TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI
IDARA YA LUGHA YA KISWAHILI NA ISIMU
MSIMBO WA KOZI: KI 604
JINA LA KOZI: SEMANTIKI YA KISWAHILI
PROGRAMU: M.A. KISWAHILI
MSIMAMIZI: Prof. MALANGWA, P.
AINA YA KAZI: KAZI YA SEMINA
MWASILISHAJI: ESTER AMOS MWAKISITU
NAMBA YA USAJILI:
TAREHE YA KUKUSANYA: 17/12/2020
SWALI
Jadili aina za maana.
IKISIRI
Makala hii imenuia kuelezea aina za maana zilizotajwa na kuelezewa na wataalamu mbalimbali duniani .Wataalamu kama vile Leech(1981), Lyons(1977,1996),Resani(2004), lakini tutajikita katika kuelezea aina saba za maana kama zilivyotajwa na kufafanuliwa na Leech(1981) katika kitabu chake kinachoitwa Semantics. Leech (k.h.j) ameenda mbali zaidi kuliko wengine amezifafanua aina saba za maana kwa upana kwa kufuata vigezo mbalimbali vya kiisimu. Aidha katika kujibu swali hili tutaligawa katika sehemu kuu tatu ambapo sehemu ya kwanza ni utangulizi hapa tutajadili dhana mbalimbali zilizojitokeza katika swali , sehemu ya pili ni kini cha swali ambapo tutabainisha aina saba za maana kama zilivyobainishwa na Leech(1981) katika kitabu chake cha Semantics na mwisho hitimisho la swali.
1.0 UTANGULIZI
Dhana ya maana ni wazo lililoshughulikiwa kwa mitazamo tofautitofauti na wanazuoni tofauti. Mathalani Habwe na Karanja (2007) wanasema dhana ya maana ni ya kidhahania kwa sababu haina muundo thabiti, hivyo maana ni dhana tata ambayo si rahisi kueleweka kwa uwazi. Kamusi ya Oxford Advanced learners (2010) imefasili maana ya maana kuwa ni kitu au uwezo ambao ishara, neno ama sauti huwakilisha. Aidha Leech (1981) anawaonesha wanazuoni Ogden and Richard kuwa wao waliorodhesha maana za maana takribani ishirini ikiwemo inayodai maana ile ambayo mtumiaji wa ishara anapaswa kurejelewa.
Kwa ujumla tunaona kuwa maana ni dhana tata kwani wanazuoni wengi hawakubaliani hususani kwenye kueleza kuhusu maelezo yapi yanaweza kubeba maana ya maana. Pamoja na hayo tunaweza kusema kuwa maana ni alama, ishara au dhana maneno au neno linalotumika kuelezea kuhusu kitu, mtu au jambo fulani
2.0 Aina za Maana
Uainishaji wa maana upo katika mitazamo tofauti tofauti ya wanaisimu. Hata hivyo kuna mitazamo kadhaa iliyochambua aina mbalimbali za maana. Zifuatazo ni aina saba za maana kwa mujibu wa Leech (1981).
2.1.1 Maana Msingi
Ni kiini cha mawasiliano katika lugha. Aina hii ya mawasiliano hubeba sifa za kisintaksia na kimofolojia. Leech (1981) anafananua kuwa hii ni maana ambayo haibadiliki kulingana na miktadha mbalimbali kwani huwa na sifa bainifu na sifa ya kimuundo kwani neno huweza kupata maana baada ya kuwekewa sifa bainifu; kwa mfano,
Mvulana + mtu Mwanamke +mtu
+Me(jinsia) -me(jinsia)
-umri mkubwa +umri mkubwa
Iwapo nduni mojawapo ya dhana fulani itabadilika basi maana nayo hubadilika, haiwezi kubaki ileile.Tunaweza kuchunguza maana za msingi za vitu kwa kuangalia jinsi nduni zake zinavyotofautiana. Aidha maana ya msingi inatusaidia kutofautisha maana ya tungo moja na ile ya tungo nyingine. Kimsingi, lugha hutegemea maana ya msingi ili kufanikisha mchakato wa mawasiliano . Maana ya msingi ndiyo msingi wa aina nyingine zote za maana.
