, udongo wa mfinyanzi?

Kutokana na mabishano hayo ya kutoweza kutunga na kuweza kutunga mashairi yalisababisha itokee namna nzuri ambayo kwayo ingewakutanisha katika kujadili na kufikia mwaka hatimaye mjadala wa kuhusu ushairi wa Kiswahili ukawepo.

Sita, Wanamapokeo walidai kuwa wanausasa walikuwa na nia ya kuiua sanaa adhimu ya ushairi wa Kiswahili. Wanajadi wana hofu kuwa mawazo ya wanamabadiliko yataenea na kuua au kuuangusha kitakotako ushairi wa Kiswahili. Wanamabadiliko walidai kuwa hakuna mtu mwenye nia mbaya ya kuua ushairi kuwa hawakuwa na nia ya kuua ushairi bali kuuendeleza katika mazingira mapya ya leo kwa kuongeza mbinu za kuwasilisha ujumbe, jambo lililosababisha kukubaliana kutokukubaliana hatimaye mjadala zaidi ili kufikia muafaka.

Hivyo, hizi ndizo sababu zilizosababisha haja ya mjadala kuhusu ushairi wa Kiswahili kuwapo ili kupata jukwaa la kueleza madai yao kila upande kisha upande mwingine nao kujibu hoja za upande wa pili, mjadala ambao umeenda kwa muda mrefu, tangu miaka ya 1970 mpaka kufikia sasa. Kutokana na maelezo hapo juu ni wazi kwamba haja ya mjadala kuhusiana na ushairi wa Kiswahili ilikuwa ni kubwa sana ili kusaidia kufikia hatua ambazo kwayo wangekubaliana upi ni ushairi wa Kiswahili.

2.0 Dhana ya Tungo/Ushairi Mchoro

Tungo/ushairi mchoro ni utungo wa shairi ambao hutungwa na kupangwa katika umbo lenye kufanana na kile kinachozungumziwa, hivyo mada ya shairi hilo huonekana machoni licha ya kusikia masikioni. Kwa mfano, kama mtunzi anazungumza kuhusu yai basi tungo za mishororo ya shairi lake hupangwa katika umbo la yai. Mulokozi (2017:170) anaendelea kufafanua kuwa matini ya shairi la mchoro hupangwa katika umbo lenye kufanana na kile kinachozungumziwa, hivyo mada ya shairi hilo huonekana machoni licha ya kusikilika masikioni.

Tungo au ushairi mchoro ni ushairi kama ushairi mwingine hivyo, dhima zake hazitofautiani na dhima za ushairi kwa ujumla. King’ei na Amata (2001:3-8)


2.1 Tungo Mchoro Huburudisha

Tungo mchoro hufanya kazi ya kuliwaza, kufurahisha na kuvuta hisia za msomaji kwa muundo wake baada ya kazi. Kutokana na matumizi ya lugha ya mkato mpangilio maalumu wa maneno mashairi huleta mnato, mguso na burudani kwa msomaji na msikilizaji wa shairi.


2.2 Tungo Mchoro ni Pambo la Lugha

Ushairi ni chombo kinachomwezesha mwandishi kufumbata upana na urefu wa maisha katika maeneo teule machache yaliyofinyangwa kisanaa. Uteuzi huo wa maneno hupangiliwa kama vito kwenye kazi ya sanaa anayefua chombo cha dhahabu ambacho humfanya msikilizaji na mtazamaji avutiwe kama mtu angaaliavyo mkufu wa dhahabu. Mpangilio wa maneno mateule katika ushairi hujenga picha na tashibiha.  Maana na mantiki inayochorwa na mshairi humzindua msomaji au msikilizaji. 


2.3 Ushairi Mchoro Huvuta Hisia za Msomaji au Msikilizaji

Usanifu wa ushairi hauwezi kuwa yenye mvuto iwapo hayatahusu hisia na mambo yanayowafamikia wote waishio katika jamii inayohusika. Sehemu kubwa ya utukufu na msisimuo wa shairi ni kwa msikilizaji au msomaji wake kuweza kulielewa kimaudhui na pia katika kiwango cha lugha. hata hivyo fasihi ni njia ya kuwasilisha ukweli fulani kuhusu maisha, hadhira inatarajiwa kuchukua ujumbe uliomo katika ushairi wowote na kuhusisha na uhalisi wa maisha yao.


2.4 Tungo Mchoro Huendeleza Utamaduni wa Jamii

Ushairi ni sehemu mojawapo ya lugha na utamaduni wa jamii husika. Mtu mgeni ni vigumu kuelewa ushairi wa jamii fulani bila kufahamu utamaduni wake. Mshairi mbali na kubuni tungo zenye usanifu wa kuvutia pia ana nia ya kuwasilisha ujumbe kwa jamii yake. Kwa mfano, msanii anapokuwa anaandika kuhusu mila na desturi zinazofaa kurithishwa na jamii anakuwa anaendeleza utamaduni wa jamii yake. Chombo kikubwa anachokitumia mshairi ni lugha ambayo hubeba ujumbe wake kwa jamii yake. Pia, anapotumia lugha hiyo huwa anaendeleza utamaduni wa jamii yake.


