MADA: *NAMNA YA KUPATA MAMBO YA KUANDIKIA VITABU*

Wapendwa, karibuni katika somo la Kumi na Mbili. Somo hili linahusu namna ya kupata mada au mambo ya kuandikia vitabu. Pengine, huenda somo hili likawafaa zaidi waandishi wachanga au wale ambao hawajaandika kabisa, lakini wanatamani kuandika. Somo letu lijibu swali kwamba, *nikiwa na hamu ya kuandika lakini nikawa sina jambo la kuandikia, nifanye nini?*

Baada ya utangulizi huo, nikiri wazi tu kwamba huenda nitakayoyagusia yakawa maoni yangu tu na wala si kanuni za lazima. *Namna ya kupata mambo ya kuandikia, hutofautiana kutoka kwa mtu mmoja na mwingine kutokana na mazingira, majukumu, kiwango cha elimu, msukumo wa ndani wa kufuatilia mambo, umri, juhudi binafsi, kwa kutaja tu machache.*

Pamoja  na ukweli huo, katika somo hili, mimi nitapendekeza mambo kadhaa ya kufanya ili kupata mada au data za kuandikia vitabu vya aina mbalimbali. Vitabu tunavyozungumzia, vinaweza kuwa vya kiroho au visiwe vya kiroho. Hata hivyo, mimi kwa kiasi kikubwa nitatolea mifano zaidi katika uandishi wa vitabu vya kiroho. *Njia za kupata mambo ya kuandikia ni pamoja na hizi zifuatazo:-*

1. Kufanya utafiti wa kitaaluma. *Njia hii hupendekezwa zaidi kwa kuwa kinachoandikwa kinaweza kuhakikiwa.* Katika dunia hii, yapo mambo yanayofahamika na yasiyofahamika. Yale yanayofahamika wakati mwingine huonekana ya kawaida. Yale yasiyofahamika, yanapoibuliwa hushangaza watu, na wengi huvutiwa kufuatilia ili kupata maarifa mapya.   Ili mtu afanye utafiti anatakiwa afahamu mbinu za kukusanya data (taarifa), namna ya kuzitumia mbinu hizo, namna atakavyotafsiri data na kuzipa maana ili wasomaji waelewe, na kadhalika. Baadhi ya njia za kukusanyia data ni kama ushuhudiaji (observation), ushiriki (participation), usaili (interviews), majadiliano ya vikundi (Focus group discussions), Upitiaji wa nyaraka (Documents review), n.k. *Yapo mengi sana katika njia hii.* Hata hivyo, tuseme tu kwamba mwandishi anayefanya utafiti, *lazima anakuwa na maswali yanayomsumbua kichwani na anatamani kuyapatia majibu.* Tena majibu yanayopatikana lazima yaambatane na ushahidi na  si hisia za mwandishi tu. Kwa wale wenye vitabu vya mwalimu, soma kwa makini kitabu cha *Utafiti kuhusu Karismatiki.* Katika sura ya kwanza ya kitabu hicho, mwalimu ameeleza kwa kina maswali yaliyokuwa yanamsumbua na kumsukuma kulitafiti vuguvugu hilo la Karismatiki. Aidha, kitabu kingine cha mwalimu kwa jina la *Wakristo Msiogope Nguvu za Giza* ni cha kitafiti. Ukikisoma vizuri kuanzia mwanzo mpaka mwisho utabaini yaliyokuwa yanamsumbua mwandishi, namna alivyokusanya data na kuzitafsiri, matokeo aliyopata na ushauri wa kutatua tatizo. Kwa mfano, kitabu kimeanza kwa kuonesha hisia za watu mbalimbali katika jamii. Kulifanyika mjadala mkali ambao ulijadili kwamba *hivi nguvu za giza ni nini? Kwanza zipo? Kuna ushahidi? Jamii inasemaje? Tafiti zinasemaje? Kama nguvu hizo zipo, tutazibainije? Hivi, Mkristo anaweza kuvamiwa na nguvu za giza? Je, kama ndiyo, anapovamiwa afanye nini?* Maswali hayo machache ndiyo yaliyosukuma utafiti wa kitabu. Jambo jingine la msingi katika njia hii ni kwamba *unapoandika kitabu cha namna hii lazima utafute namna nzuri ya kuwasilisha matokeo yako ilo walau wasomaji wengi wakuelewe.* Kwa kulizingatia hilo, ndiyo maana vitabu viwili nilivyotolea mfano, kama ukivisoma vimekwepa taratibu ngumu za kuwasilisha matokeo. *Lengo lilikuwa ni kumwezesha msomaji hata wa chini kabisa, kuelewa yaliyoandikwa.* Kwa hiyo, mengi yameandikwa kwa namna ambayo ni rahisi ili wasomaji wengi waelewe. *Ukiandika kitaalamu zaidi, ukumbuke kwamba unapunguza wingi wa wasomaji.* Wengi hawatakuelewa. Utaeleweka zaidi kwa watalaamu kama wewe.

