Mwandishi , SARAH M. MAYUNGA IKS UDSM @ MASSHELE

Mzee Limbu alipatikana katika kijiji cha Sapiwi huko Simiyu.

 Mzee Limbu alikuwa ni mzee mwenye mali nyingi katika kijiji cha Sapiwi na alifanikiwa kuoa wanawake 7 kwa kutumia kigezo cha mali zake.

Mkewe wa kwanza alijulikana kwa jina la Nyakahoja, Nyakahoja alifanikiwa kupata watoto wanne ambao ni Masanja, Mbuke, Maige na Ndono.

Masanja alikua amefikia umri wa kuoa na hivyo baba yake alimsihi atafute msichana yoyote atakaye vutiwa naye ili wapeleka posa kwa wazazi wa binti huyo.

Masanja aliamua kutafuta msichana mzuri katika kijiji chao na kufanikiwa kumpenda msichana aitwaye Zabhe. Zabhe ni binti wa mzee Nkwabi na mama yake Zabhe aliitwa Ngwana Madoshi, Zabhe alikuwa ni binti mwenye umri wa miaka 12 aliyekuwa akisoma darasa la 3.

Zabhe aliipenda sana shule japo hakukuwa na hamasa yoyote katika jamii ya Wasukuma kwa watoto wa kike kusoma. Baada ya Masanja kumpenda Zabhe alienda kumwambia baba yake kuwa amepata msichana mzuri hivyo wapeleke barua ya posa.
Mzee Limbu na baadhi ya ndugu wengine walipeleka barua ya posa kwa mzee Nkwabi, baada ya barua hiyo mzee Nkwabi alifurahi sana kupata ugeni huo.

Kwani alijua wazi kuwa familia ya mzee Limbu ni familia yenye mali nyingi, hivyo akimuozesha binti yake atapata mahari kubwa pamoja na kujipatia umaarufu katika kijiji cha Sapiwi. Mzee Nkwabi aliongea na mwanae Zabhe kumuelezea juu ya ugeni uliofika nyumbani kwake.


Zabhe alikataa kabisa kuolewa kwani alisisitiza kuwa anataka kuendelea na masomo yake na hayuko tayari kuolewa na mvulana asiye mpenda. Mzee Nkwabi alichukizwa na kauli ya mtoto wake na kumwambia kuwa atake asitake ni lazima aolewe katika familia ya mzee Limbu.


Ngwana Madoshi alimsihi sana na kumuomba mumewe amuelewe mtoto juu ya kile anachokitaka asimlazimishe kuolewa, kitendo cha Ngwana Madoshi cha kumuomba mumewe amsikilize mwanaye juu ya kile anachokihitaji kilimkasirisha sana mzee Nkwambi. Hivyo mzee Nkwabi alimpiga mkewe kwa kigezo kuwa yeye ndiye anaye mshauri binti yake akatae kuolewa katika familia ya mzee Limbu, kitendo cha Ngwana Madoshi kupigwa na mumewe kilimpa hofu kubwa na mawazo Zabhe hata Ngwana Madoshi aliogopa sana na hivyo kumshauri mwanae akubaliane tu na baba yake kuwa yupo tayari kuolewa. Baada ya hayo shangazi na bibi yake Zabhe wanakaa na kumfunda kuwa; uendapo kwa mumewe unatakiwa ujitume, ufanye kazi kwa bidii ili iwe sifa kwetu kuwa tulikulea vizuri.


Pia shangazi anasisitiza kwa kusema kuwa uendapo kwa mumeo hakikisha unamsikiliza kwa kila jambo atakalokwambia pia wasikilize ndugu wa mumeo na uwafanyie kile watakachokwambia.

 Harakati za mahari zinakamilika na familia ya mzee Limbu inapeleka mahari kwa mzee Nkwabi ng’ombe 70, magunia ya mpunga 10 pamoja na mbuzi 5 kwaajili ya wajomba. Sherehe kubwa inafanyika watu wanakula na kulewa kisha Zabhe anaondoka kwao na kwenda kuanza maisha mapya kwa mumewe Masanja. Baada ya wiki moja ya Zabhe kuolewa, mumewe na mama mkwe wake wanamuita na kumwambia kuwa anatakiwa kwenda shamba kulima ili aweze kufidia mahari waliyoitoa kwao.

