kazi za mofolojia nikuainisha lugha



1.0.   IKISIRI.

Swali hili tumeligawa katika sehemu kuu tatu ambazo ni Utangulizi, Kiini, na Hitimisho. Katika utangulizi tumeonyesha na kujadili dhana mbalimbali ambazo zimejitokeza katika swahi hili kulingana na wataalam mbalimbali wa Isimu , na katika kiini tumeonyesha  jinsi Mofolojia inavyofanya kazi ya kuainisha Lugha kwa kutumia vigezo vyake muhimu, na mwisho ni hitimisho la swali hili.

2.0. UTANGULIZI.
       Mathews (1974), anasema kuwa Mofolojia ni tawi la taaluma ya Isimu ambalo huchunguza  maumbo ya maneno  na hususani maumbo ya mofimu. Dhana hii imejikita sana katika kuelezea maumbo ya maneno hususani mofimu lakini imeacha nyuma nafasi ya mofu ambayo ndiyo kipashio cha msingi katika mofolojia.
        TUKI (1990), wanasema kuwa Mofolojia ni tawi la Isimu ambalo huchunguza maneno na aina zake. Katika fasiri hii tunaona kuwa hakuna uwazi wowote unaoonekana kwamba ni kwa jinsi gani au ni kwa namna gani maneno haya yanachunguzwa, je yanachunguzwa kwa kuzingatia mpangilio, maana au maumbo yake.
        Obuchi na wenzake (2015), wanasema kuwa Mofolojia ni taaluma ya Isimu inayoshughulikia uchambuzi  wa muundo wa maneno katika lugha. Taaluma hii hudhihirisha maneno kwa kurejelea mofu mbalimbali zenye kazi za kisarufi.
       Kwa ujumla, Mofolojia ni taaluma ya Isimu ambayo inashughulika na uchunguzi wa maumbo na muundo wa maneno katika lugha.
      Massamba (2009), anasema kuwa uainishaji wa lugha ni uwekaji lugha katika  makundi yake kwa kuzingatia uhusiano wake kiasili.
      Mgullu (1999), anasema kuwa uainishaji wa lugha unaweza kufanywa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ambavyo ni uainishaji wa lugha kinasaba, uainishaji wa lugha kijiografia, uainishaji wa lugha kiuamilifu na uainishaji wa lugha kimuundo/  kimofolojia. 
Uainishaji wa lugha kinasaba huzigawa lugha kwa kuzingatia unasaba wake yaani lugha zilizotokana na lugha mame moja huwekwa katika kundi moja. Katika kiwango cha kimataifa mfano kuna makundi ya lugha ambayo yamegawanywa kwa kuzingatia unasaba wake  mathalani jamii ya lugha za Kihindi-Kizungu ambazo zinaitwa  (Indo- European languages family), jamii ya lugha za Kiamerika- Kihindi (American- Indian languages family)  vile vile na kwa upande wa lugha za Kiafrika uainishaji huu wa kinasaba  umetumika pia mfano katika lugha za Kibantu kuna Kilumba, Kibena, Kizulu na Kiswahili. 

Uainishaji wa lugha kijiografia ulikuwa unazingatia zaidi mahali au eneo ambapo lugha fulani huzungumziwa mathalani lugha za Kibantu zinavyoainishwa tunaona kuwa uainishaji huu ulikuwa ukizingatia kigezo cha mahali, mfano kulikuwa na Kibantu cha Mashariki ambayo inapatikana katika maeneo ya Tanzania, Kenya na Uganda, Kibantu cha Kaskazini ambacho kinapatikana Uganda, Burundi na Rwanda. 

Katika uainishaji wa lugha Kiuamilifu au matumizi ya lugha wataalamu wameweza kuzipa  lugha majina  mbalimbali  kulingana na namna lugha hizo zinavyotumika , mfano wa lugha ambazo zinatokana na kigezo hiki cha uainishaji ni kama vile lugha rasimi ambazo zinaonekana kutumia mtindo wa zamani ambao ulitumiwa na watu fulani mashuhuri sana na kuaminika kuwa ni wa kweli na mtindo bora wa lugha ambao ulitakiwa kuigwa na watu watakaokuja nyuma yao, mfano lugha za kigiriki na Kilatini.