2. *Kuchunguza na Kukusanya kazi unazozifanya kila kila siku.* Huu pia ni utafiti wa aina yake. Kila siku na kila unayoyafanya huenda yakawa njia nzuri ya kupata mambo ya kuandika. Kwa mfano, kutokana na majukumu yako, kuna mambo unalazimika kuwa unayaandika. Padre, Askofu au mchungaji anayeipenda kazi yake, lazima ajiandae kabla ya kuwahubiria au kuongea na waamini wa imani yake. Mahubiri, masomo, semina, warsha, mikutano, makongamano n.k. huwasukuma viongozi hao wa kiroho kuandika. *Kwa hiyo, yale anayoandika ili kuwahudumia waamini huwa ni vyanzo vizuri vya mada za kuandikia vitabu.* Kwa njia hii, kuna vitabu vingi sana vya Mapadre, Maaskofu na wachungaji wengine, ambavyo ni mkusanyo wa maandiko yao. *Kwa ufupi, ukiwa na nafasi hiyo, ufahamu kwamba uko sehemu nzuri sana ya kukuchochea kuwa mwandishi wa vitabu. Wewe utakuwa tu na kazi ya kukusanya na kuratibu vizuri kazi zako.* Si kila unachohubiri au kuandika kwamba kinafaa kuwa kitabu. Lakini hoja yetu ni kwamba ukikusanya yote uliyoandika ndani ya kipindi kirefu (mfano mwaka mzima) lazima utapata vitabu kadhaa. *Ukiwa na welewa huu, basi kuanzia leo ujue kwamba unapoandaa mahubiri au masomo, unapaswa kutumia akili nyingi, kuwa serious na kumwomba Roho Mtakatifu akuongoze daima ili uandae kazi nzuri.* Ili usichanganyikiwe, unapoandaa masomo au tafakari andaa tu kwa ajili ya nia husika na si kusema unaandika kitabu. Unaweza kweli kuandika kitabu na ukawa unatoa masomo humo. Lakini hoja yangu ni kwamba ili ufanikiwe kuwa na vitabu vingi, wewe andaa masomo yako vizuri na uwe unayahifadhi kwa mwaka mzima au hata miezi 6. *Baada ya hapo, pitia kazi zako uone kama unaweza kuziratibu na kupata sura za vitabu.*

3. *Kutazama mambo ya kawaida kwa jicho tofauti la kiudadisi.* Katika maisha ya jamii yapo mambo mengi ya kawaida ambayo watu huyatazama tofauti na wakapata mada za kuandikia. Hii ni aina fulani ya utafiti, lakini inayotokana na tafakuri. *Si wote wenye uwezo wa kufanya hili. Wengi wanaofaulu katika hili huwa ni wale wenye fikra za kifalsafa.* Watu wa aina hii wapo na wanapotutafakarisha katika mambo tuliyozoea, hutuwezesha kujitathmini, kujihoji zaidi, kujirudi, kushangaa, n.k. *Kwa mfano, wengi wetu hudai kwamba tunashindwa kuendelea kiroho kwa sababu shetani anatuzuia katika mengi. Lakini mtu anaweza kuja na tafakuri ya kichokozi kwamba shetani ni sisi wenyewe.* Kwamba tunazo fursa na nguvu za kiasili (potentials) ambazo Mungu alitupatia kwa maksudi ili tuubadili ulimwengu na kuachana na umaskini. *Sasa badala ya kutumia akili/fikra, nguvu, fursa katika kutafuta mtaji, sisi tunaelekeza mawazo kwa shetani.* Vitabu hivi huwa vinazindua ubongo na kushangaza wasomaji kwamba kwa nini walikuwa wanawaza ujinga au tofauti na uhalisia? Huo ni mfano tu. *Hoja yangu kuu ni kwamba kuna vitabu vinavyoweza kuandikwa kutokana na tafakuri ya maisha binafsi, ya kijamii, n.k.*