 Zabhe anakubaliana na mama mkwe wake hivyo alikua akiamka asubuhi saa kumi kila siku na kwenda shambani kulima na kurudi nyumbani jioni saa 11, alipofika nyumbani alitakiwa kufata maji na kuwapikia chakula cha usiku, Zabhe alikuwa akichoka sana ila hakua na jinsi ilibidi avumilie tu, na alifanaya kazi zote kwa moyo mmoja japo muda mwingine alikumbuka kwao lakini hakuweza tena kwenda.


Siku zinaenda na baada ya miaka miwili Zabhe anafanikiwa kupata ujauzito, kitendo cha Zabhe kupata ujauzito kilimkera sana mume wake. Kwani Masanja aliwaza kuwa ikiwa mkewe kapata ujauzito kwa muda huo hataweza tena kufanya kazi za shambani, hivyo atashindwa kurudisha mali walizotoa kama mahari. Kwa hiyo Masanja anatafta njia mbadala anaenda kutaafuta dawa kwa mganga kwaajili ya kuondoa mimba hiyo, anapofika kwa mganga, mganga anamshauri Masanja kuwa ampatie dawa ya kuuficha ujauzito wa Zabhe usiweze kuonekana, kwani usipoweza kuonekana Zabhe ataendelea kufanya kazi zake kama ilivyokawaida yake.

Masanja anakubaliaana na wazo la mganga na anapewa dawa hiyo, kisha Masanja anampelekea dawa Zabhe na kumwambia kuwa anatakiwa anywe dawa hiyo ili aweze kuificha mimba hiyo isionekane kwani isipoonekana aataendelea kufanya kazi zake kama kawaida. Zabhe aliogopa sana lakini anakumbuka maneno ya shangazi yake kuwa amtii na kumsikiliza mumewe kwa kila jambo, hivyo Zabhe anakunywa dawa hizo.


Mara baada ya kunywa dawa hizo Zabhe anapata maumivu makali sana na anapojaribu kumwambia Masanja juu ya maumivu makali anayoyapata mumewe anakuwa mkali. Siku zinazidi kusonga mbele na mimba ya Zabhe haionekani tena japo maumivu anayapata lakini anajitahidi kujikaza na anaendelea kazi za shambani ili aweze kufidia mahali aliyotolewa.


Baada ya miaka minne Ngwana Madoshi anaingiwa na wasiwasi juu ya mwanae, anawaza kwanini mwanaye hajashika ujauzito kwa miaka yote hiyo au mwanangu ana matatizo? Ngwana Madoshi anafunga safari na kwenda kuongea na mwanaye ikiwezekana amtafutie dawa ili aweze kuzaa kwa sababu itakua ni aibu sana katika kijiji chao asipoweza kupata mtoto.

 Zabhe anamkatalia mama yake kumtafutia dawa na anashindwa kumwambia mama yake juu ya mimba yake na dawa alizopewa za kuirudisha mimba ndani isiweze kuonekana mpaka pale atakapoweza kupewa dawa ndipo iweze kuonekana.

 Ngwana Madoshi anamsisitiza sana Zabhe lakini Zabhe anakataa na anashindwa kumueleza mama yake ukweli, hivyo mama yake anaondoka.
Baada ya miaka mitano Masanja anaridhika na ufanya kazi wa Zabhe, hivyo anampa dawa ya kuirudisha mimba yake na iweze kuonekana.

Kitendo cha Zabhe kurudishwa kwa mimba yake kilimpa furaha kubwa kwani hakuweza kupata wala kuhisi maumivu yoyote aliyokuwa akiyahisi hapo mwanzo. Pia Ngwana Madoshi alifurahi sana mwanaye kupata ujaauzito. Mimba inakua na Zabhe anafanikiwa kujifungua mtoto wa kike. Majonzi yanatawala katika familia ya mzee Limbu baada ya Zabhe kujifungua kwani mtoto aliyezaliwa alionekana kuwa ni mlemavu yaani zeruzeru.


