aina za kisukari

Kisukari ni kundi la magonjwa yanayohusiana na ufanyaji kazi wa mwili ambapo mtu anakuwa na kiwango kikubwa cha sukari aina ya glucose katika mwili kutokana na  mwili wake kukosa uwezo wa kutengeneza insulin ya kutosha au seli za mwili wake haziwezi kutumia insulin iliyopo au pengine mwili kuwa na matatizo yote mawili kwa pamoja. Mgonjwa wa kisukari hupata haja ndogo mara kwa mara (polyuria), kusikia kiu kila wakati (polydipsia) na njaa (polyphagia).
Kuna aina tatu za kisukari; Type 1 Diabetes, Type 2 Diabetes na Gestational Diabetes.

1. Type 1 Diabetes


Mwili wa mgonjwa wa aina hii ya kisukari hautengenezi insulin kabisa. Kisukari cha aina hii mara nyingine huitwa insulin-dependent diabetes, juvenile diabetes, au early-onset diabetes. Watu huwa na kisukari aina hii wanapokuwa na umri wa chini ya miaka 40 na hasa katika miaka ya mwanzo kabisa ya ujana wao. Kisukari cha aina hii huwapata watu wachache ukilinganisha na aina nyingine za kisukari, karibu asilimia 10 tu ya wagonjwa wote wa kisukari huwa na aina hii ya kisukari.
Mgonjwa mwenye kisukari cha aina hii atapaswa kutumia sindano za kumwongezea insulin mwilini katika maisha yake yote na lazima kila wakati ahakikishe kuwa kiwango chake cha sukari mwilini kinakuwa sawa kwa kuchukua vipimo na kufuata mpango wa chakula maalum.

2. Type 2 Diabetes


Mwili hautengenezi insulin kwa kiwango cha kutosha au seli za mwili zinashindwa kuitumia insulin iliyopo (insulin resistance). Karibu asilimia 90 ya wagonjwa wa kisukari katika ulimwengu husumbuliwa na aina hii ya kisukari.
Watu wenye unene usio wa kawaida na wenye uzito mkubwa wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata kisukari cha aina hii ukilinganish na wale wenye miili ya kawaida. Kuwa na uzito mkubwa au unene usio wa kwaida husababisha mwili kutoa kemikali zinazovuruga mfumo wa namna ya mwili unavyotumia chakula kilichoyeyushwa ili kuupa mwili nguvu na kuuwezesha kukua.
Kuwa na uzito mkubwa, kutofanya mazoezi na kutozingatia namna ya kula chakula kinachofaa, humweka mtu katika hatari kubwa ya kupata aina hii ya kisukari . Kwa mfano, kunywa soda moja tu kwa siku kunaongeza uwezekano wa kupata aina hii ya kisukari kwa kiwango kikubwa sana.
Hatari ya kupata kisukari cha aina hii huongezeka pia na umri, sababu kamili haijajulikana bado lakini labda kwa vile umri ukiongezeka mtu huongezeka uzito na hupunguza shughuli za kuutumia mwili wake.
Inaonekana pia kuwa mtu mwenye ndugu wa karibu mwenye ugonjwa huu, naye pia huweza kuupata ugonjwa huu. Watu wa asili ya Mashariki Ya Kati, Afrika na kusini mwa mwa Bara la Asia hupatwa sana na kisukari cha type 2 Diabetes.
Kuwa na kiwango kidogo cha homoni ya testosterone kumeonyesha kuwa na mchango katika kusababisha aina hii ya kisukari. Wataalamu wanasema kuwa kuwa na kiwango kidogo cha testosterone katika mwili kunahusiana na tatizo la mwili kutoweza kuitumia insulin (insulin resistance).
Kuna baadhi ya watu ambao wameweza kuudhibiti ugonjwa huu kwa kupunguza uzito wa miili yao, kufuata mipango mizuri ya chakula, kufanya mazoezi ya miili yao na kuchukua vipimo vya mara kwa mara kujua viwango vya sukari katika miili yao. Lakini kisukari cha aina hii ya pili ni ugonjwa unaokua kila siku na dalili zake kuongezeka kila siku, hivyo mwishowe mgonjwa itabidi aongezewe insulin. Mara nyingi wagonjwa wa aina hii ya kisukari mwishowe huongezewa insulin ya vidonge.

