Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta  amesema kuwa raia 14 wameuawa katika shambulio lililotokea katika Hoteli ya DusitD2 jijini Nairobi, huku wengine wakijeruhiwa, na 700 wakiokolewa. 

Ameongeza kuwa, magaidi sita waliotekeleza shambulio hilo wameuawa na operesheni imekamilika.

Kenyatta amesema hayo jana  wakati akilihutubia taifa hilo lililokumbwa na tukio la kushambuliwa na magaidi wa Al Shabaab katika eneo la Westlands kwenye jengo lenye Hoteli ya Dusit D2, benki na ofisi mbalimbali jana Jumanne.

Vikosi vya usalama nchini Kenya vimeanza kuondoka katika eneo la tukio baada ya waziri wa usalama, Fred Matiangi, kuzuru eneo hilo na kutangaza kukamilika rasmi kwa operesheni ya kuwasaka washambuliaji.

Septemba. 21, 2013, magaidi hao walishambulia maduka ya Westgate na kuua watu 148 lakini pia Aprili 2, 2015, walishambulia Chuo Kikuu cha Garissa na kuua watu 71.