Masanja anakasirika sana na anamfukuza mkewe kwa kudai kuwa kaleta laana ndani ya ukoo wao na zeruzeru katika ukoo wao hajawaahi tokea. Zabhe anarudi kwao na kupokelewa vizuri na mama yake, mzee Nkwabi pia alisikitika sana juu ya mwanaye hivyo alimpokea mjukuu wake pamoja na mwanaye.

 Baada ya miezi mitatu Masanja anaoa mwanamke mwingine na kumlipia mahari kama ilivyokuwa kwa Zabhe.
Akiwa nyumbani kwao Zabhe alipata sononeko, mawazo na mkanganyiko mzito akilini mwake baada ya Masanja kuoa mwanamke mwingine.

 Jambo hili lilimfanya aumie na kuomba ushauri kwa rafiki yake Mageni. Mageni anamshauri Zabhe aende kwa mganga wa kienyeji akaeleze shida zake na aweze kumloga Mumewe Masanja. Zabhe anafanikiwa kwenda kwa mganga na kumloga mume wake ugonjwa wa Busha.

 Masanja anapata maumivu makali kutokana na ugonjwa huo anatafuta dawa kwa waganga mbalimbali lakini hakufanikiwa kupata dawa za kumtibu.
Zabhe anapata mwanaume mwingine na anaolewa, maamuzi ya Zabhe kuolewa mapema yanamgharimu maisha yake kwa sababu anaangukia kwa mwanaume ambaye baada ya kuolewa tu anakumbwa na tatizo la kiafya. Mumewe wa pili wa Zabhe anakohoa sana hali ambayo inawatisha ndugu wa mumewe na kumpa shutuma Zabhe kuwa ndiye kamloga ndugu yao. Zabhe anaishi maisha ya kusimangwa inafikia hatua ananyimwa chakula wakidai kuwa amponye ndugu yao ndipo ataweza kula.

Mwisho wa siku mwanaume huyo anakufa, baaada ya mazishi wanakaa kikao cha ndugu na kupendekeza kuwa kwa kuwa Zabhe alikua hajazaa na marehemu hivyo mdogo wake marehemu atatakiwa amuoe ili waweze kuzaa. Basi Zabhe hakuweza kupinga alikubaliana na mawazo ya ndugu wa mumewe na anaolewa na mdogo wa aliyekua mume wake.

Zabhe anaishi maisha yenye matatizo makubwa sana inafikia wakati anajiona hana thamani kutokana na changamoto anazokumbana nazo. Mama yake Zabhe alimfariji mwanaye na kumwambia hana haja ya kulaumu anatakiwa kukubaliana na hali kwa sabab imeshatokea.

Maneno ya faraja kutoka kwa Ngwana Madoshi yanamjenga upya Zabhe na kumfanya asahau matatizo yote aliyokumbana nayo na kuamua kuanza maisha mapya.

Mwisho.




Namna hadithi hii inavyo msawiri mwanamke










Wamitila (2010) anaeleza kuwa mwanamke ni mtu mwenye uwezo wa kujifungua. Anaendelea kueleza kuwa ni mtu mwenye jinsia ya kike.