 3. Gestational Diabetes


Hiki ni kisukari wanachopata wanawake wakati wanapokuwa wajawazito. Baadhi ya wanawake wanakuwa na viwango vikubwa sana vya glucose katika damu zao na miili yao haina uwezo wa kutengeneza insulin ya kutosha kuweza kusafirisha glucose hiyo hadi kwenye seli za miili yao hivyo kusababisha kuongezeka kwa kiwango cha sukari katika miili yao.
Kisukari hiki huweza kudhibitiwa vizuri kwa kula chakula kinachofaa na kufanya mazoezi, Ni asilimia ndogo kati yao ambao huhitaji kupewa dawa. Gestational diabetes isipodhibitiwa huweza kusababisha matatizo wakati wa uzazi au kufanya mtoto anayezaliwa kuwa mkubwa kuliko alivyostahili.

madhara ya kisukari

Kisukari Ni Tatizo La Matumizi Ya Chakula Mwilini


Kisukari (diabetes mellitus) huhesabiwa kama ni tatizo la matumizi ya chakula katika mwili. Mwili wa binadamu hutumia chakula kilichoyeyushwa ili kuuwezesha kuwa na nguvu na kukua. Chakula cha aina nyingi tukilacho huvunjwavunjwa na kupata glucose, aina ya sukari katika damu ambayo ndiyo chanzo kikuu cha nguvu katika mwili wa binadamu.
Chakula baada ya kuyeyushwa, glucose huingia katika mfumo wa damu. Seli za mwili hutumia glucose hiyo ili kupata nguvu na kukua. Lakini seli haziwezi kuchukua glucose hiyo bila uwepo wa insulin, insulini ndiyo inayoziwezesha seli hizo kuchukua glucose.
Insulin ni homoni inayotengenezwa na kongosho. Baada ya kula, kongosho hutoa insulin ya kutosha kuwezesha seli kuchuka glucose iliyopo katika damu, na mara baada ya glucose hiyo kuchukuliwa na seli, kiwango cha sukari katika damu hushuka.
Mtu mwenye kisukari ni yule ambaye kiwango chake cha glucose katika damu ni kikubwa mno (hyperglycemia) kutokana na kwamba mwili wake hautengenezi insulin, hautengenezi insulin ya kutosha au seli kushindwa kuitumia insulin inayotengenezwa na kongosho. Mapato yake ni kuongezeka kwa kiwango cha sukari katika damu ambayo baadaye hutolewa nje ya mwili kupitia katika mkojo. Mgonjwa wa kisukari ana zahana kubwa ya glucose katika damu yake lakini mwili unashindwa kuitumia glucose hiyo kwa matumizi yake ili upate nguvu na kukua


Dalili Na Madhara Ya Kisukari



madhara ya kisukari

Tuliona katika ukurasa mwingine kuwa kisukari ni ugonjwa ambao humsababishia mtu kuwa na kiwango kikubwa cha sukari katika damu na kushindwa kuitumia sukari hiyo ipasavyo ili kumpa nguvu na hivyo sukari hiyo kutoka nje ya mwili wa mgonjwa kupitia njia ya mkojo. Ugonjwa huu pia huitwa Diabetes Mellitus, maneno yanayotokana na kigiriki na kilatini. Diabetes linatokana na kigiriki likimaanisha kijibomba kinachonyonya maji na mellitus linatokana na neno la kilatini “Mel” lenye maana ya asali, hivyo diabetes mellitus ni “kunyonya maji yenye utamu kama asali” baada ya madaktari wa enzi hizo kugundua kuwa mkojo na damu ya mgonjwa wa kisukari vilikuwa na glucose kwa wingi sana.
Wachina wa zamani nao waligundua kuwa mchwa walijaa kwa kwingi kwenye eneo la mkojo wa mtu mwenye kisukari kutokana na mkojo huo kuwa mtamu na wakatoa neno “Sweet Urine Disease” -Ugonjwa wa kutoa mkojo mtamu.