4. *Kusoma sana vitabu vya watu wengine.* Mara nyingi, Pd. Faustin Kamugisha (PhD), huwa anasisitiza na kutetea hoja kwamba mtu anayesoma sana vitabu, ipo siku ataandika kitabu cha kwake. Unaposoma vitabu vingi kwa nyakati tofauti, unajifunza mbinu za uandishi tofauti, unaona ubora na udhaifu wa waandishi, unaona mapengo ya maudhui n.k. *Kwa mfano, ukisoma vitabu ukafika hatua ya kuona kwamba kuna vitabu dhaifu ambayo vimeandikwa kwa kubabaisha na wewe unaweza kuandika kwa ubora ukavizidi, basi ujue umeshakuwa mwandishi ila tu hujaanza kuandika rasmi.* Waandishi wanaotokana na mazingira haya huwa ni wazuri sana. *Wanakuwa wazuri kwa sababu wanafahamu waandishi wengine wameandika nini, wapi wameandika vizuri, wapi wamepwaya na wao wajikite wapi ili kuziba pengo au kuchangamotisha kiuandishi!* Hata hivyo, hoja hii isichukuliwe kwamba waandishi wengine si lazima wasome vitabu vingi. Hii inapaswa kuwa kanuni ya jumla kwa yeyote anayetamani kuandika ili kukwepa kurudiarudia kazi zilizoandikwa, kubaini mapengo ambayo utayaziba kiuandishi, kujitofautisha na kadhalika. *Kwa mfano, huwezi kuandika kwa mtindo wa pekee kama haujui waandishi wenzako wanaandikaje. Kwa mfano huo basi, kila mwandishi makini anapaswa kuwa msomaji mzuri wa vitabu hasa vinavyoendana na anachotamani kuandika.* Kuna waandishi wengi wachanga nimekuwa nikiwapa changamoto kwa sababu ya kutosoma. Wanapoleta miswada, ninawaorodheshea vitabu vingi vinavyoelezea mada zao. *Huwa ninawauliza kwamba sasa utajitofautishaje na waandishi hawa?* Hii huwa ni changamoto inayowasukuma kwenda kusoma vitabu husika ili kupanua maarifa. *Usipokuwa msomaji mzuri, unaweza kushangaa unatoa kitabu, halafu kinafanana kabisa na cha mwandishi mwingine. Ikitokea hivyo, unaweza kuishia kuzushiwa kwamba umeiba kazi ya mtu mwingine.* Kwa hiyo, usomaji ni hitaji la lazima katika kupata mada au mambo ya kuandikia.

5. *Kuhudhuria warsha, semina mbalimbali, mikutano, makongamano ya kitaaluma na kiroho, mijadala mbalimbali ya kukujenga kifikra, na kadhalika.* Mtu anayependa kutangamana na wenzake, lazima atapata mada nyingi za kuandikia vitabu. Unapokuwa na watu ujue kwamba una fursa ya kujua mengi. Hata hivyo, unapaswa kuwa mtu ambaye unalenga kujifunza na kutumia fursa za kutangamana na watu. *Watu husema, palipo na wengi pana mengi pia.* Njia hii inawafaa sana wadadisi wa mambo. Unaposikia hoja kwa watu, au wewe mwenyewe kuianzisha, unaweza kujifunza na kupata mawazo mapya ambayo yanakusukuma kudadisi zaidi. Ukiwa na ung'amuzi huo ujue basi kwamba utakuwa na mada nyingi sana kila utakapokuwa unapata nafasi ya kutangamana na watu. *Kwa ufupi kabisa, kila upatapo fursa ya semina na makongamano, andaa kijidaftari cha kuwa unaandika mambo yote unayojifunza huko.*