 Aidha maelezo haya hayajatofautiana sana na TUKI (2004) ambapo wanaeleza kuwa mwanamke ni mtu mwenye uwezo wa kujifungua. Hivyo basi mwanamke ni mtu mwenye jinsia ya kike.
Wamitila (2003) anaeleza kuwa hadithi ni masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na mtiririko wake huwa mwepesi au sahihi. Anaendelea kueleza kuwa urefu wa hadithi hutofautiana kutoka kipera kimoja na kingine, pia anaeleza kuwa hadithi huweza kuwa za kubuni au za kihistoria. Naye, Mulokozi (2017) ni masimulizi au ganizi kutokana na kughana au kusimulia. Anaendelea kueleza kuwa ni fani yenye kusimulia habari fulani.
Kwa ujumla hadithi ni masimulizi ambayo yanaweza kuwa yakimapokeo au ya kubuni yenye lengo la kuburudisha na kuielimisha jamii juu ya changamoto mbalimbali zilizo wahi tokea na zinazoendelea kutokea katika jamii. Zifuatazo ni hoja zinazoonesha namna hadithi hii inavyomsawiri mwanamke.
Mwanamke hana haki na uhuru wa kuchagua mchumba, Tadon (2008) anaeleza kuwa mwanamke ana haki na uhuru wa kuchagua na kuyatawala maisha yake na mwili wake awapo nyumbani na kwingineko. Hivyo suala la kumchagulia msichana mchumba na kumlazimisha kuolewa ni kumuongezea mawazo na matatizo mwanamke. Kwa mfano katika hadithi yetu tunaona namna mzee Nkwabi alivyomlazimisha mwanaye kuolewa na Masanja, ilihali Zabhe hakuwa tayari kuolewa. Baada ya kuolewa Zabhe anakumbana na matatizo mengi kama vile; kwanza anaachishwa shule na kupoteza ndoto zake za kuendelea kusoma, kufanyishwa kazi za shamba pasipo kupumzika na kufichwa kwa mimba yake. Kwahiyo jamii inatakiwa kuelewa kuwa msichana anayo haki na uhuru wa kumchagua mchumba amtakaye na suala la kumlazimisha kuolewa na mwanaume asiye mhitaji wala kumpenda linamuathiri mwanamke kisaikolojia.
Mwanamke ni bidahaa, mwanamke anaonekana ni sawa na bidhaaa kutokana na mahari ilipwayo wakati wa kuolewa kwa mwanamke huyo. Aidha, mwanamke kama bidhaa ni usawiri ambao unaimarishwa zaidi na taratibu za jamii nyingi. Katika jamii za Kisukuma mwanaume hulipa mahari kama vile mifugo na pesa kwa familia ya mke mtarajiwa. Katika hadithi yetu tunaona jinsi mahari inavyomuweka mwanamke katika nafasi inayomuonesha kuwa yeye ni sawa na bidhaa ambapo Zabhe anaolewa na Masanja kwa kulipiwa mahari ya ng`ombe 70, magunia ya mpunga pamoja na mbuzi wa 5 kwaajili ya wajomba. Mzee Nkwambi anaridhia na kuona kuwa atapata umaarufu mkubwa katika kijiji cha Sapiwi. Na suala la mahari ndilo lilimfanya mzee Nkwabi amlazimishe mwanaye kuolewa kwa lazima ili aweze kupata mali. Pia suala la mwanamke kuhusishwa kama bidhaa limehusishwa pia na Mnyampala (1965) katika shairi la Useja anaeleza kuwa mwanamke amegeuzwa bidhaa ambayo inaweza kuuzwa na kununuliwa kama bidhaa nyingine zipatikanazo dukani au sokoni kwani utakapo kuoa ni lazima mwanaume utoe mahari, mwandishi anasema;
                           “Yatulazimu kuoa, kwa gharama na haraja,
                            Na mahari tukitoa, na wake tuwapembeja,
                            Sitaha kuiokoa, ilitusije ifuja,
                             Hauna sifa useja, kuoa yatulazimu…”
 Hivyo shairi hili linadhihirisha dhahiri kuwa mahari ni kitu cha lazima kitu ambacho ni kumfanya mwanamke sawa na bidhaa. Vilevile, wazazi wengi huweza kutumia nafasi hii na kuwaozesha watoto wao wa kike kama sehemu ya kuwaingizia kipato. Hivyo basi jamii inapaswa kutambua kuwa suala la kumuozesha msichana kwa lazima ili tu mzazi apate mali ni sawa na kumfanya mwanamke kama bidhaa.
