Mbunge CUF, Dkt. Suleiman Ally Yussuf amefunguka na kuhoji ni sababu zipi zilizopelekea mpaka Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kuwekwa mahabusu ya Polisi kwa kipindi kirefu bila ya kufikishwa Mahakamani kusomewa mashtka

Dkt. Suleimani amehoji hayo leo (Aprili 3, 2018) katika Mkutano wa 11 wa kikao cha Bunge cha kwanza kinachoendelea kufanyika katika mkoa wa Dodoma wakati alipokuwa anauliza swali ya nyongeza kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ambapo alitaka kufahamu uhalali wa Jeshi la Polisi juu ya kuwashikilia watuhumiwa.

"Wako watu wengi wanaowekwa mahabusu ya Polisi kwa zaidi ya siku 15 bila ya kupelekwa Mahakamani akiwemo mwanafunzi Abdul Nondo. Nataka nijue ni sheria gani ambayo inatumika au inatumiwa na Jeshi la Polisi kuwaweka watu mahabusu ya Polisi zaidi ya muda huo mrefu bila ya kupelekwa Mahakamani", amehoji Dkt. Suleiman.

Aidha, katika kujibu hoja hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema polisi ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa katiba na sheria na linatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba.

"Polisi wana mamlaka kisheria kutuhumu, kukamata, kuhoji na kuweka watuhumia mahabusu kwa muda ulioruhusiwa kisheria endapo itabainika kuwa kuna viashiria au taarifa ya kuhusika katika kutenda kosa la jinai. 

"Kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utendaji zinazoongoza Jeshi la polisi inapobainika askari amembambika kesi kwa sababu zozote zile huchukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu ikiwemeo kufukuzwa",amesema Waziri Mwigulu.

Pamoja na hayo, Waziri Mwigulu ameendelea kwa kusema "kwa kuwa jambo la kiusalama ni kipaumbele, kwa mtuhumiwa na rai wengine waliosalia, Jeshi la Polisi hutumia wajibu wake waliopewa wa kulinda usalama wa raia kwa kuweza kuhakikisha kwamba linatimiza majukumu yake na huku likiwaacha watu wakiwa salama kabisa".

Kwa upande mwingine, Waziri Mwigulu hakuweza kujibu suala lolote kuhusu Nondo kama jinsi lilivyo hojiwa na Mbunge Sulleiman juu ya uhalali wa Jeshi la Polisi kumuweka kijana huyo zaidi ya siku 15 mahabusu ya polisi.