6. *Kusoma vitabu na machapisho kuhusu imani yako na ya wengine.* Hii inawahusu hasa waandishi wa vitabu vya kiroho. Ili uwe mwandishi wa vitabu vya kiroho unatakiwa kusoma kwa kina vitabu na machapisho ya imani yako na ya wengine. *Sote tunafahamu kwamba kwa mfano, Wakristo ni wamoja, lakini bado wanatofautiana katika masuala kadhaa. Waislamu nao siku hizi wanatofautiana. Sasa kama wewe unataka kuandika kitabu kinachozungumzia suala fulani la kiteolojia/kiimani, si rahisi kuelezea jambo hilo kwa kuwarejelea Wakristo wote. Utajikuta kwa mfano, unaeleza mambo ya ndoa kwa mtazamo wa Kanisa au dhehebu fulani.* Sasa ili utofautishe tamaduni au mivigha (rituals) ya Kanisa au dhehebu moja na jingine, utalazimika kusoma kwa kubobea au kusoma vitabu vya eneo husika. *Hapo utaweza kujua kwamba jambo hilo katika dhehebu hili linatazamwa hivi na katika dhehebu jingine linatazamwa namna nyingine.* Ukijifanya kwamba wewe hujali, utajikuta unabananga (haribu) na kuwachanganya wasomaji. Kwa kuzingatia hoja hii ndiyo maana kitabu cha *Je, Nikibatizwa Ninakuwa "Nimeokoka" na "Mtakatifu?"* mwalimu alilazimika kuweka sentensi nyingine chini kwamba *Kanisa Katoliki Linasemaje?* Maana yake, dhana ya wokovu na utakatifu ni pana na kuna mitazamo mingi na tofauti kuhusu maneno hayo. Sasa mwandishi aliona akite mjadala wake kwenye mtazamo wa imani fulani. Hata ukisema umhukumu, zaidi utalazimika kumhukumu baada ya kusoma mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu dhana hizo za "kuokoka na kuwa mtakatifu." Kwa bahati mbaya, huwa kuna watu wanadhani kwamba ufafanuzi wao una ukweli wote (absolute truth). Kwa hiyo, usishangae kukutana na kitabu kimeandikwa *Maana halisi ya kuokoka.* Mwandishi anayekuwa ameandika hivyo, anakuwa anajipambanua kwamba tafsiri yake ndiyo bora na tafsiri nyingine zote ni dhaifu. *Hapa nisisitize kwamba, yapo mambo mengi ya kiroho ambayo huwezi kuyaandikia kwa ujumla bila kujikita kwenye imani fulani mahususi.*

Mfano mwingine ni kuhusu maisha baada ya hukumu ya siku za mwisho. *Wapo Wakristo wanaoamini kwamba baada ya siku za mwisho wema watapelekwa mahala paitwapo mbinguni. Tena sehemu hiyo ni maalum aliyoiandaa Mungu. Wakati huohuo, kuna Wakristo wengine ambao nao wanaamini kwamba ni kweli kuna maisha baada ya kifo, lakini hakuna mbinguni mbali na hapa duniani. Wao huamini kwamba Mungu akishahukumu watu wake, ataondoa ubaya wote na kuifanya dunia hii hii kuwa mbinguni.*
Hivyo, tuandikapo vitabu vya kiroho tujipe maarifa ya kutosha kuhusiana na imani zetu. *Hoja yangu haiondoi ukweli kwamba kuna masuala kadhaa ya kiroho ambayo ni ya jumla kwa waamini wa mkondo wa imani husika.* Kwa mfano, yapo mambo ambayo Wakristo wote hukubaliana kiimani.

7. *Kupokea maono ya mambo ya kuandika.* Baadhi ya waandishi huwa wanatoa ushuhuda kwamba kuna nyakati hupokea maono kutoka kwa Mungu kwamba waandike nini kwa wakati gani. *Naomba kusisitiza hapa kwamba hawa wako wachache.* Tena kuna haja ya kuwa makini sana katika jambo hili. Kwa mfano, si kila unachokiota, kinafaa kuandikia vitabu. Ndoto nyingine ni za kibinadamu kutokana na mawazo yetu, hofu zetu, na kawaida tu za miili ya wanadamu. Hivyo, siyo kila unachokiota utudanganye kwamba ni maono. *Hata hivyo, ukweli unabaki palepale kwamba wapo wachache ambao Mungu huwataka waandike vitabu katika masuala fulani ya kiroho.* Mungu akiamua ufanye kazi hiyo, atatumia njia nyingi kukuletea ujumbe. Ni jukumu lako wewe kutumia akili na nguvu ya Roho Mtakatifu kuchuja na kujua kwamba hii ni sauti ya Mungu, ya shetani, ya watu au yako mwenyewe. *Nisisitize tu kwamba ukipata maono ya kuinjilisha kwa njia ya vitabu, basi chekecha na uamue kwa hekima na uifanye kazi kwa uaminifu.*

Haya ni machache tu. *Mengine huenda tukayapata katika mijadala.*
=============

*©️ Leonard Bakize (02.04.2020)*

Kwa hisani ya EWCP
=============