Insulin Na Kongosho


Insulin ni homoni inayotoa ishara kwa seli za mwili ili ziweze kuchukua glucose kotoka kwenye damu na kuitumia katika kuupa mwili nguvu na kuujenga. Kama kiwango cha insulin mwilini ni kidogo au hakuna insulin kabisa katika mwili, glucose haitachukuliwa na seli za mwili hivyo kusababisha mwili kuyeyusha mafuta yaliyomo mwilini ili upate nguvu.
Insulin karibu za wanyama wote hufanana, tofauti ni katika nguvu ya ufanyaji wake wa kazi. Kwa mfano, insulin ya nguruwe “Porcine insulin”, inafanana sana na insulin ya binadamu, hii ikiwa na maana kuwa binadamu anaweza kutumia insulin ya wanyama. Lakini kwa bahati nzuri, insulin inaweza kutengenezwa kwenye maabara.
Kongosho ni sehemu ya viungo vilivyo katika mfumo wa uyeyushaji (mmeng’enyo) wa chakula na kinapatikana sehemu ambapo mbavu hukutana kwa chini. Kongosho lina umbo la jani na lina urefu upatao kama nchi sita. Kongosho ina kazi ya kutengenza insulin na homoni zingine za kusaidia uyeyushaji wa chakula.

Dalili Za Kisukari Ni Zipi?


Baada ya kujikumbusha hayo, sasa tutazame mambo ambayo yakikutokea ujue kwamba ni dalili za kuwa na ugonjwa huu wa kisukari. Watu wengi wanakuwa na ugonjwa huu bila kujijua kwa sababu dalili za awali za ugonjwa huu hazimsababishii mtu kushindwa kuendelea na shughuli zake za kawaida, lakini ni vizuri kuugundua ugonjwa huu katika hatua zake za awali ili kuepukana na madhara makubwa yanayoweza kutokea baadaye. Tutaorodhesha hapa dalili zinazojionyesha mara nyingi zaidi:
Kukojoa mara kwa mara: Jee, umekuwa na tabia ya kwenda kupata haja ndogo mara kwa mara? Kama jibu ni ndiyo, basi figo zako sasa haziwezi kuirudisha glucose kwenye mfumo wa damu na badala yake zinachukua maji kutoka kwenye damu na kusababisha kibofu kijae mara kwa mara.
Kiu Isiyoisha: Kama unakojoa mara kwa mara, utapata kiu isoisha kwa sababu mwili unahitaji kurudisha maji uliyopoteza kwenye mkojo.
Njaa Kali: Kama isulin yako haifanyi kazi au kama huna insulin, mwili wako unakosa glucose ya kuupa nguvu. Katika kutafuta njia nyingine ya kupata nguvu, mwili utakuwa na njaa ili uupatie chakula.
Kuongezeka kwa uzito (unene): Hii inatokana na dalili ya kusikia njaa kali.
Kupungua uzito kusiko kawaida: Hili huwatokea zaidi wagonjwa wa Type 1 Diabetes kwa sababu kwa kukosa insulin na seli kukosa chanzo cha kupata nguvu, mwili huanza kuvunjavunja misuli na kuyeyusha mafuta ya mwili ili upate nguvu hiyo hali inayochangiwa zaidi na tabia ya kisukari cha aina hiyo kujitokeza kwa ghafla.
Uchovu wa mwili: Mwili unapokosa glucose ya kuzipa seli nguvu, uchovu hutokea.

dalili za kisukari

Hasira: Hasira zinaweza kuwa ni sababu ya mwili kukosa nguvu.
Kutoona vizuri: Ugonjwa huu husababisha mtu kushindwa kuviona vitu vizuri. Tatizo hili hutibika lakini mara nyingine hali huweza kuwa mbaya kiasi cha kuwa na tatizo la kudumu au kupata upofu.
Vidonda kutopona vizuri au haraka:Unapokuwa na sukari nyingi katika damu, uwezo wa mwili kuponya vidonda hupungua.
Magonjwa ya ngozi: Mwili wenye sukari nyingi ndani ya damu huwa na uwezo mdogo sana wa kujiponya kutokana na maambukizi ya wadudu. Wanawake wenye kisukari huwa na maambukizi zaidi na hupata shida kubwa ya kuponya maambukizi ya sehemu nyeti za miili yao.
Kuwashwa kwa ngozi: Kuwashwa kwa ngozi mara nyingine ni dfalili ya kuwa na kisukari.
Kuwa na fizi nyekundu au zilizovimba:Fizi nyekundu na/au zilizovimba huweza kuwa kuwa ni dalili ya kuwa na ugonjwa wa kisukari, mara nyingine meno hulegea.
Uwezo mdogo wa kushiriki tendo la ndoa: Hili ni tatizo hasa la wanaume wenye umri unaozidi miaka 50, ambapo mara nyingi watakosa uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kikamilifu au uwezo wao wa kufanya tendo hilo kufa kabisa (Erectile Dysfunction).
Ganzi mikononi au miguuni: Uzidifu wa sukari mwilini huweza kuharibu neva au mishipa midogo ya damu inayolisha neva, hivyo kusababisha hali ya ganzi mikononi au miguuni.