2.5 Ushairi Mchoro Huhifadhi Historia ya Jamii

Mshairi anapoandika huiakisi jamii ya kipindi hicho. Ushairi hubeba kumbukumbu na taarifa za vipindi mbalimbali vya kihistoria. Kwa mfano, mashairi ya kipindi cha ukoloni yalizungumzia athari za kikoloni na mashairi baada ya uhuru yalisifia na kupongeza nchi kupata uhuru kama vile mashairi ya Azimio la Arusha yalisisitiza siasa ya ujamaa na kujitegemea. Ushairi mchoro huiakisi jamii ya sasa na maendeleo yaliyopo ambapo hubeba historia kwa kizazi kilichopo na kijacho.


2.6 Ushairi Mchoro Unahamasisha Watu Kujikomboa

Katika enzi za ukoloni na hata baada ya uhuru ushairi ulitumiwa kama chombo cha kuchochea wanajamii kuungana dhidi ya tawala za kidhuluma. Washairi walitunga tungo za kishairi na wakati mwingine kwa mafumbo kwa lengo la kupinga utawala mbovu. Mashairi mchoro nayo yanahamasisha watu kupinga utawala mbaya. kwa mfano, katika diwani ya “Bara Jingine” (2001) iliyoandikwa na Kithaka wa Mberia katika shairi “Mruko wa Nyuki” Katika mtungo huo tunakumbana na nyuki wa Afrika ambao utulivu wao ulisambaratishwa na wageni na hapo wakaanza safari ya kutafuta tiba. Katika safari yao walifika njia panda ambapo wengine walifuata kushoto na wengine kulia. Baada ya kitambo njia ya kushoto iliporomoka. Baadaye waliobaki wakajiunga na wengine katika njia ya mkono wa kulia.


2.7 Tungo Mchoro Hukosoa na Kushutumu Maovu

Mshairi anaweza kueleza kutoridhika kwake na hali fulani katika jamii yake kwa kueleza hoja moja kwa moja kwa kuikosoa jamii kutokana na maovu yanayotendeka katika jamii. Kwa mfano mshairi huweza kukosoa vitendo vya rushwa vilivokithiri katika jamii, imani potofu zinazoendekezwa na jamii yake, wizi, ulevi, uzembe n.k. Mshairi wa tungo mchoro pia huandika tungo mchoro kukosoa jamii kutokana na maovu yanayotendeka katika jamii yake kama vile, ulevi, rushwa, uongozi mbaya, uzembe,  udhalilishaji wa kijinsia n.k


3.0 Hitimisho 

Kwa namna yoyote ile mjadala kuhusiana na ushairi wa Kiswahili usingekwepeka kutokana na madai ya pande zote kuhusiana na upi ni ushairi wa Kiswahili. Hivyo, mjadala ungetumika kama jukwaa lakila mmoja kujibu na kueleza kinagaubaga kile anachokitetea. Pamoja na kusigana kwa muda mrefu mjadala wa ushairi wa Kiswahili ulikuwa na matokeo chanya kwa sababu ulipevua taaluma ya ushairi wa Kiswahili, hususani ufafanuzi wa dhana ya ushairi, mawanda yake, bahari zake, na mbinu za kijadi, wanausasa walijifunza mengi kutoka kwa wanajadi, na hali kadharika wanajadi walijifunza kutoka kwa wanausasa. Pia, vitabu na makala nyingi ziliandikwa na kuchapishwa kwa mfano Mashairi ya Kisasa, Karibu Ndani, Kichomi, Kunga ya Ushairi na Diwani Yetu, Diwani ya Ustadhi, na Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka. 

Hivyo, ushairi ulikomaa na kupevuka zaidi na hatimaye mwafaka na maelewano yalipatikana, badala ya kuzozana kukawa na kuvumiliana na kuelewana. Uchapishaji na ufundishaji wa tungo huru ulianza kukubalika na kuwa sehemu ya mitaala ya shule. Aidha, fani na bahari mpya za ushairi wa Kiswahili zilipata nafasi ya kuibuka na kushamiri.













Marejeleo

Andanenga, A.S. (2001). Diwani ya Ustadhi. Peramiho: Benedictine Publications Ndanda 

 Indende, F. (2008). “Mabadiliko Katika Umbo La Ushairi na Athari Zake Katika Ushairi wa Kiswahili” katika Swahili Forum 15.

Kahigi, K. na Mulokozi, M.M (1973). Mashairi ya Kisasa. Dar es salaam: Tanzania Publishing House Ltd.

Kezilahabi, E. (2008). Karibu Ndani. Dar es salaam: Dar es salaam University Press.

King’ei na Amata (2001). Taaluma ya Ushairi. Nairobi: Acacia Stantex Publishers.

Mulokozi, M .na Kahigi, K. (1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es salaam. Tanzania Publishing House.

Mulokozi, M.M. (2017.) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es salaam: Mocony Printing Press.