Dar es Salaam. Siku chache baada kuwapo kwa taarifa za tiba ya ukimwi, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi amesema hilo lisiwafanye vijana wajiachie kwa kuwa matibabu hayo ni magumu na yanagharimu fedha nyingi.
Amesema kupatikana kwa tiba hiyo kunaleta matumaini makubwa, lakini haileti maana kuwa watu wasijikinge.
Profesa Kambi ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la saba la sayansi na afya.
Juzi vyombo vya habari vya kimataifa  viliripoti kuhusu mgonjwa aliyekuwa akiishi na VVU ameonekana kupona Ukimwi baada ya kupandikizwa uboho (bone marrow) kutoka kwa mtu mwingine.
Kiongozi wa jopo la madaktari waliomtibu mgonjwa huyo, Profesa Ravindra Gupta ambaye ni mtaalamu wa baiolojia ya VVU, ameeleza kuwa mgonjwa aliyepewa huduma ya kupandikizwa uboho virusi viliondolewa ndani ya mwili wa mgonjwa huyo.
Hata hivyo, Profesa Kambi amesema kufanikiwa kwa chanjo hiyo ni kugumu na kunagharimu fedha nyingi hivyo si jambo la rahisi kama ambavyo watu wameanza kufikiri.
“Naweza kusema inaleta matumaini makubwa ila tusifikiri ni rahisi, ni ngumu kuifanikisha na inagharimu fedha nyingi sana.”
“Vijana wasione kwamba mambo yamepatiwa ufumbuzi ni muhimu waendelee kujilinda dhidi ya ugonjwa wa ukimwi,”
Kuhusu kongamano hilo, alisema limekuja wakati muafaka ambao Tanzania inaelekeza nguvu zake katika mfumo huo.
Amesema kwa dunia inavyoendelea sasa teknolojia ya mawasiliano (Tehama) ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya kuanzia kwenye tiba na ufanyaji tafiti.
“Tunakoelekea Tehama itakuwa kila kitu hivyo kwenye sekta ya afya hakuna namna tunaweza kuikwepa, niwaombe wataalam wa mawasiliano kutumia fursa hii, waje kujifunza ubunifu na namna gani inaweza kutumika kwenye afya.”
“Tanzania tayari tumeshaanza kuchukua hatua kupitia wizara ya afya na tunao mkakati wa kuhakikisha mfumo wa Tehama unaunganishwa kwenye hospitali na zipo ambazo zimeanza kuutumia,” alisema.
Profesa Kambi alieleza kuwa, Tehama ina manufaa makubwa na katika sekta ya afya inasaidia utoaji wa huduma kwa muda mfupi na wakati mwingine kurahisisha mambo.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Utafiti katika afya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ndio waratibu wa kongamano hilo, Profesa Gibson Kibiki amesema katika siku tatu zitawasilishwa mada 91 na yatakuwapo pia maonyesho ya afya.
Amesema kongamano hilo litawakutanisha wataalamu wa afya kutoka nchi sita za Afrika Masharikina linatarajiwa kufanyika Machi 27 hadi 29, mwaka huu na litafunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.