Mwanamke ni mvumilivu na jasiri, mwanamke amekua ni mtu mwenye kuridhika na hali pamoja na kila kitu anachopewa na mwanaume au mumewe. Mwanamke huvumilia akitambua na kujipa matumaini kuwa kesho yatakwisha na maisha yataendelea. Mathalani katika haditihi yetu tunaona jinsi Zabhe anavyokumbana na changamoto mbalimbali katika ndoa ya mumewe wa kwanza hata mumewe wa pili lakini anajikaza na kuvumilia. Katika ndoa yake na mumewe Masanja tunaona namna alivyovumilia mateso ya maumivu makali ya tumbo baada ya kupewa dawa ya kuficha mimba. Halikadhalika Zabhe aliweza kuvumilia kero za ndugu wa mumewe wa pili baada ya kuambiwa kuwa yeye ndiyo chanzo cha mumewe kuugua, ananyimwa chakula lakini anavumilia tu kwa lengo la kutunza ndoa yake. Aidha, Ngwana Madoshi aliweza kuvumilia kipigo kwa mumewe mzee Nkwabi baada ya kumsihi mumewe amsikilize mwanaye kwa kile anachomuomba, Ngwana Madoshi alionesha uvumilivu na ujasiri kwani hakuweza hata kumpinga mumewe juu ya kipigo alichopewa. Hata katika jamii zetu tunaona jinsi wanawake wanavyovumilia shida na mateso katika ndoa zao kwa lengo la kuhofia kuvunjika kwa ndoa zao. Kwani mwanamke anapoachika huonekana kuwa hafai na ana matatizo. Kwahiyo jamii inatakiwa kuelewa kuwa japo mwanamke ni mvumilivu lakini hatakiwi kufanyiwa vitendo viovu.
 Mwanamke ni mshirikina, suala la ushirikina na uganga ni jambo lililopo katika jamii zetu. Na mara nyingi mwanamke amekuwa akihusishwa na masuala hayo kwa kiasi kikubwa tofauti na wanaume japo kuna baadhi ya wanaume wanaojihusisha na ushirikina katika kuomba msaada wa ufumbuzi wa matatizo yao. Katika hadithi hii Zabhe anaonekana akijihusiisha na suala la ushirikina baada ya kufukuzwa na mumewe Masanja aliamua kwenda kwa mganga ili aweze kumsaidia kumpatia dawa zitakazo msaidia kumloga mume wake, Zabhe anafanikiwa kupata dawa na kumloga mumewe. Katika hadithi hii Zabhe alijihusisha na ushirikina baada ya mumewe kumjengea chuki na kumuona kuwa ni mwanamke mwenye laana na hafai kuishi naye. Pia katika jamii wapo pia wanawake wanaokumbana na changamoto mbalimbali zinazowafanya waende kwa waganga kwa lengo la kutatua chanagamoto hizo. Kwahiyo jamii inatakiwa kuiondoa dhana ya kuwa wanawake ni washirikina kwa sababu wanawake hufanya ushirikina baada ya kutendewa mambo mabaya na wanaume zao kama ilivyokuwa kwa Zabhe. Kwahiyo wanaume wanatakiwa kubadilika hasa katika suala la mahusiano. Lakini pia wanawake wanatakiwa kutojihusisha na masuala ya ushiikina kwani unampomloga mtu kwa kumpa ugonjwa unapunguza nguvu kazi ya jamii vilevile mwanamke haifai kabisa kujihusisha na ushirikina.
Mwanamke ni kiumbe duni, nafasi ya mwanamke huonekana kuwa duni ya kuonewa na kunyanyaswa. Wamitila (2002) anaeleza kuwa ndoa ni asasi ya kitamaduni ambayo hutumiwa kumgandamiza na kumnyanyasa mwanamke na kumfanya aonekane ni kiumbe duni. Hata hivyo katika hadithi hii tunaona jinsi nafasi ya mwanamke ilivyo duni na isiyokuwa na uwezo hata wa kupinga yale yanayo mkandamiza na kumnyanyasa kwa kuhofia kuvunja ndoa yake. Kwa mfano Zabhe anaonewa na kunyanywa na mumewe kwa kupewa dawa za kuficha mimba na anashindwa kukataa na kuzitumia dawa hizo. Aidha, Zabhe baada ya kufiwa na mumewe wa pili analazimishwa kuolewa na mdogo wake marehemu yaani shemeji yake. Zabhe anashindwa kupinga na kukubali kuolewa na shemeji yake jambo ambalo linampa msongo wa mawazo. Katika jamii zetu mwanamke