 Lugha zingine katika uainishaji huu wa kiuamilifu ni lugha Kienzo, lugha mame, lugha nasaba, lugha rasmi,lugha ya taifa na lugha sanifu.   
      3.0. KIINI.
Kumekuwa na swala la uainishaji wa lugha hasa katika karne ya ishirini kwa sababu hapo mwanzo kulikuwa na haja ya kuelewa lugha ya Kilatini na Kigiriki ambazo zilikuwa zikiaminika kama ni mfumo bora wa lugha kwa watu wote lakini uelewa wa lugha zingine uliendelea kukua siku hadi siku na ndipo lugha zikaanza kuainishwa kifamilia. 

Katika swali hili tutajadili uainishaji wa lugha kwa kutumia kigezo cha Kimofolojia au Kimuundo ambayo inaainisha lugha kulingana 
na muundo wa maneno ya lugha hizo.

         Mgullu ( kashatajwa), anasema kuwa uainishaji wa lugha kwa kutumia kigezo hiki cha Kimofolojia umeainisha lugha kwa kuzingatia au kutumia miundo ya lugha mbalimbali za jamii na uainishaji huu unatupatia aina tano za lugha ambazo ni lugha Tenganishi, lugha Ambashi, lugha Ambishi-mchanganyo, lugha Ambishi- bainishi, lugha Muundogubi.

          Lugha Tenganishi, ni lugha ambazo maumbo yake hayaambishwi au kunyambuliwa, hayabadiliki na na hayana viambishi vyovyote. 

Hii inamaanisha kuwa maana za tungo hudhihirika na kutofautishwa kwa kutumia mpangilio wa maneno ambapo maneno katika lugha za jamii hii huwa na mofu moja tu ambayo huwakilisha mofimu moja.

    Mathews (1991), anasema kuwa lugha tenganishi ni ile amabayo maumbo ya maneno yake huonekana kama mofu moja moja tu, mfano katika lugha ya Kiingereza, Kichina, Kituruki. 

Mathalani katika lugha ya Kiingereza maneno kama “With” na “Rice” katika maneno haya  haiwezekani kuongeza viambishi vya aina yoyote.

          Lugha Ambishi, ni lugha ambazo maneno yake huambishwa viambishi mbalimbali ambavyo huwakilisha maana mbalimbali au kuwakilisha uamilifu mbalimbali wa kisarufi na lugha hizi hupokea viambishi katika mashina yake au katika mizizi yake. Katika lugha hii tunapata lugha mojawapo ya Kibantu ambayo ni Kiswahili ambayo maneno yake huruhusu viambishi, mfano katika maneno yafuatayo:-
                                           Kitenzi: Piga, inaweza kuwa;-
                                        Pigia, Pigisha, Anapiga, Atapigwa,Alipigwa, Alipigia  na Pigishwa.
                                             Cheza, inaweza kuambishwa  na kuwa:-
                                           Chezea, Atacheza, Alichezewa, Anacheza, Wanacheza, Watacheza.
             Lugha Ambishi- Mchanganyo, Hizi ni lugha amabazo maneno yake huambishwa na maneno hayo yanapoambishwa viambishi hivyo huchanganyika na mizizi ya maneno kiasi kwamba huwa ni vigumu kuligawa neno kwa namna ambayo inaweza kuonyesha kuwa  viambishi ni vipi na mizizi ni ipi kwa sababu huwa vimechanganyika  na kuwa kitu kimoja.

 Kwa kuwa  mofu hizi  huchanganyika  mara nyingi na mofu ambayo ni mchanganyiko wa mofu mbili au zaidi itakuwa ni mofu changamano ambayo itakuwa imesitiri mofu zaidi ya moja, mathalani katika lugha ya Kiingereza  kuna maneno kama vile :-
                                               (a)  Mice (wingi wa mouse).  
                                              (b)   Do (done-wakati uliopita) .
Katika mfano huu maneno haya yanaonyesha mchanganyo wa mizizi ya maneno na mofu zinazowakilisha idadi ya wingi  katika mfano (a) na katika (b) hatuwezi kuonyesha mipaka kati ya mizizi na viambishi, mifano mingine ya lugha Ambishi- Mchanganyo ni pamoja na Kilatini, Kigiriki pamoja na Kiarabu. 
                  Kigezo hiki cha kimofolojia imeainisha lugha nyingine ambayo inaitwa lugha Ambishi-bainishi, Lugha hizi ni zile ambazo maneno yake huweza kuwekewa  viambishi mbalimbali. Ni tofauti na lugha ambishi-mchanganyo ambayo huchanganya viambishi vya maneno na mizizi. Katika lugha Ambaishi- bainishi mizizi na viambishi huwa havichanganyiki kwani ni rahisi kabisa kuweza kuonyesha kuwa viambishi ni vipi na mizizi ya maneno ni vipi. Viambishi hivi vinaweza kuwa vya awali au vya mwishoni/ tamati. Lugha inayopatikana katika uainishaji huu ni Kiswahili, mfano katika maneno yafuatayo:-
                                                Nomino:    M-toto    -       wa-toto.
                                                                    Ki-ti       -     vi-ti.
                                                                    Ji-cho      - ma-cho.
                                            

