Mapunye ni aina ya maradhi ya fangasi yanayoshambulia ngozi haswa ngozi ya kichwa. Mapunye kwa lugha ya kitaalamu huitwa “Tinea capitis”. Ugonjwa huu hushambulia watu wote wa jinsia na umri wote,ingawa huonekana zaidi kwa watoto wadogo. Ugonjwa huweza kushambulia eneo lote la kichwa au sehemu tu ya kichwa, sehemu iliyoshambuliwa na mapunye huwa na umbo lililofanana na sarafu.

Dalili za mapunye.

  1. Kunyonyoka kwa nywele katika eneo lililo athiriwa.
  2. Eneo la ngozi lililoshambuliwa kuwasha.
  3. kubadilika kwa rangi ya ngozi ya eneo lenye maambukizi. Eneo hubadilika na kuwa na rangi nyeupe.
  4. Kukauka na kubanduka kwa ngozi katika eneo lenye maambukizi.

Maambukizi ya ugonjwa mapunye

Maambukizi ya mapunye hutokea pale ambapo kuna mshabihiano kati ya mtoto  mwenye maambukizi ya ugonjwa huo wa mapunye  na yule asiye na maambukizi. Maambukizi haya hutokea kwa njia zifuatazo:
1.Kutumika kwa vifaa vya kunyolea kw azaidi ya mtoto mmoja bila kuvifanyia usafi.
2. Kutumia taulo au nguo ya kujikaushia kwa mtoto zaidi ya mmoja, hasa pale ambapo mmoja wa watoto hao akiwa na maambukizi ya ugonjwa wa mapunye.
3.Kutumia vifaa vya nywele kama chanuo la kuchania nywele kwa zaidi ya mtoto mmoja.
4.Kugusana na mtu aliye na maambukizi tayari.

Ni nani yuko hatarini?

-Watoto wanaoshirikiana na wenzao vifaa vya kunyolea bila kuvisafisha vizuri.
-Watoto wanaoshirikiana vifaa vya kufanya usafi wa mwili zikiwamo taulo.
-Watoto wanaotoka jasho hasa kichwani kwani huweza kuweka mazingira mazuri zaidi kuruhusu maambukizi yatokee kirahisi.
-Watoto ambao tayari  wana fangasi za kichwani kwani ni rahisi kwa fangasi hao kujirudia.
-Watoto wanaofanyiwa usafi wa mwili kwa kutumia maji yaliyobeba vimelea.
-Watoto wasiojikausha vichwa baada ya kuoga au kufanya usafi wa kichwa.
-Watoto wadogo ambao hawajafikia umri wa balehe.

Jinsi ya kumkinga mtoto dhidi ya mapunye.

a) Usafi wa mwili wa mtoto kama kuhakikisha mwili haswa kichwa cha mtoto kinabaki na ukavu muda wote.
b) Hakikisha nguo, taulo na mashuka yanafuliwa kwa sabuni na maji yaliyo safi.
c) Kwa watoto wanaosoma shule za bweni ni vyema kuhakikisha watoto hawa wanaepuka kushirikiana katika utumiaji wa vifaa vya kufanyia usafi wa mwili mfano taulo.
d) Epusha kushirikiana vifaa vya kunyolea nywele na vifaa vya kuchania nywele haswa kwa watoto wanaosoma shule za bweni.

Matibabu ya ugonjwa wa mapunye.

Mapunye hutibiwa kwa dawa za kutibu magonjwa ya fangasi. Dawa hizi ni za kupaka, hii ni kwa kuwa ni rahisi kwa dawa ya kupaka kupenya kwenye ngozi na kusababisha matokeo yanayohitajika. Ni vyema zaidi dawa za mapunye kwa watoto kushauriwa na daktari kulingana na jinsi alivyoathirika na ugonjwa huo.