Lakini katika upande wa kimuundo maana huweza kupatikana baada ya viambajengo kuungana na kuunda kiambajengo kikubwa chenye maana; kwa mfano
N+V+T+E=S
Mtoto mdogo anatembea polepole =sentensi
N v T E
Mfano huo umedhihirisha kuwa muungano wa viambajengo vidogo vidogo (N+V+T+E) hupelekea kufanyika kwa kiambajengo kikubwa zaidi ambacho ni sentensi.
Aidha, maana msingi huweza pia kupatikana katika kamusi. Resani (2014) anaeleza kuwa maana msingi ni maana inayowakilishwa na vidahizo katika kamusi. Hivyo maana msingi lazima iwiane na maana ya kamusi na huwa haibadiliki badiliki kufuatana na muktadha.
Kwa mfano:
Mama Ni mzazi wa kike
Neno la heshima ambalo hutumika kumwita mwanamke
Hii ni kwa mujibu wa kamusi Peru ya Kiswahili (2016)
Hivyo ni dhahiri kwamba maana ya msingi hupatikana kwenye kamusi na huwa haibadiliki badiliki kutokana na muktadha fulani.
2.2 Maana ya Ziada
Hii ni maana ambayo hutegemea uelewa, uzoefu na tajriba ya mtu mmoja mmoja katika kutumia lugha, kuielewa na hata kuichangua. Pia Leech (1981), anaendelea kusema kuwa aina hii ya maana inatofautiana kulingana na tamaduni, nyakati za kihistoria na tajriba ya mtu binafsi. Baadhi ya viumbe mbalimbali hususani wanyama na wadudu , miongoni mwa matendo na tabia zao zimetumika kurejelea tabia za watu kutokana na miktadha mbalimbali.
Kwa mfano,
Simba Ni kiongozi mwenye nguvu kutokana na muktadha wa kisiasa.
Kupe mtu mnyonyaji katika muktadha wa jamii
Aidha, neno simba limemrejelea kiongozi mwenye nguvu kutokana na muktadha wa kisiasa. Vilevile neno ‘kupe’ limebebeshwa maana nyingine ya mtu asiyependa kufanya kazi ingawa anataka kufaidika kutokana na jasho la watu wengine . Kutokana na maelezo hayo tunaona kuwa, baadhi ya maneno yana maana zaidi ya ile ya msingi ambayo huibuka kutokana na uelewa na tajriba za watumiaji wa lugha husika kutokana na miktadha mbalimbali.
2.1.1 Maana Hisi
Leech (k.h.j) anaeleza kuwa maana hisi inazingatia vipengele viwili vya mawasiliano ambavyo vimejigawa kutokana na hali pamoja na mazingira ambapo neno au sentensi ilivyotumika katika lugha. Massamba (2009) anafafanua kuwa hii ni maana ambayo si ya moja kwa moja bali inakuwa ya kuashiria kutokana na hisia ambazo mtu anakuwa anaelezea hisia binafsi au mtazamo wake juu ya mtu fulani. Pia hisi hizi huhusiana na mtazamo wa mwandishi au msemaji na maana hii yaweza kuwasilishwa kwa namna mbili kama ifuataatavyo:
Kwa kutumia maana ya msingi au dokezi :"wewe mwanaume mzembe kweli"au umelegea kama mwanamke! ni wazi kuwa msemaji akitoa mojawapo ya msemo atakuwa anamdharau msikilizaji.
Kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa mfano badala ya kutoa amri : nyamazeni au fungeni midomo ! msemaji anaweza kusema kwa staha : Samahani mnaweza kupunguza sauti zenu? Au kama yuko maktaba, na kuna vijana wanaopiga kelele anaweza kusema jamani hapa ni maktaba! (sauti hizo zimemuudhi na kumkera!).