amekuwa ni mtu wa kunyanyaswa na kutopewa haki zake za msigi kama kuzuiliwa kusoma na kumsikiliza mwanaume kwa kila kitu. Na suala hili limekua ni mtazamo wa jamii nyingi kuwa, mwanamke hatakiwi kuwa na sauti mbele ya mwanaume na hivyo ni wajibu wake kufata na kusikiliza kila kitu kutoka kwa mwanaume. Kwahiyo jamii inatakiwa kubadili mtazamo wao wa kumuona mwanamke kama ni kiumbe duni na kuzani kuwa mwanamke hana nafasi ya kuheshimiwa na kuthaminiwa katika jamii, kwa kufanya hivyo jamii itaweza kumkomboa mwanamke kutoka katika mateso makali anayoyapata kupitia nafasi ya kuonekana kuwa ni kiumbe duni.
Mwanamke amechorwa kama chanzo cha matatizo na laana katika familia, jamii nyingi zimekua na mtazamo hasi juu ya mwanamke. Mwanamke ni kiumbe kinachogandamizwa na kunyanyaswa kwa kuamini kuwa mwanamke ni chanzo cha laana na matatizo katika familia, koo na jamii kwa ujumla. Katika hadithi hii tunaona namna Zabhe alivyohusishwa na suala la laana na mikosi katika familia baada ya kujifungua mtoto zeruzeru, mara baada ya Zabhe kujifungua mtoto zeruzeru anafukuzwa na mumewe. Masanja anamwambia kuwa kiumbe alichokizaa kina laana kubwa katika familia. Pia, katika jamii wapo watu wanaoendeleza mila hizi potofu za kuwaona wanawake kuwa ni chanzo cha mikosi mara baada ya kujifungua watoto walemavu, ikumbukwe kuwa walemavu nao wana nafasi kubwa katika jamii zetu hivyo suala la kumnyanyasa na kumgandamiza mwanamke kwaajili ya kiumbe alichopewa na Mwenyezi Mungu si jambo jema na halifai kuigwa wala kuendeleza mila hizo potofu.
Mwanamke ni mzazi, Mulokozi (2012) anaeleza kuwa uzazi ndio njia ya uzima wa milele na ugumba ni laana mbaya kuliko zote. Hivyo uzazi ni suala linalopewa kipaumbele na kuthaminiwa sana miongoni mwa wanajamii, aidha suala la uzazi ni muhimu sana kupitia ontolojia ya kibantu ambayo huamini kuwa mwanamke mgumba ni sawa na laana. Pia katika hadithi yetu tunaona namna Ngwana Madoshi alipoingiwa na hofu baada ya mwanaye kukaa kwenye ndoa kwa muda mrefu na kutokupata ujauzito, hivyo ilimlazimu Ngwana Madoshi kuongea na mwanae na kumshauri amtafutie dawa ili aweze kupata ujauzito, lakini mwanaye anakataa kwa sababu alikuwa na siri kubwa ambayo hakumshirikisha mama yake juu ya mimba yake kufichwa. Vilevile, katika kitabu cha Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka mwandishi anadhihirisha kuwa suala la uzazi ni muhimu sana katika jamii na ikitokea mwanamke akashindwa kuzaa basi itakua ni aibu na laana kwake ndio maana Bi. Bugonoka baada ya kushindwa kushika ujauzito ndugu wa mwanaume wanapatwa na hasira na kumshauri Myombekere kuoa mwanamke mwingine. Mwandishi anadhihirisha hayo kwa kusema;
“Hapo jamaa wa Myombekere wakaanza kuwaka hasira
  na kupayuka wakimwambia amkatae mke wake, wakisema,
    wewe ni ndugu yetu, sasa unakubali kweli kukaa na mke wako
huyu akiwa mgumba hivi, uzuri wako huu wote uishie chini!!....” uk1.
 Pia katika jamii zetu mwanamke anapoolewa na kuchelewa kupata ujauzito jamii inayomzunguka humuona hafai na huweza kufukuzwa kwa mumewe jambo ambalo si sawa. Kwani tatizo la kutokushika mimba linaweza likawa lipo kwa mwanaume lakini kutokana na mtazamo wa jamii wa kuamini kuwa mwanamke ndiye mwenye matatizo, basi wanaume hutumia kigezo hicho na kumfukuza mke wake. Kwahiyo jamii ibadili mtazamo wao wa kuamini kuwa mwanamke ndiye mwenye matatizo katika suala zima la uzazi, pia isiwatenge na kuwanyanyasa wagumba kwani ni mipango ya Mwenyezi Mungu.