                                             Vitenzi:    A-na-chez-a               ( Anacheza).
                                                            A-na-lim-iw-a            ( Analimiwa).
                                                            A-na-pik-a               (Anapika).
                                                           Wa-li-pig-an-a         (Walipigana).
Katika lugha Ambishi – bainishi tunaona kuwa maneno yanayopokea viambishi mbalimbali ambavyo vina maana ya kisarufi, maneno yaliyokolezwa huonyesha mizizi ya maneno. Lugha zingine katika kigezo hili cha uainishaji ni lugha za Kituruki, Kihangari na Kijapani.
                 Uainishaji wa lugha kimofolojia umeainisha aina nyingine ya lugha yaani Lugha Muundogubi, Hii ni jamii ya lugha ambazo hutumia maneno ambayo huundwa kwa kuweka pamoja mfulilizo wa mofu au hata mfulilizo wa maneno katika neno moja.  Lugha hizi hazitofautiani sana na  Lugha Ambishi- Mchanganyo. Sifa kubwa ya lugha hii ya Muundogubi ni kuwa muundo wa maneno yake ni changamano zaidi.Uhusiano wa kisarufi huonyeshwa kwa kugubikwa mofu mbalimbali pamoja na kujenga neno moja  lenye muundo changamano ambayo ni zaidi ya lugha ambishi bainishi, mfano wa lugha hizi ni zile za  Kieskimo ambazo zinapatikana katika maeneo ya Amerika, Alaska, Greenland, Kanada, Urusi na maeneo mengine ya China.
       4.0. HITIMISHO.
       Kwa ujumla uainishaji wa lugha kimofolijia au kimuundo ndio uainishaji uliotumika sana licha ya kuwepo kwa vigezo vingine, hii ni kwa sababu wanaisimu wameona kuwa kigezo hiki kinatumia muundo wa lugha ambao unaweza kujulikana kwa urahisi zaidi katika kuzichunguza  na kuziainisha katika makundi yao, Vilivile  kigezo hiki ni muhimu kwani inatuwezesha kuzitofautisha lugha moja na nyingine kwa kuangalia muundo wa maneno na mpangilio wake  na pia husaidia ujifunzaji wa lugha za kigeni kiurahisi pale ambapo wajifunzaji wanapoelewa muundo wa maneno wa lugha hizo.    
          











CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI
JINA LA KOZI: MOFOLOJIA YA KISWAHILI.
MSIMBO WA KOZI: KI 209,
KIONGOZI WA SEMINA: MADAM   FIDES
KUNNDI: 02,
SIKU YA SEMINA: JUMANNE
MUDA: 09:00 – 10:00 AM,
MAHALI: ALRB,
                
                       WASHIRIKI.
        JINA
NAMBA YA USAJILI
PROGRAMU
SAHIHI

DUWANGHE   PASHALI  B
2016-04-00978
BAED


OJWANG’O   HAPPINESS
2016-04-02484
BAK






MAREJELEO
Mathews, P.H. ( 1991), Mofolojia ( toleo la pili) : United Kingdom. Cambridge  University 
                         Press.
Massamba, D.P.B, (2009), Kamusi ya Isimu na  Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam. TUKI
Mgullu, R.S. (1999), Mtalaa wa Isimu, Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Longhorn  
                      Publishers. Nairobi.
Obuchi, S.M. na Mukhwana ,A.(2015), Muundo wa Kiswahili, Ngazi na Vipengele. Jomo 
                      Kenyatta Foundation: Nairobi, Kenya
TUKI  (1990), Kamusi Sanifu  ya Isimu na Lugha. Dar es S alaam: TUKI