Aidha maana hisi mara nyingi hutegemea kiimbo katika usemaji. Tungo ileile inaweza kuwa na maana tofauti kulingana na kiimbo kilichotumika lakini pia mtu akiwa amechukia hutumia kiimbo cha juu kuonyesha hisia kuwa ameudhika.
2.1.2 Maana Jamii
Hii ni maana ambayo hutokana na lugha inayotumika katika mazingira ya jamii fulani ambapo lugha hiyo inaweza kueleweka na mtu wa ndani ya jamii hiyo. Aidha lugha hiyo inakuwa si rahisi kueleweka na watu ambao hawatoki katika jamii hiyo. Pia maana jamii hutofautiana kulingana na tofauti za kilahaja na mtindo wa mazungumzo. Aidha maana kijamii inafanana na namna mtu anavyolitumia neno katika lugha.
Kwa mfano,
i) Tembo-kiunguja neno hili linamaanisha mnyama lakini kimakunduchi humaanisha sehemu za siri za mwanamke.
ii) Kinu-kwa watu wa kaskazini humaanisha sehemu za siri za mwana mke lakini kwa watu wa pwani neno kinu ni kifaa kinachotumika kutwangia nafaka mbalimbali.
iii) Bibi-matumizi ya neno ‘bibi’ kwa Tanzania na Kenya ni tofauti. Neno bibi kwa Tanzania humaanisha mama mzaa baba au mama mzaa mama,lakini kwa nchi ya Kenya neno bibi linatumika kwa maana ya mke.
Aidha katika mifano hiyo utaona kwamba, maana ya maneno hayo hutofautiana kutoka jamii moja na nyingine sababu kubwa ni tofauti za kilahaja.
2.1.3 Maana Akisi
Hii ni maana ambayo huibuka pale neno linapokuwa na maana msingi moja au zaidi ya moja. Maana ya neno moja huzalisha au inapelekea kuibuka kwa maana nyingine. Aidha maana akisi huwa ni maana inayoashiria maana fulani , mara nyingi vikundi vya vijana ndio wanaokuwa na maana akisi katika mazungumzo yao .Aidha maana akisi hutumika kama lugha za mitaani.
Kwa mfano
Neno shoga- ni mtoto wa kiume mwenye tabia za akina dada kama vile kushiriki umbea, kupaka manukato kama vile poda, kupaka rangi kwenye kucha ,kuvaa heleni na bangili.
Neno papa ni sehemu ya uzazi wa mwanamke
Hivyo, katika mifano hiyo tunagundua kwamba, pindi maneno hayo yanapotumika katika mazungumzo huweza kuibua maana nyingine miongoni mwa wazungumzaji.
2.1.4 Maana Ambatani
Hii ni maana ambayo inatokana na uhusiano wa neno na neno ambapo husababishwa na tabia au mazoea ya utokeaji wa pamoja wa maneno. Aidha katika maana ambatani maneno huteuana yale tu yanayoendana ili yaweze kuleta maana isiyo kinzana, pia maneno haya sharti yaendane na misemo ya jamii.
Kwa mfano,
Bibi kizee - Ajuza ( katika maneno ‘bibi kizee’ yanapoambatana na neno ajuza huleta maana isiyokinzana isipokuwa maneno hayo yakiambatana na neno ‘shaibu’ yataleta maana inayo kinzana kwani kinyume cha neno ajuza ni shaibu). .
Mrembo - msichana (neno mrembo huambatana na jinsia ya kike tu. Jamii mbalimbali hususani katika Tanzania hutumia neno ‘mrembo’ kumaanisha msichana mzuri). Hivyo neno mrembo likiambatana na neno mvulana litaleta maana inayokinzana.