madhara ya kisukari

Madhara Ya Kisukari


Kama ugonjwa wa kisukari hautadhibitiwa ipasavyo, madhara makubwa huweza kutokea. Baadhi ya madhara ambayo yamehusishwa na ugonjwa huu ni kama ifuatavyo:
  • Matatizo ya macho-glucoma, cataracts na mengineyo.
  • Matatizo ya miguu-vidonda na gangrene ambavyo mara nyingine husababishwa miguu ikatwe.
  • Matatizo ya moyo-pamoja na upungufu wa damu inayoelekea kwenye misuli ya moyo.
  • Hypertension-ambayo huweza kulsababisha figo kushindwa kufanya kazi, matatizo ya macho, magonjwa ya moyo na kiharusi.
  • Matatizo ya kusikia-kisukari husababisho tatizo la kushindwa kusikia vizuri.
  • Gastroparesis-misuli ya tumbo kushindwa kufanya kazi yake vizuri.
  • Kiharusi (Stroke)-endapo blood pressure, cholesterol na sukari havitadhibitiwa, uwezekano wa kupatwa na kiharusi huwa ni mkubwa sana.
  • Ugumba-kisukari humfanya mgonjwa ashindwe kufanya tendo la ndoa.


Tiba Za Kisukari: Chakula Na Mazoezi Kwa Mgonjwa Wa Kisukari



Hapo zamani, kabla ya uvumbuzi wa insulin (1921), ugonjwa wa kisukari, Type 1 Diabetes, ulikuwa ni ugonjwa ulioua watu wengi sana miaka michache tu baada ya mtu kuupata ugonjwa huo. Lakini sasa mambo yamebadilika kwa kiasi kikubwa sana. Mtu mwenye ugonjwa huu anaweza kuishi maisha ya kawaida kabisa, ili mradi anakuwa na mpango mzuri wa chakula, mazoezi ya kutosha na anatumia insulin. Kuwa mgonjwa wa kisukari maaana yake ni kukubali namna ya kuishi na siyo kushindwa kufanya jambo lo lote lile ulilokusudia. Unaweza kufanya biashara zako, kushiriki michezo na kufikia malengo yako bila tatizo lo lote.
Kuna orodha ya watu wengi waliokutwa na kisukari na wakafanya vizuri katika michezo, siasa, uigizaji wa filamu, muziki, uandishi wa habari n.k. Kinachotakiwa ni kuwa na mpango mzuri wa kula, mazoezi ya kutosha na kuzingatia tiba unayopewa na daktari wako. Hakuna sababu KAMWE ya kushindwa kufikia malengo yako. Mfano mzuri ni Sir Steven Redgrave, mwanamichezo aliyeweza kunyakua medali za dhahabu katika michezo ya Olympiki kwa miaka mitano mfululizo akiwa mwathirika wa Type 1 Diabetes kuanzia mwaka 1997.
Mgonjwa wa kisukari anapaswa kuchukua vipimo mara kwa mara ili kujua kiwango cha sukari alicho nacho, anapaswa vilevile kuhakikisha kuwa anapima blood pressure na kudhibiti kiwango cha cholesterol kwani vinaweza kumsababishia magonjwa ya moyo.

Kisukari Cha Juu Na Kisukari Cha Chini

Mgonjwa anatakiwa ahakikishe kiwango chake cha sukari katika damu hakibadiliki sana. Kuwa na kiwango kidogo cha sukari katika damu (Hypoglycemia) kuna madhara mengi katika mwili wa mgonjwa kama vile ilivyo kwa mgonjwa kuwa na kiwango kikubwa cha sukari katika damu (Hyperglycemia).

