Wakati wazungu wanagawana bara la Afrika, walipokuja walikuta baadhi ya maeneo kuna tawala zenye nguvu, zilizokua na mfumo rasmi wa uongozi. Wao waliziita tawala za jadi (Chiefdoms).

Moja ya tawala iliyokua na nguvu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ni dola ya wachagga (Chagga state). Zilikuwepo nyingine zenye nguvu kama Himaya ya Sultani wa Zanzibar, Dola ya Buganda, Nyamwezi, Ngoni, Haya, Hutu, Tutsi, Hehe, etc.

Dola ya wachagga imetamalaki eneo la pembezoni mwa mlima Kilimanjaro kuanzia maeneo ya Rongai hadi Siha.

Eneo hili lilikua na mtawala mkuu mmoja (aliyeitwa Mangi Mkuu). Huyu alikua kama Rais ama Mfalme wa jamii hiyo. Chini yake walikuwepo watawala wakuu wawakilishi wa majimbo. Hawa waliitwa 'Mangi Waitori'. Chini yao walikuwepo watawala wa wa maeneo madogo, hawa waliitwa Mangi kama vile Mangi Meli wa Old Moshi, Mangi Sina wa Kibosho, Mangi Salakana wa Useri etc.

Kwa mfano eneo kama Rombo lilikuwa na Mangi wengi. Alikuwepo Mangi wa Keni, Mangi wa Mashati, Mangi wa Mengwe etc. Lakini wote waliunganishwa na Mangi Mwitori wa Rombo. Vivyo hivyo katika maeneo ya Kibosho, Machame, Siha, Old Moshi, Marangu etc.

Mangi mdogo aliripoti kwa Mangi Mwitori. Mangi Mwitori naye aliripoti kwa Mangi Mkuu aliyeunganisha wachagga wote.

Kwa mfano kufikia mwaka 1953 Mangi Mwitori wa Vunjo alikua Petro Itosi Marealle, Mangi Mwitori wa Hai alikua Abdiel Shangali, Mangi Mwitori wa Rombo alikua James Selengia Kinabo kabla ya kustaafu mwaka 1952 na John Maruma kuchukua nafasi yake.

Mangi Mwitori alichaguliwa na wamangi wadogo. Kisha wamangi wadogo na wamangi waitori waliunda baraza kuu la uongozi (Supreme council) ambalo lilimchagua Mangi Mkuu.

January 1952 kulifanyika uchaguzi wa kumchagua Mangi Mkuu wa Wachagga. Wagombea walikua watano. Abdieli Shangali wa Machame, Jackson Kitali wa Mbokomu (Old Moshi), Petro Marealle wa Vunjo, John Maruma wa Rombo, na Thomas Marealle wa Marangu.

Baada ya kila mgombea kunadi sera zake, hatimaye kura zilipigwa na Mangi Thomas Marealle kutangazwa mshindi, akifuatiwa kwa mbali na ndugu yake Mangi Petro Itosi Marealle, aliyekuwa Mangi Mwitori wa Vunjo.

Mangi Mkuu ndiye aliyekuwa Kiongozi mkuu wa dola ya wachagga. Baraza la uongozi (Supreme council) ndicho kilikua chombo cha juu kinachosimamia utendaji wa serikali.

Kwahiyo Mangi mkuu alijitahidi sana kushirikiana mangi waitori na mangi wadogo kuhakikisha jamii nzima ya wachagga inajiletea maendeleo.

Kila Mangi alikua na baraza lake la ushauri lililojulikana kama 'baraza la wachili', ambalo lilifanya kazi kama baraza la mawaziri kwa sasa.

Ushirikiano huu ulifanya dola ya Wachagga kupiga hatua kubwa kimaendeleo kuliko jamii nyingi za wakati huo.

Kwa mfano kufikia mwaka 1920 dola ya wachagga ilikua ya kwanza kwenye ukanda wa Afrika Mashariki kuanzisha na kumiliki gazeti lake (Komkya). Miaka 10 baadae dola ya Buganda (Buganda Kingdom) nayo ilianzisha gazeti lake (Buruuli) na mwaka 1940 Himaya ya Sultani wa Zanzibar (Zanzibar Sultanate) nayo ikaanzisha jarida lake (Imperial).

Si hivyo tu, huduma za maji, umeme, miundombinu ya barabara, hospitali na shule vilifika mapema kulinganisha na maeneo mengine ya nchi. Ikulu ya kisasa ya Mangi Mkuu wa wachagga, iliyojengwa karibu miaka 100 iliyopita ndiyo inayotumika hadi sasa kama Ikulu ndogo ya Rais kwa mkoa wa Kilimanjaro.

Zilizokuwa ofisi za watendaji wa serikali ya Mangi mkuu (eneo la KDC Moshi) ndio ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Moshi kwa sasa.