Kudamshi - Mwanamke ( neno kudamshi hutumika kumwambia mwanamke au jinsia ya kike huwa amependeza. Kwa maana hiyo, neno ‘kudamshi’ haliendani na jinsia ya kiume.
Mtanashati -mvulana (neno ‘mtanashati’ huendana na jinsia ya kiume tu na hivyo huwezi kusema "Yule msichana ni mtanashati".
Kutokana na mifano hiyo ni dhahiri kuwa maneno katika lugha huweza kuambatana. Aidha, iwapo maneno hayataleta maana kinzani na maneno mengine si rasmi kutumika katika mawasiliano yakiambatana na baadhi ya maneno kwani huleta maana kinzani. Mfano huwezi kusema ng`ombe amejifungua mtoto’ badala yake utasema ‘mama amejifungua mtoto’ pia huwezi kusema ‘waziri wa pesa’ badala yake utasema ‘waziri wa fedha’ kwani neno ‘fedha’ na neno ‘pesa’ yana maana inayokaribiana lakini neno ‘fedha’ lina urasmi fulani hasa unapotaja cheo cha ngazi fulani katika uongozi hususani waziri wa fedha kwani huwezi kusema waziri wa pesa. Aidha neno ‘kuoa’ katika mila na desturi za Kiafrika huambatana na kuendana na jinsia ya kiume. Hivyo huwezi kusema ‘Neema ameoa’ badala yake unapaswa kusema ‘Musa ameoa’ .Vivyo hivyo katika neno ‘kuolewa’ huwezi kusema ‘Musa ameolewa’ badala yake utasema ‘Neema ameolewa’. Hii ndiyo maana halisi ya maana ambatani kwani maneno yanapoteuana na kuendana na kuwa kitu kimoja huleta maana isiyokinzana.
2.1.5 Maana Kidhima
Ni ile ambayo kile kinachozungumzwa na msemaji au mwandishi katika kupangilia ujumbe wake kwa kuzingatia mtiririko, lengo na msisitizo katika kufikisha ujumbe. Pia maana kidhima inaweza kuelezwa kwa kutumia mkazo na kiimbo kuonyesha msisitizo katika sehemu mojawapo ya sentensi. Pia katika kiswahili msisitizo wa jambo katika sentensi mara nyingi huwa ni mwanzoni mwa tungo. Kwa mfano
i. Wanafunzi walipewa zawadi na mwalimu
Msisitizo upo kwenye neno wanafunzi”
ii. Zawadi ilitolewa na mwalimu kwenda kwa wanafunzi
Msisitizo upo kwenye neno zawadi
iii. Kesho nitakuja kukutumbelea
Hapa msisitizo upo kwenye neno “kesho”
Maana ya kidhima huonesha zaidi kusudio la mwandishi ama msemaji. Aidha pale palipowekewa msisitizo ndipo panapobeba maana, hivyo maana hupatikana mahali palipowekwa vipamba lugha kama vile kiimbo.
3.0 Hitimisho
Kwa ujumla, baada ya kuzitazama aina saba za maana kwa mujibu wa Leech (1981) tunaweza kusema kuwa Leech (keshatajwa) amewasaidia watumiaji wa lugha katika kutofautisha maana kwani katika kila aina ya maana ameonyesha ni kwa namna gani neno moja linaweza kuwa na maana zaidi ya moja kimuktadha.
Marejeleo
Habwe . J na karanja P.(2004). Misingi ya sarufi ya Kiswahili. .Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Leech .G..(1981). Semantic A study of Meaning London : Penguin
Massamba. .D.P. B.(2009).Kamusi ya Isimu na falsafa ya lugha.Dar es salaam :TUKI
Resani. M.(2014). Semantiki na Pramatiki ya Kiswahili Dar es Salaam: Karjamer Print Technology.
TUKI. (2014). Kamusi ya Kiswahili sanifu. Nairobi: Oxford University press
Wamitila, K.W. (2016) .Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi:Vide Muwa
0 Comments