Mpango Wa Chakula Kwa Mgonjwa Wa Kisukari


Mgonjwa wa kisukari hana masharti ya ajabu kuhusu chakula anachotakiwa kula, kimsingi anaweza kula chakula cho chote anachopenda. Kuna mambo matatu ambayo yanabidi kuangaliwa katika kuweka kiwango cha sukari cha mgonjwa kwenye kiwango kinachofaa. Mambo hayo ni:
  • Ni chakula gani
  • Chakula hicho kinaliwa kwa kiasi gani
  • Chakula hicho kinaliwa muda gani
Watalaamu wa afya na mambo ya chakula wanabainisha kwamba chakula kinachotakiwa kuliwa kwa wingi zaidi ni chakula chenye wanga (carbohydrates), kikifuatiwa na mboga na matunda, kisha chakula chenye protini na mwisho ni chakula chenye mafuta (fats). Wataalamu na washauri wa magonjwa ya kisukari wanamshauri mgonjwa wa kisukari kupata chakula kwa mpango huo huo.

Chakula Chenye Wanga

Chakula chenye wanga hupatikana zaidi kutoka kwenye nafaka, mboga, maziwa ya mgando na matunda.
Mwili wa binadamu huhitaji chakula chenye wanga, hatuwezi kuishi bila chakula cha aina hii. Mwili hubadilisha wanga na kuwa glucose-aina ya sukari ambayo hutumiwa na seli za mwili kwa ajili ya kupata nguvu na kukua.
Imeonekana kuwa mtu akila kiasi kile kile cha chakula chenye wanga na muda ule ule kila siku, anakuwa na nafasi kubwa sana ya kudhibiti kiwango chake cha sukari katika mwili. Ni muhimu kuhakikisha kuwa mgonjwa haruki mlo wo wote kwani kufanya hivyo kutasababisha badiliko kubwa la kiwango cha sukari katika damu yake kitu ambacho kinatakiwa kikwepwe kwa mgonjwa wa kisukari. Kuwa na ongezeko la glucose katika damu ambalo ni la kawaida kunasaidia kuweza kujua namna ya kuweka uwiano kati ya chakula, dawa na mazaoezi ya mwili na hivyo kudhibiti kiwango cha sukari katika mwili wa mgonjwa.
Uwiano mzuri wa chakula chenye wanga, protini na mafuta umeonekana kuwa:
  • Wanga asilimia 45-65
  • Protini asilimia 15-20
  • Mafuta asilimia 20-35
Kuchanganya aina tofauti tofauti za nafaka, matunda na mboga kumeonyesha kusaidia zaidi na mboga zinasidia kupunguza sukari mwilini kwa sababu ya nyuzinyuzi zake. Hilo pia ni sahihi kwa nafaka ambazo ni nzima, zile ambazo hazikukobolewa.

Mazoezi Ya Mwili Kwa Mgonjwa Wa Kisukari


Mazoezi ya mwili kwa mtu anayeishi na tatizo la kisukari ni muhimu kwa sababu zifuatazo:
  • yanasaidia katika kudhibiti kiwango cha sukari katika mwili
  • yanasaidia kupunguza uzito wa mwili
  • yanasaidia kudhibiti blood pressure
  • yanasaidia kuweka cholesterol kwenye kiwango kizuri


mazoezi kwa mtu wa kisukari

Pamaoja na faida hizi hapo juu, mazoezi pia yanasaidia kupata usingizi mzuri na kupunguza msongo wa mawazo. Inashauriwa kufanya mazoezi angalau kwa siku tano katika wiki na mazoezi hayo yawe ya kawaida, siyo ya nguvu, ambayo yatafanywa kwa muda usiopungua nusu saa kila siku. Mazoezi ambayo unaweza kuyafanya ni pamoja na kutembea kwa mwendo wa haraka, kuogelea, kuendesha baiskeli kwenye sehemu ya tambalale au milima ya kadri, kucheza muziki au hata kukata majani kwenye bustani.
Kama hujafanya mazoezi kwa muda mrefu, anza na mazoezi madogo na kuongeza viwango taratibu. Zingatia kuwa mazoezi yawe kama ya nusu saa kila siku na yafanywe angalau kwa siku tano katika wiki na siyo mazoezi ya saa mbili mara moja kwa wiki.
Unaweza kujiunga na gymn, sehemu ambayo utapata mtaalamu wa kutoa mazoezi kwa watu wenye matatizo mbalimbali. Kupata mtu wa kukusaidia na kukuelekeza katika mazoezi kutakupa ari ya kufanya mazoezi kwa umakini zaidi. Isitoshe, gymn zina vifaa vya kisasa vya kukupa vipimo vya mazoezi yako na maendeleo yako.