Maendeleo haya na mengine mengi, wachagga waliamini yalitokana na elimu. Kwahiyo mwamko wa elimu ulikua mkubwa hasa baada ya wamisionari kujenga shule na huduma za afya kila walipojenga kanisa. Vitu hivi vitatu viliambatana. Kanisa, Shule, na Kituo cha afya.

Kwahiyo hata kwenye kuchagua viongozi, yule aliyekuwa na elimu nzuri ndiye aliyepewa nafasi kubwa ya kushinda ikiaminika kwamba elimu yake itachochea kasi ya maendeleo. Na hii ni moja ya sababu iliyomfanya Thomas Marealle kushinda kiti cha umangi mkuu mwaka 1952, kwani kati ya wagombea wote yeye ndiye aliyekua na shahada ya uzamili (masters degree) kwa wakati huo.

Kabla ya uhuru kulikua wachumi wawili tu wazawa ambao ni Thomas Marealle na mzee Fredrick Mchauru ambaye walisoma pamoja London School of Economics, kabla ya Marealle kupata ufadhili Cambridge University (Trinity College).

Iliaminika pia kwamba Uingereza ilitaka dola ya wachagga ijitenge kutoka Tanganyika na itafute uhuru wake yenyewe, kama Rwanda na Burundi zilivyojitenga kutoka Tanganyika baada ya vita vya kwanza vya dunia, wakati huo zikiitwa Ruanda-Urundi.

Hata hivyo mpango huo ulishindikana kwa kuwa Tanganyika ilikua 'Trusteeship colony' ya Umoja wa mataifa, na Uingereza alikabidhiwa tu aisimamie hadi iweze kujitawala. Kwahiyo hoja ya Muingereza ilitupwa kwa maelezo kwamba wakati wa kugawanya bara la Afrika pale Berlin mwaka 1884/85 hakuna nchi inayoitwa 'Chagga state' iliyogawanywa. Hivyo uhuru unaopaswa kuwa wa Tanganyika kwa ujumla na sio wa jamii moja moja.

Baada ya jaribio hilo kushindwa, inadaiwa shirika la ujasusi la Uingereza (M16) lilimpendekeza Mangi Thomas Mareale kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika baada ya uhuru.

Katika moja ya barua za Richard Turnbull (Gavana wa mwisho wa Uingereza) kwenda kwa shirika la ujasusi la nchi hiyo (M16) ilieleza mapendekezo hayo kwa Thomas Mareale.

Sehemu ya nyaraka hiyo iliyoandikwa mwaka 1958 ilisema 'I consider Thomas Marreale an outstanding Chagga leader. I dont know him personally but he would be the leader of Tanganyika if British had to leave. However he lack support from other tribes'

Turnbull alikua akiwaelezea M16 kuhusu Mangi Thomas Marealle na umahiri wake katika uongozi. Hata hivyo alionesha hofu kuwa Marealle hakuwa na ushawishi mkubwa kwa makabila mengine nje ya wachagga.

Na hii ni moja ya hofu kubwa aliyokua nayo Mwalimu Nyerere wakati wa kudai uhuru. Alipofika uchaggani alikuta dola ya wachagga ina mamlaka kamili. Ilikua na 'well defined leadership structure', bendera yake, wimbo wake, na askari wake.

Nyerere alisema ili Tanganyika iwe uhuru lazima dola ya wachagga ife kwanza, kwa sababu hatuwezi kuwa na taifa moja ndani ya taifa jingine. Mwaka 1961 Nyerere aliagiza bendera ya Tanganyika isipandishwe kabla bendera ya wachagga haijashushwa kwanza. Tarehe 8 December 1961 saa 5 usiku bendera ya wachagga ilishushwa katika Ikulu ndogo ya Moshi, na muda mfupi baadae (saa 6 usiku, December 9) bendera ya Tanganyika ikapandishwa.

Hata hivyo hofu ya Nyerere haikua na mashiko kwa sababu Mareale mwenyewe alimpa ushirikiano mkubwa wakati wa kudai Uhuru. Na ili kuonesha kwamba hakuwa na mpango wowote wa kumhujumu, aliamua kujiuzulu nafasi yake ya umangi mkuu mwaka 1960, na kuruhusu askari wake kujiunga na jeshi la Tanganyika.

Pichani ni wagombea watatu kati ya watano walioshiriki uchaguzi wa Mangi Mkuu mwaka 1952. Kutoka kushoto ni Mangi Thomas Mareale aliyeshinda uchaguzi huo), Mangi John Maruma (Mangi Mwitori wa Rombo), na Abdieli Shangali (Mangi Mwitori wa Machame).

Malisa GJ
01/01/2019
Moshi.!

Reposted by @masshele