Mwanamke ni mficha siri, dhana ya kuficha ama kutunza siri ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Yapo mambo bayana yanayopaswa kuelezwa bayana kwa watu wengine na maisha ya ndoa yakaendelea kuwa salama na amani. Kwa upande mwingine ni wazi kuwa si kila jambo linaweza kuelezwa kwa watu lakini inategemea na jambo husika ikiwa jambo ni baya yapaswa kuliweka wazi ili kupata ufumbuzi wa jambo hilo. Na mara nyingi wanawake wamekuwa wakifanyiwa mambo mabaya na waume zao lakini wanakaa kimya kwa kuhofia kuvunja ndoa zao. Mathalani katika hadithi hii tunaona namna Zabhe alivyoweza kukaa na siri baada ya mumewe kumpa dawa za kurudisha mimba ndani ili aweze kufanya kazi. Zabhe anakaa na siri hii huku akiugulia maumivu makali na anamficha hadi mama yake juu ya jambo hilo kwani mama yake alimfata na kuzungumza naye juu ya Zabhe kuchelewa kupata ujauzito lakini Zabhe anashindwa kumwambia mama yake ukweli. Pia Muhando (1974) katika Tamthiliya ya Heshima Yangu, anamsawiri mama Salum kuwa ni mama aliyetunza siri ya ujauzito wake kwa muda mrefu pasipo kumtaja baba wa mtoto. Mama Salum alitunza siri hii kutokana na kuhofia vitisho alivyofanyiwa na mzee Issa, ambaye ndiye mwenye ujauzito huo. Kitendo cha mama Salum kukaa na siri hiyo, ilimanya mwanaye kumpenda dada yake jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya jamii kuoana ndugu wa baba mmoja. Vilevile, katika jamii wanawake wanakumbana na changamoto nyingi kama vile kupigwa na waume zao lakini wanakaa kimya na kuwafichia siri waume zao, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao. Hivyo wanawake wanatakiwa kubadilika na wasikae na siri tena, kwani kuna vyombo ya dola vinavyotetea haki za wanawake.
Kwa ujumla, hadithi ni muhimu sana katika jamii kwani huonya, huadibu, na kuelimisha jamii pamoja na kuishauri na kuiainisha jamii. Hadithi huwa na wahusika wenye wasifu Fulani wanaotumia kuelekeza kwenye sifa nzuri na sifa zinazopaswa kuupuuzwa. Aidha katika hadithi hii tunaona namna mwanamke alivyoswiriwa na kuonesha changamoto mbalimbali anazokumbana nazo, hivyo kupitia hadithi hii tunaona mwanamke anachorwa kwa mitazamo hasi. Mathalani katika suala la ushirikina pamoja na mateso mbalimbali ambayo yanasawiri maisha halisi ya wanawake katika jamii zetu. Kwahiyo wanawake wanatakiwa kushirikiana ili waweze kujikomboa wao kwa wao juu ya matatizo wanayokumbana nayo.















MAREJELEO
Kiteleza, A. (1964). Bwana Myombekere na Bi. Bugonoka. Dar es Salaam: Tanzania Publishing
                     House.
Mnyampala, E. M. (1965), Waadhi wa Ushairi. Dar es Salaam: East African Literature Bureau.
Muhando, P. (1974). Heshima Yangu. Nairobi: EAPH
Mulokozi, M. (2012), Riwaya ya Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Haijachapishwa
Mulokozi, M. (2017), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: KAUTTU
Tandon, N. (2008), Feminism A Paradigm Shift. New Delhi: Atlantic Publishers and Distributors
               (P) Ltd.
TUKI (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu.Kenya: Oxford University Press.s
Wamitila, K. W. (2002), Uhakiki wa Fasihi, Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi: Phoenix
                  Publishers.
Wamitila, K. W. (2003), Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi. Nairobi: English Press.
Wamitila, K. W. (2010), Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi: Vide~Muwa Publishers Ltd.