Tiba Ya Kisukari Kwa Kutumia Insulin



upofu kutokna na kisukari

Tumekwisha kuona ni chakula gani apate mgonjwa wa kisukari na kwa mpango upi mgonjwa wa kisukari apate chakula hicho. Pia tulijadili jinsi ya kufanya mazoezi ya mwili na kuona faida za mazoezi hayo kwa mgonjwa huyu. Katika mada yetu ya leo, tutazungumzuia namna ambavyo mgonjwa wa kisukari anavyoweza kupewa au kutumia insulin.
Kimsingi mgonjwa anaweza kupewa insulin ya vidonge, lakini pindi atakapokunywa vidonge hivyo na vikafika tumboni, vitameng’enywa mara moja bila hata kuingia katika mkondo wa damu. Hivyo basi inapasa kumpa mgonjwa insulin ya sindano ambayo itachonmwa kwenye mafuta yaliyo chini tu ya ngozi, ili taratibu dawa hiyo iingie kwenye mkondo wa damu.
Kuna aina zaidi ya 20 za insulin ambazo kila kila moja inafanya kazi tofauti na nyingine, imetengenezwa kwa njia tofauti na nyingine na ina bei tofauti na nyingine. Insulin nyingi hutengenezwa kwenye maabara na nyingine hutokana na wanyama, hasa nguruwe.

Tiba Ya Kisukari Kwa Insulin Ya Sindano



Tiba ya kisukari kwa sindano ya insulin

Rapid-acting insulin
Rapid-acting insulin ni aina ya insulin ambayo hufanya kazi kwa haraka sana, dakika 5 tu baada ya mgonjwa kuchomwa sindano hiyo na hufikia kilele cha ufanyaji kazi wake baada ya saa moja. Insulin za aina hii huendelea kuwa na nguvu ya kufanya kazi katika mwili kwa muda wa saa 2 hadi 4. Mifano ya Rapid-acting insulin ni lispro, insulin aspart na insulin glulisine.
Short-acting insulin
Insulin ya aina hii huingia kwenye mkondo wa damu ndani ya dakika 30 tu na hufikia kilelele cha utendaji kazi wake ndani ya saa 2 hadi 3. Insulin hii huendelea kufanya kazi ndani ya damu kwa muda wa saa 3 hadi 6.
Intermediate-acting insulin
Intermediate-acting insulin huchukka muda wa saa 2 hadi 4 kuingia kwenye mfumo wa damu baada ya sindano kuchomwa na hufikia kilele cha ufanyaji wake kazi baada ya saa 4 hadi 12. Inaendelea kufanya kazi mwilini kwa muda wa saa 12 hadi 18.
Long-acting insulin
Insulin ya aina hii huingia ndani ya damu baada ya saa 6 hadi 10 baada ya kuchomwa sindano na zinafanya kazi ndani ya damu kwa muda wa saa 20 hadi 24.
Pre-mixed insulin
Wagonjwa wengine wa kisukari hutakiwa wachanganye insulin za aina mbili. Ili kuwarahisishia, kuna insulin ambazo zinakuja zikiwa zimeshachanganywa tayari. Insulin za aina hii huwasaidia zaidi watu wenye matatizo ya kuona.

Tiba Ya Kisukari Kwa Kutumia Insulin Pump


Insulin pump ni kifaa maalumu kilichotengenezwa kukuongezea insulin mwilini kwa haraka muda wote unapokuwa unakitumia. Ni kifaa ambacho unaweza kukifunga kwenye mkanda, kukiweka ndani ya mfulo wa nguo yako au kukifunga kwenye mkono au mguu na kukifunika na nguo zako. Usiku unapolala, unaweza kukiweka chini ya mto au po pote unapoona panafaa karibu na kitanda chako.

tiba ya kisukari kwa insulin pump

Kifaa hiki hutumika zaidi na watu wenye Type 1 Diabetes ingawa taratibu watu wenye Type 2 Diabetes nao wameanza kukitumia. Ni kifaa chenye faida nyingi sana katika kudhibiti kiwango cha sukari katika mwili wa mgonjwa.
Mada hii ya kisukari ni mada ndefu iliyotuchukua toka kujua chanzo cha kisukari na aina zake, ikatupeleka kujua dalili na madhara ya kisukari na vile vile ilizungumzia njia nyingine za kupambana na kisukari kabla ya leo kuzungumzia tiba ya kisukari kwa kutumia insulin